Saturday, December 15

Kadi ya Bima ya Afya yazua utata jijini Dar

HOSPITALI ya Hindu Mandal, Dar es Salaam imeuzuia mwili wa Marystela Alfonce aliyefariki juzi baada ya kubainika kuwa alikuwa akitumia kadi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ya mtu mwingine aliyetajwa kwa jina la Honorata Magezi ili kupata matibabu.
Hospitali hiyo jana ilikataa kutoa mwili wa marehemu Marystela hadi ilipwe Sh7.2 milioni ambazo ni gharama za matibabu tangu alipolazwa hospitalini hapo, Novemba 12, mwaka huu.
Mwandishi wetu alishuhudia gari la kubeba maiti aina ya Marcedes Benz lililofika katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali hiyo kuchukua mwili wa Marystela likiondoka bila kubeba mwili huo.
Ilielezwa kuwa, marehemu alikuwa akitumia kadi ya ndugu yake kupata matibabu katika hospitali hiyo hadi kifo kilipomkuta.
kutokana na tukio hilo, mume wa Honorata, Jovis Magezi anashikiliwa na polisi.
Magezi ambaye ni Daktari wa Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga, alikamatwa jana baada ya kufika Hindu Mandal kwa lengo la kuchukua mwili wa marehemu kabla uongozi wa hospitali hiyo na Bima ya Afya kushtuka.
Daktari huyo alikamatwa baada ya maofisa hao kumbana kwa maswali.
Mahojiano ya daktari huyo na kikosikazi hicho yalikuwa kama ifuatavyo:
Ofisa wa Bima: Mna uhusiano gani na marehemu.
Magezi: Ni mke wangu.
Ofisa wa Bima: Mke wako alilazwa lini hapa hospitalini?
Magezi: Wiki mbili zilizopita.
Ofisa wa Bima: Huyo siyo mkeo ina maana hufahamu hata siku aliyolazwa mkeo hapa hospitali?
Magezi: Kimya.
Ofisa wa Bima: Tunaomba namba ya simu ya marehemu mkeo.
Magezi: Siikumbuki kwa sasa.
Ofisa wa Bima: Tueleze ukweli ili tujue namna ya kukusaidia. Sisi sote tunafahamu matatizo, usitufiche kwa sababu huonyeshi kama umefiwa na mke wako.
Magezi: Ukweli ni kwamba marehemu ni shemeji yangu. Alikuwa akitumia kadi ya bima ya dada yake ambaye ni mke wangu Honorata Magezi… jina halisi la marehemu ni Marystela Alfonce.
Baada ya kukiri, maofisa upelelezi wa Kituo cha Polisi Kati, walifika na kumweka chini ya ulinzi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Ilala, Marieta Komba alisema Magezi alikamatwa na kufikishwa katika kituo hicho lakini akaagiza aachiwe huru mara moja na atafutwe mkewe ambaye ndiye mwenye kadi iliyotumiwa na marehemu.
“Hatuwezi kumkamata Magezi kwa kosa la mkewe. Nimeagiza aachiwe na akamatwe mkewe ambaye ndiye mhusika,” alisema.
Mkurugenzi wa Masoko na Utafiti wa (NHIF), Raphael Mwamoto alisema baada ya kubaini kadi hiyo kutumiwa na mtu ambaye si mwanachama, mfuko huo hautalipa deni hilo la Sh7.2 milioni.
“Tumemfikisha Magezi polisi ili asaidie kupatikana kwa mkewe Honorata ambaye kadi yake ndiyo ilitumika kutoa matibabu,” alisema na kuongeza:
“Kuhusu utata uliopo wa mwili wa marehemu tunawaachia Hospitali ya Hindu Mandal na ndugu wa marehemu, wao wataangalia namna ya kulitatua tatizo hilo.”
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Hindu Mandal, Dk Ramaiya Kaushik alisema mwili huo unashikiliwa na hospitali yake kutokana na matumizi yasiyo halali ya kadi ya Mfuko wa Bima ya Afya.
“Ni kweli tumepata tatizo hilo. Hii ni changamoto kwetu kuhakikisha kwamba tunaimarisha ukaguzi wa kadi hizi ili tatizo hili lisijirudie tena,” alisema Kaushik.
Alisema mgonjwa anaweza kufika mapokezi na kuonyesha kadi ya Mfuko wa Bima ya Afya na kwamba akijiandikisha mapokezi hadaiwi kadi hiyo katika idara nyingine yeyote.
“Sasa tutaanza kupokea kadi mapokezi na mgonjwa atatakiwa kuionyesha kila eneo la huduma atakapokuwa akienda ili kuimarisha zaidi usimamizi,” alisema Dk Kaushik.
Alipoulizwa mwili huo utashikiliwa hadi lini alisema: “Ninawasiliana na viongozi wengine wa hospitali hii ili tukae na ndugu wa marehemu tuone tutafanya nini, hili ni suala ambalo tunatakiwa kulimaliza kibinadamu bila upande wowote kuathirika,” alisema.
Waombolezaji
Nje ya hospitali hiyo kulikuwa na idadi kubwa ya waombolezaji, wengi wao wakiwa wanawake.
Mmoja wa waombolezaji ambaye alikataa kutaja jina lake alidai kwamba marehemu hakuwa na uhusiano wa kindugu na waliompa kadi hiyo na kuongeza kuwa ni watu wanaofahamiana lakini siyo ndugu.
Mwingine atiwa mbaroni
Mkazi wa Kigamboni, Andrew Mjetu anashikiliwa katika Kituo cha Polisi Kati, Dar es Salaam akidaiwa kumpatia, Elias Jones kadi yake ya NHIF ili aitumie kupata dawa zenye thamani ya Sh1.2 milioni kinyume na sheria.
Mwamoto alidai kuwa Elias alikuwa akitibiwa katika Hospitali ya Saratani Ocean Road na aliandikiwa dawa za kununua kwenye maduka lakini hakuwa na kiasi hicho cha fedha.
“Ndipo akakutana na Andrew ambaye alikubali kumsaidia kwa kumpa kadi yake ili akachukulie dawa,” alisema Mwamoto.
Alisema alipopata kadi hiyo alikwenda katika ofisi za NHIF ili kupata dawa bila kujua kwamba kufanya hivyo ni kosa.
Akizungumza tukio hilo, Elias alisema ni bora angekamatwa yeye kwa sababu ugonjwa wake ndiyo uliomponza `msamaria mwema’.
“Yule si ndugu yangu lakini ameniona ninavyohangaika na maumivu akaamua kunisaidia, sasa cha ajabu yeye anawekwa ndani mimi nikiwa nje,” alisema huku akilia kwa sauti.

Pengo asema Shule TZ zimekuwa vitega uchumi

ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amesema elimu inayotolewa nchini ni ya kibaguzi.
Kardinali Pengo alisema hayo Dar es Salaam jana alipokuwa akiwasilisha ujumbe wa maaskofu wa Kanisa Katoliki walioutoa katika mkutano wao uliofanyika Oktoba 7 hadi 28, mwaka huu huko Roma, Italia.
Alisema watu wote wenye mapenzi mema na nchi hii wanapaswa kutoa kipaumbele katika upatikanaji wa elimu bora kwa kila Mtanzania.
Kardinali Pengo alisema hapendezwi na namna elimu inavyotolewa nchini kwani kimfumo, baadhi ya shule zimekuwa vitegauchumi, hivyo kuwa kikwazo kwa watu wenye kipato cha chini.
“Wenye vipato vya chini hawawezi kusoma katika shule hizi kwa sababu zinatoza ada kubwa ambayo maskini hawezi kumudu gharama zake,” alisema.
Askofu Pengo alionya kuwa endapo hali hiyo itaachiwa, inaweza kuwafanya wale waliokosa elimu kuwa chanzo cha vurugu kwa kuwa watasimama kidete kudai haki yao.
Maoni ya Katiba
Katika hatua nyingine, Kardinali Pengo alizungumzia mchakato wa Maoni ya Katiba unaoendelea nchini, huku akiwaonya baadhi ya wanasiasa na taasisi mbalimbali za dini kuacha kuwashinikiza wananchi kutoa maoni kwa ajili ya masilahi yao binafsi.
“Kila mtu aruhusiwe kutoa maoni yake, lakini lazima tukubaliane kuwa kila mtu ana maoni yake na maoni yote hayawezi kuingizwa katika Katiba Mpya,” alisema Pengo.
Alisema kwa kuwa Katiba inagusa masilahi ya nchi, ni vyema kila mwananchi akatumia fursa yake ya kuwasilisha maoni yake mwenyewe.
Alitahadharisha kuwa wananchi wasiposhirikishwa katika mchakato wa Katiba Mpya, wanaweza kuja kuikataa kwa sababu maoni yao hayakuzingatiwa.
Suala la udini
Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, ameitaka Serikali kuchukua hatua za makusudi kwa wale wote watakaobainika kusababisha uharibifu wa mali za dhehebu la dini yoyote hapa nchini, kama wanavyofanya pindi kunapotokea uhalifu katika benki au wizi katika maeneo ya viongozi na sehemu nyingine.
Alisema nchi imegawanyika katika madhehebu mbalimbali, hivyo inapotokea dhehebu moja kulitukana na kuharibu mali za jingine, Serikali haipaswi kukaa kimya.
Alisema Serikali inapaswa kuwa makini, ikiwamo kuwafuatilia na kuwachukulia hatua wale wote wanaoonyesha dalili za uvunjifu wa amani.
Aliwataka viongozi wenye dhamana kuacha kushabikia udini katika kusimamia haki za jamii kwa Watanzania.
Kardinali Pengo pia aliitaka Serikali kuchukua hatua juu ya mihadhara isiyofaa majukwaani.
“Mungu ametuumba ili tumwabudu kila mtu kwa dini yake, huna sababu ya kumtukana mwenzako au kuikashifu dini ya mwenzako, tunachotakiwa ni kufuata misingi na mema yote,” alisema.
Alisema kama Serikali inashindwa kuwakemea na kuwachukulia hatua wale wanaowatukana wenzao, hali hiyo ikiachwa inaweza kuvuruga amani na mshikamano na hivyo nchi kuingia kwenye mgogoro wa kidini.
Kardinali Pengo alisema haoni tatizo kama mtu atasema Yesu si mwana wa Mungu katika nia na mtazamo wake na mwingine akasema Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na siyo kutupiana maneno ambayo mwisho wa siku inakuwa ni chuki kubwa.