Tuesday, November 21

UHAMIAJI YAFUNGA ‘MITAMBO’ YA UTAMBUZI KATIKA UWANJA WA NDEGE WA KIMATAIFA WA MWALIMU JULIUS NYERERE

Idara ya Uhamiaji katika Kituo cha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) imefunga Vifaa vyenye mfumo mpya wa utambuzi na ulinganisho wa sura (Facial Recognition and Matching System) kwa abiria wanaoingia nchini.

Akiongea baada ya kupokea vifaa hivyo, Kamishna wa Uhamiaji anayesimamia Divisheni ya Usimamizi na Udhibiti wa Mipaka Samwel Rhobby Magweiga, amesema kuwa huo ni muendelezo wa mikakati ya Idara katika kuimarisha na kuhuisha KANZIDATA ya wanaoingia nchini.

“Vifaa na mfumo huu utasaidia sana katika kukusanya taarifa za abiria wote wanaoingia nchini kupitia hapa (JNIA), kama mlivyofahamishwa, mfumo huu unachukua sura ya mtu na kulinganisha na sura nyingine zilizomo kwenye kanzidata ili kuhakikisha taarifa zilizo kwenye pasipoti yake ni za pekee na hakuna mtu mwenye sura kama yake au mtu mwenye sura ingine kuwa na taarifa kama zake.”Alieleza Kamishna Samwel Magweiga.

Awali wakati akabidhiana vifaa hivyo, Mwakilishi mkazi wa Shirika la Uhamiaji la Kimataifa (IOM) Dr. Qasim Sufi alisema kwamba IOM itashirikiana na Idara ya Uhamiaji katika suala zima la udhibiti wa uingiaji na utokaji wa raia na wageni.

Idara ya Uhamiaji kwa kushirikiana na shirika hilo, wamefunga vifaa vingine vyenye mfumo huo kwenye vituo vya Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA) pamoja na mpaka wa Holili kwa pande zote mbili za Tanzania na Kenya.

Kupitia ushirikiano huo na IOM, Idara ya Uhamiaji itaendelea kuimarisha maeneo yote ya mipaka kwa kufunga vifaa na mfumo huu wa kisasa zaidi kutumiwa hapa Afrika Mashariki.
Dr. Qasim Sufi Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji akifanyiwa majaribio katika mfumo wa utambuzi wa sura (Facial Recognition and matching system) katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es salaam
Kamishna wa Uhamiaji (Usimamizi na Udhibiti wa Mipaka) Samwl Magweiga (wa kwanza kulia) akisikiliza kwa makini namna mfumo huo unavyofanya kazi wakati wa ufungaji wa vifaa vyenye mfumo huo.
Kamishna wa Uhamiaji (Usimamizi na Udhibiti wa Mipaka) akikabidhiwa nyaraka za mfumo huo na Mwakilishi Mkazi wa IOM Dr. Qasim Sufi mara baada ya ufungaji wa vifaa hivyo.

CHUO CHA MAFUNZO YA KIJESHI MONDULI CHAZINDUA KOZI MPYA YA SAYANSI YA KIJESHI

Katibu Mkuu wa wizara ya ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa, Dokta Florens Turuka amesema kuwa jeshi hilo hivi sasa limejipanga katika kukabiliana na changamoto za ulinzi na usalama kwa
kuwapatia askari wake mafunzo maalumu ya sayansi ya kijeshi. 

Aliyasema hayo Jana wakati akizungumza katika uzinduzi wa shahada ya kwanza ya sayansi ya kijeshi inayotekelezwa na chuo cha uhasibu Arusha kwa kushirikiana na Chuo cha mafunzo ya kijeshi Monduli (TMA). 

Alisema kuwa, kumekuwepo na matishio mengi ambayo yamekuwa yakijitokeza Kwa namna tofauti ambapo hivi sasa matishio hayo yamegeuka na kuhamia kwenye mitandao, hivyo kama jeshi wana wajibu wa kujipanga zaidi kwa kuwaandaa maaskari ili waweze kukabiliana na hali hiyo mahali popote. 

Dokta Turuka alisema kuwa, wao Kama jeshi ni wajibu wao kujipanga mapema kwa kuangalia namna ya kuwajengea uwezo hasa katika maswala ya sayansi na teknolojia ili kuboresha ulinzi na usalama hapa nchini. 

Kwa upande wa Mkuu wa majeshi nchini, Jenerali Venance Mabeyo alisema kuwa wamekuwa wakitoa mafunzo hayo kwa maaskari wake kulingana na mabadiliko ya kidunia hasa katika maswala ya sayansi na teknolojia kwani ni eneo ambalo linahitaji elimu kubwa zaidi.  Alisema kuwa, ni lazima wasonge mbele na kwenda na wakati kwani wasipofanya hivyo watabaki nyuma na kamwe hawataweza kukabiliana na vitisho vilivyopo hivi sasa. 

Naye Mkuu wa chuo cha mafunzo ya kijeshi Monduli (TMA), Dokta Paul Massao alisema kuwa, wamekuwa wakitoa masomo ya kijeshi na kiraia ili kuwaandaa vijana katika hatua ya ngazi za juu zaidi kielimu ambapo kwa kuanzia kozi hiyo watahiniwa 158 wataanza kozi hiyo mapema. 

Kwa upande wa Kaimu mkuu wa chuo cha uhasibu Arusha, Dokta Faraji Kasidi alisema kuwa, mahusiano kati yao na chuo hicho cha kijeshi yameanza muda mrefu ambapo wao wamekuwa wakifundisha askari hao mafunzo ya kiraia ambayo yamekuwa yakileta manufaa makubwa Sana. 
Katibu Mkuu Wizara ya ulinzi na jeshi la kujenga Taifa Florens Turuka akisalimia na Mkuu wa Wilaya ya Monduli Iddy Kimanta mara baada ya kuwasili katika chuo cha mafunzo ya kijeshi Mondoli(TMA) kwa ajili ya uzinduzi wa shahada ya kwanza ya mafunzo ya Sayansi ya kijeshi
iliyofanyika chuoni hapo leo(Picha na Pamela Mollel Arusha)
Mkuu wa majeshi ya ulinzi na usalama Tanzania Jenerali Vanance Mabeyo akisalimiana na Kaimu Mkuu wa chuo cha uhasibu Arusha Dokt Faraji Kasidi, katikati ni Mkuu wa chuo cha mafunzo ya kijeshi Monduli (TMA), Dokta Paul Massao 
Katibu mkuu wizara ya ulinzi na jeshi la kujenga Taifa Florens Turuka akisalimia na Meja Jenerali Othman mara ya kuwasili katika chuo cha mafunzo ya kijeshi Mondoli(TMA) kwa ajili ya uzinduzi wa mafunzo ya shahada ya kwanza ya Sayansi ya kijeshi iliyofanyika chuoni hapo.
Katibu mkuu wizara ya ulinzi na jeshi la kujenga taifa Florens Turuka akisalimiana na Dr. Adolf B. Rutayuga ambaye ni kaimu mtendaji mkuu wa NACTE.
Katibu mkuu wizara ya ulinzi na jeshi la kujenga taifa Florens Turuka akizungumza katika uzinduzi wa uzinduzi wa shahada ya kwanza ya Sayansi ya kijeshi iliyofanyika chuoni hapo
Mkuu wa majeshi nchini, Jenerali Venance Mabeyo akitoa hotuba fupi katika halfa ya uzinduzi wa mafunzo ya shahada ya kwanza ya Sayansi ya kijeshi iliyofanyika chuoni hapo
Meja jenerali Paul Peter Masao ambaye ni mkuu wa chuo cha mafunzo ya maafisa wanafunzi jeshi la ulinzi la Tanzania(TMA).
Mwenyekiti wa Bodi ya chuo cha uhasibu Arusha Bi.Rukia Adam akisoma maelezo mafupi juu ya uzinduzi wa wafunzo ya shahada ya kwanza ya sayansi ya kijeshi inayotekelezwa na chuo cha uhasibu Arusha kwa kushirikiana na Chuo cha mafunzo ya kijeshi Monduli (TMA). 
Kaimu mkuu wa chuo cha uhasibu Arusha, Dokta Faraji Kasidi akizungumza katika uzinduzi huo ambapo alisema mahusiano kati yao na chuo hicho cha kijeshi yameanza muda mrefu ambapo wao wamekuwa wakifundisha askari hao mafunzo ya kiraia.
kushoto aliyevalia suti ni Profesa Johannes Monyoambaye aliwahi kuwa mkuu wa chuo cha uhasibu Arusha(IAA)
Wanafunzi wa mafunzo ya shahada ya kwanza ya Sayansi ya kijeshi iliyofanyika chuoni hapo leo
Maafisa wa jeshi wakitumbuiza wata wa uzinduzi wa wafunzo ya sayansi ya kijeshi.
Picha ya pamoja

NAIBU WAZIRI,KAMISHNA JENERALI WA UHAMIAJI WAZUNGUMZA NA WANANCHI

Naibu Waziri Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, akizungumza na wananchi wanaofanya shughuli zao katika Mpaka wa Tanzania na Kenya Sirari , wakati wa ziara ya kikazi aliombatana na Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Makakala(watatu kulia) na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa huo.Lengo la ziara hiyo ni kukagua shughuli mbalimbali zilizopo chini ya idara za wizara na kukagua mipaka iliyopo katika mkoa huo.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Makakala, akizungumza na wananchi wanaofanya shughuli zao katika Mpaka wa Tanzania na Kenya Sirari, wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima, akijibu baadhi ya hoja zilizoulizwa na wananchi wanaofanya shughuli zao katika Mpaka wa Tanzania na Kenya Sirari, wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (wapili kulia), akiambata na Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Makakala (kulia) 
Naibu Waziri Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji,Dkt. Anna Makakala(wapili kulia),Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima() na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Glorius Luoga(kulia), wakisikiliza maswali ya mmoja wa wananchi wanaofanya shughuli karibu na kituo cha Mpaka wa Tanzania na Kenya Sirari , wakati wa ziara ya kikazi yenye lengo la kukagua mipaka iliyopo ndani ya mkoa huo. 
Naibu Waziri Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji,Dkt. Anna Makakala( kulia) na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima(watatu kulia) wakisikiliza maswali ya mmoja wa wananchi wanaofanya shughuli karibu na kituo cha Mpaka Tanzanua na Kenya Sirari , wakati wa ziara ya kikazi yenye lengo la kukagua mipaka iliyopo ndani ya mkoa huo

Na Abubakari Akida-WMNN
NAIBU Waziri Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, amewataka wananchi na wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao karibu na Kituo cha Mpaka wa Sirari unaotenganisha nchi za Tanzania na Kenya kuhakikisha wanashirikiana na Jeshi la Polisi mkoani Mara kudhibiti matukio ya uhalifu kwa kutoa taarifa za wahalifu hao kwa jeshi hilo.

Hayo ameyasema akiongea na wananchi wakati wa ziara ya kikazi katika mkoa wa Mara, ikiwa na lengo la kutembelea mipaka iliyopo katika mkoa huo inayotenganisha nchi ya Tanzania na nchi jirani za Kenya na Uganda ambapo katika ziara hiyo aliongozana na Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dk. Anna Makakala, Kaimu Mkurugenzi Idara ya Uzalishaji Vitambulisho vya Taifa, Alphonce Malibiche na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama.

“Tumekuwa tukipata taarifa wananchi wa hapa kushirikiana na wahalifu katika kupitisha mali za magendo hapa hasa wakitumia vijana wanaoendesha bodaboda kupitisha mizigo yao na kuripotiwa matukio mbalimbali yanayohatarisha usalama wa raia wetu, natoa wito kwa wananchi wa hapa kushirkiana na jeshi la polisi kudhibiti matendo hayo ya kihalifu,” alisema Masauni

Aidha,Naibu Waziri Masauni amewataka wananchi hao kuacha mara moja tabia inayokua kwa kasi katika eneo hilo ya kulizuia Jeshi la Polisi kufanya shughuli zake na endapo atabainika mtu yoyote atakumbana na mkono wa sheria huku akitoa ushauri kwa jeshi kuzifanyia utafiti taarifa zitakazoletwa ili kuepuka kumuonea mtu.

Akizungumza na wananchi hao Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dk. Anna Makakala, amewataka wananchi hao kupeleka taarifa za wahamiaji haramu pindi watakapowagundua ili kuweza kudhibiti tatizo la wahamiaji hao kuingia nchini huku akiweka wazi viwango vya udhibiti vilivyoweka na idara yake kuzuia wahamiaji haramu kuingia nchini.

“Idara ya Uhamiaji kupitia wawakilishi wetu mkoani hapa tupo tayari na tunaomba mtu yoyote mwenye taarifa za wahamiaji haramu azifikishe kwenye ofisi ya uhamiaji nasi tutazifanyia kazi kwani tushapunguza tatizo hilo na tuko katika jitihada za kulimaliza kabisa,” alisema Dk. Makakala

Akizungumza kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taida (NIDA), Kaimu Mkurugenzi Idara ya Uzalishaji Vitambulisho vya Taifa, Alphonce Malibiche, alisema NIDA imezindua zoezi la usajili wa vitambulisho kwa wakazi wa Mkoa wa Mara na wanatarajia kumaliza zoezi hilo mapema ili wananchi wa Mkoa huo na wilaya zake wawe na vitambulisho vya Taifa vitakavyozuia baadhi ya changamoto lakini lengo kubwa ni kuhakikisha kila Mtanzania anakua na Kitambulisho cha Taifa.

UJENZI MAGOMENI KOTA KUKAMILIKA MACHI MWAKANI


Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Mhe. Elias Kwandikwa (katikati), akitoa maelekezo kwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Msanifu Majengo Elius Mwakalinga (kulia) wakati akikagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi eneo la Magomeni Kota jijini Dar es Salaam.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Msanifu Majengo Elius Mwakalinga (kulia) akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Mhe. Elias Kwandikwa (katikati), kuhusu hatua zilizofikiwa katika utelezaji wa mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi eneo la Magomeni Kota, wakati akikagua maendeleo ya ujenzi huo, jijini Dar es Salaam.
Muonekano wa mtambo wa kuchakata zege unaotumiwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), katika mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi eneo la Magomeni Kota, jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Mhe. Elias Kwandikwa, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani), mara baada ya kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi eneo la Magomeni Kota, jijini Dar es Salaam.
Muonekano wa baadhi ya vitalu vya makazi eneo la Magomeni Kota zinazojengwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 35.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Mhe. Elias Kwandikwa, akizungumza na menejimenti ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), wakati alipowatembelea wakala huo leo, jijini Dar es Salaam.
Meneja Rasilimali Watu kutoka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Bi. Gerwalda Luoga, akitoa neno la shukrani kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Mhe. Elias Kwandikwa (hayupo pichani) mara baada ya kikao kazi na Naibu Waziri huyo, jijini Dar es Salaam.


Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mheshimiwa Elias Kwandikwa (Mb), ameutaka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kufanya kazi kwa bidii katika miradi yote inayopewa na Serikali ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na ubora unaotakiwa.

Akikagua hatua zilizofikiwa katika mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi eneo la Magomeni kota, Naibu Waziri Kwandikwa, amesema kuwa Serikali itaendelea kuanisha miradi mingine ili kuhakikisha fedha za Serikali zinaokolewa na kusimamiwa kwa uzalendo.

“Hakikisheni mnafanya kazi zenu kwa weledi, uzalendo na kukamilisha miradi kwa wakati na kuokoa fedha ambazo zitatumika katika utekelezaji wa miradi mingine hapa nchini”, amesisitiza Mhe. Kwandikwa.

Ametoa wito kwa wataalamu wengine kuja kupata mafunzo kwa TBA ambao ni chachu ya utekelezaji wa miradi mingi hapa nchini kwa kuwa wanatumia mfumo wa kisayansi na mitambo yenye kusaidia kupunguza gharama za ujenzi.

Aidha, Naibu Waziri huyo ameushukuru uongozi wa TBA kwa kutoa ajira za vibarua takribani 200 kwa siku katika mradi huo na kuwataka wafanyakazi hao kuwa waadilifu na waaminifu ili kuwa na sifa za kupata ajira za kudumu.

Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Msanifu Majengo Elius Mwakalinga, amemhakikishia Naibu Waziri Kwandikwa kukamilika mradi huo kwa wakati, ubora na kwa gharama nafuu.

Amefafanua kuwa mradi huo utakuwa una jumla ya vitalu vitano ambapo vitalu vinne vina majengo ya ghorofa nane na kitalu kimoja kina jengo la ghorofa tisa na hivyo mradi utatoa makazi kwa kaya 656.

Mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi eneo la Magomeni Kota unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Machi mwakani na utagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 20 zote ikiwa ni fedha za Serikali.

Mufuruki aipa somo Serikali kuhusu Tanzania ya viwanda


Dar es Salaam. Mwenyekiti wa maofisa watendaji wakuu wa kampuni nchini (CEOrt), Ali Mufuruki ameishauri Serikali kushirikiana kikamilifu na wawekezaji binafsi ili dhana ya Tanzania ya viwanda iweze kufanikiwa.
Mufuruki aliyepata kuwa mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), alisema huko nyuma Serikali iliwahi kumiliki viwanda, lakini ikaja kuvibinafsisha kwa wawekezaji.
Aliyasema hayo juzi usiku katika hafla ya uzinduzi wa mwonekano mpya wa gazeti la The Citizen ambalo sasa litakuwa likiangazia zaidi masuala ya kibiashara.
Mufuruki alisema katika ubinafsishaji Serikali zilizopita hazikujikita kuwalea wawekezaji ziliowabinafsishia viwanda, hivyo wakajikuta wakipata matatizo ya uendeshaji kwa kuwa hawakupatiwa malezi mazuri ya uwekezaji.
Alisema kama Serikali inawakaribisha wawekezaji, lakini inashindwa kutoa ushirikiano siku uwekezaji ukiyumba inaweza kulaumiwa.
Alishangaa kuona wawekezaji wakati mwingine wakilaumiwa kwa viwanda hivyo kufa huku Serikali ikiwa haijafanya lolote kutoa sapoti kama kuongezewa mitaji.
Mufuruki aliitaka MCL inayozalisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti kutoogopa kuandika habari zinazozingatia maadili ya taaluma hiyo.
Mufuruki alisema The Citizen inayoonekana leo ni msingi uliojengwa miaka 13 iliyopita kwa kujikita kuandika habari zenye kuzingatia weledi licha ya kuwapo na changamoto kadhaa.
Alisema wakati mwingine wanasiasa wamekuwa hawawaelewi, lakini akaisisitiza menejimenti ya kampuni hiyo kuhakikisha inaitendea haki taaluma ya habari kwa masilahi mapana ya Taifa, huku akidokeza kuwa Serikali na sekta binafsi zinapaswa kufanya kazi kwa ushirikiano.
Akizungumza katika uzinduzi huo, kaimu mkurugezi wa Idara ya Uwekezaji, Aristides Mbwasi aliyemwakilisha waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alisema Serikali inatambua mchango mkubwa unaofanywa na MCL katika dhana nzima ya Tanzania ya viwanda.
“Tunaishukuru sana MCL kwa kumwalika waziri na leo (jana) angetamani kuwapo ila yupo Dodoma kwa majukumu mengine, tunaipongeza MCL kwa kusaidia kuelimisha wananchi hasa ajenda ya Tanzania ya viwanda katika miaka miwili hii tangu (Serikali ya Awamu ya Tano) ilipoingia madarakani,” alisema Mbwasi.
“Serikali inatambua mchango wenu hasa kuunga kaulimbiu ya Rais John Magufuli ya Tanzania ya viwanda na kama itawezekana ‘products’ (bidhaa) zenu zote hata ile ya Mwanaspoti na Mwananchi muelimishe kuhusu falsafa ya Tanzania ya viwanda.”
Alisema Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji wa ndani na nje huku akiwaomba wawekezaji mbalimbali wa kampuni kujitokeza kushiriki maonyesho ya pili ya viwanda yatakayofanyika mwezi ujao katika viwanja vya maonyesho vya Saba saba jijini Dar es Salaam ambapo kiingilio kitakuwa bure.
Mwenyekiti wa Bodi ya MCL, Leonard Mususa alisema kwa sasa kampuni hiyo imeelekeza nguvu katika kuhakikisha inawafikia wananchi kwa njia mbalimbali ikiwamo za kielektroniki.
“Products za MCL ni ‘credible’ (za kuaminika) sio ‘fake’ (bandia), tupo katika ‘print’ na ‘elektronic’ na The Citizen ni gazeti linaloongoza kwa ubora na uzinduzi huu tuwahakikishie wasomaji wetu kwamba tutawafikia kila walipo na kuwapa habari za aina zote,” alisema Mususa.
Akitoa maelezo ya ujio mpya wa The Citizen, mhariri mtendaji mkuu wa MCL, Bakari Machumu alisema kwa sasa asilimia 60 ya gazeti hilo litakuwa na habari za biashara na asilimia 40 ni za matukio ya kila siku.
Awali, mkurugenzi mtendaji wa kampuni hiyo, Francis Nanai aliwashukuru wageni waalikwa waliofika katika hafla hiyo iliyofanyika ukumbi wa Hoteli ya Hyatt Kilimanjaro na kuwaomba kuendelea kuunga mkono bidhaa zinazozalishwa na MCL.

Heche afika Polisi kuitikia wito wa kuhojiwa


Morogoro. Mbunge wa Tarime Vijijini (Chadema), John Heche ameripoti Kituo Kikuu cha Polisi Mkoa wa Morogoro kuitikia wito wa jeshi hilo.            
Heche amefika kituoni hapo leo Jumatatu Novemba 20,2017 saa sita mchana. 
Wakati Heche akiwa kituoni hapo baadhi ya wanachama na viongozi wa Chadema wa Manispaa ya Morogoro walionekana wakizunguka maeneo ya kituo hicho.
Akizungumza kwa simu, Heche ameiambia Mwananchi kuwa atatoa taarifa ya kilichoendelea baada ya kutoka kituoni hapo. 
"Nipo na maofisa wa polisi naendelea kuhojiwa nikitoka nitazungumza zaidi," amesema Heche. 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei amesema Heche aliahidi kwenda kituoni hapo leo. 
Polisi walioelezwa kutoka mkoani Morogoro Ijumaa Novemba 17,2017 walifika eneo la Bunge na Heche alilieleza Mwananchi kuwa walimpatia wito kuwa anatakiwa kwenda kuhojiwa mkoani Morogoro.
Mbunge huyo alisema hajui kosa alilotenda, isipokuwa anatakiwa kuhojiwa kwa kauli alizotoa alipomsindikiza mbunge wa Kilombero (Chadema), Peter Lijualikali alipotoka gerezani.
Akizungumza na Mwananchi Jumamosi Novemba 18,2017 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei alisema mbunge huyo alifanya mkutano wa hadhara wilayani Kilombero Aprili 8, 2017.
Kamanda Matei alisema wanamtafuta Heche kwa kosa la kutotii amri za viongozi na kufanya mkutano Kilombero na kutoa lugha ya matusi hivyo kutaka kusababisha vurugu.
Amesema tangu siku ya tukio jeshi hilo limekuwa likimtafuta mbunge huyo bila mafanikio ndipo lilipoamua kulishirikisha Bunge.
Polisi iliandika barua kwa Spika wa Bunge kumtaarifu kuwa mbunge huyo anatafutwa kwenda kujibu tuhuma zinazomkabili mkoani Morogoro.

Wabunge wa Congress wataka Marekani isaidie suluhu Liberia


Monrovia, Liberia. Baadhi ya wajumbe wa Baraza la Congress la Marekani wamesema kuwa amani na utulivu viko hatarini; siyo Liberia tu, bali pia ukanda wote wa Afrika Magharibi.
Wabunge Sheila Johnson Lee na Bobby L. Rush waliguswa na mkwamo wa kisiasa nchini Liberia uliosababishwa na madai ya udanganyifu na dosari katika uchaguzi mkuu wa rais na wabunge uliofanyika Oktoba 10.
Watunga sheria hao wa Congress wamemwandikia barua Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Rex Tillerson wakiitaka Serikali ya Marekani ifanye haraka kuingilia mambo yalivyo Liberia ili kuhakikisha madai ya udanganyifu katika kura yanashughulikiwa haraka kuepuka usijitokeze mgogoro wa kikatiba.
Katika barua ambayo gazeti la FrontPageAfrica lilipata nakala yake, watunga sheria hao wa Marekani wameonyesha masikitiko yao kuhusu uwezekano wa shauri kuchukua muda mrefu na mgawanyiko katika mchakato wa kidemokrasia.
Walifurahishwa na namna vyma vya siasa vyenye malalamiko vilivyoanzisha mchakato wa kisheria kupata haki na wakapongeza vyama hivyo kuzingatia utawala wa kisheria, lakini wameitaka serikali ya Marekani kuhimiza na kuunga mkono juhudi za kupata ufumbuzi haraka.
Wasiwasi wao kuhusu mgawanyiko ni kwamba unaweza usiishie Liberia tu kwani wanaamini ikiwa mkwamo wa kisiasa hautapata suluhu haraka unaweza kusambaa na kusababisha ukosefu wa utulivu kwa eneo lote na hivyo kuvuruga mchakato wa amani uliofikiwa

Bombardier pasua kichwa Canada



Dar es Salaam. Wakati katibu mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano akiwa nchini Canada kushughulikia suala la ndege ya Bombardier, waziri mkuu wa nchi hiyo, Justin Trudeau amesema hawezi kuingilia uhuru wa mahakama ambayo anaamini itatenda haki.
Hivi karibuni Rais John Magufuli alisema amemwandikia barua waziri huyo mkuu wa Canada ili kujua hatima ya ndege hiyo.
Hata hivyo naibu waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye alisema jana kuwa hawezi kuzungumzia jambo hilo kwa sababu waziri mkuu yupo na wao hawajapata taarifa rasmi.
“Lakini kingine naomba utambue kuwa katibu mkuu bado yupo Canada, kwa hiyo mambo mengi mimi sijayapata hadi atakaporudi aje kutu-breaf kilichojiri huko,” alisema Nditiye.
Akizindua uwanja wa ndege mjini Bukoba, Novemba 6, Rais Magufuli alisema amemwandikia barua waziri mkuu wa Canada kumuomba kuachiwa kwa ndege hiyo na amemtuma mwanasheria mkuu wa Serikali, George Masaju kwenda nchini humo kushughulikia suala hilo.
Kwenye barua yake ya majibu ambayo yameripotiwa na gazeti la National Post la nchini humo, waziri mkuu wa Canada Trudeau amesema hana cha kufanya kwa kuwa shauri hilo lipo mahakamani.
“Ni bahati mbaya kwamba suala hili limechelewesha kuwasili kwa ndege hii. Serikali ya Canada haina uwezo wa kuingilia, ila tuna imani mahakama itaamua kwa weledi na haki,” amekaririwa akisema Trudeau katika gazeti hilo.
Ndege hiyo, Bombardier Q400-8 inashikiliwa kwa amri ya mahakama nchini humo kutokana na shauri lililopo kati ya Serikali na kampuni ya Stirling Civil Engineering.
Kampuni hiyo ilikuwa na mkataba wa ujenzi wa Barabara ya Wazo Hill – Bagamoyoambao ulivunjika kabla haujakamilika, hivyo ikaamua kukimbilia kwenye Mahakama ya Usuluhishi ya Kimataifa ambako ilishinda kesi. Baada ya kushinda kampuni hiyo ilipewa kibali cha kukamata mali za Tanzania katika nchi za Ufaransa, Uholanzi, Uingereza, Ubelgiji, Uganda na Canada.
Kwa miezi mitatu sasa, mahakama nchini Canada inaendelea kuishikilia ndege hiyo iliyonunuliwa kwa Dola 32 milioni za Marekani (zaidi ya Sh70.4 bilioni) kwa niaba ya kampuni ya Stirling inayoidai Serikali Dola 28 milioni (zaidi ya Sh61.6 bilioni) ambazo ni thamani ya mkataba uliovunjwa pamoja na riba.
Ndege hiyo ni miongoni mwa zile ambazo Rais Magufuli aliahidi kununua ikiwa ni mikakati ya kulifufua Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL).
Awali, ndege hiyo litarajiwa kuwasili nchini mwezi Julai, lakini hilo halikufanyika na Agosti 18, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, mwanasheria mkuu wa Chadema, Tundu Lissu alisema ndege hiyo imekamatwa nchini Canada na inaweza kupigwa mnada kutokana na deni ambalo Serikali inadaiwa na kampuni hiyo yenye makao yake Montreal, Canada.
Agosti 19, Serikali ilifanya mkutano na wanahabari kukanusha taarifa hizo, lakini ilikiri kuwapo mgogoro na kampuni hiyo.
Aliyekuwa kaimu mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Zamaradi Kawawa alisema mgogoro kuhusu ndege hiyo upo na kimsingi umetengenezwa na Watanzania ambao kwa bahati mbaya wameweka masilahi ya kisiasa na ya binafsi mbele zaidi ya masilahi ya Taifa.
Alisema Serikali ilikuwa imeanza majadiliano ya kidiplomasia kwa ajili ya kulimaliza suala hilo. Kwa sasa, ATCL inamiliki ndege mbili mpya aina ya bombardier zilizoingia nchini Septemba 2016, na imeagiza ndege nyingine tatu za aina hiyo na Boeing Dreamliner moja.
Akizungumzia mafanikio ya miaka miwili ya Rais John Magufuli hivi karibuni msemaji mkuu wa Serikali, Hassan Abbasi alisema mpaka Juni mwakani ndege zote zitakuwa zimewasili nchini.

Rais Magufuli amesema 3,004 wamejitokeza kuwania nafasi 261


Dar es salaam. Wagombea 3,004 wamejitokeza kuwania nafasi 261 za uenyekiti wa mikoa na jumuiya za CCM.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), ambaye Rais John Magufuli hiyo imetokana na imani ya wanachama kuongezeka na kuwa kubwa.
Amesema hatua hiyo inatokana na idadi ya wagombea 3004 kati ya viongozi 261 tu wanaohitajika kupitishwa leo Jumanne katika Kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM.
Akizungumza wa kikao hicho leo Jumanne, Rais Magufuli amesema kazi ya pitisha majina hayo ilifanyika kwa muda wa wiki mbili chini ya Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana.
"Majina ni mengi yanafika 3004 lakini wanaohitajika ni 261, hii ni tafsiri ya CCM jinsi gani inavyokubalika,” amesema Rais Magufuli.
Amesema katika kuimarisha chama hicho, wanachama watakaobaki ndani ya CCM ni waadilifu, wanaochukia ubadhirifu na siyo CCM maslahi binafsi.

Mke wa Lissu atoa ya moyoni kuhusu waliofanya shambulio

Mke wa Tundu Lissu, Wakili Alicia Magabe

Mke wa Tundu Lissu, Wakili Alicia Magabe akizungumza na waandishi wa Mwananchi Communication Limited (MCL), katika mahojiano maalum kuhusu matibabu ya kiongozi huyo jijini Nairobi. Septemba 7 mwaka huu Lissu alipigwa risasi na watu wasiojulikana akiwa nyumbani kwake mjini Dodoma. Picha na Francis Nderitu (NMG). 
Mke wa mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, amesema angependa kuwajua watu waliomshambulia mumewe, aliyewaamuru wafanye shambulio hilo na sababu za kufanya uovu huo.
Mke huyo ambaye pia ni wakili, Alicia Magabe anasema kuwafahamu watu hao ni muhimu kwa kuwa familia haijui kwa sasa watu hao wanatafakari na kupanga kitu gani baada ya jaribio la kwanza la kumuua kushindikana.
Lissu, mmoja wa wanasiasa wasio na hofu kusema lolote wanaloliamini, alishambuliwa na watu wasiojulikana Septemba 7 akiwa ndani ya gari lililokuwa limewasili kwenye makazi yake Area D mjini Dodoma akitokea bungeni.
Tangu wakati huo, wakili huyo wa kujitegemea na mwanasheria mkuu wa Chadema, amelazwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya na hadi sasa Jeshi la Polisi halijaeleza kama limeshapata fununu ya waliohusika zaidi ya kujibu kuwa linaendelea na upelelezi kila waandishi wanapotaka kujua maendeleo ya suala hilo.
Na sasa mke huyo wa Lissu na ambaye pia ni wakili, Alicia Magabe anataka kuwajua waliomfyatulia mumewe zaidi ya risasi 30, aliyewatuma na sababu za kuwatuma.
Magabe pia anasema familia yake kwa sasa ipo shakani kwa kuwa hajui hao waliofanya shambulio hilo ambalo linaonekana la kukusudia kumuua, wanatafakari nini na kupanga nini.
Akizungumza na Mwananchi katika Hospitali ya Nairobi, Wakili Magabe alisema Lissu ametumia sehemu kubwa ya ujana wake kupigania masilahi na haki za Watanzania, hivyo angependa kuona haki inatendeka.
“Binafsi nimewasamehe kwa kitu walichokifanya, lakini hiyo haina maana kwamba nisingependa kuona haki inatendeka,” alisema wakili huyo.
“Sitaki kuwe na mkanganyiko baina ya kusamehe na hali ya kutamani kuona haki inatendeka.”
Alisema tukio hilo limemfanya aanze kuamini kuwa kuna watu walitaka kumuua Lissu, lakini hawajafanikiwa na anaamini watu hao wapo, hivyo anahofia usalama wa familia yake.
“Mpaka sasa sijasikia kama kuna uchunguzi wowote umefanyika na sijawahi kusikia watu wamekamatwa,” alisema Wakili Magabe.
“Hivyo nawaza kuwa hayupo salama na mimi kama mke wake sijisikii kama niko salama sana. Nawaza hawa watu watakuwa wanatafakari au wanapanga nini. Hiyo ndiyo hali niliyonayo kwa sasa. Sijui hao watu wako wapi.”
Hata hivyo, Wakili Magabe alisema Lissu yuko imara na shambulio hilo halijamrudisha nyuma katika harakati zake za kupigania haki na za kisiasa.
Alisema hilo alilionyesha mara tu alipopata fahamu.
“I have survived to tell a tale, I have lived to tell a tale (nimeepuka kifo ili nieleze jambo) ndivyo alivyosema baada ya kuzinduka,” alisema Wakili Magabe.
Alisema baada ya fahamu kumrejea sawasawa amekuwa akizungumza maneno yanayoashiria kwamba ana ari zaidi.
“Spirit yake ipo very high (ari yake iko juu sana). Si mtu wa kusema kuwa baada ya tukio amekuwa mnyonge, mwoga au ujasiri wake umepungua,” alisema wakili huyo.
“Sijawahi kupata hata kauli yake moja inayoashiria kwamba sasa atarudi nyuma. Kama mke nataka mume wangu apone, tutoke hospitali turudi nyumbani. Lakini wanapokuja viongozi wenzake kutoka Tanzania; wastaafu na wa sasa na hata hapa Kenya, kauli zake zote zinaashiria amekua zaidi kisiasa.
“Anasema ‘kuna siku nitapona na nitaendelea na kazi zangu’ ili kuwatia moyo wanasiasa na wanaharakati.”
Kuhusu mumewe kuendelea na siasa baada ya kupona, Wakili Magabe alisema Lissu ndiye anaweza kulizungumzia suala hilo.
“Mimi nikiwa msaidizi wake wa kwanza, nitakuwa mtu wa mwisho kusema Lissu asifanye analotaka kwa kuwa hata akiyatamka hayatakuwa na nguvu mbele za Mungu,” alisema.
“Binafsi nasema alikuja duniani kwa makusudi. Mungu alimleta duniani kwa sababu na alijua hata kabla hajazaliwa maisha yake yatakuwaje na atafanya nini hapa duniani.
“Sidhani kama kuna binadamu anaweza kuzuia yale ambayo Mungu amepanga. Sitaki kusema kama ataendelea na siasa, hataendelea nazo, yupo kwa kusudi lake.”
Magabe alisema kuna watu wanapigwa risasi moja na wanafariki dunia, lakini Lissu alipigwa risasi 16 za moto ambazo zilipita kwenye mwili wake na anaendelea kuishi.
Alisema anafarijika kuona Lissu yu mzima kwa kutumia nguvu za watu wote ambao kwa namna moja au nyingine wanapenda aishi, akianzia na waliochanga fedha, waliomtolea damu, walioomba, waliomnyanyua, waliomtibu mara ya kwanza na wanaoendelea kumtibu.
“Hatujawahi kuwa peke yetu na nimegundua kumbe kupigwa risasi kwa Lissu ni tukio ambalo limewagusa Watanzania na mataifa mengi na wapo tayari kusaidia,” alisema mwanamke huyo.
“Hii ni kwa kuwa ametumia ujana wake kupigania masilahi na haki za Watanzania.”
Magabe alisema risasi zilizompata Lissu ziliharibu zaidi mifupa, tishu zilizo karibu na mifupa ya mguu wa kulia na mikono, lakini hakuumia kwenye neva, mishipa mikubwa ya damu, ya fahamu au ogani.
“Madaktari wanasema risasi zilikuwa zinakwepa maeneo muhimu. Ni kitu ambacho hawajawahi kukiona,” alisema.
“Hapa kuna mshipa mkubwa wa damu, lakini risasi imepita pembeni. Walikuwa wanashangaa inawezekana vipi risasi nyingi zikaingia lakini zikakwepa maeneo muhimu.”
Alisema madaktari wamemweleza Lissu kuwa ataendelea kuimarika lakini itachukua muda kabla hajapona na kuweza kutumia viungo vyake vyote kama kawaida.
Mama huyo alisema awamu ya kwanza ilikuwa kumtibu majeraha na ya pili ni kumjengea uwezo wa kutumia viungo vyake ili baadaye aweze kusimama na kurudi katika hali yake.
Magabe alisema ilichukua mwezi mmoja Lissu kutoka ICU na hakuweza kumhudumia kwa ukaribu kutokana na masharti ya chumba cha uangalizi maalumu.
“Kila siku naamka kama nakwenda kazini. Lazima niamke asubuhi kuja hospitali kisha narudi usiku nyumbani. Siruhusiwi kulala hapa,” alisema.
Simulizi ya siku ya tukio
Magabe alisema siku ya shambulio alikuwa ametoka Kerege wilayani Bagamoyo na alipanga kukutana na rafiki yake eneo la Mpiji, Bunju.
“Saa 6:30 nilifika kwake, akaniambia lazima nipate chakula cha mchana, baada ya chakula nilimwambia nipumzike kwenye kochi,” alisema.
“Baada ya dakika 25 akaniamsha akaniambia Alicia amka ukilala sana mchana huu usiku unaweza usipate usingizi,” alisema.
Alipoamka aliwasha simu zake na kukuta ujumbe usemao, “hello sister, kuna taarifa inazunguka sina hakika kama ni ya kweli. Kama kweli pole sana dada yangu.”
Alisema moja kwa moja wasiwasi ulimjia kwamba huenda mumewe amekutwa na jambo baya, alisema alichowaza awali huenda amepata ajali na ndipo akamuomba rafiki yake ampigie mtu huyo simu kujua zaidi kuhusu ujumbe huo.
“Niliingia kwenye magroup ya Whatsapp ya Chadema nikakutana na hiyo taarifa. Nilipiga kelele kwa nguvu, rafiki yangu aliniuliza umeona nini nikamwambia kuna ujumbe huu,” anasema na kumpa rafiki huyo simu asome ujumbe huo uliosema “Tundu Lissu amepigwa risasi.”
“Nilianza kuwaza yupo hai au amekufa. Niliwaza nifanye nini nikamwambia nataka kwenda nyumbani. Huko niliamini kuwa ningewaza kwa utulivu nini cha kufanya.”
Anasema baadaye simu zilianza kuingia mfululizo na ndipo alipoamini kuwa habari hizo ni za kweli.
“Nilimpa jukumu hilo (la kupokea simu) kwa sababu ni rafiki yangu wa karibu tangu sijaolewa,” alisema.
Baadaye waliingia kwenye gari na yeye kuanza kuendesha huku rafikiye akizungumza na waliokuwa wakimpigia simu.
Magabe alisema baada ya kuiingia mtaa wa nyumbani kwake, aliona vijana wanamwangalia katika namna ambayo ilionyesha kuna kitu wanakijua. “Mwonekano wao ulikuwa tofauti wananiangalia kwa huruma, kwa mshangao. Wanatamani waongee,” alisema.
Anasema nyumbani aliwakuta shemeji zake wawili na mtoto wa baba yake mdogo, lakini alishindwa kuingia ndani na badala yake alikaa bustanini.
“Nilipigiwa simu na watu waliokuwepo hospitali na wakaniambia ni kweli amepigwa risasi, lakini yupo hai. Walinitaka nitulie mpaka nitakapopewa taarifa nini cha kufanya,” alisema.
Alisema mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alimweleza nini cha kufanya kwa wakati huo.
Alisema baadaye aliambiwa Lissu angepelekwa Nairobi na hivyo aende uwanja wa ndege kwa ajili ya safari ya Dodoma na baadaye Nairobi.
Aliondoka na kaka yake na marafiki wa karibu, lakini alipigiwa simu na kutakiwa kushuka kwa kuwa muda haukuwa rafiki.
“Nilipanda bodaboda,” alisema.
“Wale vijana walikimbiza sana na ilikuwa ni mara ya kwanza kupanda pikipiki Dar es Salaam. Niliogopa na kusali Mungu anisaidie kufika uwanja wa ndege salama.”
Alipofika Dodoma ndipo alipomuona kwa mara ya kwanza Lissu tangu apate taarifa za shambulio.
“Baada ya dakika chache akaja akiwa kwenye kitanda kutoka chumba cha upasuaji. Kwa kumuangalia nilijua ameumia sana hakuwa anajitambua,” alisema.