Monday, November 27

Baiskeli zinavyosaidia wananchi kukabiliana na uhaba wa maji Mwanga


Kutokana na uhaba wa upati-kanaji wa majisafi na salama katika Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, wananchi wanalazimika kutumia usafiri wa baiskeli kwenda maeneo ya mbali kutafuta huduma hiyo. Asilimia kubwa ya wananchi wa vijiji vya Mwanga hata katika baadhi ya maeneo ya mjini hutu-mia baiskeli kama usafiri wa kubeba maji kutoka eneo moja kwenda lingine.
Katika maeneo yaliyoendeleana yenye maji ya kutosha ni nad-ra kuona mtu amebeba maji kwa baiskeli, lakini wilayani hapa ni jambo la kawaida kwa sasa.Jambo hili huchangiwa na uhaba wa maji katika baadhi ya maeneo, hivyo baiskeli kubakia kuwa ndio usafiri unaotegemewa kuwasaidia wananchi hasa wan-awake wilayani humo.
Kiwango cha maendeleo ya jamii yoyote kinategemea kuwe-po kwa maji ya kutosha yaliyo safi na salama. Maji ni mojawapo ya huduma muhimu katika kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Mwaka 2025. Licha ya malengo hayo kusema kila mwananchi anapaswa kutembea umbali wa mita 400 tu ndipo apate majisafi na salama, kwa Wilaya ya Mwanga jambo hilo bado ni kutendawili. Inaendelea uk 24
Ukosefu wa maji katika wilaya hii umekuwa ni tatizo sugu na linalowapa mateso wakazi wa wilaya hiyo.
Tatizo hili limekuwa likiwatesa zaidi akina mama na watoto ambao huwa wakiamka usiku wa manane kwenda kusaka maji kwenye maeneo yanakopatikana.
Licha ya kuwepo kwa miradi mbalimbali ya Serikali na ile iliyojengwa na taasisi mbalimbali za kiraia, bado tatizo hili limekuwa ni kitendawili kisichokuwa na majibu.
Namna baiskeli zinavyotumika
Sikushangaa kuona baiskeli zikitumika kubebea maji, bali nilishangaa kuwa katika nchi inayoelekea kuwa ya viwanda bado wapo watu wengi wanaohangaika kubeba maji kwa kutumia baiskeli kutokana na uhaba mkubwa wa huduma hiyo.
Juma Amini mkazi wa Kata ya Jipe, anasema kuwa usafiri wa baiskeli umekuwa msaada mkubwa kwao kupata maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.
Amini anasema takribani kila nyumba ina baiskeli ya kubebea maji. Anatahadhalisha kuwa tatizo hilo si la kupuuzwa na Serikali kwakuwa linahatarisha maisha ya watoto na wanawake ambao mara nyingi wao ndio wanategemewa kusaka maji.
Watoto wa kike nao wanatumia usafiri huo kwa kubeba madumu matatu hadi manne ya maji hali ambayo inaweza kuhatarisha usalama wa afya zao.
Mkazi wa Kijiji cha Kivisini Kata ya Kivisini, Amina Ally anasema wanawake na watoto wanachangamoto nyingine ya kusubiri maji kwenye foleni kwa muda mrefu.
Anasema baada ya kuyapata huduma hiyo hutumia baiskeli au mkokoteni ili kubeba madumu mengi ya maji kwa wakati mmoja.
Amini anaeleza kuwa matumizi ya baiskeli yanawasaidia wananchi kuokoa muda na kupata maji mengi kwa wakati mmoja.
Anasema wanatoka nyumbani saa 11 alfajiri kwaajili ya kuwahi foleni ya maji.
“Kama unavyoona foleni ya maji haya ni ya mvua yanatiririka kutoka mlimani, wakati wakiangazi tunachota maji kijiji kingine hivyo mtu hawezi kuchota ndoo moja akarudi inambidi aje na baiskeli au mkokoteni,”anasema Amini.
Haruna Msofe, anasema bila kutumia usafiri wa baiskeli wanaume wengi hawawezi kubeba maji kichwani hasa wanapoyafuata maji maeneo ya mbali.
Msofe anasema, baiskeli na mikokoteni hutumika zaidi kipindi cha kiangazi wakati ambao uhaba wa maji huwa mkubwa zaidi.
Anaongeza kuwa wakati wa msimu wa kiangazi ndio matumizi ya baiskeli huongezeka mara dufu kwakuwa maji hupatikana mbali zaidi katika maeneo ambayo kuna kisima.
Kwa upande wake Hawa Amani anasema licha ya kuyafikia maji hayo, wanachota ndoo sita kila mtu kwa siku kutokana na uchache wa maji.
Hata hivyo, matumizi haya yanatumiwa na wahudumu wa Serikali kwakuwa alionekana mhudumu wa afya katika zahanati ya Kivisini akiwa katika foleni ya kuchota maji.
Mhudumu huyo ambaye alikataa kutaja jina lake, alipoulizwa alisema kuwa wanalazimika kutumia mikokoteni kubebea maji ya kufanyia usafi pamoja na shughuli nyingine katika zahanati hiyo.
“Nafanya kazi Zahanati ya Kivisini, nimelazimika kuja hapa kuchota maji kwaajili ya zahanati, natumia mkokoteni kila siku kuja kubebea maji ili yatoshe,” anasema mhudumu huyo.
Katika Kijiji cha Jipe, Kata ya Jipe ambako wanatumia maji ya ziwa, wakihitaji maji kwaajili ya kunywa wanayapata mbali kwa kuyanunua ni lazima waende na usafiri huo.
Wakati nikielekea Kijiji cha Jipe wananchi wamebeba ndoo za maji kwa kutumia baiskeli, mikokoteni na wengine vichwani.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Jipe, Abdalah Hatibu anaeleza shida wanayoipata wananchi wa kijiji hicho ikiwa ni pamoja na hatari ya kukumbwa na magonjwa kutokana na matumizi ya maji ya Ziwa Jipe.
Hatibu anasema kutokana na ukosefu wa majisafi na salama katika eneo hilo, usafiri huo hutumika kufuata maji walau ya kupooza kiu tu.
Anasema: “Katika ziwa hilo, mifugo wanakunywa maji hapo, wavuvi nao wanafanya kila aina ya uchafu huko ziwani halafu hapo hapo tunachota maji tunakunywa na kupikia.”
Hatibu anasema kuwa wakitaka kupata maji mazuri ya kunywa wanalazimika kwenda kununua katika kijiji kingine kwa Sh500 kwa ndoo moja.
“Kwa mtu ambaye ana uwezo mdogo ndiye anaweza kwenda na baiskeli kununua maji hayo walau ya kunywa,” anasema Hatibu.
Watumia Punda
Katika Kijiji cha Pangaro, Kiverenge na mgagao Kata ya Mgagao wanawake wa kabila la Wamasai nao wanakabiliana na adha hii ya maji hivyo hutumia usafiri wa punda.
Pamoja na kwamba wao hutumia maji yaliyo kwenye malambo, lakini lazima usafiri wa punda uwepo.
Wanawake na watoto ndio wahusika wakuu na wanateseka zaidi wanalazimika kutumia maji ya lambo kwa matumizi ya nyumbani.
Agnes Moleli, anasema licha ya maji hayo kuwa mabaya lakini yamekuwa mkombozi kwao na usafiri wa punda unawasaidia kwakuwa bwawa hilo lipo mbali kidogo.
“Hatuna njia nyingine ya kupata majisafi na salama hivyo lazima tutumie haya, tunakuja hapa na punda halafu tunaingia nao kwenye bwawa tunajaza madumu ya maji kisha tunaondoka,” anasema Mollel.
Anasema kuwa kipo kijiji cha jirani ambacho kuna maji ya kisima lakini hata kwa usafiri huo ni mbali zaidi.
Akizungumza kijijini hapo, diwani wa Kata ya Mgagao, Longoviro Kipuyo anasema kuna kisima kimoja ambacho kipo Pangaro lakini kipo mbali na Kijiji cha Kiverenge.
Anaiomba Serikali kuwasaidia kutafuta mashine na mabomba kwaajili ya kusambaza maji katika vijiji hivyo, kwakuwa kipo kisima ambacho kimechimbwa, lakini hakitoi maji kutokanana ukosefu wa vifaa hivyo.
Kauli ya Mkuu wa Wilaya
Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Aron Mbogho anasema kuna mradi mkubwa wa maji unaoendelea kwa sasa, unaofadhiliwa na Serikali kwa asilimia 50.18 na asilimia 49.82 ni kutoka Benki ya Kiarabu kwa Maendeleo ya Afrika (Badea) na Shirika la Opec Fund For International Development (OFID).
Anasema, mradi huo utakapokamilika unatarajia kuwahudumia wananchi zaidi ya laki nne wa vijijini 24 vya tambarare wilaya za Same na Mwanga na vitano katika Wilaya ya Korogwe.

No comments:

Post a Comment