NA BASHIR YAKUB -
Yafaa kujua utaratibu unaotakiwa kufuatwa kabla ya kufutiwa hati miliki ya ardhi (nyumba/kiwanja). Unapojua utaratibu huu ndipo unapojua kama ulionewa au hapana. Na kuonewa ni pamoja na kukiuka utaratibu. Na kukiuka taratibu yoyote ya kisheria kunabatilisha mchakato wa kufutwa kwa hati yako na kutakiwa kurudishiwa eneo lako au fidia.
Makala yaliyopita tulieleza mambo ambayo ukifanya unahesabika kukiuka masharti ya umiliki wa ardhi na ni hapo unapoweza kufutiwa umiliki. Leo tuangalie utaratibu wa kufuta umiliki ikiwa imethibitika kuwa tayari umekiuka masharti hayo. Sheria namba 4 ya 1999 , Sheria Ya ardhi imeeleza utaratibu wa kufuta umiliki wa ardhi.
UTARATIBU.
1.Ni lazima uwe umekiuka masharti au moja ya masharti uliyopewa wakati unakabidhiwa ardhi/hati kwa mujibu wa kifungu cha 48 ( 1) cha Sheria ya ardhi. Usikubali kufutiwa umiliki ikiwa hujakiuka sharti/masharti ya umiliki uliyopewa, labda iwe vinginevyo.
2. Baada ya kuwa umekiuka masharti yafaa upewe taarifa maalum( notice) kwa mujibu wa kifungu 48(2). Ni taarifa inayoeleza masharti ya umiliki uliyokiuka na onyo la kufutiwa umiliki. Taarifa hiyo ni ya siku 90(miezi mitatu). Taarifa hiyo utapewa wewe mmiliki na kila mwenye maslahi katika ardhi hiyo mf, mpangaji, mrehani nk.
3. Baada ya siku 90 kuisha na pengine hujajirekebisha au kufanya kile ulichoambiwa kufanya basi kamishna wa ardhi atatakiwa kupeleka pendekezo kwa rais ili kufutiwa umiliki. Ni rais tu mwenye mamlaka ya kufuta umiliki wa ardhi.
Zingatia, barua au nyaraka nyingine yoyote ambayo inasema umefutiwa umiliki lakini aliyefuta sio rais wa nchi, sio halali.
4. Ikiwa rais atakubali kukufutia umiliki wa ardhi basi inatakiwa kufutwa huko kutangazwe katika gazeti maalum la serikali/taarifa ya serikali(GN) na katika gazeti la kawaida(newspaper) ambalo linafika eneo ardhi yako ilipo. Hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 49(1). Ili utaratibu uhesabike umefuatwa ni lazima matangazo haya yatolewe la sivyo kufutiwa huko kunabatilika.
5. Rais atakapofuta umiliki wa ardhi basi ardhi hiyo itahama kutoka kwa mmiliki wa awali kwenda serikalini au vinginevyo itakavyoamriwa kwa mujibu wa kifungu cha 49(2).
6. Ikiwa kuna maendelezo yoyote ya kudumu ambayo ulifanya kwenye hiyo ardhi basi ni lazima ulipwe fidia ya maendelezo hayo kwa mujibu wa kifungu cha 49(3).
Isipokuwa maendelezo hayo yawe yalikuwa ni sehemu ya masharti ya umiliki wa ardhi hiyo. Yasiwe nje ya yale uliyokuwa umepewa kwenye umiliki.
7. Ikiwa ardhi hiyo ilikuwa inadaiwa kodi au tozo za ardhi basi kodi na tozo hizo zinaondolewa na deni hilo linakufa, mpaka isemwe vinginevyo. Hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 49(2)(e)..
NAMNA YA KUDAI HAKI YAKO IKIWA TARATIBU ZIMEKIUKWA.
Kwanza, waweza kupeleka malalamiko yako kwa kamishna wa ardhi na baadae kwa rais. Utaandika barua ikieleza kile ambacho unahisi kuonewa au taratibu kukiukwa.
Pili, ni kupeleka malalamiko yako mahakamani. Hapo sio barua bali utapeleka nyaraka maalum za kufungulia shauri(Plaint/Application). Humo pia utaeleza pahala unapohisi kuonewa au taratibu kukiukwa pia.
Pia unaqweza kuchukua hatua hizi kwa pmoja na kwas wakati moja.
MWANDISHI WA MAKALA HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA JAMHURI KILA JUMANNE. 0784482959, 0714047241bashiryakub@ymail.com