Sunday, January 29

Madaktari wawagomea mawaziri mkutanoni


SAKATA la madaktari nchini linazidi kuchukua sura mpya baada ya wataalamu hao kukataa hoja za ujumbe wa Serikali ulioongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi, Hawa Ghasia huku wakigoma kusikiliza kauli yoyote kutoka kwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk Hadji Mponda

Wakati mawaziri hao wakikumbwa ana tafrani hiyo tayari wauguzi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na ile ya Mkoa wa Dodoma wametishia kusitisha utoaji huduma ifikapo Jumatatu kama masuala yao hayajapatiwa ufumbuzi.

Vigogo wa Serikali waliofika kukutana na madaktari hao jana ni Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hadji Mponda na naibu wake, Dk Lucy Nkya, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Blandina Nyoni, Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Deo Mtasiwa.
Tukio hilo lilitokea jana kwenye Ukumbi wa Hoteli ya Star Light, Jijini Dar es Salaam ambako madaktari hao walikusanyika na baadaye kupewa taarifa kuwa kuna ujumbe wa Serikali utafika kwa majadiliano. Madaktari hao waliwatimua ujumbe huo baada ya kuusikiliza juu ya wito wao wa kuwataka wasitishe mgomo ili wafungue ukurasa wa majadiliano, wakajibiwa kuwa kwa sasa ni wakati wa kutekeleza kwa vitendo na siyo ahadi.

Ujumbe huo wa Serikali uliwasili ukumbini hapo majira ya mchana na kukaribishwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Stephen Ulimboka ambaye baada ya kuwawekea viti pembeni mwa jukwaa kuu, aliwatambulisha kwa washiriki. “Ugeni tuliokuwa tunasubiri umefika, si rahisi sisi wote kuwafahamu ni vema wangejitambulisha wao kwa majina kisha tuendelee na utaratibu tuliojiwekea,” alisema Dk Ulimboka.

Mara baada ya kauli hiyo, wageni hao walianza kujitambulisha. Wa kwanza alikuwa Waziri Ghasia aliyewasalimia madaktari hao na kujitambulisha kisha kueleza kuwa aliongoza ujumbe huo kuwasilisha taarifa ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda. Dalili mbaya kwa ujumbe huo, zilianza kujitokeza walipoitika kwa nguvu salamu ya Waziri Ghasia huku wakiwanyamazia Waziri wa Afya na maofisa waandamizi wa wizara hiyo.

Baada ya tukio hilo kumalizika, Dk Ulimboka alitoa taratibu za mkutano kuwa ni kusoma taarifa maalumu iliyoandaliwa kwa ajili ya kupelekwa kwa Waziri Mkuu. “Sisi hapa tutawakabidhi taarifa iliyoandaliwa na madaktari ambayo ni maalumu kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda na baada ya kuwasomea, tutawakabidhi kisha tusubiri majibu ya taarifa yetu tukiwa hapahapa,” alisema Dk Ulimboka.

Dk Ulimboka alisoma taarifa hiyo mbele ya wageni hao ambayo ilitaja madai yao kadhaa ikiwemo kumtaka Waziri Ghasia kumshauri Rais Jakaya Kikwete kuwaondoa katika wizara hiyo, Waziri Mponda na naibu wake Dk Nkya, Katibu Nyoni na Mganga Mkuu, Dk Mtasiwa.

Mara baada ya kusoma taarifa hiyo alikabidhi barua hiyo kwa Waziri Ghasia huku akisisitiza kuwa wataendelea na mgomo hadi watakapopatiwa majibu ya hoja zao.

“Tunaomba taarifa hiyo imfikie haraka Waziri Mkuu, ijadiliwe kwa haraka na kutoa majibu yatakayotupatia ufumbuzi ili nasi turudi kazini tukaokoe maisha ya Watanzania,” alisema Dk Ulimboka ambaye kwa kauli yake iliashiria kufunga mjadala.

Baada ya kauli hiyo, Waziri Ghasia alisimama na kueleza kuwa wao walifika wakiwa na ujumbe toka kwa Waziri Mkuu hivyo ni vema wangekubaliwa wauwasilishe ambapo alimtaja Waziri wa Afya Dk Mponda kuwa angeusoma.
Dk Ulimboka alijibu hoja hiyo akisema “Madaktari hatuna tatizo na ujumbe toka kwa waziri Mkuu Mizengo Pinda ila ujumbe kutolewa na Waziri wa Afya Dk Hadji Mponda hatukubali kwasababu hatuna imani naye labda kama kweli ni taarifa, ungesoma wewe,” alisema Dk Ulimboka na kukaa chini.

Waziri Ghasia alikubaliana na hoja hiyo na katika kuwasilisha taarifa hiyo, alisema alisononeshwa kusoma majibu yanayohusu madai ya madaktari hao kwa niaba ya waziri mwenye dhamana ya Wizara ya Afya wakati yeye (Dk Mponda) akiwepo.

Ghasia alisema wizara imetafakari kwa kina suala la madaktari waliokuwa kwenye mafunzo katika Hosptali ya Taifa ya Muhimbili na kuwarudisha kwenye kituo hicho cha kazi huku ikiahadi kuwalipa stahili zao.
“Wazira imetafakari kwa kina na imeamua kuwarejesha madaktari wote waliokuwa kwenye mafunzo ya vitendo katika Hosptali ya Taifa ya Muhimbili na wanatakiwa kuripoti katika vituo hivyo vya kazi kuanzia Jumatatu,” alisema Ghasia.

Kuhusu madai mengine, alisema Serikali itaendelea na majadiliano ya pamoja huku akiwaomba warejee kazini.
“Sisi tuwaombe tu kwamba madai yenu yote Serikali inayafanyia kazi. Suala la nyumba tayari tumeshapata fedha kutoka Global Fund kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za madaktari ili waweze kukaa karibu na vituo vyao vya kazi,” alisema Ghasia. Akijibu ombi la kuwataka warejee kazini, Dk Ulimboka alisema hilo litategemea majibu ya taarifa walioiwasilisha kwa Waziri Mkuu, ambapo alisisitiza kuwa wao wataendelea na mikutano katika ukumbi huo.

“Sisi tutaendelea na mikutano kujadili taarifa yenu na pia tungeshauri taarifa hii mtuletee kwa maandishi, lakini pia tunasubiri majibu ya taarifa yetu tuliyoiwasilisha kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambayo tumeitoa kwa maandishi,” alisema Dk Ulimboka. Dk Uliomboa aliwataka wawakilishi hao wa Serikali kutambua kuwa ujumbe haukuwa wa kushawishiana kurudi kazini bali ni wa kupeana taarifa.

Kauli hiyo iliashiria kwamba hoja ya ujumbe huo haina uzito wa kuwashawishi kuacha mgomo huku wakikataa hoja zao sasa kujadiliwa na wizara badala yake walisisitiza Waziri Mkuu kushughulikia suala hilo. Walimtaka Waziri Mkuu, kutoa majibu ya madai yao kwa wakati ili asiwafanye kufikia hatua ya kusitisha huduma katika vitengo vya dhararu.

“Mgomo huu unaendelea nchi nzima hadi majibu ya madai yetu tuliyowasilisha kwa Waziri Mkuu yamepatiwa majibu.
Tunashauri kazi hiyo ifanywe haraka vinginevyo tusije tukashawishika kusitisha huduma kwenye vitengo vya dharura,” alisema Ulimboka.

Tishio la mgomo zaidi
Wakati huo huo, Chama cha Wauguzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, kimesema kuwa wauguzi wataendelea kutoa huduma kwa kusuasua hadi Jumatatu na kama suala hilo litakuwa halijapatiwa ufumbuzi, watasitisha huduma na kufunga hospitali.

“Sisi tutaendelea kutoa huduma katika mazingira ya shida hivi mpaka Jumatatu tu,” alisema Mwenyekiti wa chama hicho, Paul Magesa.

Habari kutoka katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma zilieleza pia kuwa, kwa sasa hakuna wagonjwa wapya wanaopokelewa na kuwa waliopo wodini wakitoka, hospitali hiyo nayo itasitisha kutoa huduma.

Urais CCM 2015 balaa

KIGOGO AMWAGA MAMILIONI, ATUMA MAKADA MIKOANI KUMNYOSHEA NJIA
WAKATI Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikionya wanachama wake kuacha ndoto za urais wa mwaka 2015, kauli hiyo sasa imeonekana kupuuzwa na kugeuka kichocheo cha kuongeza kasi ya kujipanga kwa baadhi ya makada wenye nia ya kusaka nafasi hiyo ya juu ya uongozi wa taifa.Hivi karibuni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya CCM, Nape Nnauye, alionya kwamba chama hicho hakiko tayari kuendelea kuwakumbatia wanachama wake wanaunda makundi ndani ya chama, kwa lengo la kusaka umaarufu wa kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao mwaka 2015.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam, Nape alisisitiza kuwa endapo mwanachama yeyote atabainika kuvuruga mshikamano ndani ya chama kutokana na kigezo hicho, CCM haitasita kuchukua hatua kali dhidi yake.

Pamoja na CCM kutoa onyo hilo kali, mbio za urais wa mwaka 2015 ndani ya chama hicho, zimeelezwa kuingia katika sura mpya baada ya mmoja wa makada anayetajwa kuwania nafasi hiyo, kufanya kikao kizito jijini Arusha, kwa lengo la kuweka mikakati ya kujipanga na kuimarisha kambi yake.

Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na baadhi ya wana CCM mjini Arusha, zinaeleza kuwa, kigogo huyo alifanya kikao chake wiki chache zilizopita katika moja ya majengo ya mfanyabiashara mmoja kutoka Kanda ya Ziwa, yaliyopo nje kidogo ya jiji.

Kikao hicho kilichohudhuriwa na baadhi ya viongozi wa CCM kutoka mikoa mbalimbali nchini, wakiwamo baadhi ya wenyeviti wa mikoa wa chama hicho na baadhi ya viongozi wa Serikali, pamoja na mambo mengine, kilifanya tathmini ya kina kujua maeneo ambayo mgombea huyo hakubaliki.

Chanzo chetu kilidokeza kwamba tathmini hiyo ilionyesha kuwa kada huyo hakubaliki sana katika mikoa ya Lindi , Mtwara pamoja na maeneo ya mikoa ya Kanda ya Ziwa, ukiwemo Mkoa wa Mara.

Kutokana na hali hiyo, ilikubaliwa kuwa fedha nyingi zitumike na watu mahiri wenye ushawishi, watumwe katika maeneo haya ili kuwalainisha baadhi ya viongozi wa CCM ambao wanaonekana kuwa mbali na mgombea huyo, na jambo hilo lifanyike haraka kabla ya kuanza kwa chaguzi mbalimbali ndani ya CCM mwaka huu.

Kauli ya Nape
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alipoliuzwa kuhusiana na kikao hicho, alisema hana taarifa zozote lakini alionya kuwa endapo itathibitika kuwa kuna makada wa chama hicho wanafanya ‘rafu’ hizo, watachukuliwa hatua za kisheria za chama kwani huu si muda wa kufanya kampeni za urais.

Aliwataka wanachama wa CCM kuipa nafasi Serikali yao kutekeleza majukumu yake na ilani kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania.Awali, pia Katibu huyo wa Itikadi na Uenezi, aliwahi kukaririwa akisema kuwa wanaotarajia kutumia fedha kupata urais kupitia chama hicho wanajidaganya, ni bora watafute kazi nyingine za kufanya.


Kikao cha mkakati
Habari zaidi kutoka ndani ya kikao hicho, zililidokeza Mwananchi Jumapili kuwa makada watakaotumwa kuzunguka mikoani, baada kukamilisha kazi yao, watatakiwa kurejesha ripoti itakayofanyiwa kazi, ili kundi hilo liweke mikakati zaidi ya kufanikisha lengo lake.

Inaelezwa kuwa hofu kuu ya kundi hilo, ni kutoka kwa baadhi ya makada wengine wa CCM, wanaotajwa kuonyesha nia ya kuwania nafasi ya urais, kukubalika zaidi ndani ya chama katika mikoa hiyo, ambapo baadhi yao wanatoka huko.
Chanzo chetu kilidokeza pia kuwa mbali ya kuweka mikakati hiyo kabambe ya kuwania urais, pia wajumbe wa kikao hicho ‘kizito’, walifanyiwa sherehe kubwa ambapo nyama na vinywaji mbalimbali vilimwagwa kwa wingi, ndani ya majengo ya mfanyabiashara huyo, ambayo yamezungushiwa ukuta mrefu.

“Aisee! kikao kilikuwa kizito mno mikakati mizito imewekwa , jamaa yuko serious (makini) kuutaka urais, “alidokeza kada mmoja aliyekuwa ndani ya kikao hicho kwa sharti la kutoandikwa jina gazetini.
Uchunguzi wa Mwananchi Jumapili umebaini kuwa tayari, makada waliotumwa kwenda mikoani ‘kumnyoshea njia’ mgombea huyo wa urais, hivi sasa wanavinjari kwenye maeneo hayo, wakiwa na fedha za kutosha na vitendea kazi vingine, yakiwemo magari ya uhakika.

Waliotumwa kufanya kazi hiyo, ni wenyeviti wa baadhi ya mikoa ambao imeelezwa kuwa watatumia nafasi zao kufanya ushawishi huo kwa urahisi.

Ingawa hadi sasa hakuna kada ndani ya CCM ambaye ametangaza hadharani kutaka kuwania urais, inadaiwa kwamba kuna kundi kubwa la watu ambao tayari wanapigana vikumbo chini chini kutaka nafasi hiyo, kutokana na Rais wa sasa Jakaya Kikwete, kufikia ukomo wake kikatiba mwaka 2015.

Hatua hiyo imedaiwa kuibua makundi yanayosabisha nyufa zinazoweza kuleta mgawanyiko mkubwa ndani ya chama hicho.
Tayari CCM kimekiri kupitia Katibu Mkuu wake, Wilson Mukama kuwa harakati za kuwania urais ndani ya chama hicho, zinakivuruga.

Taarifa ya Kamati Kuu ya CCM iliyosomwa ndani ya Kikao cha Halmashuari Kuu (NEC) ya CCM mjini Dodoma Novemba mwaka jana ,pamoja na mambo mengine, ilikiri kuwa mbio za kuwania urais mwaka 2015 ndani ya chama hicho, ndicho kiini kikuu cha mgawanyiko.

Kamati Kuu ilionya kuwa wanaotaka kuwania nafasi ya urais kupitia chama hicho, wanapaswa kudhibitiwa na kwamba matumizi ya fedha katika kampeni hayatakubalika.

Ushauri wa Kinana
Alhamisi wiki hii, Mjumbe wa Kamati Kuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alikaririwa na gazeti la Mwananchi akieleza kuwa vigogo wa chama hicho walioanza kampeni za urais, sasa wanavuruga utendaji wa Serikali ya Rais Kikwete.
Akiwa kwenye ziara ya kutembelea matawi ya CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Kinana alisema vigogo hao ni wabinafsi, wanaivuruga nchi na hawana lolote wanalolifanya kwa maslahi ya chama hicho tawala.

Kinana ambaye pia alikuwa Mkurugenzi wa Kampeni za Rais Jakaya Kikwete wakati akigombea urais kwa CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, alionesha kukerwa na watu hao na kueleza kuwa si sahihi kuanza kuzungumza masuala ya urais sasa wakati Rais Kikwete bado ana miaka minne ya kutekeleza Ilani ya chama hicho.

“Sasa hivi Rais Kikwete ana miaka mingine minne mbele kabla ya kumaliza uongozi wake na CCM ina kero nyingi za kushughulikia ili kutekeleza ilani yake, halafu wengine wanazungumzia urais sasa,” alikaririwa akisema Kinana.
Alisema anasikitishwa na hali hiyo hasa ikizingatiwa kuwa wanaoanza kupiga kampeni za urais ni watu wazito ndani ya nchi na ni wajumbe wa vikao vikuu ndani ya CCM.

Tishio lingine
Mbali ya chama hicho kukabiliwa na tishio la mgawanyiko kutokana na urais wa 2015, pia kinakabiliwa na kazi ngumu ya utekelezaji wa mkakati wake, kuwavua gamba baadhi ya makada wake wanaohusishwa na kashfa za ufisadi.

Kikao kilichopita cha NEC ambacho kilitarajiwa kuchukua maamuzi magumu ya kuwavua gamba wanachama hao, kilishindwa kufanya hivyo, badala yake kikatoa muda kwa wanachama hao kujitathmini wenyewe na kuchukua uamuzi kabla ya CCM kuwachukulia hatua.