Rais wa Tanzania John Magufuli amefichua kuwa anapokea mshahara wa shilingi milioni 9 za Kitanzania kwa mwezi, sawa na dola 4000, hivyo kumfanya miongoni mwa viongozi wachache wa Afrika wanaopokea mishahara midogo.
Rais Magufuli yuko katika harakati za kufanikisha sera ambayo imeshutumiwa vikali ya kupunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya fedha za umma. Katika hotuba aliyoitoa mjini Dar Es Salam siku ya Jumanne wiki hii, Kiongozi huyo wa Tanzania alisema serikali imepunguza mishahara ya maafisa wakuu watendaji wa mashirika ya serikali hadi shilingi milioni 15 ambazo ni sawa na dola 6,700 kiasi ambacho ni cha juu kuliko mshahara wake.
Magufuli alisema kama wanahisi kiwango hicho cha fedha ni kidogo, wana uhuru wa kuziacha kazi zao akiongeza kuwa matumizi mabaya ya fedha za umma yamekithiri katika mashirika ya serikali na amekataa maombi kutoka kwa baadhi ya maafisa kuongeza marupurupu yao akihoji hawezi kuongeza mishahara ya watumishi wa umma wakati raia wa kawaida hawana huduma za maji, afya na umeme.
Tangu kuchukua madaraka mwezi Novemba mwaka 2015, Magufuli ajulikanaye kwa jina maarufu la Tinga Tinga, amepunguza matumizi ya serikali kwa kuchukua hatua kadhaa kama kudhibiti safari za nje za maafisa wa serikali, kuondolewa kwa wafanyakazi hewa kutoka kwa utumishi wa umma.
Zuma apokea Dola za Kimarekani 20,000
Baadhi ya wakosoaji wake wanamshutumu kuwa baadhi ya hatua zake zimevuka mipaka wakihoji zitaathiri ukuaji wa kiuchumi wa taifa hilo la pili kwa nguvu za kiuchumi katika kanda ya Afrika Mashariki na baadhi ya maamuzi yake yanaoekana kurudisha nyuma uwekezaji katika sekta muhimu kama madini.
Mshahara wa Magufuli ukilinganishwa na wa viongozi wengine wa Afrika ni mdogo mno. Kiongozi huyo wa Tanzania hana vyanzo vingine vya kujipatia kipato vinavyojulikana na serikali yake mwaka jana ilisema ina mipango ya kuwasilisha mswada bungeni utakaowazuia viongozii wa umma kujishughulisha na biashara ili kuepusha mgongano wa maslahi.
Rais wa nchi jirani ya Kenya Uhuru Kenyatta anapokea mshahara wa takriban dola 14,000 kwa mwezi, Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma analipwa mshahara wa dola 20,000 kwa mwezi kufuatia bunge mwaka 2015 kuidhinisha nyongeza ya mshahara wa rais.
Kiongozi mwingine wa Afrika ambaye ana mshahara wa wastani ni Rais wa Nigeria Muhamadu Buhari ambaye alikubali mshahara wake upunguzwe kwa asilimia 50 alipoingia madarakani mwezi Mei mwaka 2015. Awali mshahara wa Rais wa Nigeria ulikuwa naira milioni 14.1 ambazo zilikuwa ni sawa na dola 70,000 wakati huo.