Friday, November 10

Diamond ambwaga Hamisa Mobeto


Dar es salaam, Mwanamitindo Hamisa Mobeto amekwaa kisiki mbele ya Diamond Platnumz baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu upande wa Watoto kutupilia mbali kesi aliyofunguliwa mwanamuziki huyo juu ya matunzo ya mtoto Prince Abdul.
Uamuzi huo umetolewa leo Ijumaa Novemba 10 ,2017 na Hakimu Devotha Kisoka wa Mahakama hiyo baada ya kusikiliza hoja za pande hizo mbili husika.
Diamond aliwasilisha pingamizi dhidi ya kesi hiyo iliyofunguliwa na Mobeto akidai kuwa kesi hiyo imefunguliwa kwa kutumia kifungu ambacho si sahihi.  Hoja ambayo ilipingwa na Mobeto.
Mobeto alifungua kesi hiyo mahakamani hapo, pamoja na mambo mengine anaiomba matunzo ya mtoto waliozaa na msanii Diamond.
Mobeto  anaiomba mahakama imwamuru Diamond kutoa matunzo ya mtoto ya kila mwezi na alifungua kesi hiyo kupitia mawakili wake Abdullah Lyana na Walter Godluck kutoka kampuni ya uwakili ya Century Attorneys.
Kupitia hati hiyo ya madai, Mobeto  anaomba Diamond amuombe msamaha kwa kumsababishia madhara yaliyoishtua familia yake.
Diamond aliwasilisha hati ya majibu hayo kinzani akipinga maombi hayo ya Mobeto  akidai  gharama anazodai kulipwa kwa mwezi ya Sh 5 milioni  kwa ajili ya matunzo ya mtoto ni kubwa hawezi kuzimudu.

Nape asema miradi ya Serikali inaongeza deni la taifa


Dodoma. Mijadala imetawala bungeni  leo huku Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye akisema miradi mikubwa itakayotekelezwa na Serikali, itafanya deni la taifa kufikia Trilioni 47.
Mbali na Nape ambaye mchango wake umeonekana  kuwa mwiba kwa Serikali, lakini wabunge kutoka Zanzibar wamechachamaa kutokana na mpango wa maendeleo wa taifa kutoihusisha Zanzibar.
Katika mijadala hiyo, Waziri wa zamani wa Fedha, Saada Mkuya,  ameenda mbali na kumtuhumu waziri wa sasa wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango kutofanya kikao cha kazi Zanzibar tangu ateuliwe.
Hayo yalijitokeza wakati wabunge wakichangia mapendekezo ya Mpango wa maendeleo wa Taifa na mwongozo wa kuandaa bajeti kwa mwaka wa fedha 2018/2019 uliowasilisha bungeni na, Dk.Mpango.
Akichangia taarifa hiyo kwa hisia, Nape amesema  binafsi hapingi kutekelezwa kwa miradi mikubwa ila anapingana na Serikali jinsi ya kuifadhili na kuiendesha kwa kutumia fedha za Serikali.
“Niliposoma nilishtuka kidogo kuona Serikali inapendekeza kuwekeza pesa za Serikali kwenye miradi ambayo inaweza kuendeshwa kibiashara. Nilitegemea miradi hii tungeruhusu sekta binafsi,” amesema.
Ametaja baadhi ya miradi ya ambayo amesema ingeweza kutekelezwa na sekta binafsi kuwa ni ujenzi wa reli ya kisasa ya kati, mradi wa umeme Rufiji, mradi wa bandari na uboreshaji shirika la ndege.
“Kama mpango huu utatekelezwa kama ulivyo, miradi hii inakwenda kuua uchumi wa nchi yetu. Miradi hii mikubwa inaweza kujiendesha kibiashara na ikajilipa yenyewe,” amesisitiza Nape.
Kwa mujibu wa Nape, miradi hiyo ni mikubwa na itagharimu fedha nyingi ambazo zitailazimisha Serikali kukopa fedha nyingi, hali ambayo itaathiri deni la taifa ambalo kwa sasa Dola bilioni 26.
“Serikali ikienda kukopa  na kwa sababu miradi hii inachukua muda mrefu maana yake tutaanza kulipa deni kabla ya miradi hiyo haijaanza kurudisha faida kwa taifa,” amesema katika mchango wake.
“Kuna madhara makubwa kwa deni la taifa. Ndio hapa ninapohoji uzalendo wa wachumi wetu katika kuishauri Serikali na Rais Magufuli katika kuchukua pesa za Serikali na kuwekeza katika miradi hii”.
“Kwa mujibu wa takwimu ripoti uliyotupa hapa, deni letu la taifa limefikia Dola 26 bilioni ambayo ni sawa na asilimia 32 ya ustahimilivu wa deni la taifa. Ukomo ni asilimia 56”.
“Sasa kama Dola bilioni 26 zimetupeleka kwenye asilimia 32 unahitaji Dola bilioni 45 kufikia ukomo wa asilimia 56 ambao ni mwisho wa kukopesheka. Tuchukue mifano ya miradi mitatu tu” amesema.
“Ujenzi wa reli ya Kati ambayo kwa tathmini yake unaweza kugharimu Dola bilioni 15. Stiegler’s  Gorge utagharimu Dola bilioni 5 na uboreshaji wa shirika la ndege karibia Dola bilioni 1”
“Kwa hiyo unazungumzia Dola bilioni 21. Ukijumlisha na deni la taifa la bilioni 26 unazungumzia Dola bilioni 47. Kwa vyovyote vile hii ime bust (imepasuka)”alisema Nape na kuongeza kusema;-
“Kama inakwenda ku bust maana yake tunakwenda kutokopesheka. Kwanini tunataka kung’ang’aniza kuchukua pesa ya Serikali”. Hebu tufikirie upya. Dk Mpango rudini mkafikiri upya”
Nape alisema kuanzia awamu ya pili chini ya Rais Alli Hassan Mwinyi hadi awamu ya nne, Serikali ilitengeneza mazingira mazuri ya kuishirikisha sekta binafsi katika miradi mbalimbali ya kiuchumi.
“Wakati wa awamu ya nne  Rais Magufuli alikuwa Waziri wa Ujenzi. Wakati wake waliruhusu wakandarasi kutoka sekta binafsi. Wakachukua mikopo benki wakaanzisha makampuni”
“Leo dhamana walizozitumia kukopa fedha  zinauzwa kwa sababu ya madeni wanayoidai Serikali lakini Serikali nayo imeanza mkondo wa miradi yake ya ujenzi kutekelezwa na Serikali yenyewe”
“Kwa hiyo hawa tuliowatengeneza kwa miaka yote tumewakosesha pesa. Huu mpango wako mzuri lakini rudini kwenye mawazo ya kutumia sekta binafsi. Tukienda hivi tunaenda kuua uchumi,”alisema.

Waziri Mpango adaiwa kuitenga Zanzibar


Dar es Salaam. Waziri wa Fedha wa utawala uliopita wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete, Saada Mkuya amemshukia Waziri wa Fedha, Dk Philip Mpango kwa kuandaa mpango wa taifa wa maendeleo pasina kuihusisha Zanzibar.
Mkuya ambaye ni mbunge wa Welezo visiwani Zanzibar amesema Dk Mpango amekuwa na kawaida ya kutokujibu hoja ambazo zinatolewa na wabunge wa kutoka Zanzibar jambo ambalo limemsikitisha.
Akichangia leo Novemba 10 bungeni mjini Dodoma Mpango wa Maendeleo ya Taifa, Mkuya ambaye katika mchango wake alisikitishwa na jinsi Waziri Mpango anavyoitenga Zanzibar licha ya kuwa ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“…Nadhani taifa hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linaundwa na pande mbili sasa Mheshimiwa Mwenyekiti  (Azzan  Zungu) cha kusikitisha na fedheha kabisa ni kuona hakuna hata eneo moja lililopangiwa mpango angalau tu likaelekezwa katika upande mwingine wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema Mkuya
“Hili niliseme wazi mheshimiwa mwenyekiti kupitia kwako, mheshimiwa Waziri wa Fedha (Dk Mpango) wakati tunajadili bajeti Juni mwaka huu baadhi ya wenzangu tunaotoka upande wa pili wa Muungano tulichangia maeneo fulani fulani,” ameongeza
Mkuya akichangia kwa sauti ya msisitizo amesema ‘’Lakini kwa masikitiko makubwa mheshimiwa mwenyekiti hakuna eneo hata moja lililoguswa likajibiwa hoja angalau kule upande wa pili wakasikia na mimi nilichukua hatua kwenda kumuuliza mheshimiwa waziri wa fedha mbona angalau hata hoja mbili ili nao waone ni sehemu ya muungano.”
“Mheshimiwa waziri  aliniambia muda ni mchache na majibu yalikuwa mengi, nilijisikia vibaya kwa sababu kama una ‘responsibility’ ya pande mbili za Jamhuri maanake angalau ungechukua hata hoja mbili ukazijibu sasa aliniambia kabisa muda mchache hoja zilikuwa nyingi sasa nitakupa document…nimesikitika,” amesema
Mkuya amesema sasa tunachangia hapa na nimeonda tendency ya wabunge ambao wanatoka upande mwingine wanachangia, tuombeni Mungu angalau hoja mbili tatu zijibiwe muda uwepo.
 “Kuna masuala mengine hayahitaji lazima iwe ni wizara inayoshughulika na Muungano, kuna mambo mengine ishu zingine zinahitaji coordination za pande mbili hivi kweli kama hii ya utalii kunaweza kuwa na project bila kuihusisha Zanzibar haipo? 

UN yachagua majaji wanne kuingia ICC

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama limewachagua majaji wanne Alhamisi kuingia katika Mahakama ya Kimataifa, ni taasisi ya kisheria ya juu ya UN.
Katika kura ya peke yake, lakini iliyofanyika kwa pamoja, Mkutano na Baraza limewachagua tena Ronny Abraham wa Ufaransa na Abdulqawi Ahmed Yusuf wa Somalia.
Pia majaji wawili wapya, Antonio Augusto Cancado Trindade wa Brazil na Nawaf Salam wa Lebanon, pia wamechaguliwa.
Wote hao wamechaguliwa kutumikia mahakama hiyo kwa kipindi cha miaka tisa, kuanzia Februari mwakani.
Mahakama hiyo iliundwa mwaka 1945, chini ya mkataba wa UN, ambapo Mahakama ya ICC ndiyo taasisi ya kisheria ya juu ya UN.
Shughuli za mahakama hii kwa mujibu wa sheria za kimataifa, ni kusuluhisha migogoro inayowasilishwa na mataifa mbalimbali na kutoa ushauri wa kisheria juu ya masuala yanayoletwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa na taasisi maalum.

Shule ya Kihinga yafungwa kwa muda


Ngara .Uongozi wa  Shule ya Msingi  Kihinga umaamua kuifunga kwa muda shule hiyo kwa lengo la kuwajenga kisaikolojia wanafunzi wake baada ya wenzao kupoteza maisha kutokana na mlipuko wa bomu.
Akizungumza  Mwananchi leo Novemba 10 ,Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Aidan Makobero amesema   shule hiyo imefungwa kimasomo hadi Jumatatu ili wanafunzi waweze kupata malezi ya  kisaikolojia
Aidha amesema kwa shule jirani  ya Nyarukubala iliyo karibu na mpakani na  Burundi mahudhurio yamepungua kutoka wanafunzi 700  na kufikia 100  leo  Novemba 10
“Hata shule nyingine ya Nyarulama nayo wanafunzi wake wamepungua  baada ya tukio la shuleni kwangu na kusalia majumbani wakiogopa kwenda shule wakidai nao wanaweza kukumbwa na tukio  kama la shule jirani’’ amesema  Makobero
Pia majeruhi 33 kati ya 42 waliojeruhiwa kwa bomu wameruhusiwa na kurejea makwao baada ya afya zao kuimarika
Mganga wa hospitali ya misheni ya Rulenge Dk Mariagoleth Frederick amesema majeruhi hao  ni wanafunzi wa shule ya msingi Kihinga wilayani humo wameruhusiwa  na kubaki majeruhi 11
Amesema majeruhi waliosalia watano baada ya kufanyiwa uchunguzi bado kwenye sehemu za mifupa kunaonekana kuwepo vipande vya bomu na jitihada zinafanyika kuondoa vipande hivyo
Amesema wengine sita wanaendelea kuhudumiwa na mpaka sasa zimepatikana uniti 67 za damu kutoka kwa  wasamaria wema wakiwemo wanafunzi wa sekondari ya Mbuba Rulenge na vijana waendesha pikipiki
Aidha amesema shirika la kuhudumia wakimbizi UNHCR tawi la Ngara limetoa blanketi  60 kwa  zahanati jirani, MSD wilaya ya Muleba na ofisi ya mganga mkuu wa mkoa vilitolewa vifaa tiba na dawa.
" Changamoto kubwa ni jinsi ya kumudu watoto hao kwa kuwapatia chakula hivyo ombi ni wasamaria wema kusaidia chakula maana wazazi wao hawana uwezo kiuchumi " Amesema
Pia amesema mwalimu wa shule hiyo aliyejeruhiwa Policaripo Clemens naye ameruhusiwa na kwamba jopo la madaktari linashughulikia majeruhi hao watano ambao hali ikishindikana watapewa rufaa hadi Bugando.
Mwenyekiti  wa kijiji cha Kihinga Hasan Mohamed amesema  idara ya mali asili na kamati za ulinzi na usalama zingeondoa vivuko  mto Ruvubu unaounganisha Tanzania na Burundi kuzuia watu kuvuka  kutoka na kuingia  mataifa hayo

Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda awataka wafanyakazi waache mazoea


Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Profesa Elisante Ole Gabriel amekutana na wakuu wa taasisi zilizo chini ya wizara hiyo leo Novemba  9 na kuwataka kuacha kufanya kazi kwa mazoea ili kuleta matokeo yanayotarajiwa.
Profesa Gabriel amesema wizara hiyo imepewa majukumu makubwa ya kusimamia utekelezaji wa azma ya serikali ya kujenga uchumi wa viwanda, kwa hiyo ili kufikia malengo hayo lazima utendaji wa watumishi wa umma ubadilike.
Amesema hatavumilia uzembe wa aina yoyote ambao utakwamisha serikali kufikia malengo yanayotarajiwa. Amewataka kuwasimamia watendaji katika taasisi zao na wajipange kutoa huduma kwa saa 24.
Kiongozi huyo amewataka wakuu hao wa taasisi kuandaa mpango kazi ifikapo Novemba 30 ambao utawawezesha kufanya kazi kwa saa 24. Amesema waangalie pia kuwa na simu za bure kwa ajili ya kusikiliza wateja au wawekezaji.
"Tunataka discipline (nidhamu) kwenye taasisi mnazozisimamia. Utamaduni wa kufanya kazi kwa mazoea sasa ufikie mwisho, tuanze kufanya kwa saa 24 kwa wiki," amesema katibu mkuu huyo ambaye Oktoba 26 alihamishwa kutoka wizara ya habari.
"Hatuwezi kushindana kwenye soko huria la Afrika Mashariki kama tutaendelea kufanya kazi kwa mazoea. Nitafanya kazi chini ya falsafa ya 'fast' kwa maana ya kufanya kazi kwa haraka, ukweli na kimkakati," amesema.
Amesisitiza kwamba mazingira ya Tanzania ya kisiasa, kijamii, kiuchumi na kiteknolojia yako vizuri, hivyo hakuna sababu ya kushindwa kufikia malengo yao kwa wakati.
Baadhi ya taasisi zilizo chini ya wizara hiyo na zilizowakilishwa katika mkutano huo ni pamoja na TBS, TIC, Brela, TanTrade, FTC, TIRDO, Cosota na chuo cha CBE.

Mbunge asikitika wafanyabiashara kunyanyaswa bandarini


Mbunge wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BWL), Jaku Hashim Ayoub amesema  mtu anayekutwa na bidhaa za Zanzibar katika bandari ya Dar es Salaam ananyanyaswa kupindukia.
“Leo mali za Zanzibar ukiingia nayo utadhani umeingiza unga (dawa za kulevya). Wazanzibar mnatuonea sana”alisema na kuongeza kusema;-
“Leo Mzanzibar anachukua gauni zake tatu anakuja nazo bandarini (Dar es Salaam) anaambiwa kaa chini. TV moja tu. Huu muungano wa upande mmoja tu? Amehoji.

Mwakilishi huyo wa Paje, amesema ukiacha zao la Karafuu biashara  ndio nguzo muhimu ya uchumi wa Zanzibar ila kikwazo ni kuwapo kwa tozo mbalimbali kwa wafanyabiashara ambao wanaingiza na kutoa bidhaa mbalimbali kuptia bandari ya Dar es Salaam.
“Suala hili sio la upande mmoja na nakuomba ufike visiwani ili ujionee hali halisi na kujua changamoto zinazowakabili ndugu zetu, ukifanya hivyo na kukusanya mapato stahiki utastahili pongezi kwani kuwaonea katika kila kitu kinachopita bandari ulipie ni uonevu,”amesema Jaku.
Amesema suala la mizigo kutoka nchi jirani ikiwemo Kenya, Rwanda, Burundi na Uganda kuingia nchini bila ya usumbufu wa kulipia kodi katika bandari ni jambo ambalo halikubaliki kwani kwa watu wa Zanzibar imekua tofautio kwa kulipia hata miche mitatu ya sabuni.
“Waziri kwa hili haliwezi kuwa haki kwani kuku ana uwezo wa kutaga yai moja ukimlazimisha kutaga matatu utamkosa na kuku huyo,”amesema Jaku.
Mbali na hilo mwakilishi huyo alisema hali ya biashara imekuwa mbaya kwa baadhi ya milango ya fremu kufungwa bula ya kuwa na biashara kutokana na kodi kubwa ya Serikali.

Uongozi wa Chadema kujikita kwenye kampeni

 

Viongozi wa juu wa Chadema , Freeman Mbowe na Edward Lowassa wataongoza kampeni za uchaguzi  mdogo wa  nafasi za udiwani kwenye kata 43.
Chama hicho kimeunda Kamati za Kitaifa 10, zitakazoongeza nguvu, hamasa na mikakati ya kampeni za uchaguzi wa marudio kwenye nafasi hizo  kuanzia kesho hadi siku ya uchaguzi.
Timu hizo ambazo zitafanya kazi kwa kushirikiana na kamati zingine za hamasa katika ngazi za kanda, mikoa, majimbo, kata na matawi katika maeneo yenye uchaguzi huo, zitaongozwa na Mwenyekiti wa Chama Taifa, Freeman Mbowe.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa chama hicho Tumaini Makene imeeleza kuwa Mbowe  ataanza kuzindua kampeni kesho katika Kata ya Saranga, jijini Dar es Salaam.
Makene ametaja watakaoongoza timu hizo zilizopangwa kwa makundi A hadi G, kuwa ni  Mwenyekiti wa Chama Taifa Freeman Mbowe, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama na Waziri Mkuu Mstaafu,  Edward Lowassa, Makamu Mwenyekiti Taifa (Bara), Profesa  Abdallah Safari, Makamu Mwenyekiti wa Chama Taifa (Zanzibar) Said Issa Mohamed, Katibu Mkuu wa Chama  Dk. Vincent Mashinji.
Amewataja wengine watakaoongoza timu hizo kuwa ni  Naibu Katibu Mkuu wa Chama (Bara),  John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu wa Chama (Zanzibar), Salum Mwalimu.
Amesema timu hizo zitasaidiwa kwa ukaribu na timu zingine tatu chini ya uratibu na mikakati ya mabaraza ya chama, ikiwamo  Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) na Baraza la Wazee wa Chadema.
Timu hizo zitazunguka katika maeneo yote ya uchaguzi wa kata hizo 43, lengo ni kuwafikia wananchi wote kuelekea uchaguzi huo.
“Chadema  tutaweza kuwafikia na kuzungumza na wananchi katika majimbo 37, halmashauri 36, mikoa 19 nchi nzima.
“Chama kimedhamiria kuweka ushindani mkubwa na kushinda kata hizo 43 ambazo chama kimeweka wagombea, tunaamini ushindi upo na ndiyo maana tunakutana na wananchi kuwahamasisha na kuwasikiliza wanataka nini ” amesema Makene.

Madaktari wanaogoma Uganda watoa masharti matatu

MulagoHaki miliki ya pichaAFP
Rais wa chama cha madaktari nchini Uganda amewaambia waandishi wa habari nchini humo kwamba wako tayari kumaliza mgomo wao endapo mashariti yao matatu yatatekelezwa na serikali.
Miongoni mwa masharti hayo ni kulipwa marupurupu mbalimbali.
Daktari Ekwaru Obuku amesema kwamba wao wako tayari kurudi kazini iwapo serikali itazingatia masuala yao muhimu ikiwemo kuondoa kitengo maalum cha ungalizi wa afya kutoka ofisi ya Rais.
"Tunasema kabla ya turudi kazi, dawa zipo? Kabla ya turudi kazi, mshahara je? Na kitengo hiki wanaita kitengo cha uangalizi wa afya, wanawakamata na kuwaaibisha madaktari?" amesema Dkt Obuku.
Licha ya wananchi kutopata huduma za afya kutokana na mgomo huo na wao wametowa hisia zao:
"Serikali inatumia fedha nyingi kuwalipa wabunge milioni 30 mtu mmoja, ikiwa madaktari wanaambiwa hakuna fedha ni jambo la kusikitisha," amesema mmoja wa wakazi.
"Kwa maoni yangu serikali inatakiwa kuwalipa vizuri madaktari na walimu ni watu muhimu katika taifa."
Raia mwingine Peter Kwizera Ronald alisema ni jambo la kusikitisha kwamba pesa za madaktari hazipatikani ilhali wabunge wanalipwa pesa nyingi.

Urusi yatishia kulipiza kisasi hatua ya Marekani

RT studioHaki miliki ya pichaSPUTNIK INTERNATIONAL
Image captionRT imetuhumiwa kueneza propaganda za Urusi
Urusi inajiandaa kulipiza kisasi dhidi ya hatua ya Marekani ya kuagiza shirika la utangazaji la RT kujiandikisha kama "ajenti wa kigeni".
Urusi inapanga kulipiza kisasi dhidi ya mashirika ya utangazaji ya Marekani.
Mmoja wa wabunge wenye ushawishi mkubwa mwenye uhusiano na ikulu ya rais wa Urusi amesema nchi hiyo itachukua "hatua pana" ambazo "huenda zikahusisha mitandao mingi ya kijamii".
RT imetajwa kama chombo cha habari cha propaganda huku tuhuma za Urusi kuingilia uchaguzi wa Marekani wa mwaka jana zikiendelea.
CNN, Sauti ya Amerika (VoA) na Radio Free Europe/Radio Liberty yametajwa kama mashirika ambayo huenda yakaandamwa na Urusi.
Seneta wa urusi anayehusika katika sera ya vyombo vya habari Alexei Pushkov amesema mashirika hayo ya habari ya Marekani "yanafaa kuwekewa masharti ikiwa ni pamoja na huduma zake za runinga."
Sergei Neverov, kiongozi wa chama cha United Russia - chenye uhusiano wa karibu na serikali ya Urusi - bungeni, amesema "sio tu kwamba tutaandika mapendekezo, bali pia tume itaandaa mikakati pana, ambayo huenda ikahusisha mitandao ya kijamii."
RT yalalamikia kukandamizwa kwa "uhuru wa habari"
Awali, RT kupitia taarifa walikuwa wamesema Wizara ya Haki ya Marekani ilikuwa imelipa shirika hilo hadi Jumatatu kujiandikisha kama ajenti wa kigeni la sivyo wakuu wa shirika hilo wakabiliwe na hatari ya kukamatwa na kwamba akaunti zake za benki huenda zikazuiliwa.
Maagizo hayo yametolewa chini ya Sheria ya Kuwasajili Maajenti wa Kigeni (FARA), iliyopitishwa 1938 kukabiliana na kuenea kwa itikadi za Kinazi nchini Marekani.

Rodrigo Duterte: Rais wa Ufilipino akiri kwamba aliwahi kumuua mtu akiwa kijana

Duterte akielekea VietnamHaki miliki ya pichaEPA
Rais wa Ufilipino Rodrigo Duterte amekiri kwamba alimuua mtu kwa kumchoma kisu akiwa kijana.
"Nikiwa na miaka 16, nilimuua mtu," aliwaambia raia wa Ufilipino katika mji wa Da Nang nchini Vietnam ambako anahudhuria mkutano mkuu wa viongozi wa nchi za Asia na Pasifiki.
Amesema alimdunga kisu mtu huyo "kwa sababu ya kutazama tu".
Msemaji wake baadaye amesema tamko la kiongozi huyo lilikuwa "utani tu".
Bw Duterte amewahi kusema awali kwamba aliwaua washukiwa wa uhalifu alipokuwa meya wa mji wa Davao.
Kiongozi huyo wa Ufilipino anahudhuria mkutano huo wa Apec pamoja na viongozi wengine akiwemo Rais wa Marekani Donald Trump.
Bw Duterte anatarajiwa kushauriana moja kwa moja na Rais wa Marekani Donald Trump siku chache zijazo - mkutano wa kwanza kati ya wawili hao.
Rais huyo wa Ufilipino ameongoza kampeni yenye utata ya kukabiliana na wahalifu na walanguzi wa dawa za kulevya.
Wakosoaji wake wanasema kampeni hiyo imehusisha ukiukaji mkubwa wa haki za kibinadamu.
Bw Duterte amewahamasisha watu kuua washukiwa wanaohusika na dawa za kulevya bila kuwafikisha kwa polisi na alisema anaweza kufurahia sana iwapo angeweza kuwaua waraibu milioni tatu wa mihadarati nchini humo.
Akihutubia raia wa Ufilipino mjini Da Nang, amesema alimuua mtu wakati wa ukali wake miaka yake ya ujana na kwamba kulikuwa na vita vingi pamoja na "kuingia na kutoka jela" mara kwa mara.
Lakini msemaji wake Harry Roque, ameambia AFP kwamba Duterte alikuwa anatania tu na kwamba kiongozi huyo mara nyingi hutumia "lugha iliyoongezwa chumbi" akihutubia Wafilipino nje ya nchi yake.
Obama na DuterteHaki miliki ya pichaEPA
Image captionRais Obama na Rais wa Ufilipino Rodrigo Duterte waangaliana mjini Laos
Bw Duterte aliwahi kusema kwamba kuna uwezekano mkubwa kwamba alimuua mtu akiwa kijana.
Mwaka 2015, aliambia jarida la Esquire la Ufilipino kwamba wakati wa vita vikali ufukweni alipokuwa na miaka 17 "huenda nilimuua mtu kwa kumdunga kisu".
Haijabainika iwapo anazungumzia kisa hicho kimoja.
Amedai kwamba amewahi pia kuwarusha watu kutoka kwenye helikopta ikiwa angani.
Tangu achukue hatamu, polisi wanasema wamewaua watu karibu 4,000 katika operesheni ya kukabiliana na walanguzi wa mihadarati.
Watu wengine zaidi ya 2,000 wameuawa kwa makosa yanayohusiana na dawa za kulevya.
Trump atazuru Ufilipino akikaribu kumalizia ziara yake barani Asia.
Bw Duterte alizua utata alipomwelezea mtangulzii wa Trump, Barack Obama kama "mwana wa kahaba".
Bw Obama alifuta mkutano uliokuwa umepangwa kati ya wawili hao.

CUF yazuiwa kuwavua uanachama ‘wabunge’ wanane




Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imekizuia Chama cha Wananchi (CUF) kujadili na kuwafukuza uanachama waliokuwa wabunge wanane wa Viti Maalumu na madiwani wawili.
Hata hivyo, Mahakama imetoa uamuzi huo huku tayari chama hicho kikiwa kimeshawavua uanachama na baadaye kupoteza nafasi zao za ubunge na udiwani.
Uamuzi huo umetolewa leo Ijumaa Novemba 10,2017 na Jaji Lugano Mwandambo kutokana na maombi yaliyofunguliwa na Miza Bakari Haji na wenzake saba waliokuwa wabunge wa viti maalumu na madiwani wawili wa viti maalumu, ambao pia walivuliwa uanachama.
Zuio hilo la mahakama linaihusu Bodi ya CUF, Mwenyekiti wake wa Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Magdalena Sakaya, ambao walikuwa ni miongoni mwa wajibu maombi, ambao pia ni wadaiwa katika kesi ya msingi.
Hata hivyo, wakati ikitoa zuio hilo, Mahakama imenawa mikono dhidi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ambayo pia ilikuwa ni miongoni mwa wajibu maombi, kuwa haina mamlaka ya kuchunguza uamuzi wake.
Pia, Mahakama ilitupilia mbali madai dhidi wakurugenzi wa manispaa za Ubungo na Temeke, ambao nao walikuwa ni wajibu maombi hayo.
Katika maombi hayo, waombaji walikuwa wakiiomba Mahakama kutoa amri ya zuio la muda dhidi ya Bunge kutokuwaapisha wabunge wapya walioteuliwa na NEC badala ya walalamikaji.
Pia, waliiomba Mahakama itoe amri ya zuio la muda dhidi ya wakurugenzi wa manispaa za Ubungo na Temeke kutokuwateua madiwani wengine badala yao na kuwaapisha, kusubiri kumalizika kwa kesi yao ya msingi waliyoifungua wakipinga kuvuliwa uanachama.
Hata hivyo, Agosti 25 Mahakama ilitupilia mbali  maombi ya zuio dhidi ya Bunge kutokuwaapisha wabunge walioteuliwa kuchukua nafasi zao baada ya kukubaliana na pingamizi la awali lililowekwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
 Wadai wengine ambao walikuwa wabunge wa Viti Maalumu  ni Savelina Silvanus Mwijage, Salma Mohamed Mwassa, Raisa Abdallah Musa na Riziki Shahari Mngwali.
Wengine katika nafasi ya ubunge ni Hadija Salum Al- Qassmay, Halima Ali Mohamed na Saumu Heri Sakala wakati madiwani ni Elizabeth Alatanga Magwaja na Layla Hussein Madib.

Mbunge amtaka mwenzake kuacha kuwashwa washwa


Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Agnes Marwa amemtaka mbunge mwenzake wa Tarime Vijijini (Chadema), John Heche kuacha kuwashwa washa kwa kuzungumzia masuala nje ya mkoa wake na ajielekeze kuwatetea wananchi wa Nyamongo jimboni kwake.
Agnes anayetoka Mkoa wa Mara pamoja na Heche ametoa kauli hiyo bungeni mjini Dodoma leo Ijumaa Novemba 10,2017 wakati akichangia mpango wa taifa wa maendeleo wa mwaka 2018/19.
Msemo wa kuwashwa washwa ulitokana na kauli ya Rais John Magufuli katika moja ya hotuba zake Ikulu jijini Dar es Salaam alipowazungumzia viongozi wastaafu akiwataka kutulia na kutozungumzia mambo yasiyo na tija.
Katika mchango wake, Agnes alisema, “Nimemwona mbunge wangu wa Tarime ambako ndiko huko Nyamongo, mheshimiwa Heche yeye anawashwa washwa na uwanja wa ndege ulioko kwa mheshimiwa Rais (Chato mkoani Geita) anashindwa kuwaombea wananchi wetu walipwe fidia zao,” alisema Agnes huku akishangiliwa.
Alisema, “Sasa yeye anatakiwa ajue kwamba wale wananchi wanahitaji yeye awatete si kuwashwa washwa na mikoa mingine kitendo ambacho kwa kweli si kizuri sana na ni kitendo ambacho hakikubaliki hata kidogo.”
“Alitaka uwanja uende nyumbani kwake au ni kosa mheshimiwa wetu Rais kuzaliwa eneo ambalo uwanja wa ndege umepelekwa na ukiangalia kwanza kutokana na mpango suala hili limeangaliwa kwa undani zaidi,” alisema.
Alisema kujengwa uwanja huo Chato kumebana matumizi na ni eneo ambalo kulikuwa na eneo kuliko ungepelekwa mkoani Shinyanga, ungeilazimu Serikali kutumia fedha kulipa fidia wananchi ili kupisha eneo hilo na wananchi wangepata usumbufu.
“Lakini mambo mengine tunapaswa kupeleka siasa mitaani si siasa bungeni… sina mengi zaidi ila nataka mbunge wangu Heche asiwashwe washwe awatetea wananchi wa Nyamongo,” alisema Agnes
Akichangia, mbunge wa Tarime Mjini (Chadema), Esther Matiko alisema kuweka taa za barabarani katika mji wa Chato ni matumizi mabaya ya fedha za umma.
"Tumeona traffic light (taa za barabarani) Chato. Kuna miji ina msongamano wa magari ninyi mnaenda kujenga Chato?" alihoji Matiko.
Alisema Chato haina msongamano wa magari na kuna picha aliona punda wakivuka katika taa hizo japo hana uhakika kama ilikuwa Chato lakini akasema hayo ni matumizi mabaya ya fedha.
Mbali na suala hilo, alisema hata ujenzi wa uwanja mkubwa wa ndege Chato haukustahili bali uwanja wa aina hiyo ungejengwa Dodoma.
Matiko alisema kama uwanja huo  ungejengwa Dodoma, hata ndege kubwa inayombeba Rais wa Marekani, Donald Trump ingeweza kutua badala ya Rais Magufuli kulazimika kwenda Dar es Salaam kumpokea endapo atafanya ziara nchini.
Alisema badala ya Serikali kutumia Sh39 bilioni kujenga uwanja huo, ni vyema fedha hizo zingejenga hospitali kubwa Chato au kujenga chuo kikuu eneo hilo.
Kwa mujibu wa Matiko, Chato kungeweza kujengwa uwanja mdogo ambao utawezesha kutua ndege kama Bombadier na uwanja mkubwa ujengwe Dodoma.

RAIS MHE. DKT. MAGUFULI AFANYA MAZUNGUMZO NA RAIS YOWERI MUSEVENI KATIKA IKULU YA MASAKA NCHINI UGANDA


 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni mara baada ya kuwasili katika Ikulu ndogo ya Masaka nchini Uganda.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisaini kitabu mara baada ya kuwasili katika Ikulu ndogo ya Masaka nchini Uganda.
 Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni akimkaribisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli katika eneo la mkutano baina ya wajumbe wa nchi mbili za Tanzania na Uganda katika Ikulu ya Masaka nchini Uganda.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa pamoja aliombatana nao katika Mazungumzo na ujumbe wa Uganda uliokuwa ukiongozwa na Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni katika Ikulu ya Masaka nchini Uganda.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo wa pamoja na ujumbe wa Uganda.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akicheza ngoma na kikundi cha Ngoma za Asili cha Cranes Performance mara baada ya dhifa ya kitaifa aliyoandaliwa na mwenyeji wake Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni katika Ikulu ya Masaka nchini Uganda.
Kikundi Cranes performance kikitumbuiza katika dhifa ya kitaifa iliyoandaliwa kwa ajili ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli katika Ikulu ya Masaka Uganda. PICHA NA IKULU