UHUSIANO wa mwanamuziki maarufu wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ na mjasiriamali Mganda, Zarina Hassan ‘Zari The Boss Lady’, unawaka moto na huenda wasiwe na mwisho mzuri, MTANZANIA linaripoti.
Penzi la wawili hao ambao wamejaaliwa watoto wawili; Tiffah na Nillan, limeonekana kupoteza afya tangu wakati na baada ya Diamond kukiri kwenye redio moja jijini Dar es Salaam, kuzaa na mwanamitindo Hamisa Mobetto.
Katika maelezo yake, wakati akithibitisha madai hayo ya muda mrefu, Diamond aliomba radhi kwa mzazi mwenzake Zari, lakini inaelezwa kuwa Zari hakuridhika na kurudisha moyo wa kumsamehe mpenzi wake.
Baada ya tukio la kuomba radhi, Diamond alionekana kwa mara ya kwanza akiwa pamoja na Zari kwenye sherehe ya kuzaliwa ya mzazi mwenzake huyo iliyofanyika nchini Afrika Kusini.
Aidha, Diamond kupitia ukurasa wake wa Instagram aliandikia ujumbe mzuri wa kumpongeza Zari kwa kumbukumbu yake ya kuzaliwa, huku akionyesha kujutia kwa kuchepuka na Hamisa.
Kinyume na matarajio ya wengi, wakati Diamond naye akiadhimisha siku yake ya kuzaliwa Oktoba 2, Zari hakuandika chochote kama walivyozoea kufanya wapendanao, badala yake zikaanza ‘vurugu za mitandao’ zilizoonyesha wazi penzi lao kwa sasa lipo kwenye wingu zito.
Tukio la hivi karibuni linaloonyesha kuwa ‘picha limeanza’ ni lile la Zari kufuta picha zote za Diamond kwenye ukurasa wake katika Mtandao wa Kijamii wa Instagram na kuacha picha tatu tu ambazo wamepiga na familia ya Diamond.
Baada ya Zari kufanya hivyo, Diamond naye alijibu mapigo kwa kufuta picha zote za mwaka huu za mrembo huyo isipokuwa picha mbili tu; moja ikiwa ya sherehe ya siku ya kuzaliwa ya Zari.
Zari alikwenda mbali zaidi kwa kuandika ‘maneno yenye ukakasi’ kupitia ukurasa wake kwenye Mtandao wa Kijamii wa Snapchat ambapo aliandika: “Hakuna tena uthibitisho wa wanaume kwenye mitandao ya kijamii na kukufanya kuonekana mjinga.”
Kituo cha Runinga cha NTV nchini Kenya katika taarifa yake ya habari ya juzi, kiliripoti taarifa za wawili hawa kuonekana kutengana.
Hatua hiyo imeendelea kuwaacha watu bila majibu ya uhakika, huku kila mmoja akiamini huo unaweza kuwa mwanzo wa mwisho wa penzi lao licha ya wenyewe kutoweka wazi kinachoendelea kati yao.
Wakati huohuo, mwanamitindo Hamisa Mobetto, mzazi mwenzake na Diamond amemburuza mahakamani msanii huyo kwa madai ya matunzo ya mtoto wao, Daylan ‘Abdulatiff’.
Habari zilizopatikana Dar es Salaam jana, zinasema kuwa kesi imefunguliwa katika Mahakama ya Watoto.
Katika madai yake Hamisa kupitia mawakili wake, Abdullah Lyana na Walter Godluck wa Kampuni ya Uwakili ya Century Attorneys, anaomba Diamond amuombe radhi kwa umma kwa kumsababishia madhara yaliyoishtua familia yake na pia amkubali mtoto huyo kuwa wake kwa masharti ya wazi.
Msanii huyo alitumiwa wito Septemba 14, mwaka huu akitakiwa mahakamani hapo kwa ajili ya mwafaka wa madai yaliyofunguliwa dhidi yake ambapo hakujibu. Kutokana na hali hiyo, Hamisa kupitia mawakili wake hao akafungua kesi kwa mujibu wa Sheria ya Watoto Namba 42, 43 na 98 ya mwaka 2009.
Anadai Diamond amlipe Sh milioni tano kwa mwezi kwa ajili ya matunzo yake na mtoto au zaidi kama mahakama itakavyoamua kutokana na hali yake kutotengemaa tangu amejifungua ambapo amekuwa akijihudumia mwenyewe.
Hamisa anadai alipwe Dola za Marekani 15,000 ambazo ni zaidi ya Sh milioni 30 kama gharama za mtoto hadi sasa.
Katika madai hayo, Hamisa pia anadai maombi hayo yakishindwa kutimizwa ndani ya siku saba baada ya mlalamikiwa kupokea wito huo, watafungua madai mapya dhidi yake ambayo yanajumuisha uamuzi wa baba wa mtoto.
Aidha, katika madai hayo atalazimika kudai fidia kutokana na matusi na maneno yasiyofaa dhidi yake yaliyotolewa na Diamond na mpenzi wake Zari ambayo yamemsababishia maumivu.
Aidha, Hamisa amekubali kuwa alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Diamond, ambapo walikubaliana uwe wa siri uliomsababishia kupata mimba na kufanikiwa kupata mtoto wa kiume.
“Kutokana na ujauzito huo, alikubali kuachana na kazi yake ya uanamitindo ili kupata nafasi kubeba kitu ambacho ulikuwa unakihitaji sana (mtoto) kwa mujibu wa maneno yako mwenyewe, ambapo alijitolea kwa ajili ya kujiandaa kuwa mama.
“Katika uhusiano wenu mara baada ya kujifungua Agosti 8, mwaka huu ndipo maigizo yalipoanza baada ya wewe kuamua kuchagua hospitali ya yeye kujifungulia na daktari wa kumhudumia, lakini hukufanya malipo yoyote, hatua iliyosababisha mteja wetu na mama yake kuhangaika na kulipa gharama zote peke yao.
“Mwisho wa siku uliacha kabisa kumhudumia mteja wetu pamoja na mtoto wake, ambapo ilimlazimu mama yake kumhudumia yeye na mjukuu wake hasa ukizingatia mteja wetu amejifungua kwa njia ya upasuaji, ambapo anahitaji zaidi uangalizi wa karibu, maziwa, nguo na fedha za matumizi kutoka kwako ukiwa baba mtoto wake lakini aliambulia matusi, kudhalilishwa na maneno machafu kutoka kwa timu yako,” anadai Hamisa katika madai yaliyoandikwa na wakili wake.
Pamoja na mambo mengine, Hamisa anadai Diamond ameendeleza vitimbi kwa kumdhalilisha kwenye vyombo vya habari pamoja na mtoto wake, hali inayomuumiza pamoja na familia na mashabiki wake.
“Pamoja na hayo, mteja wetu hakuwahi kujibu chochote hata pale uliposema mimba si yako katika mahojiano mbalimbali uliyofanya na vyombo vya habari.
“Mteja wetu amekuwa mvumilivu ambapo ulitumia udhaifu wake huo wewe na mpenzi wako, Zarina Hassan kwa kumtishia maisha, kumtukana na kumdhalilisha yeye na mtoto wake kwa kumtumia ujumbe mfupi wa maandishi na katika mitandao ya kijamii ikiwamo Instagram, Facebook na mingineyo,” maelezo hayo yamesema yakimnukuu Hamisa.