Tuesday, March 22

Salma asimulia alivyotekwa


Mwandishi wa habari wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) na DW, Salma Said amedai alitekwa na wanaume wawili baada ya kumkamata na kumuingiza kwenye gari lao kisha kuondoka naye na kumpeleka kusikojulikana.
Salma aliyetekwa Ijumaa iliyopita na watu hao katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) akitokea Zanzibar kwa ajili ya  kuchunguzwa afya yake kwenye moja ya hospitali za jijini hapa, alisimulia mkasa huo jana mbele ya  waandishi wa habari huku akimwaga machozi.
Alisema alipoteremka uwanjani hapo, alimpigia simu dereva wake amfuate na wakati akimsubiri,  ndipo wakatokea watu hao.
Salma alisema watu hao walimfunga mtandio wake mweusi usoni ili asibaini mahali walikokuwa wakimpeleka na kumfungia chumbani
Alisema ndani ya chumba hicho kulikuwa na vitambaa.  
“Waliponiingiza ndani ya chumba kile siku ya kwanza, wakanifungua tambala usoni kwa hivyo nikawaona nyuso zao, mmoja alikuwa na kovu shavuni, mrefu na mwingine mweupe kidogo, waliniweka kule ndani bila kupata chakula chochote,” alisema.
Salma alisema alitakiwa kurudi Zanzibar kwa ajili ya kuripoti marudio ya Uchaguzi Mkuu wa marudio uliofanyika juzi, lakini alishindwa baada ya watu hao kumteka na kumfungia kwenye chumba hicho.
Alidai kuwa watu hao walimwambia watamuachia baada ya uchaguzi huo kufanyika na mgombea wa CCM kutangazwa kuwa mshindi.
Katika mkutano huo na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi za Baraza la Habari Tanzania(MCT), Salma aliongozana na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Theophil Makunga, Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga na Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Bara (THRDC), Onesmo Ole Ngurumwa, ambao kwa pamoja walieleza kupinga ukatili huo huku wakiliomba Jeshi la Polisi kuwasaka wahalifu waliohusika.
“Walinisababishia maumivu makali, walinipiga mabuti na makofi huku wakiniambia maneno ya vitisho kama ilivyokuwa kwa Dk Ulimboka na Kibanda,” alidai Salma.
Kabla ya watekaji hao kumrudisha katika eneo walilokuwa wamemteka, Salma alidai kuwa watu hao walimpiga kila walipoingia na kutoka nje ya chumba alichowekwa na kumsababishia apumue kwa tabu.
Akijibu swali la mwandishi wa habari aliyetaka kupata ufafanuzi wa taarifa za uvumi wa kujiteka mwenyewe, Salma alijibu swali hilo  huku akidondosha machozi: “Hakuna sababu ya kusema uongo, mimi ni Mwislamu na dini yangu inakemea kufanya hivyo.” 
Pia, alisema amefanya kazi kwa miaka zaidi ya 20 na matukio ya vitisho yalianza alianza kuyapata muda mrefu kwa kupigiwa simu, kutumiwa meseji na kufuatwa nyumbani kwake.
Salma ambaye alizungumza huku akionyesha ushahidi wa meseji za makundi ya mitandao yanayojadili kufurahishwa na kutekwa kwake, alisema kujiteka ni kauli zisizokuwa na uhusiano wowote na ukweli, kwani alijitambulisha kuwa mwandishi mtetezi wa haki za binadamu na siasa ambazo zinazokinzana na maslahi ya wachache.
Wakati huohuo; Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Siro alisema ni mapema kuzungumzia tukio la kutekwa kwa Salma kwa madai kuwa bado wanaendelea kufanya uchunguzi.

MOTISHA KWA WALIMU NA ARI YA UFUNDISHAJI

Siri ya madini Tanzanite kutoroshwa yabainika


Dar es Salaam. Udhaifu wa sheria zinazosimamia uchimbaji wa Tanzanite umetajwa kuwa chanzo cha madini hayo kuuzwa kwa wingi na nchi za Kenya, India na Afrika Kusini badala ya Tanzania yanakopatikana.
Hayo yalibainika wiki iliyopita katika ziara ya wahariri wa vyombo vya habari kwenye mgodi wa TanzaniteOne Mine Limited (TML), uliopo Mirerani Simanjiro mkoani Manyara.
Mkuu wa Usalama wa TML, George Kisambe alisema ingawa wameimarisha ulinzi kwa asilimia 90 kwa kushirikiana na Stamico chini ya Serikali, udhaifu kwenye sheria unatoa mwanya kwa hujuma dhidi ya Tanzanite na kampuni yao.
“Usimamizi wa sheria ndiyo unaosababisha Kenya na India zionekane kuongoza katika uuzaji Tanzanite inayochimbwa Tanzania pekee,” alisema Kisambe.
Hali hiyo inatajwa pia kudhoofisha usalama na kuwasukuma wawekezaji kuweka idadi kubwa ya walinzi kwenye migodi yao kudhibiti hali ya usalama kwa kuhofia uvamizi wa maeneo yao ya uchimbaji.
“Ili kurekebisha hali hiyo ni vyema Serikali ije na mkakati mbadala wa usimamizi wa madini haya, ikiwezekana iweke ukuta kama ilivyo kwa Israel na Palestina kuzitenganisha na kutambua maeneo yote ya uchimbaji,” alisema.
Alisema kitakwimu kampuni hiyo inachimba chini ya asilimia 30 ya madini yote ya Tanzanite na mapato yake yanajulikana na Serikali kwa kuwa na udhibiti huku ikilipa kodi.
Kaimu Mkurugenzi wa TML, Modest Apolinary alisema uvamizi wa wachimbaji wadogo katika mgodi huo ni changamoto inayopoteza kiwango kikubwa cha mapato na kuiomba Serikali kumaliza tatizo hilo.
“Serikali ina mamlaka ya kufanya uamuzi dhidi ya wachimbaji wavamizi ili TML iendelee kuchimba eneo lake, iongeze ajira kwa vijana na ichangie zaidi mapato ya Serikali kwa kulipa kodi inayotakiwa,” alisema Apolinary.

Wawili wafariki Dar kwa dalili za ebola

Dar es Salaam. Watu wawili wamefariki dunia kwa maradhi ambayo dalili zake zinafanana na ugonjwa wa ebola.
Watu hao walifariki baada ya kufikishwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) wakiwa wanatoka damu sehemu mbalimbali za miili yao ikiwamo kwenye ngozi, mdomoni, puani na matundu mengine ya mwili.
Mgonjwa wa kwanza alifariki dunia Machi 16 saa nane usiku na mwingine jana mchana. Wote walifariki ndani ya saa 12 baada ya kufikishwa hospitalini hapo.
Mkuu wa Kitengo cha Uchunguzi wa Magonjwa MNH, Dk Praxeda Ogweyo alisema wamewapokea wagonjwa hao wawili,  lakini vipimo havijaonyesha kama wana ebola.  “Ni kweli kuwa tumewapokea wagonjwa hao wawili na vipimo vya mgonjwa wa kwanza kinaonyesha hana ebola, lakini bado wanaendelea kufanya uchunguzi wa kina kujua ni ugonjwa gani,” alisema.
Dk Ogweyo alisema majibu ya mgonjwa wa pili aliyefariki jana bado hayajatoka.
Taarifa za awali zilizopatikana kutoka kwa ndugu wa marehemu zinaeleza kuwa wagonjwa hao wote walipita Mafinga, Iringa kabla ya kuja Dar es Salaam.
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema wizara yake imepokea taarifa hizo: “Tumepeleka sampuli kwenye maabara ya Taifa, majibu yote ni negative (hawana ebola). Hata hivyo, tumeamua kupeleka nje ya nchi kwa ajili ya kujiridhisha zaidi,” alisema.
Waziri Mwalimu alisema sampuli hizo mbili za damu zimepelekwa Taasisi ya Uchunguzi wa Magonjwa Kenya (KIMR).
Hata hivyo, alisema miili yao itazikwa na Serikali kupitia ofisi ya Mganga Mkuu wa Serikali na ndugu wa marehemu watapewa ushauri nasaha.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Grace Mganga alisema kutokwa na damu kunaweza kuwa na sababu nyingi, ikiwamo homa ya dengue, ebola na upungufu wa chembe ndogo za damu zinazouia damu kutoka kwa wingi.
Shemeji wa mmoja wa marehemu hao, Juma Seromba alisema ndugu yao alianguka akiwa kazini kama mgonjwa wa kifafa, akaanza kutokwa damu sehemu mbalimbali mwilini na baadaye walimpeleka MNH.

Pengo la CUF lajitokeza wazi Pemba

https://youtu.be/LCY1dmtFE1E
Pemba. Kitendo cha CUF kususia uchaguzi kimeelezwa kuwa kwa kiwango kikubwa kimesababisha watu wachache kujitokeza katika uchaguzi wa marudio uliofanyika jana.
Wasimamizi wa vituo vya uchaguzi, wapigakura, ambao hawakupiga kura na baadhi ya viongozi waliozungumza na gazeti hili kisiwani Pemba walisema pamoja na mambo mengine, kitendo cha CUF kutoshiriki uchaguzi huo kimechangia hali hiyo.
Uchaguzi huo wa marudio umefanyika baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Jecha Salim Jecha kufuta matokeo ya udiwani, uwakilishi na urais Oktoba 28 mwaka jana kwa maelezo kuwa ulikuwa na kasoro nyingi.
Mwandishi wetu alitembelea vituo zaidi ya 10 katika mikoa ya Kusini Pemba na Kaskazini Pemba na kukuta idadi ndogo ya wapigakura, jambo ambalo liliwafanya wasimamizi wa vituo hivyo kutumia muda mwingi kupiga stori.
Mbali na wasimamizi hao, hata mawakala wa vyama waliokuwapo katika vituo hivyo wengi walikuwa wa CCM na wachache wa ADC na Tadea, tofauti na idadi ya vyama vilivyotangazwa kushiriki uchaguzi huo.
Pemba kuna vituo vya uchaguzi 463 na kila kimoja kilipaswa kuwa na wapigakura takribani 1,000 hadi 3,500, lakini mpaka kufikia jana saa sita mchana vingi vilikuwa tupu huku wasimamizi wakikiri kuwa idadi ya waliojitokeza ni ndogo.
Msimamizi wa uchaguzi katika kituo cha Wawi A, Kusini Pemba, Ismail Issa Juma alisema jambo pekee lililojitokeza katika kituo hicho ni idadi ndogo ya wapigakura.
Alisema kituo hicho kina wapigakura 1,400 na waliokuwa wamejitokeza mpaka kufikia saa nne asubuhi walikuwa hawajafika robo ya idadi hiyo.
Mgombea urais kwa tiketi ya ADC, Hamad Rashid Mohamed ambaye alipiga kura katika kituo hicho alisema kutoshiriki kwa CUF ni sababu ya wananchi kutojitokeza.
“Hapa Pemba CUF wana nguvu. Hii ni ngome yao, hivyo usitegemee kuona watu wengi hapa ila binafsi ninaamini asilimia 40 ya watu wote waliojiandikisha kupiga kura watajitokeza leo (jana) kuchagua viongozi wanaowataka,” alisema Hamad ambaye alivuliwa uanachama wa CUF na kuanzisha ADC.
Alisema anaamini atashinda urais katika uchaguzi huo kutokana na CUF kujitoa, huku akisisitiza kuwa kasoro zilizopo ZEC na Serikali ya Mapinduzi  Zanzibar (SMZ), zitamalizwa likipatikana baraza la wawakilishi na rais na si kususia uchaguzi.
Msimamizi wa uchaguzi katika kituo cha Wawi B ambacho mgombea urais wa AFP, Said Sudi Said alipiga kura, Mussa Abdallah Kilindo alisema si rahisi wapigakura 950 katika kituo hicho wote wakapiga kura.
Mkazi wa Wawi, Omar Mohammed Hassan alisema idadi ya watu waliojitokeza ina tofauti kubwa na ya uchaguzi wa Oktoba 25 kauli ambayo iliungwa mkono na mkazi mwingine wa eneo hilo, Mafunda Abdalla.
Hali ilikuwa tofauti zaidi katika vituo vya kupigia kura vilivyopo Wilaya ya Wet, Kaskazini Pemba ambako pia kunatajwa kuwa ngome ya CUF kutokana na kujitokeza kwa watu wachache zaidi.
Mwandishi wetu alishuhudia baadhi ya wasimamizi wa vituo hivyo wakiwa wamelala katika madawati wakisubiri wapigakura ambao walikuwa wakifika mmojammoja.
“Kama unavyoona shughuli ya kupigakura inaendelea vyema kabisa na kuna usalama wa kutosha. Watu wanakuja ila si wengi kama ilivyokuwa Oktoba 25. Kituo hiki kina wapigakura 1,950,” alisema Maalim Haji, msimamizi wa uchaguzi Kituo cha Shule ya Msingi Kizimbani.
Mkazi wa Kizimbani, Sada Hamad Shamata aliyekutwa akipiga kura katika kituo hicho alisema: “Uchaguzi umekwenda vyema na hakuna usumbufu wala kusukumana maana watu ni wachache tofauti na uchaguzi uliopita.”
Mkazi mwingine wa Kizimbani, Ali Juma Fakih alisema: “Hilo siyo swali sheikh ni jibu. CUF kususia uchaguzi huu ndiyo sababu ya wapigakura kuwa wachache.”
Mkuu wa wilaya ya Wete, Rashid Hadid Rashid aliyekuwa akizunguka vituo vyote vya uchaguzi vilivyopo katika wilaya hiyo alisema ni kawaida uchaguzi wa marudio kujitokeza watu wachache.
“Pemba CUF wapo wengi hilo lipo wazi ila binafsi kama mkuu wa wilaya nina jukumu la kuhakikisha hali ya usalama inakuwa shwari,” alisema Rashid.
Katika Kituo cha Ukunjwi, Jimbo la Gando, Kaskazini Pemba mwandishi wetu alishuhudia wapigakura watatu waliojitokeza baada ya kukaa hapo kwa nusu saa.
Katika kituo hicho baadhi ya majina ya wapigakura yaliyobandikwa ukutani yalikuwa yamechanwa hivyo kuwapa wakati mgumu waliofika kupigakura.