RAIS Dk. John Magufuli amesema watumishi wa umma 59,967 watarekebishiwa mishahara na promosheni zao na kuanza kulipwa mwezi ujao.
Rais alitoa kauli hiyo jana ikiwa ni siku moja baada ya Serikali kupitia msemaji wake, Dk. Hassan Abbasi kukanusha tuhuma za Chama cha Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) ambazo zilidai Rais Dk. John Magufuli amekataa kupandisha mishahara ya watumishi.
Katika hotuba yake aliyoitoa jana visiwani Zanzibar wakati wa kuadhimisha Kumbukumbu ya Kifo cha Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Rais, Dk. Magufuli alisema Serikali baada ya kusafisha kwa kuondoa watumishi hewa na wale wenye vyeti vya kughushi, imetenga jumla ya Sh bilioni 159, 326 kwa ajili ya kulipa marekebisho ya mishahara na promosheni za watumishi hao.
Ufafanuzi huo wa Rais aliutoa wakati akielezea moja ya mifano ya kizalendo ambayo aliitenda Mwalimu Nyerere wakati wa utawala wake, ambapo alikataa kupandisha mishahara ya watumishi ili kuboresha huduma za kijamii.
Akielezea mfano huo, Rais Magufuli alisema baada ya Tanzania kupata uhuru baadhi ya wasomi waliokabidhiwa madaraka walianza kutoa shinikizo kwa Serikali kutaka kuongezewa mishahara na marupurupu.
Alisema kutokana na mashinikizo hayo Mwalimu Nyerere hakukubaliana nao na hakusita kuikemea tabia hiyo ya ubinafsi.
Kwa mujibu wa Rais Magufuli, Mwalimu Nyerere kwa kuonyesha mfano wa kukerwa na ubinafsi aliamua kupunguza mshahara wake ili kuwakumbusha wasomi hao kwamba, haiwezekani watu wachache kuongezeana mishahara wakati wananchi wengi masikini hawapati huduma muhimu ya afya, elimu na maji.
“Tujiulize je, na sisi tupo tayari kuacha mishahara hewa. Je, mishahara tunayopata tumeifanyia kazi. Je, nasi tupo tayari kujipunguzia au kuishinikiza Serikali kuongeza mishahara na marupurupu yetu ili ituwezeshe kuboresha huduma za jamii kwa manufaa ya Watanzania?
“Ninasema hivyo simaanishi kuwa mishahara ya watumishi isiongezwe la hasha, ninachotaka kusema ni kwamba, kabla ya kudai nyongeza ya mshahara ni lazima kwanza kufahamu uwezo wa Serikali lakini pia tutambue kuwa kuna Watanzania wenzetu wengi tu wanahitaji kuboreshewa huduma…nimesema hili sina maana ya kwamba watu wasiongezewe mishahara. Tuna mifano inayoishi kwa hapa Zanzibar, Rais Shein baada ya kushika madaraka mishahara ya kima cha chini imepandishwa kutoka Sh150,000 hadi Sh 300,000. Lakini sisi kama tusingefanya ukaguzi wa kutosha tungelipa Sh bilioni 89 kwa wafanyakazi hewa,” alisema Rais Magufuli.
KUHUSU NYERERE
Akimzungumzia Mwalimu Nyerere, Rais Magufuli alisema Watanzania wanatakiwa kujikumbusha mchango wake mkubwa wa kulitumikia taifa hili.
Alisema katika kujikumbusha huko Watanzania wanatakiwa kujifunza na kutumia mafunzo yanayoelekeza kusukuma mbele maendeleo ya taifa.
Aliongeza kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa ni kiongozi mzalendo tangu mwanzo wa uongozi wake wa kisiasa mwaka 1953 wakati alipochaguliwa kuwa Rais wa Chama cha TAA ambacho kilizaa TANU.
“Katika kipindi hicho Mwalimu Nyerere alionyesha uzalendo wa hali ya juu na kuthamini kwake utu na usawa wa binadamu. Wakati anachaguliwa kuwa Rais wa TAA na baadaye TANU, alikuwa anafundisha St. Francis College kwa sasa inajulikana kama Shule ya Sekondari ya Pugu na umbali wa kutoka Pugu hadi ofisi za TAA na TANU kwa maana ya kwenda na kurudi zilikuwa kilomita 46 na enzi hizo hapakuwa na usafiri wa daladala kama ilivyo sasa.
“TAA na TANU hazikuwa na usafiri wala nauli ya kumlipa, lakini Mwalimu Nyerere kwa uzalendo alitumia fedha zake kujigharamia usafiri na wakati mwingine alilazimika kutembea kwa miguu na alifanya hivyo kwa kujitolea. Tujifunze leo ni viongozi wangapi wa vyama wanaweza kujitolea kwa kiasi hicho?” alihoji.
Alisema mwaka 1955 alipotakiwa kuchagua kuendelea na kazi ya kufundisha Shule ya St. Francis au kuacha kujihusisha na shughuli za kisiasa, Mwalimu Nyerere aliamua kuacha kazi na kubaki kuwa kiongozi wa TANU kazi ambayo alikuwa halipwi mshahara wowote.
Alisema Mwalimu Nyerere aliamua kuachana na kazi ili aendelee kuongoza harakati za kudai uhuru na alikuwa na hali ngumu ya maisha.
Rais Magufuli aliongeza kuwa kitu pekee kilichomlazimu Mwalimu Nyerere kuacha kazi, ni uzalendo na upendo wake kwa Watanzania kwamba kama isingekuwa hivyo kwa elimu aliyokuwa nayo wakati huo angeamua kutafuta kazi yenye kulipwa mshahara mzuri.
“Tujiulize sisi Watanzania leo hii ni wangapi wanaweza wakafanya uamuzi wa kizalendo kama huo uliofanywa na Baba wa Taifa? Leo hii kuna Watanzania wangapi ambao kwa sababu tu wanalipwa vizuri kwenye makampuni ya wageni wanaisaliti nchi kwa vitendo vya wizi na rushwa?
“Je, kuna viongozi wangapi waliopewa dhamana ya wananchi lakini kwa kukosa uzalendo wamekubali kusaini mikataba isiyo na tija ya nchi, je, kuna viongozi wangapi ambao hawazingatii Tanzania kwanza badala yake wanazingatia fedha kwanza?…majibu ndugu zangu Watanzania mnayo wenyewe,” alisema.
Rais Magufuli alisema Mwalimu Nyerere hakuishi maisha ya kifahari na anasa.
“Kuna watu waliwahi kusikika wakisema kama Nyerere angekuwa mbinafsi au mpenda utajiri angeweza kuchukua fukwe yote ya Msasani lakini hakufanya hivyo. Na kweli angeweza maana kuna mifano mingi ya viongozi wengi wa zama zake na hata zama za sasa wanafanya hivyo.
“Lakini yeye hakufanya hivyo licha ya kutumikia urais kwa takribani miaka 23, Mama Maria, watoto na ndugu zake wengi ambao waliishi na wanaendelea kuishi kwa maisha ya kawaida kabisa sawa na Watanzania wengi,” alisema.
AGOMA KUFUTA MBIO ZA MWENGE
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alisema Serikali haitafuta mbio za Mwenge wa Uhuru kwa kuwa ni alama ya Uhuru na Utaifa wa nchi na kwamba unatoa mchango mkubwa katika kuchochea maendeleo, kuwaunganisha Watanzania na kuimarisha Muungano.
Alisema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, zitaendeleza Mbio za Mwenge wa Uhuru na kuutetea Muungano kwa nguvu zote.
Rais Magufuli ametoa kauli hiyo wakati ambao kwa miaka kadhaa sasa baadhi ya watu wamekuwa wakitamani kuona mbio hizo zikifutwa kwa kuwa hawaoni faida yake zaidi ya kutumia fedha nyingi za Serikali.
“Kaulimbiu ya Mwenge wa Uhuru mwaka huu inasema, Shiriki Kukuza Uchumi wa Viwanda kwa Maendeleo ya Nchi yetu. Nimefarijika zaidi kusikia kuwa katika Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu jumla ya viwanda 148 vimezinduliwa, viwanda hivyo vimejengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 468.46 na vinatarajiwa kuzalisha ajira 13,370.
“Hii ndio sababu tumekuwa tukihimiza ujenzi wa viwanda na hizi ni baadhi ya faida za Mwenge,” alisema Rais Magufuli.
Akizungumzia vijana, Rais Magufuli amewataka kuendelea kujielimisha katika nyanja mbalimbali, kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya na kujikinga dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi.
Aidha, Rais Magufuli aliwapongeza na kuwakabidhi vyeti wakimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa walioongozwa na Amour Hamad Amour kwa kukimbiza mwenge huo kwa siku 195 katika mikoa yote 31 na Halmashauri 195, ambapo jumla ya miradi 1,512 yenye thamani ya jumla ya shilingi trilioni 1.1 imepitiwa.
Pia ameahidi kuchukua hatua dhidi ya wote waliohusika kusababisha dosari katika miradi 19 ambayo viongozi wa mwenge wamebaini.
Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Kifo cha Hayati Baba wa Taifa ambayo yaliambatana na sherehe za kuzima Mwenge wa Uhuru pamoja na Sikukuu ya Vijana yalihudhuriwa na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Majaliwa, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Seif Ali Idd, Mke wa Rais wa Magufuli, Mama Janeth Magufuli, Mke wa Rais wa Zanzibar, Mama Mwanamwema Shein na viongozi wengine wa Tanzania Bara na Zanzibar.