Dar es Salaam. Leo ni kufa au kupona kwa makada wa CCM wanaowania ubunge wakati wanachama wa chama hicho tawala watakapopiga kura wilayani kuchagua wagombea kwenye majimbo yao baada ya wiki kadhaa za vikumbo zilizojumuisha kurushiana ngumi, tuhuma za rushwa, malumbano na migomo.
Uchaguzi Mkuu umepangwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu.
Katika upigaji kura leo, wanachama watakuwa na kazi ngumu kuamua kuhusu makada waliogeukia ubunge baada ya kukosa urais, mawaziri katika Serikali ya Awamu ya Nne inayoondoka madarakani, waliotemwa mwaka 2010 wanaowania kurejea bungeni, wakuu wa wilaya ambao wameingia kwa wingi kwenye mbio hizo, na pia wabunge wanaomaliza muda wao ambao ama walikidhi mahitaji yao au kutofanya kazi ipasavyo.
Mchakato huo wa kura ya maoni unafanyika baada ya kumalizika kwa siku 10 za wagombea hao kujinadi kwa makada wenzao katika kata mbalimbali za majimbo wanayotaka kugombea, huku baadhi wakijitoa kutokana na kushindwa kulipa fedha kama mchango wao wa safari za kampeni. Mchakato wa kura za maoni, utafuatiwa na vikao vya kamati za siasa za wilaya na mikoa wakati kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM kitafanyika kwa siku mbili kuanzia Agosti 11 kwa ajili ya uteuzi wa wagombea rasmi wa ubunge na udiwani wa CCM.
Gazeti hili linakuchambulia maeneo matano yatakayozua mjadala mkali mara baada ya matokeo ya kura ya maoni kutangazwa, pamoja na kilichojitokea wakati wa kampeni za wagombea hao.
Wagombea urais waliojitosa ubunge
Macho ya wana-CCM na wananchi wengine yatakuwa yakielekezwa kwa makada wa CCM walioanguka kwenye mbio za urais na ambao wamegeukia ubunge, ambao ni pamoja na Mwigulu Nchemba (Iramba Magharibi), Lazaro Nyalandu (Singida Kaskazini) na mwanasiasa mkongwe ambaye kwa sasa ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wasira.
Wengine ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ambaye alijiuzulu kutokana na kashfa ya escrow, lakini anataka kurejea bungeni kuwakilisha jimbo la Musoma Vijijini.
Pia yumo January Makamba wa Bumbuli mkoani Tanga, William Ngeleja (Sengerema), Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe (Nachingwea), Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Titus Kamani (Busega) na Waziri wa Afrika Mashariki, Dk Harrison Mwakyembe anayerudi Kyela mkoani Mbeya na Balozi Augustine Maiga anayewania Iringa Mjini.
Majimbo yenye mchuano mkali
Moja kati ya majimbo yenye upinzani mkali kwa sasa ni jimbo la Nzega Vijijini kutokana na uwepo wa makada wawili wa chama hicho, Lucas Selelii na Dk Hamisi Kigwangalla.
Katika uchaguzi uliopita wa 2010, makada hao walivaana lakini wote wakaangushwa na Hussein Bashe aliyeibuka wa kwanza akifuatiwa na Selelii, lakini Halmashauri Kuu ya CCM ikamchukua Dk Kigwangalla aliyekuwa mshindi wa tatu.
Mgawanyo wa majimbo uliofanywa hivi karibuni na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), umefanya mpambano huo uwe wa makada hao, baada ya kumwachia Bashe jimbo la Nzega Mjini.
Jimbo jingine lenye mchuano mkali ni Iringa Mjini ambako Balozi Augustine Mahiga aliyekwama katika harakati za kuwania urais kupitia CCM, atapambana na makada wengine kuwania kupata tiketi ya kulikomboa jimbo hilo kutoka Chadema.
Makada wengine kati ya 12 wanaowania kiti hicho ni Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe, Frederick Mwakalebela, mwenyekiti wa CCM wa mkoa, Jesca Msambatavangu na katibu mwenezi wa CCM mkoa wa Iringa, Dk Yahya Msigwa.
Kundi lingine ambalo huenda likaleta upinzani katika uchaguzi huo linamjumuisha mjumbe wa NEC wa Iringa Mjini, Mahamoud Madenge, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Falles Kibassa na mwandishi wa habari, Frank Kibiki.
Wengine wanaowania Iringa Mjini ni Peter Mwanilwa, Frank Kibiki, Michael Mlowe, Nuru Hepautwa, Adestino Mwilinge na Adani Kiponda.
Jimbo la Mkalama linaongoza kwa kuombwa na makada 16 wakiongozwa na mwenyekiti wa mkoa wa Singida, Mgana Msindai, Profesa Shaaban Aman Mbogho, Nakey Samwel Sule, Orgenes Emmanuel, Joseph Mbasha na Allan Joseph Kiula.
Wengine wanaowania jimbo hilo ni Emmanuel Mkumbo, Dk Kissui Stephen Kissui, William Makali, Kyuza Kitundu, Dk Charles Mgana, Salome Mwambu, Francis Mtinga, Dk George Mkoma na Lameck Itungi.
Mchuano mkali pia upo, Kalenga linalowaniwa na mbunge wa sasa, Godfrey Mgimwa na Jackson
Kiswaga, na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro na mbunge wa zamani wa jimbo hilo, George Mlawa.
Mshikemshike mwingine unatarajiwa kuibuka katika Jimbo la Mwanga ambako Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe anapambana tena na hasimu wake mkubwa katika kiti hicho, Joseph Thadayo.
Maeneo yaliyotokea tafrani
Wakati baadhi wakikabiliana na upinzani mkali, makada wengine watakuwa wakihangaika kushawishi wapigakura baada ya kukumbana na hali ngumu kwenye kampeni.
Baadhi yao ni mbunge wa Muleba Kusini, Profesa Anna Tibaijuka, Harrison Mwakyembe (Kyela) na Assumpter Mshama (Nkenge).
Profesa Tibaijuka anayewania jimbo hilo kwa mara ya pili, alishushwa jukwaani kwa kuzomewa na wananchi wake katika kata ya Nshamba wilayani Muleba na tafrani hiyo kudumu kwa dakika kadhaa na kusababisha wagombea wengine kulazimika kuondoka.
Kwa mara ya kwanza alizomewa Juni 8, wakati wa ziara ya katibu mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kwenye kata hiyo hiyo kutokana na kutajwa kwenye kashfa ya escrow na kushindwa kutekeleza ahadi ya kuwajengea barabara ya lami.
Hasira za wananchi pia zilimkumba mbunge wa Kyela, Harrison Mwakyembe kwenye moja ya mikutano yake baada ya wananchi kupiga kelele kutotaka kumsikiliza.
Hali kama hiyo ilimkuta Profesa Maghembe kwenye jimbo lake la Mwanga wakati akijinadi katika mkutano wa kampeni uliofanyika Kisangara.
“Kidumu Chama cha Mapinduzi. Kisangara saafii,” alisalimia Profesa Maghembe na kuitikiwa na sauti za “ondoka ondoka, tumekuchoka sasa, nenda kapumzike huna jipya, waachie wenzio”.
Profesa Maghembe alipoulizwa na gazeti hili jana kuhusu kadhia hiyo, alisema vijana waliomzomea walikodishwa na kupewa pombe katika baa ya jirani ili tu kujaribu kuchafua hali ya hewa.
Profesa Maghembe anachuana tena na mshindani wake wa 2010, Joseph Tadayo na wagombea wengine ambao ni Karia Magaro, Baraka Lolila, Ramadhani Mahuna, Japhar Mghamba na Miniel Kidali.
Wakati Maghembe akikumbana na hasira za wananchi, Naibu Spika wa Bunge Job Ndugai alishindwa kuzuia hasira zake wakati maneno ya mgombea mwenzake yaliposababisha amvamie na kujikuta akihojiwa na polisi.
Ndugai alihojiwa na polisi kwa tuhuma za kumshambulia mgombea mwenzake, Dk Joseph Chilongani kwenye mkutano wa kampeni akimtuhumu kurekodi tukio la kutaka kumpiga mgombea mwingine aliyekuwa akijieleza na kuponda uongozi unaomaliza muda wake.
Hata kama atapita leo, suala lake linatarajiwa kuwa moja ya hoja kwenye kikao cha Halmashauri Kuu.
Hali kama hiyo ipo kwa mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba anayetetea jimbo lake akipambana vikali na katibu mkuu wa zamani wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, pamoja na Juma Hassan Kilimba anayerudi na Amon Gyuda.
Nchemba amekumbana na tafrani baada ya kuhojiwa na Takukuru kwa tuhuma za rushwa. Baadhi ya wagombea wanaowania pamoja naye walishtaki kuwa mwenzao anafanya vitendo ambavyo walivihusisha na rushwa na hivyo Takukuru kuchukua hatua.
Ushindani mkubwa katika jimbo la Mtera unaonekana kuwa baina ya mbunge anayemaliza muda wake, Livingstone Lusinde ‘Kibajaji’ na mtoto wa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Samuel Malecela.
Lusinde pia amekuwa akikumbana na kadhia hiyo baada ya wananchi kumzomea wakati akieleza sera zake kwenye kijiji cha Nkwenda wilayani Chamwino.
Baada ya zomeazomea hiyo, mbunge huyo anadaiwa kuagiza kikundi cha vijana kuwashambulia wananchi ambao walikuwa wakimpiga kelele kumzomea.
Kada mwingine anayewania kurejea bungeni ni mwanasoka wa zamani, Venance Mwamoto ambaye amerejea Jimbo la Kilolo kupambana na mbunge wa sasa Profesa Peter Msolla.
Wakati wanahabari wakikumbana na makada wa fani nyingine kwenye mbio hizo, Jimbo la Chemba linakutanisha wanahabari wawili, Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia ambaye atavaana na mhariri kutoka gazeti la Mtanzania, Khamis Nkyota anayelitaka jimbo hilo kwa udi na uvumba.
Tayari Nkamia ameshalalamikia bungeni harakati za mwanahabari mwenzake kwenye jimbo hilo.
Hali ushindani inayotokana na makada wengi kujitokeza pia ipo kwenye Jimbo la Manyoni Magharibi ambako John Lwanji, mbunge anayemaliza muda wake, anakabwa koo na binamu yake Eliphas Emmanuel Lwanji. Wengine ni Jamal Kuwingwa, Jane Likuda, Mohamed Makwaya, Yahaya Masare, Athumani Masasi, Yohana Msita, Moshi Mmanywa, Adimini Msokwa, Dk Mwanga Mkayagwa, Rashidi Saidi na Francis Shaaban.
Hali kama hiyo pia ipo Mbeya Mjini ambako Charles Mwakipesile aliyepambana na mbunge wa sasa Joseph Mbilinyi mwaka 2010, atakuwa akipambana na Stephen Mwakwenda, Nwaka Mwakisu, Aggrey Mwasanguti na Mchungaji Jackson Numbi
Wengine ni Ibrahim Mbembela, Fatma Ismail , Shambwe Shitambala, Solomon Swila, James Mwampondele, Ulimboka Mwakilili, Samuel Mwaisume, Eliud Mwaiteleke, Michael Mbuza Aman Kajuna na Shadrack Mwakombe.
Lazaro Nyalandu atakuwa na kazi ya kuzuia kazi ya Amos Makiya, Justin Monko, Michael Mpombo, Sabasaba Manase, Yahana Sinton, Mugwe na Aaron Mgogho.
Mgombea wa jimbo la Nanyumbu Dastani Mkapa yupo katika wakati mgumu kutokana na mgombea mpinzani wake William Dua kuonekana ana kasi ya kuchukua Jimbo hilo.
Mgombea wa jimbo jipya la Ndanda, Mariam Kasembe alijikuta akitoa machozi baada ya wananchi wa jumbo hilo kuuliza maswali kwa mgombea huyo na kushindwa kuyatolea majibu.
Mbunge wa jimbo hilo, George Mkuchika ana wakati mgumu kurudi katika nafasi hiyo kutokana na ushindani uliopo kuwa mkubwa ukilinganisha na uchanguzi wa 2010.