Sunday, October 15

KIAMA CHAJA KWA WAGAVI VIHIYO

SERIKALI imetangaza kuwachukulia hatua wataalamu wote wa ununuzi na ugavi watakaobainika kufanyakazi bila kusajiliwa na Bodi ya Wataalamu hao (PSPTB).
Kauli hiyo ilitolewa juzi na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Amina Shabani kwa niaba ya Naibu Waziri wa wizara hiyo, Dk. Ashatu Kijaji kwenye mahafali ya nane ya Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) katika Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam.
Alisema ni kosa kubwa kwa waajiri kuajiri wataalamu ambao hawajasajiliwa na bodi na kwamba kufanya hivyo ni ukiukwaji wa sheria.
“Napenda nitoe onyo kwa waajiri wote nchini kuacha kuajiri watu wasiosajiliwa na Bodi kwani kufanya hivyo ni kukiuka sheria namba 23 ya mwaka 2007 iliyoanzisha Bodi hiyo na kwamba Wizara yake itafuatilia suala la watu wanaofanya kazi bila usajili akianzia ngazi ya wizara.
“Hivyo yeyote atakayebainika kufanya kazi kinyume na maadili na taratibu za kazi, atatumbuliwa haraka kabla hajasababisha hasara kubwa kwa Taifa kama ambavyo imekuwa ikitokea mara kwa mara,” alisema Amina.
“Suala la maadili na uzalendo lipewe kipaumbele katika mafunzo yenu, warsha na makongamano, Serikali haitamvumilia mtu yeyote atakayetumia nafasi aliyopewa kujinufaisha na kusababisha huduma mbovu kwa wananchi, hivyo ili kudhibiti mienendo ya kimaadili kwa wataalamu wenu, ni lazima watu wote wanaofanya kazi za ununuzi na ugavi nchini wawe wamesajiliwa na Bodi kwa mujibu wa sheria,” alisema Amina.
Upande wake, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Sista Hellen Bandiho, alisema kwa kutambua changamoto zilizopo katika ununuzi wa umma na usimamizi wa mikataba, Bodi iliboresha mtaala na kuweka masomo mahususi ili kuwajengea uwezo wataalamu wanaohitimu waweze kusimamia mikataba ya ununuzi yenye kuleta tija.
“Serikali pamoja na kazi kubwa inayofanya lakini tunaiomba iboreshe masilahi ya wataalamu wa fani hii ili angalau yalingane na walaalamu wa fani nyingine wenye viwango sawa vya elimu. Niwaase wahitimu kufanya kazi kwa kufuata maadili ya taaluma ili kulinda heshima ya fani yetu na kuleta ufanisi katika matumizi ya rasilimali za umma kwa manufaa ya Taifa na watu wake,” alisema Sista Hellen.
Jumla ya wanafunzi 1,101 wamefaulu mtihani huo kati ya wanafunzi 3,086 waliofanya mtihani.

No comments:

Post a Comment