Monday, November 27

Ulinzi waimarishwa Nairobi Kenyatta akitarajiwa kuapishwa Jumanne

Wafuasi wa upinzani wamekuwa wakikabiliana na polisi mara kwa mara tangu AgostiHaki miliki ya pichaAFP/GETTY
Image captionWafuasi wa upinzani wamekuwa wakikabiliana na polisi mara kwa mara tangu Agosti
Ulinzi umeimarishwa katika jiji kuu la Kenya, Nairobi pamoja na miji mingine mikuu Rais Uhuru Kenyatta akitarajiwa kuapishwa kuongoza nchi hiyo kwa muhula mwingine hapo kesho.
Muungano wa upinzani umetangaza kwamba hautambui sherehe hiyo na haumtambui Bw Kenyatta kama rais aliyechaguliwa na wananchi.
Kiongozi mkuu wa upinzani Raila Odinga amepanga kuandaa mkutano mkubwa wa kuwakumbuka watu waliofariki wakati wa makabiliano kati ya wafuasi wa upinzani na polisi.
Bw Odinga na muungano wake wa National Super Alliance (Nasa) wamesisitiza kwamba mkutano huo utafanyika katika uwanja wa Jacarada, Nairobi, takriban kilomita kumi hivi kutoka uwanja wa Kasarani ambapo sherehe ya kuapishwa kwa Bw Kenyatta itakuwa inaendelea.
Polisi hata hivyo wamesisitiza kwamba hakutakuwa na mkutano mwingine Nairobi ila sherehe ya kumuapisha Bw Kenyatta.
Bw Odinga alisusia uchaguzi wa marudio uliofanyika 26 Oktoba baada ya kufutiliwa mbali kwa uchaguzi wa kwanza uliokuwa umefanyika tarehe 8 Agosti.
Mahakama ya Juu ilifutilia mbali uchaguzi huo wa kwanza kutokana na kesi iliyokuwa imewasilishwa na Bw Odinga.
Bw Kenyatta alipata asilimia 98 ya kura katika uchaguzi wa marudio, ushindi ambao uliidhinishwa na Mahakama ya Juu iliyofutilia mbali kesi mbili zilizokuwa zimewasilishwa na wanaharakati wawili na mbunge wa zamani kupinga uchaguzi huo.
Serikali imesema viongozi 20 wa mataifa mbalimbali wanatarajiwa kuhudhuria sherehe hiyo ya kuapishwa kwa Bw Kenyatta, akiwemo kiongozi wan chi jirani ya Tanzania Dkt John Magufuli.
Mwezi uliopita, ripoti ya Tume ya Taifa ya Haki za Binadamu ilisema watu 37 waliuawa tangu kutokea kwa uchaguzi wa tarehe 8 Agosti.
Tume hiyo iliwatuhumu polisi kwa kutumia nguvu kupita kiasi wakikabiliana na wafuasi wa upinzani.
Idara za usalama nchini Kenya zimekanusha tuhuma hizo.

No comments:

Post a Comment