Saturday, August 1

Nape afafanua sakata lake na Takukuru Lindi


Lindi. Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye amefafanua sakata lake la kuchukuliwa na askari wa Takukuru kwa mahojiano muda mfupi baada ya kuchukua fedha benki, akisema alikuwa akielekea kulipa mawakala.
Nape, anayewania ubunge wa Jimbo la Mtama, jana mchana aliamriwa na maofisa wa Takukuru kufika ofisi zao baada ya kutoka kuchukua fedha benki ya NMB eneo la Misonobarini mkoa Lindi.
“Ninadhani hawa jamaa walipotoshwa. Mimi nimekwenda zangu benki kuchukua fedha, lengo langu ni kuwalipa mawakala,” alisema Nape jana jioni alipopigiwa simu na Mwananchi kutoa ufafanuzi wa sakata hilo.
“Wakaja hawa jamaa, wakajitambulisha kuwa wanatoka Takukuru, wakaniuliza ‘mbona ninachukua fedha nyingi kipindi hiki?’ Nikawaambia ‘nakwenda kulipa mawakala, na fedha zenyewe ni hizi Sh3.6 milioni’.
“Basi, tukatoka taratibu tukaenda ofisini kwao, ni karibu tu na benki. Wakanihoji hata haikumalizika nusu saa, niliwaambia nataka kulipa mawakala wangu, tena fedha zenyewe hazitoshi, wako zaidi ya 100.”
Nape aliongeza kusema kuwa walimkamata na akawaambia kuwa yeye ni mwadilifu.
“Halafu ninyi, mnaacha marushwa makubwa makubwa huko, watu wanahonga halafu mnamvizia Nape masikini kwa Sh3mil?,” alisema.
Nape alielezea kufadhaishwa na tukio hilo akidai kuwa limetengenezwa kwa ajili ya kumchafua hasa kwa kuwa leo kuna kura za maoni, lakini akasema anaamini yeye ni msafi.
Kamanda wa Takukuru wa Mkoa wa Lindi, Stephen Chami alikiri kumhoji Nape, lakini akasema walijiridhisha kuwa fedha hizo ni kwa ajili ya kulipa mawakala.
“Unajua tuna watu wetu, kwenye maeneo mbalimbali hasa kipindi hiki cha uchaguzi, tumeweka watu wetu maeneo mengi, tunataka kukomesha rushwa,” alisema.
Kilango ageuka ‘mbogo’
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Anne Kilango Malecela juzi aligeuka mbogo baada ya kuzushiwa katika mitandao ya kijamii kuwa anashikiliwa na polisi.
Taarifa hizo zilizosambazwa jana, zilidai kuwa Kilango alikamatwa juzi saa 5:00 usiku katika eneo la Dimbi, kijiji cha Bagamoyo kwa tuhuma za kutoa rushwa, madai ambayo ameyakanusha.
Hata hivyo, Kilango alipoulizwa jana alisema tuhuma hizo ni uzushi uliotengenezwa na baadhi ya washindani wake wakiamini kwa kufanya hivyo watamvurugia katika kura ya maoni inayofanyika leo.
“Sijakamatwa na wala sijaona hata polisi mmoja nyumbani kwangu. Nimelala nyumbani kwangu jana (juzi) na leo (jana) nimeamka nyumbani kwangu na niko kwenye mikutano ya kuomba kura,” alisema.
Kilango aliongeza,”Sasa hivi nimetoka kuomba kura Mtii nilikuwa peke yangu wagombea wanzangu wameingia mitini. Niko Bombo sasa hivi (saa 9;00 alasiri) ndio wanakuja nishapiga bao.”
Kwa mujibu wa Kilango, baadhi ya wagombea wamekuwa wakifanya kampeni zisizo za kistaarabu kwa kuandaa vijana aliodai wamepewa pombe ili wamzomee katika baadhi ya maeneo aliyopita.

No comments:

Post a Comment