Monday, August 10

Lowassa: CCM hodari wa kuiba kura

Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad na mgombea urais wa muungano wa Ukawa, Edward Lowassa wakiwapungia mkono wananchi waliofurika makao makuu ya CUF, 
Buguruni jijini Dar es Salaam jana. 

Dar es Salaam. Mgombea wa urais kupitia Chadema, Edward Lowassa ameituhumu CCM kuwa ni hodari wa kuiba kura hivyo akawataka wananchi wajitokeze kwa wingi kupiga kura ili hata sehemu ya kura hizo ikiibiwa, Ukawa ishinde kwa kishindo.
Lowassa ambaye ni waziri mkuu wa zamani aliuambia umati wa wafuasi wa Ukawa uliojitokeza jana kumpokea katika ofisi za makao makuu ya CUF yaliyopo Buguruni kuwa ili kufanikisha ushindi wa kuwawezesha kuingia ikulu hawana budi kushikamana, kushawishiana kupiga kura kwa wingi na kuzilinda Oktoba 25.
Kauli hiyo ya Lowassa ambaye amelelewa kisiasa na CCM tangu alipojiunga akiwa mdogo mwaka 1977, inaendeleza tuhuma ambazo hutolewa na vyama vya upinzani kuwa chama hicho huchakachua matokeo wakati wa uchaguzi.
Hata hivyo, Lowassa hakuwa na vielelezo wala kuthibitisha kuhusu tuhuma hizo dhidi ya chama chake cha zamani.
“Tukiwa na umoja, tukiwa na mshikamano tutawaondoa Jumapili asubuhi sana. Tutahitaji mshikamano, tatahitaji ushawishi wa kupiga kura tupate angalau asilimia 90 ili wakiiba asilimia 10 tuwasamehe,” alisema Lowassa katika hotuba yake iliyokuwa inakatishwa na kushangiliwa na na salamu ya CUF ya “Hakiii” na kujibiwa “kwa wote.”
“Hodari sana wa kuiba CCM kura. Sasa tupate kura nyingi za kutosha hata wakiiba kura hausikii na kuna usemi wa Chadema unaosema ‘piga kura, linda kura’ na sisi CUF ni hodari sana wa mambo hayo.”
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alipotafutwa kwa simu kuhusu madai hayo, alijibu kwa ujumbe wa maneno kuwa asingeweza kuzungumza bali atumiwe ujumbe, na alipotumiwa ujumbe huo hakujibu.
Lubuva: Aeleze wanaibaje
Akizungumzia madai hayo, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)  Jaji mstaafu, Damian Lubuva alisema Lowassa angeeleza jinsi wanavyoiba kura.
“Ili kutoa majibu ya uhakika naomba tufanye utafiti wa kutosha juu ya tuhuma hizo, lazima tujue ni njia zipi watu wanaiba, vinginevyo nitaeleza kitu ambacho sina ufahamu nacho. Yeye (Lowassa) kama mtu aliyekuwa serikalini lazima ana ufahamu walikuwa wanaiba vipi, angeeleza.”
Tume huwa inaendesha uchaguzi kwa mujibu wa taratibu na sheria na iwapo kuna mtu anasema kura zinaibwa ajitokeze aeleze kinagaubaga ili ofisi yake ifanye utafiti wa kina.
“Naomba nieleweshwe kura huwa zinaibiwa vipi? Hii imekuwa ni hisia, wengine wanasema tutaibiwa kura zetu wakati upande mwingine unasema hawa wataleta fujo kwa visingizio vya kuibiwa kura,” alisema Jaji Lubuva.
Lowassa ambaye alihamia Chadema siku 11 zilizopita na baadaye kuteuliwa kugombea urais kwa mwamvuli wa Ukawa kupitia Chadema, alisema safari ya Ikulu itafanikishwa kwa kupiga kura na siyo maandamano, hivyo Watanzania watunze shahada za kupigia kura. Hata hivyo, hakuendelea kueleza undani kuthibitisha ni namna gani CCM huiba kura.
Kiongozi huyo aliyeonekana mwenye furaha, aliwataka wanawake nao kujitokeza kwa wingi siku ya upigaji wa kura huku wakiwa wameshapika vyakula majumbani mwao ili nao wapate fursa za kupiga na kulinda kura.
Lowassa alisema ameingia Ukawa ili kuandika historia ya nchi kukuza uchumi na kuondoa umaskini na kutekeleza kauli ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ya “mabadiliko ya kweli yatapatikana nje ya CCM.”
Ukawa kutoyumba
Mbunge huyo wa Monduli anayemaliza muda wake, alisema Ukawa ipo imara haitayumbishwa kirahisi na wafitini, licha ya baadhi ya watu kujipitisha kwa viongozi wa juu na kutaka kuwarubuni ili umoja huo utetereke.
“Wanakuja kupitisha hela na kuhongahonga lakini viongozi wapo imara…hawahongeki hawa! Wanapita na maneno kwenye magazeti ya ufukuzi ufukuzi, nawaambia muwapuuze,” alisema Lowassa bila kuwataja wahusika.
Alisema kuna baadhi ya watu wanaleta propaganda kuwa Ukawa ikiingia madarakani nchi haitatawalika kiasi cha kuwatisha wafanyabiashara kukimbiza fedha zao nje ya nchi, jambo ambalo si la kweli.
“Waongo wakubwa hao…nchi itatawalika kuliko awali, Ukawa ikiingia madarakani nchi itatulia tuli, wasiwadanganye mkimbize hela zenu..tupo imara,” alisema.
Juma Duni afafanua
Mgombea mwenza wa urais wa Ukawa, Juma Duni Haji alisema hajahamia Chadema kutafuta vyeo kwa kuwa ameondoka akiwa Makamu Mwenyekiti wa CUF na waziri katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, na hatua yake hiyo ni kutimiza za kuing’oa CCM madarakani.
“Ni vizuri mkaelewa kwamba tutafanya kosa kubwa tusipofika ikulu mwaka huu, tutahitaji kusubiri miaka 50 zaidi maana jamaa hawa wakija kutulia balaa yao ni mara 100 ya wanayoyafanya. Wanaoleta mabadiliko ni vijana siyo wazee,” alisema Duni Haji.
Alisema Ukawa wanatakiwa kushirikiana kwa dhati na Watanzania kwa ujumla kwa kuwa mwaka huu ni wa mageuzi na kila mmoja ana wajibu wa kufanya kampeni ya kuiondoa CCM ili kutafuta hatima bora ya nchi.
Kauli ya Mbowe
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema kuna nguvu nyingi zinatumika kuivunja Ukawa lakini umoja huo utabaki kuwa imara na kutimiza malengo yake ya kushika dola mwaka huu kwa nguvu za Mungu.
Alisema vyama vya upinzani vimefanya siasa zao kwa shida kwa miaka 25 huku baadhi ya makada wakifungwa, kufukuzwa kazi, ndoa kuparaganyika, kufungwa au kufunguliwa kesi mahakamani lakini miezi minane iliyopita imekuwa migumu zaidi kutokana na baadhi ya watawala kupatwa na hofu baada ya Ukawa kujiimarisha.
“Safari yetu imebaki kidogo tufike tunakoelekea. Sasa akitokea kiongozi mmoja wetu bila kujali ni wa chama gani akaona kwamba malengo yetu siyo ya muhimu kuliko fursa binafsi, huyo hatufai,” alisema Mbowe na kushangiliwa.
Alisema maandamano ya leo kumsindika Lowassa kuchukua fomu yataanzia CUF na kupitia ofisi za Makao Makuu ya NCCR-Mageuzi Ilala hadi NEC kabla ya kurudi ofisi za Chadema Kinondoni.
Mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi aliwataka wafuasi wa Ukawa kujitokeza kwa wingi kumsindikiza mgombea wa urais kupitia umoja huo na ikiwezekana kila mfuasi apeleke watu 10.
Mbatia amvaa JK
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema Ukawa itaendelea kuhubiri amani siku zote ili CCM na vyombo vya dola visipate sababu ya kuwatuhumu na kwamba Uchaguzi Mkuu utafanyika kwa amani.
Alisema Rais Jakaya Kikwete alihubiri chuki dhidi ya wapinzani kwa kuwaita maadui siku alipozungumza na wafuasi wa CCM baada ya kumpokea mgombea wa urais kupitia chama hicho, Dk John Magufuli alipotoka kuchukua fomu za kuwania.
 “Sikuamini kama Rais Kikwete angesema maneno yale eti anawaambia wana-CCM wana mikakati ya kila aina ya kushinda na kwamba ‘msiogope kujihadhari na nguvu za adui’. Yaani sisi wapinzani ni adui? Ukianza kuwaita wenzio adui wakati wewe ni amiri jeshi mkuu, nchi hii unaipeleka wapi?” alihoji Mbatia.
Malim Seif apongeza
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, aliwashukuru wafuasi wa Ukawa waliojitokeza kumpokea Lowassa wakati wa ziara ya kutembelea ofisi zao na kwamba moyo huo uendelee hadi Oktoba 25 siku ya kupiga kura.
“Hakuna silaha kubwa kuliko umoja, ushirikiano na mshikimano. Tukishirikiana tukawa wa kweli wa nafsi zetu bila shaka Lowassa anasubiri kuapishwa tu na sisi Zanzibar tumeshamaliza kazi,” alisema Maalim Seif na kushangiliwa na umati wa wafuasi hao.
Hali ilivyokuwa
Mapema kabla ya Lowassa hajawasili Buguruni wafuasi wa CUF walianza kujikusanya taratibu saa 4 asubuhi kwa kuzunguka na ngoma barabara za Uhuru na za mitaa kuingia ofisi za chama hicho.
Baadaye umati huo uliongezeka kiasi cha kufunga barabara ya Uhuru kwa muda wakati Lowassa anaingia saa 6:20 mchana na kupokelewa na Maalim Seif, Makaidi, Mbatia na viongozi waandamizi wa Ukawa.
Idadi hiyo ya watu iliwapa kibarua maofisa usalama wa Ukawa walioonekana wakihaha kutengeneza njia ili viongozi hao wapite.
Baada ya viongozi hao kuwahutubia wafuasi hao, waliingia katika ukumbi wa Mkutano wa Baraza Kuu la Uongozi saa 7:15 mchana na kufanya mazungumza ya takriban saa moja na baadaye viongozi kutoka nje ya CUF kuondoka.
Nafasi ya Lipumba
Kikao cha Baraza Kuu kilijadili nafasi ya mwenyekiti iliyoachwa na Profesa Lipumba na suala hilo liliachiwa Mkutano Mkuu wa chama ambao utaitishwa baada ya miezi sita kwa kuwa ndio wenye uwezo wa kufanya uchaguzi huo kwa mujibu wa katiba ya CUF.
Akitoa taarifa ya kikao hicho, Maalim Seif alisema Baraza Kuu limeunda kamati maalum ya watu watatu itakayofanya kazi na katibu mkuu kwa miezi sita kabla ya Mkutano Mkuu kukaa na kumchagua mwenyekiti na makamu wake, nafasi ambazo ziko wazi.
Waliochaguliwa kwenye kamati hiyo ni Twaha Taslima ambaye ni mwenyekiti na wajumbe wawili ambao ni Aboubakary Khamis Bakary (Waziri wa Katiba na Sheria Zanzibar) na Sererina Mwijage (mbunge mstaafu wa viti maalumu.



JK, Magufuli waendelea kunguruma Kusini


Rais Jakaya Kikwete akibonyeza kitufe kuzindua rasmi Kivuko cha MV Mafanikio 
katika eneo la Msangamkuu mjini Mtwara jana. Picha na Freddy Maro wa Ikulu.

Mtwara. Rais Jakaya Kikwete akiwa na Waziri wa Ujenzi na mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli jana aliendelea kuunguruma katika mikoa ya Kusini na kuzindua Kivuko cha MV Mafanikio cha Mtwara kilichogharimu Sh3.3 bilioni.
Kivuko hicho chenye uwezo wa kubeba watu 100 na magari sita kinamaliza kero iliyokuwa ikiwakabili wananchi wanaovuka kutoka Pwani ya Mtwara Mikindani kwenda Pwani ya Msangamkuu, kilizinduliwa siku moja baada ya kuzindua kipande cha barabara ya Ndundu-Somanga mkoani Lindi.
Kuzinduliwa kwa kipande hicho cha barabara kumeifanya Serikali kukamilisha ujenzi wa miradi 13 mikubwa katika Ukanda wa Maendeleo wa Mtwara.
Vilevile, kwa kukamilisha kipande hicho cha barabara ambayo ni sehemu ya Barabara Kuu ya Dar es Salaam-Kibiti-Lindi hadi Mingoyo, kunaifanya Serikali kutumia Sh9 trilioni katika miaka 10 ya uongozi wa Rais Kikwete.
Kilomita 60 za kipande cha Ndundu-Somanga ni sehemu pekee iliyokuwa imebakia kukamilisha ujenzi kwa kiwango cha lami, ambayo imekuwa kero kwa wananchi wa mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Lindi na Mtwara.
Baada ya tukio hilo juzi, Rais Kikwete jana aligeukia kivuko hicho na kusema kuwapo kwake ni utekelezaji wa ahadi alizotoa kwa wananchi.
Aidha aliwataka wananchi na wasafirishaji kuzingatia maadili ya kiwango cha uzito wa kivuko hicho.
“Suala la kivuko lilikuwa kero kubwa sana na tuliliona hasa watu walipokuwa wakivuka kutoka upande mmoja kwenda mwingine. Jambo muhimu ni kukitunza kivuko kwa kubeba watu na mizigo kwa kiwango kinachokubalika” alisema Rais Kikwete.
Awali, Dk Magufuli akimkaribisha Rais Kikwete alisema watu wa Mtwara walikuwa wakikabiliwa na changamoto ya kivuko.
“Mheshimiwa Rais, wakati unaingia madarakani tulikuwa na vivuko 13, lakini kwa kipindi chako tumeongeza vivuko vingine 15 na kukamilisha idadi ya vivuko 28 vyenye uwezo wa kubeba tani tofauti tofauti, kikiwamo hiki cha Mtwara ambacho gharama yake ni Sh3.3 bilioni na tumekarabati vivuko vingine saba,” alisema Dk Magufuli.
Akizungumzia viwango vya nauli vilivyopangwa, Dk Magufuli alisema ni Sh300 kwa mtu mzima, wanafunzi hawatatozwa, huku watoto na wanafunzi wasiovaa sare za shule watalipa Sh100.
Kuhusu miradi mingine ya Kusini, Waziri Magufuli aliitaja kuwa ni Daraja la Umoja lililokamika ujenzi wake, ujenzi wa barabara za lami ya Songea-Namtumbo; Peramiho Junction-Mbinga, Masasi-Mangaka na usanifu wa kina kwa ajili ya ukarabati wa Barabara ya Mtwara-Mingoyo-Masasi yenye urefu wa kilomita 200, ambao umekamilika.
Miradi mingine inayoendelea ni ujenzi kwa barabara za lami za Mangaka-Mtambaswala, Mangaka-Nakapanya, Nakapanya-Tunduru-Matemanga na Matemanga-Kilimasera yenye urefu wa kilomita 68.2.
Waziri Magufuli aliitaja miradi mingine inayoendelea ya ujenzi wa kiwango cha lami ni barabara za Kilimasera-Namtumbo, upembuzi yakinifu wa barabara ya Mtwara-Newala-Masasi na kuwa zabuni tayari imetangazwa kwa ajili ya ujenzi sehemu ya barabara ya Mtwara-Mnivata.
Madaraja 12 yajengwa
Kama ilivyo kawaida yake kutaja bila kusoma popote miradi anayojengwa na Serikali, Dk Magufuli alisema Serikali katika kipindi hicho imejenga madaraja makubwa 12, ambayo ni Rusumo (Kagera), Umoja (Mtwara), Mwanhuzi (Simiyu), Kikwete (Kigoma), Nangoo (Mtwara), Ruhekei (Ruvuma), Mbutu (Tabora), Mwatisi (Morogoro), Ruvu (Pwani), (Nanganga (Mtwara), Maligisu (Mwanza) na daraja la waendao kwa miguu la Mabatini (Mwanza).
Dk Magufuli pia alisema madaraja mengine madogo zaidi ya 7,200 yamejengwa na kukamilika katika kipindi cha uongozi wa Rais Kikwete, huku mengine makubwa saba yakiwa katika hatua mbalimbali za ujenzi ambayo ni Kigamboni (Dar es Salaam), Kilombero (Morogoro), Kavuu (Katavi), Sibiti (Singida), Ruvu Chini (Pwani), Lukuledi 11, (Mtwara) na Kolo  la Dodoma.
Kana kwamba haitoshi, alisema kuna madaraja mengine makubwa ambayo yako katika maandalizi ya kujengwa.
Ni pamoja na Momba, Mwiti, Simiyu, Wami, Ruhuhu, Daraja jipya la Salendar, Daraja jipya la Wami Chini, Pangani na daraja la wandeao kwa miguu la Furahisha.

Profesa Lipumba: CCM ina wagombea wawili wa urais


“Ukweli ni kwamba  tumejiparaganyisha wenyewe ndani ya Ukawa. Kwa hiyo Watanzania watakuwa na wanaCCM wawili wanaogombea urais wakati Ukawa tulikuwa na wagombea watatu, na tulikubaliana Dk Slaa apeperushe bendera” Profesa Lipumba

Dar es Salaam. Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amesema Chama cha Mapinduzi (CCM), kina wagombea wawili wanaowania kiti cha urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
Madai hayo mapya ya Profesa Lipumba yametolewa siku tatu baada ya kujiuzulu uenyekiti CUF, akisema hiyo ni moja ya sababu za kuachia nafasi yake kutokana na uamuzi uliofikiwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kuhusu mgombea urais.
Akizungumza wakati akitangaza kujiuzulu wiki iliyopita, Profesa Lipumba alisema dhamira yake ilikuwa inamsuta kwa kuwaingiza ndani ya Ukawa watu kutoka CCM, waliokuwa wanapingana na maoni ya wananchi kuhusu rasimu ya Katiba ya Jaji Warioba na kuwapa fursa ya kuwania urais.
Juzi usiku katika mahojiano aliyoyafanya na Azam TV kutoka Kigali alikosema anafanya utafiti, Profesa Lipumba alisema kumpa nafasi waziri mkuu mstaafu, Edward Lowassa kuwania urais kupitia Chadema ndani ya Ukawa, ni sawa na CCM kusimamisha wagombea wawili (Lowassa) na Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli.
Katika mahojiano hayo ya simu, Profesa Lipumba ambaye wiki mbili zilizopita alimpokea Lowassa akisema ni mtu safi na kwamba, ufisadi ndani ya CCM ni mfumo  alisema katika kujiuzulu kwake hakutumiwa na CCM kuparaganyisha Ukawa, bali walikuwa tayari wameparaganyika.
“Ukweli ni kwamba tumejiparaganyisha wenyewe ndani ya Ukawa. Kwa hiyo Watanzania watakuwa na wanaCCM wawili wanaogombea urais wakati Ukawa tulikuwa na wagombea watatu... mimi, Dk Willibrod Slaa, (Katibu Mkuu wa Chadema) pamoja na Dk George Kahangwa (NCCR-Mageuzi) ambaye alikiri kuwapo makubaliano hayo.
“Tulikutana nyumbani kwangu tukakubaliana Dk Slaa apeperushe bendera ya Ukawa, lakini tumewekwa kando,” alisema Profesa Lipumba.
Alisema yupo Rwanda kwa muda na anafanya utafiti kuona namna gani Tanzania inaweza kujifunza mambo ya kiuchumi kutokana na nchi hiyo kupiga hatua kubwa kiuchumi.
Pia alisisitiza kuwa hajahama nchi na kwamba wiki hii anatarajia kurejea nchini.
Agosti 6, mwaka huu Profesa Lipumba alijivua  uenyekiti wa CUF wakati mkakati wa vyama vya upinzani kushirikiana kushika dola ukiwa umeshika kasi.





Pinda: Nimeishia kuwa rais wa fikra


Waziri Mkuu Mizengo Pinda akipungia wakulima kwenye maonyesho ya Nanenane, 
Kanda ya Kusini yaliyofanyika jijini Mbeya juzi.

Mbeya. Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ambaye alianguka katika hatua za awali za mbio za urais ndani ya CCM, amesema ameishia kuwa “rais wa fikra”.
Pinda, ambaye amekuwa Waziri Mkuu kwa takriban miaka minane, hakuweza kuingia katika orodha ya makada watano ambao majina yao yalipelekwa Halmashauri Kuu kwa ajili ya kupata majina matatu ya kupelekwa Mkutano Mkuu kwa ajili ya kupata mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho tawala.
Baada ya mchakato huo kumalizika, mbunge huyo wa Katavi amekuwa kimya, lakini jana aliibuka na kuzungumzia mbio hizo zilizoacha majeraha kwenye chama hicho kikongwe.
Pinda alisema mchakato huo ulikuwa hauna kulala, wa haraka haraka, ambao uliisha kwa CCM kupata mgombea ambaye alimuelezea kuwa “ni chaguo la Mungu”.
Akizungumza baada ya kupokea taarifa fupi ya Mkoa wa Mbeya kuhitimisha maonyesho ya Nanenane jijini hapa, Pinda alisema alitamani sana kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania.
“Mimi ninaamini Mungu ndiye anayepanga kwani  sikuzaliwa kuwa Waziri Mkuu wala kuwa Rais, lakini nilipangiwa uwaziri mkuu ambao nimefanya kazi hiyo hadi nimechoka,” alisema Pinda, ambaye alikuwa mmoja wa makada 42 wa CCM waliojitokeza kuwania ridhaa ya chama hicho kugombea urais.
“Baada ya mchakato ule, alipatikana mtu mahiri ambaye Mungu alimpanga, lakini tamaa yangu, ikaishia kuwa rais wa fikra tu.”
Alisema mchakato ulifanyika kwa kasi bila kulala na wakapatikana watano, mara watatu na hatimaye mmoja.
“Suala hilo halitakiwi kuwa sababu ya kugombana, kulaumiana na kutoana macho, kwani ni sawa na kugombana na Mungu,” alisema Pinda.
“Hata mimi nilitamani sana kuwa Rais, lakini sasa yamekwisha. Sina sababu ya kuwa na hasira  au kuhama chama kwani haina tija na hasira ni hasara.
“Sina sababu ya kuhama chama, nitabaki CCM na baada ya Oktoba nitakuwa mkulima mzuri ambaye nitashirikiana na wenzangu kuendeleza nchi.” Pinda alisema mgombea wa CCM, Dk John Magufuli ni mzuri na kwamba Mungu atamsaidia kujua mahitaji mengine ya Taifa na Watanzania.
Alisema ana uhakika kwamba ifikapo mwaka 2025, hali ya umaskini katika kaya itakuwa imepungua.
Aliwataka wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na maofisa wote wa Serikali waliogombea urais, ubunge na udiwani  ambao walishindwa katika kura mbalimbali, wakubali matokeo na wachape kazi bila kinyongo na kwamba Serikali ijayo itawafikiria kwa utendaji mzuri.
Awali, katika taarifa yake fupi, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro alisema yeye na viongozi wengine waliwania ubunge, lakini wameshindwa na wataendelea kuchapa kazi ya Serikali.
Kandoro alizungumzia utekelezaji wa maagizo mbalimbali aliyopewa na Waziri Mkuu likiwamo la kuwashughulikia wanaume waliowapa mimba wanafunzi wa sekondari na alisema  watu 176 walikamatwa na 53 kati yao, kesi zipo mahakamani wakati wengine walifungwa na wengine uchunguzi unaendelea.
Kuhusu agizo la kuhakikisha wanawake wanapimwa ili kujua hali ya kansa mkoani Mbeya, alisema wanawake 7,241 walipimwa na 200  kati yao walionekana kuwa na saratani ya shingo kizazi.