Ahadi hiyo imetolewa na Makamu wa Rais wa shirika hilo, Hiroshi Kato alipokutana kwa mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango, jijini Dar es Salaam.
Kato katika taarifa iliyotolewa na wizara leo Jumatatu Novemba 27,2017 amesema mradi mwingine wanaotaka kuutekeleza katika Mji wa Dodoma ni udhibiti wa taka ngumu.
Amesema wanachosubiri ni Serikali kuainisha maeneo ya vipaumbele vilivyoko katika mpango mji wa Dodoma.
Kato amesema shirika hilo litaendelea kusaidia eneo la kilimo na hasa cha mpunga ili kuongeza thamani ya zao hilo na kuwakomboa wakulima.
Waziri Mpango amelishukuru shirika hilo kwa kuonyesha nia ya kusaidia ujenzi wa mji wa Dodoma.
Amesema mradi huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kuupanga mji wa Dodoma mapema ili kuondoa changamoto za msongamano wa huduma za jamii kwenye eneo moja kama ilivyo jijini Dar es Salaam.
“Pamoja na umuhimu wa miundombinu ya maji, umeme, usafiri wa mjini, lakini pia tunataka tujenge mapema njia za juu ili kudhibiti msongamano wa magari,” amesema Dk Mpango.
Amesema mradi mwingine wa kipaumbele katika mji huo ni ujenzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa katika eneo la Msalato, takriban kilomita 20 kutoka katikati ya mji huo ili kurahisisha usafiri kwa njia ya anga.