Saturday, August 8

Wamiminika Ofisi za Chadema ‘kumlaki’ Dk Slaa

Katibu Mkuu, Dk Willbrod Slaa 

Dar es Salaam. Baadhi ya wanachama na mashabiki wa Chadema jana walifika katika ofisi za Makao Makuu ya chama hicho, Kinondoni Dar es Salaam kumsubiri Katibu Mkuu, Dk Willbrod Slaa baada ya kuenea uvumi kuwa angeingia ofisini.

Hata hivyo, wanachama hao waliokuwa na shauku ya kumwona kiongozi huyo, hawakufanikiwa baada ya kuambiwa kuwa Dk Slaa asingefika katika ofisi hizo kinyume na taarifa zilizokuwa zimezagaa kuhusu kurejea kwake.
Kwa muda mrefu Dk Slaa hakuonekana kwenye matukio muhimu ya Chadema na yale ya Ukawa, kama wakati wa kumkaribisha Edward Lowassa ndani ya chama hicho, wakati Lowassa alipochukua kadi na alipochukua fomu ya kuwania urais.
Kadhalika kiongozi huyo hakuonekana katika Baraza Kuu la Chadema, mkutano wa Kamati Kuu na Mkutano Mkuu uliompitisha kwa kauli moja kuwa Lowassa aipeperushe bendera ya urais chini ya mwamvuli wa Ukawa.
Akihutubia Baraza Kuu la chama hicho wiki iliyopita, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema kuwa chama kiliridhia Dk Slaa apumzike wakati mchakato wa kuelekea Uchaguzi Mkuu ukiendelea baada ya Katibu Mkuu huyo kutofautiana katika uamuzi wa kumkaribisha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.
Baraza Kuu lilipiga kura ya wazi na kushauri kuwa endapo atafikiria kubadili uamuzi wake, anaweza kuendelea na harakati za chama hicho kuelekea Ikulu chini ya muungano wa Ukawa.
Mwandishi wetu aliyefika katika ofisi za Chadema zilizopo katika Mtaa wa Ufipa, Wilaya ya Kinondoni, alishuhudia idadi kubwa ya wanachama wakiwa wamekusanyika katika vikundi wakijadili masuala mbalimbali huku wakimsubiri Dk Slaa.
“Nimesikia taarifa kuwa kuna watu hapa wanamsubiri Dk Slaa nikaja kushuhudia, watu wanaongea mambo mengi kama vile Ukawa imevunjika wakati kila kitu kinakwenda sawa hapa,” alisema Ali Mundu mmoja wa wananchama hao.
Alisema kutokana na taarifa nyingi zilizosambaa mitaani kuhusu kuwepo kwa sintofahamu miongoni mwa viongozi wa Ukawa, kila mtu amekuwa akisema kitu anachojua hivyo ili kupata taarifa sahihi ni vyema wana-Ukawa wanafika kujionea kinachoendelea.

No comments:

Post a Comment