Monday, December 4

Ombi la familia ya aliyepandikizwa figo kushughulikiwa


Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema ombi la familia ya mgonjwa wa kwanza kupandikizwa figo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prisca Mwingira (30), linaweza kushughulikiwa na halina kipingamizi.
Ndugu wa mgonjwa huyo aliyefanyiwa upasuaji wa upandikizaji wa figo Novemba 21, wameiomba Serikali kumhamisha kituo cha kazi Prisca ambaye ni mwalimu wa Shule ya Sekondari Mikese iliyopo Morogoro ili apate matibabu akiwa karibu.
Akizungumza na gazeti hili, Waziri Ummy alisema suala la mgonjwa huyo kuhitaji uhamisho na mengine kuhusu ajira, uwezekano wa kusaidiwa upo, hivyo ameshauri afuate utaratibu.
“Kuhusu ombi la ajira, ninamshauri afuate utaratibu wa uhamisho wa watumishi wa umma. Sababu yake ina uzito, sina shaka kuwa maombi yake yatakubaliwa,” alisema Ummy.
Alisema anashukuru kuona upandikizaji wa figo kwa mgonjwa huyo wa kwanza nchini umekuwa na mafanikio makubwa.
“Kilichopo sasa ni kuzidi kumuombea afya njema ili aweze kuendelea na majukumu yake ya kila siku, kwa mara nyingine nawapongeza madaktari wetu wa Muhimbili,” alisema Ummy.
Akizungumzia suala hilo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mwasu Sware alisema suala la ufuatiliaji wa ajira ya Prisca lipo chini ya Wizara ya Tamisemi kwa kuwa kurugenzi zote zipo chini ya wizara hiyo.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) anayeshughulikia afya, miundombinu na uwekezaji, Josephat Kandege alisema suala la Prisca ni la kipekee hivyo anaweza kusaidiwa iwapo atakuwa na vielelezo.
“Kisheria na utaratibu uliopo tunahitaji awasilishe vielelezo ambavyo ni nyaraka ambazo zinatoka Muhimbili zilizotoa maelekezo kama hayo baada ya hapo kuna utaratibu kadhaa, ikiwemo kuandika barua. Tunamthamini mfanyakazi akiwa mzima na mgonjwa,” alisema Kandege.
Alisema wakati mwingine wanapata kigugumizi kwa Dar es Salaam kwa kuwa shule nyingi walimu wamejaa, hivyo hiyo ni changamoto kwa kuwa ni lazima kuwa na namna ya kuziba pengo la anakotoka.
“Tunaweza pia kumpatia uhamisho wa muda katika kipindi ambacho yupo kwenye matibabu aweze kuwa hapa. Nafahamu wagonjwa wengi waliopandikizwa figo si lazima ahudhurie kliniki kila wiki inafikia kipindi atamwona daktari kwa mwezi na miezi, linatakiwa liangaliwe kwa uzito wake,” alisema.
Desemba Mosi, Prisca aliruhusiwa kurudi nyumbani baada ya kuwa chini ya uangalizi wa jopo la madaktari bingwa wa figo kwa siku 10. Alipatiwa figo na mdogo wake Bartholomew Mwingira (27).
Baba mdogo wa vijana hao, Einhard Mwingira aliipongeza Serikali, uongozi wa hospitali na madaktari kwa kuleta matibabu hayo ya kibingwa na familia yake kuwa ya kwanza kuneemeka, huku akiomba binti yake apewe uhamisho.
“Ombi langu kubwa mtoto wangu anakaa Morogoro, kule anafundisha Shule ya Sekondari Mikese naiomba Serikali ahamishiwe Dar es Salaam ili iwe rahisi kuendelea na matibabu kwa ukaribu hapa Muhimbili, ikiwezekana wambadilishie kazi kwani vumbi la chaki sidhani kama litakuwa zuri kwake,” alisema Mwingira.

No comments:

Post a Comment