Macho na masikio ya Watanzania katika usiku wa Aprili 1, mwaka huu yalielekea Ukumbi wa Mlimani City, zilipokuwa zikitolewa tuzo za filamu zinazofahamika kwa jina la ‘Sinema Zetu International Film Festival Award (SZIFF)’.
Tuzo hizo ziliandaliwa na kutolewa na kituo cha Televisheni cha Azam kupitia chaneli yake ya Sinema Zetu kwa lengo la kutambua kazi za wasanii wa tasnia hiyo.
Mazungumzo katika majukwaa yote yalitawaliwa na utoaji wa tuzo hizo tangu hafla ya utoaji tuzo hizo ilipoanza saa 2:00 usiku mpaka 7:00 usiku.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Rais Mstaafu wa awamu ya nne, J
Macho na masikio ya Watanzania katika usiku wa Aprili 1, mwaka huu yalielekea Ukumbi wa Mlimani City, zilipokuwa zikitolewa tuzo za filamu zinazofahamika kwa jina la ‘Sinema Zetu International Film Festival Award (SZIFF)’.
Tuzo hizo ziliandaliwa na kutolewa na kituo cha Televisheni cha Azam kupitia chaneli yake ya Sinema Zetu kwa lengo la kutambua kazi za wasanii wa tasnia hiyo.
Mazungumzo katika majukwaa yote yalitawaliwa na utoaji wa tuzo hizo tangu hafla ya utoaji tuzo hizo ilipoanza saa 2:00 usiku mpaka 7:00 usiku.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete ambaye alikuwa mgeni rasmi, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Ali Hapi na Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu, Joyce Fisoo.
Mbali ya viongozi, pia walikuwepo wasanii wa filamu kutoka Kenya, Rwanda, Zambia na India akiwamo mwanadada anayeigiza katika tamthiliya ya Beintih, Preetika Rao, jina la usanii Aliyah.
Katika tuzo hizo jumla ya vipengele 19 vilishindaniwa, ambapo katika washindi wapo waliondoka na kitita cha Sh5 milioni na Sh2 milioni kwa msanii bora wa kike, wa kiume na muongozaji bora wa filamu.
Mratibu wa tuzo hizo ambaye pia ni msimamizi wa chaneli ya Sinema Zetu, Zamaradi Nzowa alisema Sh41 milioni ziliandaliwa kwa ajili ya zawadi.
Katika upande wa mwigizaji bora wa kike, tuzo hiyo ilienda kwa mrembo Wema Sepetu na mwigizaji bora wa kiume aliinyakua mwigizaji Salim Ahmed maarufu Gabo huku muongozaji bora ikienda kwa Daniel Manege aliyeongoza filamu ya Safari ya Gwalu.
Vitu gani vilivutia katika tukio zima
Katika tukio hilo la utoaji tuzo kulikuwa na mambo mbalimbali yaliyovutia lakini kivutio kilikuwa mwanamuziki Diamond Platnumz kuungana na mwanamitindo Hamisa Mobeto katika kukabidhi tuzo.
Wawili hawa wamekuwa kivutio kutokana na hivi karibuni kuingia katika mgogoro wa matunzo ya mtoto wao aitwaye Dyllan, mpaka kufikia hatua ya kufikishana mahakamani kutafuta suluhu ya jambo hilo.
Hata hivyo, juzi katika utoaji wa tuzo hizo, Diamond ambaye alikuwa wa kwanza kuitwa jukwaani kwa ajili ya kukabidhi na baadaye mshehereshaji kumuita Mobeto katika kuungana na msanii huyo.
Alipofika kwenye ngazi, mshereheshaji wa kike aliyetambulika kwa jina moja la Sofia, alimsaidia kumshika mkono wakati anapanda ngazi na kumkabidhi kwa Diamond ambaye naye alimkumbatia kwa kumshika kiuno na kuibua kelele ukumbini.
Baada ya hapo Diamond alisema amefurahishwa na tuzo hizo kwani zimemuwezesha kukutana na mzazi mwenzie, jambo ambalo lilisababisha tena ukumbi kulipuka kwa shangwe.
Diamond ambaye alikuwa amevalia suruali ya maua maua iliyochanganyika na rangi nyeupe na koti jeupe juu lililotanguliwa na fulana nyeupe, hakuishia hapo kwani alimsifia Mobeto kwa namna alivyopendeza na kueleza kuwa anaamini uwepo wao hapo hata mtoto wao huko alipo kama anawaona atakuwa amefurahi zaidi.
Alipomaliza hapo alimuonyesha karatasi Mobeto ili aweze kumsoma mshindi na ndio hapo akaitaja filamu ya ‘Safari ya Gwalu’ kuwa ndio imeshinda kipengele cha ‘Best Original Music’.
Baada ya kumaliza kufanya hivyo, Diamond alimshika Mobeto na kushuka naye jukwaani na kurudi alipokuwa amekaa na yeye kwenda kumsalimia Rais Mstaafu Jakaya Kikwete.
Alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu tukio hilo, Wema Sepetu, ambaye chupuchupu tuzo hiyo iende kwake kupitia filamu ya ‘Heaven Sent’, kutokana na kuwa moja ya filamu iliyoingia kwenye kipengele hicho.
Wema ambaye aliwahi kuwa mpenzi wa Diamond miaka kadhaa iliyopita na hivi karibuni kuelezwa kwamba wamerudiana, amesema kitendo hicho kwake amekichukulia kawaida kwa kuwa Mobeto na Diamond ni mtu na mzazi mwenzake.
“Wee ulitaka nichukuliaje labda, Mobeto na Diamond hawa ni wazazi jamani, ulitaka nikasirike au halafu isitoshe mimi sina mahusiano ya kimapenzi na Diamond bali ni washkaji tu na si kama watu wanavyosema,” alisema Wema akizungumzia tukio hilo ambalo pia lilikua gumzo usiku kucha kwenye mitandao ya kijamii.
Kuhusu hatua yake ya kupata tuzo mbili ya msanii bora wa kike na chaguo la watu (People’s Choice Award) kupitia filamu yake ya ‘Heaven Sent’, Wema alisema amefurahi kuona majaji wameweza kuona kipaji alichonacho.
Pia aliahidi kuendelea kuwapa mashabiki wake kazi nzuri na kuwaondoa hofu wadau wa filamu waliokuwa wanasema kuwa Bongo Movie imekufa kuwa si kweli bali ilikuwa imelala tu. Hata hivyo, hakusita kutoa shukrani kwa mashabiki zake ambao amesema ni kati ya watu ambao walishiriki zoezi la kumpigia kura kwa wingi hadi kuhakikisha anapata ushindi huo.
Diamond aingia na kutoka kama upepo
Wakati macho na masikio yalikuwa kwa Diamond usiku wa tuzo hizo, katika hali isiyo ya kawaida Diamond aliingia ukumbini bila ya waandishi kushtukia mpaka pale walipomuona akiwa amekaa ukumbini hapo.
Hata hivyo, wakati wa kuondoka nako hali ilikuwa hivyo hivyo kwani baada ya kukabidhi tuzo hiyo alitokomea pasipo kujulikana na paparazi waliokuwa wakimvizia kufanya naye mahojiano hawakufanikiwa katika hilo.
JK awananga wanaowazodoa Bongo Movie
Katika hatua nyingine, Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete alionyesha kukerwa na namna watu wanavyokosoa Bongo Movie na kueleza kuwa walikotokea na walipo kuna utofauti.
Alikiri kwamba suala la vifaa, usambazaji wa kazi zao, mitaji vimekuwa kikwazo cha wao kutofikia ubora wa filamu za nchi nyingine kama zilivyo za Bollywood na Nollywood na kuomba Watanzania kuwaunga mkono kwa kununua kazi zilizo halisi ili waweze kufaidika na jasho lao.
Washindi waliopata tuzo nyingi
Katika tuzo hizo filamu aliyoigiza msanii Gabo imeongoza kwa kuzoa tuzo nyingi ambapo katika kipengele cha filamu ndefu, imetoa muigizaji bora wa kiume, muongozaji bora, filamu bora, best screen play na best original music.
Wakati kwa upande wa filamu fupi, filamu ya Binti Musa iliyoigizwa na wasanii kutoka visiwani Zanzibar ilizoa tuzo tatu ikiwemo filamu bora, best screen play na best original music. Wakati makala iliyodhaminiwa na Mfuko wa Waandishi wa Habari Tanzania (TMF), ikipata tuzo mbili za kipengele cha filamu bora na muongozaji bora.
Wasanii kuchelewa, upigaji picha, matumizi ya lugha
Mojawapo ya mambo ambayo hayakuvutia katika tuzo hizo ni pamoja na wasanii kuchelewa kufika ukumbini hadi mgeni rasmi kuwatangulia.
Mbaya zaidi wasanii hao ni wale waliokuwa wateule akiwemo Wema Sepetu ambaye aliingia ukumbini saa moja baada ya mgeni rasmi kuketi.
Jingine ni majina ya vipengele kuorodheshwa kwa lugha ya Kiingereza wakati tukio hilo kubwa lingekuwa fursa ya kukitangaza Kiswahili.
Pia, hakukuwa na utaratibu mzuri wa kuwawezesha wanahabari kushiriki upigaji picha kwa nafasi kutokana na kituo hicho kurusha moja kwa moja matangazo yake.
Katika hili kwa kuwa walikuwa na vyombo vya kisasa wangeweza kupandisha hata mitambo yao juu na kuwaacha wapiga picha wa vyombo vingine nao kupata picha za tukio hilo vizuri.
Wasanii kuwa ‘busy’ kupiga picha za kuuzia sura nje wakati matukio yakiwa yanaendelea ndani ikiwemo kupewa nasaha za namna ya kuboresha kazi zao zilizokuwa zinatolewa na viongozi mbalimbali ni miongoni mwa mambo yaliyojitokeza.
Pia ilishuhudiwa baadhi ya wasanii ambao tangu wamefika wamekaa kwenye zulia jekundu kwa ajili ya kuchukua picha mbalimbali na hata ungewauliza nini kilitokea ndani wasingeweza kukujibu.
Jingine ni filamu za kutoka nchini Kenya kushinda, wakati tuzo hizo tuliambiwa ni kwa ajili ya filamu za hapa nchini, katika hili ingependeza wakati mwingine waongeze kipengele cha filamu za Afrika Mashariki, kwani watakuwa hawajawatendea haki wasanii wa hapa Bongo.