Tuesday, August 4

Chadema yamweka pembeni Dk Slaa



Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe
akihutubia wajumbe wa Baraza Kuu la chama hicho 
alipokuwa akifungua kikao chao Dar es Salaam jana. 


Dar es Salaam. Baraza Kuu la Chadema limeridhia Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa apumzike wakati chama hicho kikiendelea na mchakato wa Uchaguzi Mkuu baada ya kiongozi huyo kutofautiana nao katika uamuzi wa kumkaribisha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.

Baraza hilo jana lilipiga kura ya wazi huku likishauri kuwa endapo atafikiria kubadili uamuzi wake, atarejea kuendeleza safari ya chama hicho kuelekea Ikulu chini ya mwavuli wa Ukawa.
Uamuzi huo ulifikiwa jana wakati wa kikao cha Baraza Kuu kilichofanyika hapa baada ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kueleza tofauti iliyojitokeza mwishoni mwa mchakato wa kumpokea Lowassa baina ya Dk Slaa na Kamati Kuu kiasi cha kumfanya Katibu Mkuu huyo kutohudhuria baadhi ya shughuli muhimu za chama.
Mbowe alisema Kamati Kuu ilifanya vikao kadhaa kutafakari ujio wa Lowassa na mashauriano ya muda mrefu ambayo hayakuwa rahisi kufikia uamuzi wa pamoja.
“Tulifanya mashauriano yaliyoambatana na hali ya kitafiti na tukaridhika pasipo shaka kwamba ujio wa Lowassa na wenzake katika chama hiki ni mpango wa Mungu ambao tunatakiwa tuunge mkono, utusadie kuwaunganisha wenzetu wa CUF, NLD na NCCR-Mageuzi na Watanzania wote kufikia malengo ya pamoja,” alisema.
“Katika hatua zote hizo tulikuwa sambamba na Dk Slaa lakini katika dakika za mwisho akatofautina kidogo na Kamati Kuu.”
Maelezo hayo ya Mbowe yanamaliza sintofahamu iliyokuwa imetanda kwa makada wa Chadema juu ya sababu za Dk Slaa kutoonekana kwenye hafla ya kumpokea Lowassa Julai 28, wakati wa kuchukua fomu za kugombea urais Julai 30, siku aliporudisha fomu Agosti Mosi na kwenye vikao vya Sekretarieti na Kamati Kuu juzi.
Mbowe ambaye pia ni Kiongoni wa Upinzani Bungeni alisema: “Kwa hiyo tumekubaliana na Katibu Mkuu apumzike kwa muda na nina hakika kwa tabia na hulka za Dk Slaa… kwa sababu anajua tunampenda na yeye anakipenda chama hiki, tunamwombea kwa Mungu ampe nguvu na ujasiri wa kuona kwamba kauli ya wengi ni kauli ya Mungu.
“Tutaendelea kuongea naye, bado nafasi yake ipo na kwa wengine wote wenye hofu ya aina hii na naomba niseme kuwa nafasi zetu za kiuongozi au kiuchaguzi ni dhamana, hakuna yeyote mwenye hatimiliki na nafasi mliyonayo ni kwa sababu ya watu, tukielewa hivyo wala hatuna ugomvi.”
Huku akizungumza kwa hisia, Mbowe alisema kauli yake ni uamuzi wa vikao vya chama na kwamba hakuna ugomvi wowote na kiongozi huyo, hivyo makada na Watanzania waachane na uzushi wa mitandaoni akisema hofu kama ya Dk Slaa ipo pia kwa makada wengine na kwamba ilikuwa na mashiko na inayozungumzika, lakini wasingezuia matakwa safari ya mamilioni kwa “sababu ya matakwa ya Mbowe au Slaa... tunasema lazima tuendelee kwa sababu uchaguzi upo kesho.”
Katika hotuba hiyo ya dakika 35, Mbowe alisema Dk Slaa ni kiongozi ambaye wanamheshimu, wanampenda na wataendelea kumpenda siku zote kwa sababu chama chao ni cha kujengana na siyo kubomoana.
Ili kupitisha uamuzi huo, Mbowe aliwahoji wajumbe wa baraza hilo iwapo wanataka waendelee na kazi au wasubiri ili kila mmoja afanye uamuzi wake binafsi na kujibiwa “tuendelee…”
Aliuliza swali hilo mara mbili na kuungwa mkono na wajumbe wote kwa sauti kubwa na alipowataka wajumbe wanaounga mkono uamuzi huo wasimame, walifanya hivyo na kuimba wimbo wa chama “Chadema, Chadema…people’s power.”
Alisema amezungumza suala hilo mbele ya wanahabari ili kama kuhukumiwa, ahukumiwe kwa sababu wajibu wake akiwa kiongozi ni kusema ukweli daima.
Aliwataka makada wa Chadema wawe na amani na kwamba chama hicho kipo salama na wanaofikiri kitameguka ni ndoto za mchana.
“Wengine wakasema Lissu (Tundu) huyoo, wakahamia Mnyika (John), Mnyika alikuwa mgonjwa, huyoo… mtasema na Slaa amesharudisha na gari mtakuta Jumatatu huyooo, lakini kwa leo amepumzika mzee wangu,” alisema Mbowe na kushangiliwa.
Mwenyekiti huyo aligusia moja ya ajenda ya mkutano wa Baraza Kuu kuwa ilikuwa ni kujadili ilani ya uchaguzi kabla ya kupitishwa leo na mkutano mkuu.
Baada ya mkutano huo, kuanzia kesho kwa siku tatu mfululizo chama hicho kitakuwa na vikao vya Kamati Kuu kuteua majina ya wabunge na wawakilishi watakaosimamishwa na chama hicho.
Hofu ya Lowassa
Akizungumzia hofu iliyotanda baada ya Lowassa kujiunga na chama hicho, Mbowe alisema kila jambo jema mara nyingi hujitokeza likiwa na changamoto.
Alisema baada ya kutambulishwa kwa Lowassa, hofu ilionekana kutanda ndani ya wajumbe wa Mkutano Mkuu na Baraza Kuu kwa kuhofia nafasi za uongozi na hatima ya chama hicho.
“Lakini inawezekana hofu hiyo wameipata zaidi CCM, kwa kipigo ambacho wamekipata hakijawahi kutokea katika historia ya siasa nchini, hali hii inataka kufanana na kuondoka kwa Augustino Mrema lakini naweza kuilinganisha nguvu ile kwa asilimia 25 tu na nafasi ya kuondoka Lowassa.”
Kuhusu madai ya kupokea mafisadi ndani ya chama, Mbowe alisema katika mazingira yoyote kwa mwanasiasa anayetafuta mbadala wa chama, lazima atakifikiria Chadema kwa sababu ni chama kilichojijengea msingi.
Alisema ilikuwa ni lazima kwa chama kuweka mkakati wa kumpokea mwanasiasa yeyote atakayekuwa tayari kuingia.
“Kwa mpango huohuo wa Mungu, leo yamejitokeza makundi yameingia ndani ya chama na miongoni mwao aliyekuwa anawika sana ni Lowassa... sasa katika siasa kuna kitu kinaitwa ‘game change’, yaani kwamba siasa zinaelekea mrengo huu halafu ghafla zinageuka na kuelekea mrengo mwingine, hiyo ndiyo ‘dynamism’ ya siasa.
“Hatuwezi kufunga milango ya chama kwa kuhofia nafasi zetu za uongozi, eti nafasi ya mwenyekiti, udiwani itachukuliwa...je, tutakuwa tunajenga chama?
“Hali hiyo ndiyo imekuwa sababu vyama vingi vilijisahau na kuendekeza masilahi binafsi wakasahau masilahi mapana ya chama. Kila mwanachama anaheshimika katika nafasi yake ndani ya chama. Kwa hivyo fursa iliyojitokeza usipoitumia utakuwa ni mwendawazimu.”
Mwalimu abeba mikoba ya Dk Slaa
Chama hicho kimemkaimisha Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu nafasi ya Dk Slaa na papo hapo, Mwalimu aliwaeleza wajumbe kuwa hotuba maalumu ya Katibu Mkuu itatolewa leo wakati wa mkutano mkuu.
“Lazima mjue tunakwenda kuwa chama tawala, hivyo hakuna kiongozi mdogo wala hakuna mwanachama aliye mdogo ndani ya chama hiki, kila mwanachama mmoja atakuwa na thamani, hivyo mjilinde msije kunufaisha maadui zetu,” alisema Mwalimu.
Msindai atua Chadema
Mwenyekiti wa wenyeviti wa CCM, Mgana Msindai jana alijiunga na Chadema na kutambulishwa katika mkutano wa Baraza Kuu la chama hicho.
Mgana, ambaye aliwahi kuwa mbunge wa Iramba Mashariki (2000-2010) alitambulishwa pamoja na Mbunge wa Arumeru Magharibi (CCM), Goodluck Ole Medeye na ofisa mwandamizi wa chama hicho, Matson Chizii.
Makada hao wa CCM jana usiku waliambatana katika kikao hicho na aliyewahi kuwa waziri mkuu Edward Lowassa. Habari zinasema kuna makada zaidi wa CCM wakaotambulisha katika mkutano mkuu wa Chadema leo.

Rushwa barabarani yamtia kichefuchefu JK


Rais Jakaya Kikwete akihutubia 
wakati wa hafla ya uzinduzi wa Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani 
iliyofanyika kwenye Viwanja vya Tangamano 
mjini Tanga jana. 

Tanga. Rais Jakaya Kikwete amekiagiza Kikosi cha Usalama Barabarani kufanya mabadiliko ya teknolojia katika utendaji wake ili kuondoa mianya ya rushwa.
Alitoa agizo hilo jana wakati akizindua Wiki ya Nenda kwa Usalama inayofanyika kitaifa jijiji hapa kwenye Uwanja wa Tangamano.
Alisema miongoni mwa mambo yanayochangia ajali ni kukosekana kwa tekonolojia ya kisasa kudhibiti mwendo kasi wa vyombo vya moto, hivyo kutoa mianya kwa baadhi ya trafiki wasio waaminifu kudai rushwa kutoka kwa madereva wanaowakamata kwa makosa mbalimbali.
“Vikiwekwa vidhibiti mwendo kwenye barabara zote kuu, dereva atakayeendesha gari lake kwa kasi namba zinaonekana kwenye kompyuta, hapo tena hakutakuwa na mazungumzo baina ya dereva na askari,” alisema Kikwete.
Pia, Rais Kikwete aliliagiza
Baraza la Usalama Barabarani kurekebisha baadhi ya sheria zilizopitwa na wakati ili kuongeza ufanisi.
“Baraza liende na wakati, sheria pia ziende na wakati, kadhalika askari. Tukifanya hivyo, tutapunguza ajali za barabarani,” alisema.
Agizo jingine alilotoa kwa baraza hilo ni kudhibiti vyanzo vya ajali kwa kuweka alama kwenye leseni za madereva wanaosababisha ajali, kukomesha rushwa na kutoa elimu ya usalama barabarani.
Rais Kikwete alisema asilimia 99 ya vifo vinatokana na uzembe na madereva kutofuata sheria za barabarani.
“Madereza wanaendesha kwa kasi bila sababu, wanayapita magari mengine bila kuchukua tahadhari, madereva wa pikipiki wanabeba abiria kwa staili ya mshkaki na magari mabovu yako mengi barabarani,” alisema.
Mwenyekiti wa baraza hilo, Pereira Ame Silima, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani alisema takwimu zinaonyesha kati ya mwaka 2010/14, watu 19,264 wamepoteza maisha kutokana na ajali za barabarani.
Alisema kuanzia Januari hadi Juni mwaka mwaka huu, watu 1,747 wamepoteza maisha, ambapo kati ya vifo hivyo, 1,352 vilitokana na ajali za pikipiki pekee yake.

Peter Kisumo afariki dunia


Moshi. Muasisi wa Tanu na baadaye CCM, Mzee Peter Kisumo (pichani) amefariki dunia.
Mwanasiasa huyo mkongwe nchini ambaye aliwahi kushika nyadhifa kadhaa katika Serikali ya Awamu ya Kwanza, alifariki Dunia jana saa moja usiku katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Mtoto wa marehemu, Michael Kisumo alilithibitishia gazeti hili jana juu ya kifo cha baba yake akisema kilitokana na maradhi ya figo ambayo yamekuwa yakimsumbua kwa muda mrefu.
“Tulikuja hapa Muhimbili kwa ajili ya mzee kufanyiwa dialysis (usafishaji damu katika figo) sasa ikajitokeza complication (utata) akaanza kuharisha damu,” alisema.
Michael alisema baba yake alilazwa wodi ya kawaida juzi ili jana apatiwe tiba hiyo kabla ya hali yake kubadilika ghafla.
“Daktari wake alipokuja leo (jana) na kumwangalia aliagiza atolewe wodi ya kawaida ahamishiwe ICU lakini ilipofika saa moja usiku akatutoka” alisema Michael.
Kifo cha mwanasiasa huyo kimekuja takribani mwezi mmoja tangu arejee kutoka India ambako amekuwa akienda mara kwa mara kuchunguzwa afya yake.
Hali ya ugonjwa wake huo ilifikia katika kiwango cha juu na kulazimika kufanyiwa uchujaji wa figo mara tatu kwa wiki kila Jumatatu, Jumatano na Ijumaa.
Kisumo aliwahi kuwa mmoja wa mameneja wa kampeni wa Rais Jakaya Kikwete mwaka 2005 akisimamia kanda ya kaskazini iliyojumuisha mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Tanga.
Mbali ya kuwa waziri, aliwahi pia kuwa mkuu wa mkoa na mdhamini wa CCM.

Panga la urais CCM kuhamia kwa wabunge


Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM), kimesema kitatumia ‘panga’ lilelile lililotumika kumpata mgombea wake wa urais katika kuchuja wagombea ubunge na udiwani kupitia vikao vyake halali ili kupata wagombea safi.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnaye alisema hayo jana Dar es Salaam katika mkutano na waandishi wa habari, kuzungumzia mchakato wa vikao vya kamati za chama hicho ili kupata wagombea wa ubunge, uwakilishi na udiwani baada ya mchakato wa kura za maoni kukamilika.
Alisema mchakato huo utaanza kwa kikao cha Kamati Maalumu ya CCM Agosti 6 na 7 kuchuja na kupitisha wagombea ubunge na uwakilishi. Agosti 8 na 9, Sekretarieti itakutana ikifuatiwa na Kamati Kuu pia kwa siku mbili kabla ya Halmashauri Kuu kukutana Agosti 12 na 13 kuteua wagombea ubunge na uwakilishi.
“Kura za maoni siyo mwisho wa safari, ni hatua ya kwanza ya kuona ni nani anayekubalika… siyo kibali cha kupeperusha bendera ya CCM, kama kuna upungufu vikao vitachukua hatua. Kura ya maoni si kigezo… kama wamecheza rafu au kutumia rushwa, hata kama wameshinda kwa kura nyingi, ikithibitika wanaweza kuondolewa,” alisema Nape na kuongeza:
“Tutafanya kama ilivyokuwa kwa wagombea urais, kama maadili hayakufuatwa wanaweza kuondolewa siyo tu wa kwanza, hata wanne, hata kufuta matokeo. Tutachukua hatua kwenye ubunge, tutachukua hatua kwenye udiwani kwa wale watakaojihusisha na rushwa. Hawatapata nafasi ya uteuzi kwenye chama chetu. Hatuna muda wa kuanza kuosha watu na madodoki.”
Alikumbusha jinsi chama hicho kilivyomteua Dk Khamis Kigwangallah kuwania ubunge wa Nzega alikoteuliwa licha ya kushika nafasi ya tatu katika kura ya maoni.
 Changamoto kura za maoni
Kuhusu changamoto kwenye upigaji kura za maoni ikiwamo vitendo vya rushwa, Nape alisema kwa takwimu walizonazo, changamoto zilizojitokeza ni kidogo ikilinganishwa na miaka ya nyuma... “Hii ni kwa sababu tumeboresha utaratibu tofauti na huko nyuma. Maeneo mengi yamemaliza na hata yale ambayo yamekuwa na kasoro za hapa na pale tumezitatua.
“…Kura za maoni katika chama chetu zimetoa demokrasia na bila shaka tumefundisha vyama vingine. Vyama vingi vinatoa wagombea mfukoni, lakini sisi tunawapeleka kwa wanachama wanapigiwa kura,” alisema Nape.
 Vigogo kuanguka
Alisema kuwa kutokana na kukua kwa demokrasia katika chama hicho na kujenga mfumo mzuri zaidi wa upigaji kura za maoni, hata vigogo wasiofanya vizuri wameanguka katika kura za maoni.
Kauli hiyo ya Nape imekuja huku kukiwa na ripoti ya baadhi ya mawaziri na wabunge wanaomaliza muda wao kuanguka katika kura za maoni.
Vigogo kuhama CCM
Alipoulizwa kuhusu kuhama chama hicho kwa waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa na Mbunge wa Segerea, Dk Makongoro Mahanga na wanaCCM wengine, Nape alisema siyo jambo la ajabu na kwamba si wa kwanza na wala hawatakuwa wa mwisho. “Wapo wanaotoka CCM kwenda vyama vingine na wapo wanaotoka vyama vingine na kuja CCM. Lakini niseme tu kwamba wapo ambao wanataka uongozi na wapo ambao wanataka kwenda kuongoza watu:
“Anayetaka kuongoza watu ni mvumilivu, mtulivu na hufuata taratibu. Lakini wapo ambao lengo siyo kwenda kuongoza watu, lengo ni masilahi binafsi. Wakikosa uongozi huonyesha tabia zao waziwazi.”

Mtikila aandaa makabrasha ya kumburuza Lowasa, Magufuli kortini


MWENYEKITI wa Chama cha Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, amesema chama chake kinaandaa taratibu za kwenda

mahakamani ili kumshtaki mgombea urais mteule wa CCM, Dkt. John Magufuli na mgombea urais wa CHADEMA, Bw. Edward Lowassa.

Alisema wagombea hao kwa nyakati tofauti, wameshiriki kuiingizia Serikali hasara ya mabilioni ya fedha ambapo wanasheria wa chama hicho wapo katika hatua za mwisho ili wafunguliwe mashtaka mahakamani.

Mchungaji Mtikila aliyasema hayo Dar es Salaam jana, alipozungumza na waandishi wa habari akisisitiza kuwa, wagombea hao wamepoteza sifa za kuwania nafasi hiyo akidai hawana vigezo kwa mujibu wa sheria.

Aliongeza kuwa, Bw. Lowassa, anahusishwa na sakata la kampuni ya kufua umeme ya Richmond na kuishangaa CHADEMA akidai chama hicho kilipata umaarufu wa kupinga vitendo vya ufisadi lakini wamempokea Bw. Lowassa na ana tuhuma kama hiyo.

"Kipindi cha nyuma, CHADEMA walianzisha operesheni nyingi ikiwemo ya Sangara na Movement for Change zikiwa na lengo la kupinga ufisadi, kwanini wamempokea Lowassa waliyemuita fisadi.
"Hii ina maana kuwa, ndani ya CHADEMA hakuna siasa, nawapongeza baadhi ya viongozi wa chama hicho na wanachama wao ambao kimsingi hawakubaliani na matakwa ya viongozi wa juu," 
Akimzungumzia Dkt. Magufuli, alimhusisha na tuhuma ya uuzwaji wa nyumba za Serikali akidai kitendo hicho kimeisababishia hasara Serikali lakini hakupelekwa mahakamani kwa kutumia madaraka yake vibaya kama ilivyokuwa kwa Basil Mramba, Daniel Yona ambao hivi sasa wanatumikia kifungo gerezani.

Alisema nyumba hizo zilikuwa makazi ya viongozi kama Majaji, Makatibu Wakuu na Watendaji waandamizi serikalini ambao wengi wao walilazimika kuishi hotelini kwa gharama za Serikali.