Friday, October 6

Wabunge kupewa fedha kuomba ushauri ukomo umri wa rais


Kampala, Uganda. Kila mbunge anatarajiwa kupewa kiasi fulani cha fedha zitakazomsaidia kupata ushauri kwa wapigakura jimboni kwake kuhusu Muswada wa Marekebisho ya Sheria wa 2017 unaolenga kuondoa ukomo wa umri kwa wagombea urais.
Baada ya muswada huo kusomwa kwa mara ya kwanza na Raphael Magyezi, mbunge wa Igara Magharibi kutoka chama tawala cha NRM, kisha kupelekwa katika Kamati ya Kudumu ya Sheria na Huduma za Bunge, Jumanne Spika Rebecca Kadaga aliwataka wabunge kwenda kushauriana na wapigakura wao.
Baada ya uamuzi huo wa Spika, mnadhimu mkuu bungeni Ruth Nankabirwa amesema Tume ya Bunge inafikiria kutenga bajeti maalumu kwa ajili ya kuwarahisishia wabunge.
“Tume ya Bunge inajiandaa kutengeneza bajeti kwa sababu ni Bunge ambalo litaturahisishia sisi sote …Tutaelezwa ni kiasi gani na namna gani kila mbunge atapata na kwenda kushauriana kwa sababu tunahitaji usafiri,” Nankabirwa ameviambia vyombo vya habari.
Nankabirwa hakuweka wazi undani wa bajeti hiyo akisema tu kwamba Tume ya Bunge ndiyo itapanga na kubainisha kiasi kinachohitajika. Lakini mbunge wa Kakumiro kutoka NRM, Robinah Nabbanja ambaye ni mjumbe wa Tume ya Bunge alisema mgawo huo utakuwa kwa wabunge wote bila kujali vyama vyao.
“Tutakutana haraka na kukubaliana. Sitaweza kukutajia kiwango kwa sasa kwa sababu bado hatujakubaliana. Huwezi kuwatuma wabunge (kupata ushauri) bila kuwawezesha kiasi,” amesema Nabbanja.
Kuhusu suala la wapi fedha hizo zitatoka hasa ikizingatiwa hazijatengwa katika bajeti ya sasa, Nabbanja amesema watapunguza kutoka kasma ya safari za nje.
“Jambo lolote linapokuwa la dharura, kwa kawaida huwa tunagusa fedha za usafiri wan je, tunaweza kuhamisha vifungu ndani ya bajeti,” amesema.
Mnadhimu wa kambi ya upinzani Ibrahim Ssemujju amepuuza uwezeshaji huo akiuelezea kuwa ni jaribio la “kusafisha rushwa kwa wabunge”.

No comments:

Post a Comment