China imesema itasitisha mpango wa kununua makaa ya mawe, chuma na chakula cha baharini kutoka Korea Kaskazini.
Hatua hiyo ni ya utekelezaji wa vikwazo vya Umoja wa Mataifa vilivyowekwa kutokana na hatua ya Korea kaskazini kufanyia majaribio makombora yake mawili ya masafa marefu mwezi uliopita.
China inanunua asilimia 90 ya biashara yote ya Korea kaskazini.
Beijing ilikuwa imeahidi kuweka vikwazo hivyo baada ya Marekani kuishutumu kwa kutoishinikiza Korea Kaskazini kusitisha mpango wake wa kutengeza silaha.
Umoja wa Mataifa uliidhinisha vikwazo dhidi ya Pyongyang mapema mwezi huu ambavyo vinaweza kuligharimu taifa hilo mapato ya dola bilioni 1 kwa mwaka kulingana na takwimu zilizotolewa na ujumbe wa Marekani kwa baraza la usalama la umoja wa mataifa.
Ijapokuwa uagizaji wa makaa kutoka Korea kaskazini ulilipatia taifa hilo dola bilioni 1.2 mwaka uliopita,takwimu hizo zitashuka mwaka huu kwasababu China tayari ilikuwa imeiwekea vikwazo nchi hiyo tangu mwezi Februari, kulingana na wataalam.
''China tayari ishanunua makaa yake ya mawe ya kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka chini ya vikwazo vya 2017.Hivyobasi hakutakuwa na athari zozote nchini humo , huku Korea Kaskazini ikiwa inauza kiwango kidogo cha makaa yake ya mawe kwa mataifa mengine'', alisema David Von Hippel kutoka kwa taasisi ya Nautilus kundi la wataalam wanaofanya utafiti katika sekta ya makaa ya mawe Korea kaskazini.
No comments:
Post a Comment