Dk John Magufuli (Kushoto) na Edward Lowassa (kulia)
Dar es Salaam. Wakati zikiwa zimesalia siku 14 kabla ya kuanza kwa kampeni za urais, ubunge na udiwani, macho na masikio ya wengi yanaelekezwa kwa wagombea wawili kutoka vyama vikuu vya siasa, Dk John Magufuli wa CCM na Edward Lowassa wa Chadema, ambao uchambuzi wa gazeti hili unaonyesha wana mengi yanayoshabihiana.
Wawili hao ni kati ya makada saba waliosimamishwa na vyama saba kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ambao inaelekea kuwa ndiyo watakaochuana vikali, hasa kutokana na ukweli kuwa Dk Magufuli anatoka chama tawala na Lowassa, ambaye alikuwa Waziri Mkuu, anaungwa mkono na vyama vinne vya Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na NLD vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Wengine wanaowania urais ni Mchungaji Christopher Mtikila wa DP, Chifu Lutayosa Chemba (ADC), Macmillan Limo (TLP), Hashimu Rungwe (Chauma), Fahami Dovutwa (UPDP) na mgombea wa ACT Wazalendo ambaye bado hajateuliwa.
Pamoja na kwamba katika siasa lolote linaweza kutokea, wagombea hao watano hawatazamiwi kuweka ushindani mkubwa zaidi ya ule wa Dk Magufuli na Lowassa.
Dk Magufuli hakutarajiwa kupita kwenye mbio za urais ndani ya CCM, ambako Lowassa na vigogo wengine walikuwa wakipewa nafasi kubwa, lakini ushindi wake umemfanya awe mgombea wa chama chenye mtandao mkubwa nchini na hivyo mwanzoni kupewa nafasi kubwa ya kushinda.
Hata hivyo, uamuzi wa Lowassa kujivua uanachama wa chama kilichomlea na kilichompa umaarufu mkubwa, umebadili upepo na sasa vita ya kuingia Ikulu Oktoba 25 inaonekana kuwa ya watu hao wawili.
Gazeti la Mwananchi linaangalia sifa ambazo wawili hao wanashabihiana pamoja na tofauti zao, kwa kuzingatia maelezo ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa.
Wote wamesomea ualimu
Moja ya mambo ambayo wawili hao wanashabihiana ni kusomea ualimu, ingawa wa fani tofauti. Dk Magufuli, ambaye atakuwa akitimiza miaka 56 siku nne baada ya Uchaguzi Mkuu, ni mwalimu aliyejikita kwenye masomo ya kemia na hesabu.
Alipata diploma ya ualimu mwaka 1982 kwenye Chuo cha Elimu Mkwawa, kabla ya kujiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako alipata shahada yake ya kwanza, ya umahiri na ya uzamiri akijikita kwenye somo la kemia.
Lowassa, ambaye Agosti 26 atakuwa akitimiza miaka 62, alisomea shahada ya ualimu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1977, lakini shahada yake ya uzamili ilijikita kwenye masomo ya maendeleo ya jamii.
Dk Magufuli alitumia taaluma yake kufundisha kemia na hesabu kwenye Shule ya Sekondari ya Sengerema, lakini Lowassa hakufundisha.
Wote ni makini
Pengine ni kutokana na maadili ya ualimu, wawili hao wamedhihirisha kuwa ni watu makini katika utendaji wao, jambo ambalo limekuwa likiwafanya watu wanaofanya kazi chini yao kuwa na wasiwasi kila wanapowapeleka taarifa.
Dk Magufuli na Lowassa hutumia muda mwingi kujiridhisha na taarifa wanazopelekewa kabla ya kufanya uamuzi ambao wakati mwingine huonekana kama wamekurupuka.
Mhandisi mmoja ambaye amewahi kufungiwa leseni na Magufuli aliiambia Mwananchi kuwa kosa moja kubwa alilofanya ni kumwandikia Dk Magufuli taarifa ndefu, lakini iliyojaa mambo yasiyo sahihi.
Anasema kuwa aya hiyo ilikuwa ukurasa wa 20, lakini ndani ya muda mfupi Magufuli aliibaini na kibarua chake kiliota nyasi.
Hali ni kama hiyo kwa Lowassa, ambaye akiwa Waziri Mkuu aliwahi kumtimua mkandarasi wa Wilaya Temeke kwa kushindwa kukagua ujenzi wa maghorofa ikiwemo la Chang’ombe Village lililoporomoka na kusababisha maafa ya mtu mmoja na wengine kadhaa kujeruhiwa mwaka 2006.
Uchapakazi
Mbali na umakini, wawili hao wamedhihirisha kuwa ni wachapakazi hodari katika wizara na taasisi walizopitia kiasi cha kujijengea jina kubwa kwa wananchi.
Utendaji wa Dk Magufuli hauna shaka na ameshaeleza bayana kuwa hapendi wazembe na wasiowajibika sanjari, kama Lowassa ambaye hata siku ya kwanza alipoingia ofisini mwaka 2005 aliwataka wafanyakazi wa Ofisi ya Waziri Mkuu kuacha kufanya kazi kwa mazoea.
Wakati Dk Magufuli alipohamishiwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, wengi walidhani kuwa amemaliza kisiasa, lakini mbunge huyo wa Chato alifanya kazi kubwa ya kutambua fursa za kiuchumi zilizoko hasa kwenye uvuvi na akafanikiwa kuonyesha ni kiasi gani Serikali ilikuwa ikipoteza fedha.
Wakati huo, Tanzania iliingia makubaliano na Afrika Kusini na nchi nyingine za ukanda huu kufanya doria kwa pamoja kwenye pwani ya Afrika Mashariki na juhudi hizo zilifanikiwa kunasa meli ya Tawaliq 1 iliyokuwa na samaki wenye thamani ya Sh20 bilioni.
Uchapakazi wake umedhihirika hasa kwenye ujenzi wa barabara, akiwa amefanikiwa kuunganisha takriban mikoa yote ya Tanzania katikja kipindi alichokaa Wizara ya Ujenzi.
Lowassa anaonekana zaidi katika kusimamia utekelezaji wa mradi wa maji ya Ziwa Victoria katika shughuli za maendeleo baada ya mpambano mkali dhidi ya Misri, ambayo ilikuwa na ukiritimba wa maji hayo kabla ya nchi tano kuungana na kusaini makubaliano ya matumizi ya maji hayo.
Lowassa pia anajinadi na mafanikio ya ujenzi wa shule za kata, ambazo kwa kiasi kikubwa zimefanikisha watoto wengi kupata elimu kwa gharama nafuu, ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma ambao aliufanya kwa kukutanisha mifuko ya hifadhi ya jamii na kuiamuru ichangia gharama za ujenzi.
Jambo lingine walilonalo Dk Magufuli na Lowassa ni misimamo. Dk Magufuli ni kiongozi mwenye misimamo isiyotia shaka na siku zote husimamia anachokiamini, sanjari na Lowassa, ni mwenye misimo yake na itakumbukwa alipokuwa Waziri wa Maji na baadaye Waziri Mkuu alionyesha misimamo.
Dk Magufuli alitofautiana hata na Waziri Mkuu Mizengo Pinda wakati aliposimamia uendeshaji wa kivuko cha Kigamboni, na suala la kiwango cha mizigo inayobebwa na malori.
Moja ya kauli zilizonukuliwa sana ni ile ya “asiyekuwa na nauli ya kulipia kivuko, apige mbizi”, ambayo ilitafsiriwa kuwa ya kutojali wananchi, lakini faida zake ndio zinamfanya aonekane kuwa msimamo wake ulilenga kunufaisha wananchi.
Hali kadhalika Lowassa anajulikana kwa kusimamia uamuzi kama wa kubomoa maghorofa yaliyojengwa kinyume na sheria Masaki jijini Dar es Salaam. Msimamo wake pia kwenye suala la mkataba wa City Water iliyokuwa ikihusika na ugavi wa maji jijini Dar es Salaam ndio uliosababisha uvunjwe.
Ufuatiliaji
Lowassa na Dk Magufuli pia wanajulikana kwa kuwa wafuatiliaji wazuri kwa watu walio chini yao au wanaofanya kazi chini ya mamlaka zao. Dk Magufuli, ambaye anajulikana kwa kukariri tarehe, kiwango cha miradi, urefu wa barabara na kiwango cha fedha zilizotengwa kwenye miradi, hutumia talanta hiyo kufuatilia miradi mbalimbali na hasa muda wa kumalizika, hali inayomfanya kila mara atishia kuvunja mikataba na wakandarasi au kuivunja kabisa.
Hilo pia limekuwa likifanywa na Lowassa, ambaye akiwa Waziri Mkuu alikuwa akihakikisha wakuu wa wilaya na mikoa wako sehemu zao za kazi na yeyote ambaye alitaka kutoka alitakiwa awe na kibali, kwa mujibu wa baadhi ya watu waliofanya kazi naye.
Udhaifu
Mbali na sifa hizo nzuri, wanasiasa hao wanashabihiana katika udhaifu, hasa uamuzi wa papo kwa papo ambao pia husababishwa na kiu yao ya kutaka kuona kazi inafanyika.
Wote wawili hufanya uamuzi wa papo kwa pamo ambao wakati mwingine huwa na athari za kisheria. Uamuzi kama huo huwa na kadhia kwa wafanyakazi na makandarasi wanaopewa zabuni mbalimbali na Serikali.
Hawaachi mfumo wa utendaji
Udhaifu mwingine wa wawili hao ni hali ya kujituma wao bila ya kutengeneza mfumo ambao unaendeleza ufanisi na badala yake wanapoondoka, hali hubakia kama ilivyokuwa awali.
Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Dk Magufuli kwenye wizara alizopitia kama ya uvuvi na hali kadhalika kwa Lowassa.
Pia wanatofautiana
Tofauti kubwa kati ya Dk Magufuli na Lowassa ni mgombea huyo wa CCM kutokulia ndani ya chama na badala yake amekuwa kwenye nafasi za utendaji zaidi na uwaziri. Dk Magufuli amekuwa mwanachama wa CCM na mbunge, nafasi ambayo humuingiza kwenye kikao cha Halmashauri Kuu pekee.
Lakini Lowassa ameshika nafasi mbalimbali kwenye chama kuanzia katibu wa mkoa hadi mjumbe wa vyombo vya juu vya CCM.
Kauli za wachambuzi
Baadhi ya wachambuzi na wasomi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, (Udsm) wamesema kwa nyakati tofauti kwamba wagombea hao wanaonekana kuwa na tofauti kubwa zinazoweza kufanikisha ushindi katika uchaguzi huo.
Mohammed Bakari, ambaye ni mhadhiri wa Idara ya Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema wagombea hao wanafanana katika kigezo cha utendaji kazi lakini kiuamuzi na uzoefu wanatofautiana.
“Dk Magufuli ana uamuzi wa kukurupuka ila Lowassa ametulia,” alisema. “Kuhusu uzoefu pia Lowassa ni mzoefu kiuongozi kuliko Dk Magufuli.”
Alisema suala la uadilifu siyo rahisi kupata kiongozi mwadilifu kwa wagombea hao na bila kuzitaja kashfa hizo, alisema wote wana kashfa. Aliongeza kwamba, Lowassa ni mgombea anayeweza kuleta mabadiliko kwa Taifa hili, lakini Dk Maghufuli hawezi kutokana na mfumo uliopo kwenye chama chake.
Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa wa Udsm, Dk Alexander Makulilo pia anaona sifa hizo zinazolingana.
Alisema wagombea hao wanafanana kwa utendaji mzuri wa kazi na uamuzi wa papo kwa hapo. Aidha, alisema Magufuli ni kiongozi anayeweza kuleta siasa mpya zisizokuwa na makundi.
Alisema Lowassa ni mgombea anayekabiliwa na changamoto ya Richmond iliyomfanya ajiuzulu uwaziri mkuu, wakati Dk Magufuli hana kashfa kubwa iliyowahi kujadiliwa bungeni.
“Lakini hali hiyo haiwezi kuwa changamoto kubwa kutokana na mwamko mkubwa wa kundi linalohitaji mabadiliko ya uongozi serikalini. Uchaguzi huu ninaufananisha na Zambia wakati chama cha UNIP kilipoondolewa madarakani kwa kuwa makundi ya kijamii yalikuwa yameamua kiondoke madarakani,” alisema.
Kuhusu mfumo kuibeba CCM, Dk Makulilo alisema ni sehemu ya changamoto kubwa inayoweza kufanikisha ndoto za Lowassa kuingia madarakani.