Massawe anayetarajiwa kuletwa nchini wakati wowote kuanzia sasa, alikuwa anatafutwa na Polisi wa Tanzania kwa muda mrefu na alikamatwa Dubai, mapema Julai na maofisa wa usalama wa UAE baada ya alama zake za vidole kuonyesha kuwa alikuwamo kwenye orodha ya watu waliokuwa wanasakwa na Interpol.
Baada ya kukamatwa, Mkuu wa Interpol, Tawi la Tanzania, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Gustav Babile alisema Massawe alikamatwa kati ya Juni 20 na 25, mwaka huu kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dubai akitokea Afrika Kusini.
Massawe ambaye anafanya biashara zake katika Miji ya Arusha, Dar es Salaam na Moshi, inadaiwa kwamba akiwa Dubai, alikutwa na pasi tatu bandia za kusafiria zilizokuwa na majina tofauti wakati alama zake za vidole zilionyesha anaitwa Alex Massawe. “Ombi la kuleta mhalifu nchini kutoka nje ya nchi (extradition request), lina hatua ndefu.
Unajua kuna mlolongo wa taratibu za kutekeleza. Kwanza lazima Polisi wa Tanzania watoe tangazo kwa Interpol kuhusu kumsaka mtu huyo ili aletwe,” alisema Babile.
Unajua kuna mlolongo wa taratibu za kutekeleza. Kwanza lazima Polisi wa Tanzania watoe tangazo kwa Interpol kuhusu kumsaka mtu huyo ili aletwe,” alisema Babile.
Hivi karibuni, Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu Dar es Salaam ilitoa hati ya kukamatwa na kurejeshwa nchini kwa Massawe ili kukabiliana na kesi mbili ikiwamo ya madai ya kughushi nyaraka mbalimbali.
Hati hiyo ilitolewa baada ya Wakili Mwandamizi wa Serikali, Tumaini Kweka kuwasilisha ombi la kutaka mfanyabiashara huyo arejeshwe nchini kwa kuwa tayari amefunguliwa kesi namba 150/2013.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna wa Polisi, Robert Manumba alisema kwa agizo hilo, polisi kupitia kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali waliandika barua kwa Mwanasheria Mkuu wa Dubai kuangalia taratibu za kisheria za kumrudisha baada ya kumfikisha mahakamani mtuhumiwa huyo.
“Massawe alifikishwa mahakamani Dubai kwa makosa ya kukutwa na hati bandia za kusafiria, lakini vilevile kugundulika kuwa ni kati ya watu wanaotafutwa na Polisi wa Interpol kwa tuhuma za mauaji,” alisema Manumba.
“Sheria inasema mtu akikamatwa nchi nyingine, anashtakiwa nchini humo, huku taratibu za kisheria za kumrejesha zikiendelea kwa nchi ambazo zina utaratibu wa kubadilishana wafungwa kama ilivyo Tanzania na UAE,” alisema Manumba.
Alisema ushahidi dhidi ya mtuhumiwa huyo umekamilika na tayari umewasilishwa Dubai ili kuendelea na taratibu nyingine za kisheria za kumrejesha Tanzania haraka kujibu tuhuma zinazomkabili.
Kutajwa mahakamani
Aprili 4, mwaka huu, Massawe alitajwa mahakamani katika kesi ya mauaji ya mfanyabiashara Onesphory Kituly ambaye aliuawa katika mazingira ya kutatanisha Novemba 6, 2011 akiwa nyumbani kwake Magomeni, Dar es Salaam.
Katika kesi hiyo ambayo mshtakiwa wa kwanza ni mfanyabiashara maarufu, Abubakar Marijani ‘Papaa Msofe’, mshtakiwa mwingine, Makongoro Joseph Nyerere alitoa malalamiko, mbele ya Hakimu Mkazi, Agnes Mchome mara baada ya Wakili wa Serikali, Mwanaisha Kombo kudai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba tarehe mpya ya kuitaja.
Mshtakiwa huyo, aliomba jalada la kesi yao lipelekwe mahakamani hapo kwa ajili ya kulifanyia kazi na kutuhumu kuwa ndugu wa marehemu Kituly hawataki maendeleo ya kesi yao hadi Massawe akamatwe.
-Mwananchi
-Mwananchi