T'shishimbi akisaini Yanga
Kiungo wa kimataifa wa DR Congo ametua Jangwani na kusaini mkataba wa miaka miwili jambo ambalo limeshusha presha ya mashabiki wa timu hiyo
Klabu ya Yanga leo imempokea kiungo Papy Kabamba Tshishimbi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), na kumsainisha mkataba wa miaka miwili kuichezea timu hiyo.
Katibu Mkuu wa Yanga Boniface  Mkwasa, amesema, kutua kwa mchezaji huyo kunawapa uhakika  wa kukiimarisha kikosi chao katika nafasi ya ulinzi ambayo imewasumbua kwa muda mrefu ambapo ni zaidi ya misimu mitatu.
“Nikweli T’shishimbi, tumemaliziana naye na hivi ninavyokwambia tayari tumempeleka Zanzibar, kwa ajili ya kujiunga na wenzake,”amesema Mkwasa.
Katibu huyo amesema wanafurahi kukamilisha usajili wa mchezaji huyo na kwasasa wanachokiangalia ni kukiandaa kikosi chao kwa ajili ya kufanya vizuri kwenye mechi za ligi.
Amesema mipango yao ni kuhakikisha wanatetea ubingwa wao wa ligi ya Vodacom na kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa na hilo linawezekana kutoka na ubora wa kikosi walichokuwa nacho.
“Tumesajili vizuri hata kama hatukucheza vizuri kwenye mechi za kirafiki, lakini huo ulikuwa mwanzo, mwalimu wetu George Lwandamina, alikuwa bado anajenga timu ,”amesema Mkwasa.
Kiongozi huyo amesema wanatarajia kumtua T’shishimbi, kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba, ambao utapigwa wiki Ijayo uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Baada ya T’shishimbi Yanga imebakisha nafasi moja ya mchezaji wa kimataifa na kwasasa inamfanyia majaribio beki na kiungo raia wa Nigeria ambaye tayari ameshacheza mechi moja na kuonyesha uwezo mkubwa uliowavutia makocha wa timu hiyo.