Tuesday, August 4

Chadema yamweka pembeni Dk Slaa



Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe
akihutubia wajumbe wa Baraza Kuu la chama hicho 
alipokuwa akifungua kikao chao Dar es Salaam jana. 


Dar es Salaam. Baraza Kuu la Chadema limeridhia Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa apumzike wakati chama hicho kikiendelea na mchakato wa Uchaguzi Mkuu baada ya kiongozi huyo kutofautiana nao katika uamuzi wa kumkaribisha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.

Baraza hilo jana lilipiga kura ya wazi huku likishauri kuwa endapo atafikiria kubadili uamuzi wake, atarejea kuendeleza safari ya chama hicho kuelekea Ikulu chini ya mwavuli wa Ukawa.
Uamuzi huo ulifikiwa jana wakati wa kikao cha Baraza Kuu kilichofanyika hapa baada ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kueleza tofauti iliyojitokeza mwishoni mwa mchakato wa kumpokea Lowassa baina ya Dk Slaa na Kamati Kuu kiasi cha kumfanya Katibu Mkuu huyo kutohudhuria baadhi ya shughuli muhimu za chama.
Mbowe alisema Kamati Kuu ilifanya vikao kadhaa kutafakari ujio wa Lowassa na mashauriano ya muda mrefu ambayo hayakuwa rahisi kufikia uamuzi wa pamoja.
“Tulifanya mashauriano yaliyoambatana na hali ya kitafiti na tukaridhika pasipo shaka kwamba ujio wa Lowassa na wenzake katika chama hiki ni mpango wa Mungu ambao tunatakiwa tuunge mkono, utusadie kuwaunganisha wenzetu wa CUF, NLD na NCCR-Mageuzi na Watanzania wote kufikia malengo ya pamoja,” alisema.
“Katika hatua zote hizo tulikuwa sambamba na Dk Slaa lakini katika dakika za mwisho akatofautina kidogo na Kamati Kuu.”
Maelezo hayo ya Mbowe yanamaliza sintofahamu iliyokuwa imetanda kwa makada wa Chadema juu ya sababu za Dk Slaa kutoonekana kwenye hafla ya kumpokea Lowassa Julai 28, wakati wa kuchukua fomu za kugombea urais Julai 30, siku aliporudisha fomu Agosti Mosi na kwenye vikao vya Sekretarieti na Kamati Kuu juzi.
Mbowe ambaye pia ni Kiongoni wa Upinzani Bungeni alisema: “Kwa hiyo tumekubaliana na Katibu Mkuu apumzike kwa muda na nina hakika kwa tabia na hulka za Dk Slaa… kwa sababu anajua tunampenda na yeye anakipenda chama hiki, tunamwombea kwa Mungu ampe nguvu na ujasiri wa kuona kwamba kauli ya wengi ni kauli ya Mungu.
“Tutaendelea kuongea naye, bado nafasi yake ipo na kwa wengine wote wenye hofu ya aina hii na naomba niseme kuwa nafasi zetu za kiuongozi au kiuchaguzi ni dhamana, hakuna yeyote mwenye hatimiliki na nafasi mliyonayo ni kwa sababu ya watu, tukielewa hivyo wala hatuna ugomvi.”
Huku akizungumza kwa hisia, Mbowe alisema kauli yake ni uamuzi wa vikao vya chama na kwamba hakuna ugomvi wowote na kiongozi huyo, hivyo makada na Watanzania waachane na uzushi wa mitandaoni akisema hofu kama ya Dk Slaa ipo pia kwa makada wengine na kwamba ilikuwa na mashiko na inayozungumzika, lakini wasingezuia matakwa safari ya mamilioni kwa “sababu ya matakwa ya Mbowe au Slaa... tunasema lazima tuendelee kwa sababu uchaguzi upo kesho.”
Katika hotuba hiyo ya dakika 35, Mbowe alisema Dk Slaa ni kiongozi ambaye wanamheshimu, wanampenda na wataendelea kumpenda siku zote kwa sababu chama chao ni cha kujengana na siyo kubomoana.
Ili kupitisha uamuzi huo, Mbowe aliwahoji wajumbe wa baraza hilo iwapo wanataka waendelee na kazi au wasubiri ili kila mmoja afanye uamuzi wake binafsi na kujibiwa “tuendelee…”
Aliuliza swali hilo mara mbili na kuungwa mkono na wajumbe wote kwa sauti kubwa na alipowataka wajumbe wanaounga mkono uamuzi huo wasimame, walifanya hivyo na kuimba wimbo wa chama “Chadema, Chadema…people’s power.”
Alisema amezungumza suala hilo mbele ya wanahabari ili kama kuhukumiwa, ahukumiwe kwa sababu wajibu wake akiwa kiongozi ni kusema ukweli daima.
Aliwataka makada wa Chadema wawe na amani na kwamba chama hicho kipo salama na wanaofikiri kitameguka ni ndoto za mchana.
“Wengine wakasema Lissu (Tundu) huyoo, wakahamia Mnyika (John), Mnyika alikuwa mgonjwa, huyoo… mtasema na Slaa amesharudisha na gari mtakuta Jumatatu huyooo, lakini kwa leo amepumzika mzee wangu,” alisema Mbowe na kushangiliwa.
Mwenyekiti huyo aligusia moja ya ajenda ya mkutano wa Baraza Kuu kuwa ilikuwa ni kujadili ilani ya uchaguzi kabla ya kupitishwa leo na mkutano mkuu.
Baada ya mkutano huo, kuanzia kesho kwa siku tatu mfululizo chama hicho kitakuwa na vikao vya Kamati Kuu kuteua majina ya wabunge na wawakilishi watakaosimamishwa na chama hicho.
Hofu ya Lowassa
Akizungumzia hofu iliyotanda baada ya Lowassa kujiunga na chama hicho, Mbowe alisema kila jambo jema mara nyingi hujitokeza likiwa na changamoto.
Alisema baada ya kutambulishwa kwa Lowassa, hofu ilionekana kutanda ndani ya wajumbe wa Mkutano Mkuu na Baraza Kuu kwa kuhofia nafasi za uongozi na hatima ya chama hicho.
“Lakini inawezekana hofu hiyo wameipata zaidi CCM, kwa kipigo ambacho wamekipata hakijawahi kutokea katika historia ya siasa nchini, hali hii inataka kufanana na kuondoka kwa Augustino Mrema lakini naweza kuilinganisha nguvu ile kwa asilimia 25 tu na nafasi ya kuondoka Lowassa.”
Kuhusu madai ya kupokea mafisadi ndani ya chama, Mbowe alisema katika mazingira yoyote kwa mwanasiasa anayetafuta mbadala wa chama, lazima atakifikiria Chadema kwa sababu ni chama kilichojijengea msingi.
Alisema ilikuwa ni lazima kwa chama kuweka mkakati wa kumpokea mwanasiasa yeyote atakayekuwa tayari kuingia.
“Kwa mpango huohuo wa Mungu, leo yamejitokeza makundi yameingia ndani ya chama na miongoni mwao aliyekuwa anawika sana ni Lowassa... sasa katika siasa kuna kitu kinaitwa ‘game change’, yaani kwamba siasa zinaelekea mrengo huu halafu ghafla zinageuka na kuelekea mrengo mwingine, hiyo ndiyo ‘dynamism’ ya siasa.
“Hatuwezi kufunga milango ya chama kwa kuhofia nafasi zetu za uongozi, eti nafasi ya mwenyekiti, udiwani itachukuliwa...je, tutakuwa tunajenga chama?
“Hali hiyo ndiyo imekuwa sababu vyama vingi vilijisahau na kuendekeza masilahi binafsi wakasahau masilahi mapana ya chama. Kila mwanachama anaheshimika katika nafasi yake ndani ya chama. Kwa hivyo fursa iliyojitokeza usipoitumia utakuwa ni mwendawazimu.”
Mwalimu abeba mikoba ya Dk Slaa
Chama hicho kimemkaimisha Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu nafasi ya Dk Slaa na papo hapo, Mwalimu aliwaeleza wajumbe kuwa hotuba maalumu ya Katibu Mkuu itatolewa leo wakati wa mkutano mkuu.
“Lazima mjue tunakwenda kuwa chama tawala, hivyo hakuna kiongozi mdogo wala hakuna mwanachama aliye mdogo ndani ya chama hiki, kila mwanachama mmoja atakuwa na thamani, hivyo mjilinde msije kunufaisha maadui zetu,” alisema Mwalimu.
Msindai atua Chadema
Mwenyekiti wa wenyeviti wa CCM, Mgana Msindai jana alijiunga na Chadema na kutambulishwa katika mkutano wa Baraza Kuu la chama hicho.
Mgana, ambaye aliwahi kuwa mbunge wa Iramba Mashariki (2000-2010) alitambulishwa pamoja na Mbunge wa Arumeru Magharibi (CCM), Goodluck Ole Medeye na ofisa mwandamizi wa chama hicho, Matson Chizii.
Makada hao wa CCM jana usiku waliambatana katika kikao hicho na aliyewahi kuwa waziri mkuu Edward Lowassa. Habari zinasema kuna makada zaidi wa CCM wakaotambulisha katika mkutano mkuu wa Chadema leo.

No comments:

Post a Comment