Rais Jakaya Kikwete akibonyeza kitufe kuzindua rasmi Kivuko cha MV Mafanikio
katika eneo la Msangamkuu mjini Mtwara jana. Picha na Freddy Maro wa Ikulu.
Mtwara. Rais Jakaya Kikwete akiwa na Waziri wa Ujenzi na mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli jana aliendelea kuunguruma katika mikoa ya Kusini na kuzindua Kivuko cha MV Mafanikio cha Mtwara kilichogharimu Sh3.3 bilioni.
Kivuko hicho chenye uwezo wa kubeba watu 100 na magari sita kinamaliza kero iliyokuwa ikiwakabili wananchi wanaovuka kutoka Pwani ya Mtwara Mikindani kwenda Pwani ya Msangamkuu, kilizinduliwa siku moja baada ya kuzindua kipande cha barabara ya Ndundu-Somanga mkoani Lindi.
Kuzinduliwa kwa kipande hicho cha barabara kumeifanya Serikali kukamilisha ujenzi wa miradi 13 mikubwa katika Ukanda wa Maendeleo wa Mtwara.
Vilevile, kwa kukamilisha kipande hicho cha barabara ambayo ni sehemu ya Barabara Kuu ya Dar es Salaam-Kibiti-Lindi hadi Mingoyo, kunaifanya Serikali kutumia Sh9 trilioni katika miaka 10 ya uongozi wa Rais Kikwete.
Kilomita 60 za kipande cha Ndundu-Somanga ni sehemu pekee iliyokuwa imebakia kukamilisha ujenzi kwa kiwango cha lami, ambayo imekuwa kero kwa wananchi wa mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Lindi na Mtwara.
Baada ya tukio hilo juzi, Rais Kikwete jana aligeukia kivuko hicho na kusema kuwapo kwake ni utekelezaji wa ahadi alizotoa kwa wananchi.
Aidha aliwataka wananchi na wasafirishaji kuzingatia maadili ya kiwango cha uzito wa kivuko hicho.
“Suala la kivuko lilikuwa kero kubwa sana na tuliliona hasa watu walipokuwa wakivuka kutoka upande mmoja kwenda mwingine. Jambo muhimu ni kukitunza kivuko kwa kubeba watu na mizigo kwa kiwango kinachokubalika” alisema Rais Kikwete.
Awali, Dk Magufuli akimkaribisha Rais Kikwete alisema watu wa Mtwara walikuwa wakikabiliwa na changamoto ya kivuko.
“Mheshimiwa Rais, wakati unaingia madarakani tulikuwa na vivuko 13, lakini kwa kipindi chako tumeongeza vivuko vingine 15 na kukamilisha idadi ya vivuko 28 vyenye uwezo wa kubeba tani tofauti tofauti, kikiwamo hiki cha Mtwara ambacho gharama yake ni Sh3.3 bilioni na tumekarabati vivuko vingine saba,” alisema Dk Magufuli.
Akizungumzia viwango vya nauli vilivyopangwa, Dk Magufuli alisema ni Sh300 kwa mtu mzima, wanafunzi hawatatozwa, huku watoto na wanafunzi wasiovaa sare za shule watalipa Sh100.
Kuhusu miradi mingine ya Kusini, Waziri Magufuli aliitaja kuwa ni Daraja la Umoja lililokamika ujenzi wake, ujenzi wa barabara za lami ya Songea-Namtumbo; Peramiho Junction-Mbinga, Masasi-Mangaka na usanifu wa kina kwa ajili ya ukarabati wa Barabara ya Mtwara-Mingoyo-Masasi yenye urefu wa kilomita 200, ambao umekamilika.
Miradi mingine inayoendelea ni ujenzi kwa barabara za lami za Mangaka-Mtambaswala, Mangaka-Nakapanya, Nakapanya-Tunduru-Matemanga na Matemanga-Kilimasera yenye urefu wa kilomita 68.2.
Waziri Magufuli aliitaja miradi mingine inayoendelea ya ujenzi wa kiwango cha lami ni barabara za Kilimasera-Namtumbo, upembuzi yakinifu wa barabara ya Mtwara-Newala-Masasi na kuwa zabuni tayari imetangazwa kwa ajili ya ujenzi sehemu ya barabara ya Mtwara-Mnivata.
Madaraja 12 yajengwa
Kama ilivyo kawaida yake kutaja bila kusoma popote miradi anayojengwa na Serikali, Dk Magufuli alisema Serikali katika kipindi hicho imejenga madaraja makubwa 12, ambayo ni Rusumo (Kagera), Umoja (Mtwara), Mwanhuzi (Simiyu), Kikwete (Kigoma), Nangoo (Mtwara), Ruhekei (Ruvuma), Mbutu (Tabora), Mwatisi (Morogoro), Ruvu (Pwani), (Nanganga (Mtwara), Maligisu (Mwanza) na daraja la waendao kwa miguu la Mabatini (Mwanza).
Dk Magufuli pia alisema madaraja mengine madogo zaidi ya 7,200 yamejengwa na kukamilika katika kipindi cha uongozi wa Rais Kikwete, huku mengine makubwa saba yakiwa katika hatua mbalimbali za ujenzi ambayo ni Kigamboni (Dar es Salaam), Kilombero (Morogoro), Kavuu (Katavi), Sibiti (Singida), Ruvu Chini (Pwani), Lukuledi 11, (Mtwara) na Kolo la Dodoma.
Kana kwamba haitoshi, alisema kuna madaraja mengine makubwa ambayo yako katika maandalizi ya kujengwa.
Ni pamoja na Momba, Mwiti, Simiyu, Wami, Ruhuhu, Daraja jipya la Salendar, Daraja jipya la Wami Chini, Pangani na daraja la wandeao kwa miguu la Furahisha.
No comments:
Post a Comment