Chama hicho kimeunda Kamati za Kitaifa 10, zitakazoongeza nguvu, hamasa na mikakati ya kampeni za uchaguzi wa marudio kwenye nafasi hizo kuanzia kesho hadi siku ya uchaguzi.
Timu hizo ambazo zitafanya kazi kwa kushirikiana na kamati zingine za hamasa katika ngazi za kanda, mikoa, majimbo, kata na matawi katika maeneo yenye uchaguzi huo, zitaongozwa na Mwenyekiti wa Chama Taifa, Freeman Mbowe.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa chama hicho Tumaini Makene imeeleza kuwa Mbowe ataanza kuzindua kampeni kesho katika Kata ya Saranga, jijini Dar es Salaam.
Makene ametaja watakaoongoza timu hizo zilizopangwa kwa makundi A hadi G, kuwa ni Mwenyekiti wa Chama Taifa Freeman Mbowe, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama na Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa, Makamu Mwenyekiti Taifa (Bara), Profesa Abdallah Safari, Makamu Mwenyekiti wa Chama Taifa (Zanzibar) Said Issa Mohamed, Katibu Mkuu wa Chama Dk. Vincent Mashinji.
Amewataja wengine watakaoongoza timu hizo kuwa ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama (Bara), John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu wa Chama (Zanzibar), Salum Mwalimu.
Amesema timu hizo zitasaidiwa kwa ukaribu na timu zingine tatu chini ya uratibu na mikakati ya mabaraza ya chama, ikiwamo Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) na Baraza la Wazee wa Chadema.
Timu hizo zitazunguka katika maeneo yote ya uchaguzi wa kata hizo 43, lengo ni kuwafikia wananchi wote kuelekea uchaguzi huo.
“Chadema tutaweza kuwafikia na kuzungumza na wananchi katika majimbo 37, halmashauri 36, mikoa 19 nchi nzima.
“Chama kimedhamiria kuweka ushindani mkubwa na kushinda kata hizo 43 ambazo chama kimeweka wagombea, tunaamini ushindi upo na ndiyo maana tunakutana na wananchi kuwahamasisha na kuwasikiliza wanataka nini ” amesema Makene.
No comments:
Post a Comment