Uamuzi huo ulitolewa na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani, lililoongozwa na Jaji Bernard Luanda, Augustine Mwarija na Rehema Mkuye kufuatia rufaa aliyoikata mfungwa huyo kupinga hukumu aliyopewa na Jaji Augustine Shangwa wa Mahakama Kuu.
Mahakama ya Rufani imeamuru kesi hiyo irudishwe Mahakama Kuu isikilizwe upya baada ya kujiridhisha kuwa mwenendo wa kesi hiyo wakati wa usikilizwaji ni batili, kutokana na makosa yaliyofanywa na washauri wa Mahakama kwa kufanya majukumu wasiyostahili.
Kasoro hizo zilizoifanya hukumu kubatilishwa ni kitendo cha washauri hao kumfanyia udodosaji jukumu ambalo hufanywa na wakili wa upande pinzani katika kesi.
Kasoro hiyo iliibuliwa na Wakili aliyemwakilisha mrufani, Daniel Welwel, katika sababu yake ya nyongeza kati ya sababu za rufaa alizokuwa ameziwasilisha awali.
Mahakama ya Rufani katika hukumu yake iliyosomwa na naibu msajili wa mahakama hiyo, Amir Msumi ilisema ingawa sheria haiwapi washauri wa mahakama mwanya wa kumfanyia shahidi udodosaji, lakini katika kesi hiyo jaji aliwapa mwanya wa kufanya hivyo kwa mashahidi wa pande zote.
Japhary alikamatwa Aprili 23, 2004 na kushtakiwa kwa tuhuma za kumuua binamu yake, Joseph Shedula aliyekutwa amekufa chumbani walimokuwa wamepanga huko Mabibo Upogoroni, baada ya kurejea kutoka Korogwe Tanga.
No comments:
Post a Comment