Saturday, May 16

RAIS DKT MAGUFULI ATENGUA UTEUZI WA NAIBU WAZIRI WA AFYA DKT FAUSTINE NDUGULILE




Mtaalamu wa chanjo aliyefutwa kazi asema Marekani itakabiliwa na hali mbaya zaidi ya corona majira ya baridi




WASHINGTON, MAREKANI 
OFISA wa zamani wa ngazi ya juu wa afya nchini Marekani ameliambia bunge la congresi kuwa Marekani inaweza kukabiliwa na hali mbaya kuwahi kushuhudiwa wakati wa majira ya baridi kwa sababu ya virusi vya corona.
Rick Bright aliongoza shirika la serikali kujaribu kutengeneza chanjo, lakini akaondolewa katika kazi hiyo mwezi uliopita.
Awali alisema aliondolewa kazini kwa kuelezea hofu juu ya tiba zinazotangazwa na rais Donald Trump.
Rais Trump alimfuta kazi kwa madai kuwa alikua mtumishi asiyeridhika.
Bright pia aliiambia kamati ya Bunge la wawakilishi ya masuala ya afya kuwa maisha yanapotea kwa sababu ya serikali kutochukua hatua katika hatua za mwanzo za mlipuko wa virusi vya corona.
Alisema kuwa kwa mara ya kwanza alizungumzia juu ya ukosefu wa zana za matibabu mwezi Januari, na kufikisha suala hilo katika ngazi za juu za Wizara ya Afya na huduma za binadamu (HHS), lakini hakujibiwa.
Wakati wa ushahidi, Bright alionya kwamba dirisha la kushughulikia virusi vya corona linakaribia kufunga.
“Kama tutashindwa kuboresha jinsi tunavyokabiliana na ugonjwa huu sasa, kwa misingi ya sayansi, ninaogopa janga litakua baya sana na kuendelea kwa muda mrefu,” alisema.
“Bila mpango bora, 2020 unaweza kuwa na kipindi kibaya zaidi cha majira ya baridi kuwahi kushuhudiwa katika histioria ya sasa”.
Bright pia ameiambia kamati hiyo ya bunge la wawakilishi kuwa mwezi Januari alipokea barua pepe ambayo hawezi kusahau, kutoka kwa wasambazaji wa barakoa za hospitali ambao walioonya juu ya upungufu mkubwa wa vifaa hivyo.
“Alisema… tunahitaji kuchukua hatua.Na nikaituma barua hiyo kwa ngazi ya juu ya HHS – na sikupata jibu.
Alisema a kuondolewa kwake kazini kulikua ni matokeo ya kuendelea kwake kusisitiza kwamba fedha zilizotengwa na congress za kupambana na mlipuko wa virusi zinapaswa kuwekwa katika suluhu salama na zilizochunguzwa kisayansi na sio katika dawa, chanjo au teknolojia nyingine ambazo hazijathibitishwa kisayansi.
“Nilizungumza wazi wakati ule, na ninatoa ushahidi leo, kwa sababu sayansi sio siasa au upendeleo -lazima iongoze katika njia ya kupambana na virusi,” aliongeza.
Malalamiko yaliyowasilishwa mapema mwezi huu, yanasema Bright aliondolewa kwenye wadhfa wake kama Mkurugenzi wa taasisi ya utafiti wa kimatibabu – Biomedical Advanced Research and Development Authority (Barda) kwa sababu za kisiasa.Bright anasema aliondolewa muda mfupi baada ya taarifa kuhusu chloroquine, ambayo alisema alikuwa chanzo chake.
Rais Trump alikua amesema kuwa hydroxychloroquine, dawa ya malaria ina uwezekano wa “kuleta mabadiliko “ katika tiba ya Covid-19-ingawa wataalmu wengi wamesema kuwa huenda isiwe ya ufanisi, au hata ikawa hatari.
Malalamiko ya Bright yalikua ni kwamba aliamua kuzungumza na waandishi wa habari kwa sababu maofisa wa serikali walikataa kusikia tahadhari zake. Alisema alikua na jukumu la kujaribu na kulinda umma kutoka kwa madawa ambayo anaamini ni ya hatari kwa usalama na afya ya umma.
MAJIBU YA TRUMP 
Baada ya kusikia, Rais Trump aliwaambia waandishi wa habari : “Simfahamu.Sijawahi kukutana nae.Sitaki kukutana nae.”
“Lakini nilimtazama , na anaonekana kama mtu mwenye hasira, mtumishi asiyeaminika , ambaye kusema kweli kwa mujibu wa baadhi ya watu hakufanya kazi nzuri sana .”
Waziri wa afya, Alex Azar alidai kuwa maofisa walifuata mapendekezo ya Bright.
“Kila alichokilalamikia kilifanikiwa-anachokizungumzia kilifanyaka ,” alisema Azar
“Alisema alizungumzia kuhusu haja ya kupata vifaa vya kusaidia kuongeza oksijeni kwenye mapafu.Tuliagiza vifaa hivyo(respirators) kutokana na maagizpo ya rais.
Alisema tunahitaji mradi wa Manhattan wa chanjo. Tukawa na Mradi wa Manhattan.”

Zoom yashtakiwa na kanisa baada ya mafunzo ya bibilia kuvamiwa kwa picha za ngono


CALIFONIA, MAREKANI
WAKATI watumiaji wa mtandao wa Zoom wakiongezeka kutoka milioni 10 kwa siku hadi milioni 200, Kanisa moja huko Califonia linashtaki kampuni hiyo baada ya mvamizi mmoja kuvamia darasa la mafundisho ya bibilia yaliokuwa yanaendelea mtandaoni na kutuma picha za unyanyasaji wa watoto kingono.
Mvamizi huyo alivamia mkutano huo na kuchezesha picha za video zenye kutatiza akili”, kulingana na kesi iliyowasilishwa na Kanisa la Lutherani la Saint Paulus.
Viongozi wa kanisa la San Francisco waliwasiliana na kampuni ya Zoom kutafuta usaidizi lakini kampuni hiyo haikuchukua hatua yoyote.
Katika taarifa, msemaji wa kampuni ya Zoom ameshtumu tukio hilo baya na la kiovu.
“Tunahuzunika pamoja na wale walioathirika,”kampuni hiyo imesema, “Siku hiyo hiyo tulipogundua tatizo hili, tulimtambua aliyetekeleza kitendo hicho, tukachukua hatua kwa kumfungia asiweze kuingia kwenye mtandao wetu na kuwasilisha taarifa kwa mamlaka husika.”
Kampuni hiyo imezungumzia hatua za kiusalama walizochukua hivi karibuni katika mtandao wao”, na kuongeza kwamba watumiaji wa kampuni ya Zoom hawastahili kushirikisha watu wengi sana namba zao za siri za kuwawezesha kufanya mkutano kama ilivyoonekana kwa kundi hilo la kanisa.
Umaarufu wa mikutano kwa njia ya video kupitia mtandao wa Zoom umeongezeka sana katika miezi ya hivi karibuni hasa kwa wafanyakazi na hata kwa shughuli za kibinafsi wakati ambapo nchi kadhaa zimechukua hatua ya kusalia ndani kama njia ya kukabiliana na virusi vya corona.
Utumiaji mkubwa wa mtandao huo wa zoom umekumbwa na mashaka ya kiusalama na faragha ya watu, ambapo wavamizi wamekuwa wakivamia mikutano ya watu bila kualikwa na wakati mwingine wakituma ujumbe wa chuki, kibaguzi, unyanyasaji au hata picha za ngono.
Kanisa la Saint Paulus – moja ya makanisa ya zamani huko San Francisco – limesema kwamba kesi hiyo iliyowasilishwa katika mahakama moja iliyopo San Jose Jumatano, inalalamikia tukio la Mei 6 wakati wa mafundisho ya bibilia ambayo yalivamiwa na mtu aliyefahamika – ambaye pia ameripotiwa kwa mamlaka mara kadhaa.
Wanafunzi wanane wanaojifunza mafundisho ya bibilia, wengi wao wakiwa wale wanaopokea malipo ya uzeeni, mfumo wao wa kompyuta ulikatishwa wakati mvamizi huyo alipocheza video za ngono.
Wakati ambapo programu ya zoom imeendelea kupata umaarufu, imekumbwa na ukosoaji mkubwa kwasababu za kiusalama.
“Video hizo zilikuwa mbaya na ilikera zaidi kuonesha watu wakubwa wakijihusisha na vitendo vya ngono miongoni mwao, kufanya vitendo vya ngono dhidi ya watoto na wale wachanga, pamoja na kuwanyanyasa kimwili,” kesi hiyo inasema
Wakati wanafunzi hao walipojaribu kufunga video hiyo na kuanza tena, mvamizi huyo alivamia tena, kesi hiyo inaongezea.
Kanisa hilo limewasilisha mashtaka likitaka hatua kuchukuliwa dhidi ya kampuni ya Zoom yenye makao yake San Jose.
Katika kesi hiyo, waliowasilisha mashtaka wanataka kufidiwa kwa madai ya kupuuzwa, kukiukwa kwa mkataba, ukosefu wa haki na tabia zisizofaa katika biashara.
Kampuni ya Zoom iliandika kwenye blogu kwamba imechukua hatua zaidi za kiusalama wiki hii na kuahidi hatua za kuimarishaji usalama ikiwemo mipango ya kumzuia mtu wa kando kuingilia mawasiliano ya mtumiaji.
Awali, kampuni hiyo ilikosolewa kwa kudai kwamba tayari hatua za kumzuia mtu wa kando kuingilia data ya mtumiaji zipo kumaanisha kuwa ni mtumiaji pekee anayeweza kufikia ujumbe wake na video zake.
Kile kilichoikumba kanisa hilo ndicho kilichotokea katika kikao cha bunge cha Afrika Kusini wiki moja iliyopita.
Mkutano wa kamati ya bunge kwa njia ya mtandao Afrika Kusini uliwahi kuvamiwa na wadukuzi na spika kudhalilishwa.
 Kikao hicho kilikuwa tu ndio kimeanza picha za ngono zilipojitokeza kwenye skrini huku sauti ya mwanamume ikisikika kumtusi Spika Thandi Modise, ambaye alikuwa mwenyekiti wa kikao hicho.
Spika huyo aliyeshikwa na hasira alipaza sauti akisema hiyo ndio sababu anapinga mikutano ya mitandaoni.
“Hiki kilichotokea ni kilekile nilichokuwa ninakisema kuhusu kufanya mikutano kwa njia ya Zoom!” Modise amenukuliwa akisema hivyo na tovuti ya Times Live.
Wabunge walielezea tukio hilo kama lenye kukera na kutatiza akili, kulingana na Tovuti ya habari ya Eyewitness.
Iliwalazimu wahandisi wa Bunge kutuma kiunganishi kingine ambapo wabunge waliungana tena na kuendelea na kikao chao.
Kampuni ya mtandao wa Zoom imekuwa ikikosolewa kimataifa kwa taarifa kwamba kuna wavamizi wanaotuma picha za ngono au maudhui ya matusi wakati wa mikutano.
Kuvamiwa kwa mtandao kwa njia ya Zoom kumekuwa kukifanyika mara kwa mara katika wiki za hivi karibuni wakati ambapo watumiaji wengi wapya wameanza kutumia mtandao huo kama njia moja ya kukabiliana na kusambaa kwa ugonjwa wa Covid-19 na kuahirishwa kwa mikutano na matukio ambayo awali ilikuwa ifanyike ana kwa ana.



KEYDOLI; MREMBO KUTOKA KENYA AMWAGIA SIFA HARMONIZE



MOMBASA, KENYA 
ONGEZEKO la wasanii wapya halipo Bongo pekee bali mpaka nchini Kenya, mashabiki wameendelea kushuhudia vipaji vipya kila siku. 
Swaggaz tumekutana na KeyDoli, mrembo kutoka Mombasa nchini Kenya anayefanya vyema kwa sasa na wimbo, Infinity aliomshirikisha rapa Country Boy akitumia staili ya Afro Arabic Soul. 
Swaggaz: KeyDoli ni nani na lini ulianza kujihusisha na muziki? 
KeyDoli: Jina langu halisi ni Yusriyah Ahawa, nilianza muziki nikiwa mdogo sana kama miaka 14 hivi, ilikuwa mwaka 2002. 
Nilipata kutambulishwa na prodyuza mmoja anayeitwa Bruce Othiambo ambaye alikuwa rafiki wa baba yangu kwa sababu walikuwa wanafanya kazi sehemu moja. 
Prodyuza Bruce ambaye sasa ni marehemu alikuwa kwenye studio zinaitwa Johari Cleff na ndio ilikuwa inasimamia wasanii wakubwa kutoka Kenya. 
Ngoma yangu ya kwanza iliitwa Nipe na baba yangu ndio alirekodi akishirikiana na prodyuza Bruce, wimbo huo ulinipa umaarufu sio tu hapa Kenya bali na Afrika Mashariki na Uingereza. 
Swaggaz: Wanamuziki gani walikuvutia mpaka ukaingia kwenye muziki? 
KeyDoli: Nilizaliwa kwenye familia ya muziki ndiyo maana nikajikuta napenda kuimba kwa kuwa hata baba yangu alikuwa anapenda muziki. 
Nikawa nasikiliza muziki wa Yondo Sister, Mbilia Bel na Franco huku Madonna akiwa ni msanii wangu pendwa na haipiti siku sijamsikiliza. 
Swaggaz: Kwanini uliamua kutangaza muziki wako Tanzania kwa kumshirikisha rapa Country Boy? 
KeyDoli: Toka zamani ilikuwa ndoto yangu nifike Tanzania. Kwa hadithi za mama aliniambia amezaliwa Bongo pia nilikuwa nikiwasikia kina Juma Nature, Lady Jay Dee na Ray C kwahiyo nilikuwa natamani nifike. 
Nilitamani kufika Tanzania nikiwa mdogo ila kwa sababu nilikuwa shule nilishindwa lakini nashukuru Machi 1, mwaka huu nilifika Dar es Salaam na kuweza kutimiza ndoto yangu kufanya kazi na Country Boy. 
Swaggaz: Ukiwa kama msanii wa kike na mrembo sana, changamoto zipi unapitia kwenye muziki wako? 
KeyDoli: Sio rahisi ila mimi nilifunzwa toka nikiwa mdogo kuwa wakati wa biashara ni biashara tu, ukiwa na mazungumzo ya biashara hakuna mtu anaweza kukutongoza ndio maana nikiwa nakwenda kwenye studio kurekodi au redioni au kwenye Tv huwa nakuwa na mtu kando yangu ili kukwepa hizo changamoto. 
Swaggaz: Mbali na Country Boy, wasanii gani wengine wa Tanzania unatamani kufanya nao kazi? 
KeyDoli: Harmonize au Darassa lakini Harmonize zaidi maana mashallah yuko na moyo mweupe na nilipata bahati ya kumwona hana dharau wala kiburi na uimbaji wake ni mzuri pia Darassa navutiwa na floo zake. 
Swaggaz: Changamoto zipi zipo kwenye tasnia ya muziki hapa Kenya? 
KeyDoli: Mimi naona sapoti hamna sana lakini siwezi kulaumu vyombo vya habari kwa sababu kuna wengine hawajafikishiwa kazi pia mashabiki nao hawajafikishiwa muziki kwa usahihi ili waweze kuusapoti. 
Swaggaz: Baada ya kuachia ngoma yako na Country Boy, mashabiki watarajie nini kutoka kwako? 
KeyDoli: Niko na ngoma mpya nitaiachia Mei 21, mwaka huu nikiwa nimemshirikisha msanii mkubwa wa Tanzania. Huo wimbo upo kwenye albamu yangu yenye jumla ya nyimbo 12. 
Pia niko na EP yenye nyimbo nne ambazo zote nimeshirikisha Country Boy na tayari zina video ambazo nilifanyia Tanzania. 
Mashabiki waendelee kunitafuta kwenye mitandao ya kijamii kama Facebook, Instagram, YouTube naitwa Keydoli ili wapate kunifahamu zaidi nawapenda sana Watanzania. 
Pia nawakumbusha tuendelee kuvaa barakoa na kunawa mikono na kutumia sanitaiza mara kwa mara ili Mungu atulinde na ugonjwa wa corona. 

Mashine ya kupima virusi vya corona iliyotolewa na Rostam yawasili Zanzibar



MASHINE ya kupima virusi vya corona yenye uwezo wa kutoa majibu ndani ya saa nane ambayo iliagizwa nchini Korea Kusini kwa ufadhili wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mfanyabiashara maarufu nchini, Rostam Aziz, hatimaye imewasili visiwani humo.
Mashine hiyo ina uwezo wa kutoa majibu ndani ya saa nane kwa vipimo vya watu 96 na kwa saa 24 ina uwezo wa kutoa majibu kwa watu 496.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, Zanzibar, Juma Mohammed Salum jana ilieleza kuwa mashine hiyo ni miongoni wa tatu zilizokuwa zimeagizwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Itakumbukwa Machi 25 Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein aliiagiza Wizara ya Afya kuhakikisha ndani ya miezi mitatu wanakamilisha maabara ya kupima magonjwa ya mripuko.
Shein alikuwa amefanya ziara ya kuangalia ujenzi wa Maabara ya Uchunguzi ya Microbiology katika kijiji cha Binguni na kuagiza Wizara ya Afya kuanza mara moja ujenzi wa maabara itakayochunguza maradhi yanayosababishwa na virusi (Virology Laboratory).
Zaidi alitaka ujenzi wa maabara hiyo ukamilike haraka iwezekanavyo ili Zanzibar iweze kuwa na mashine za kupima virusi vya corona.

Polisi yaeleza sababu za kumwita Mbowe


MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe jana aliitwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano na kisha kuachiwa.
Hatua ya kuitwa kwa Mbowe ilikuja saa chache kabla ya kufanya mkutano mubashara kupitia mitandao ya kijamii ya Chadema kuwasilisha ujumbe kwa Watanzania.
Taarifa kutoka ndani ya Chadema ilieleza kwamba Mbowe akiwa nyumbani kwake Dar es Salaam, alifuatwa na maofisa wa Jeshi la Polisi, lakini wasaidizi wake waligoma kufungua mlango.
Hata hivyo, saa chache kabla ya kuanza kwa mkutano wake, alipokea wito wa polisi na kutakiwa kwenda kuripoti ofisi ya Upelelezi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni katika Kituo cha Oysterbay.
Mbowe aliitikia wito huo na kwenda polisi huku akiwa na jopo la wanasheria wake.
KAULI YA POLISI
MTANZANIA ilipomtafuta Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Mussa Taibu, alisema kuwa alimwita Mbowe ili kufahamiana.
 “Ni kweli nilimwita tufahamiane kwa sababu yeye ofisi yake ya Chadema iko maeneo haya haya ya Kinondoni, hivyo baada ya kufahamiana yeye ameendelea na ratiba zake,” alisema Kamanda Taibu.
Jana, muda mfupi baada ya Mbowe kutaka kufanya mkutano na waandishi wa habari kuhusu masuala mbalimbali ya kitaifa na kimataifa, Msemaji wa Chadema, Tumaini Makene alitoa taarifa kupitia mitandao ya kijamii akisema mkutano huo hautafanyika tena.
“Mkutano wa Mwenyekiti Mbowe uliokuwa ufanyike mubashara kuzungumza na umma, hautafanyika kama ilivyopangwa baada ya Jeshi la Polisi kumhitaji akaripoti ofisi ya RCO Kinondoni, Kituo cha Oysterbay,” ilisema taarifa hiyo ya Makene.
Awali gazeti hili lilipomtafuta Makene kutaka kujua kuhusu kuitwa kwa Mbowe, alisema polisi hawakusema sababu ya kumwita mwenyekiti huyo.
“Kweli alikwenda polisi kitambo, tangu muda ule wa saa tano na polisi hawakusema sababu, nadhani mkiwauliza kwa sasa wanao wajibu wa kusema hilo,” alisema Makene.
MAAMUZI YA CHADEMA
Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kwa wiki za hivi karibuni aliendesha kikao cha Kamati Kuu ya Chadema kwa njia ya mtandao ambacho kiliazimia kuwavua uanachama wabunge wake wanne.
Wabunge waliofutwa uanachama ni pamoja na Joseph Selasini (Rombo), Antony Komu (Moshi Vijijini) ambao wote kwa nyakati tofauti walitangaza kujiunga na Chama cha NCCR-Mageuzi mara baada ya Bunge kumaliza muda wake.
Wengine ni Wilfred Lwakatare (Bukoba Mjini) na David Silinde (Momba).
Mbali na wabunge hao, Mbunge wa Viti Maalumu, Mariam Msabaha ambaye alikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu alivuliwa nyadhifa zake zote ndani ya chama na kutakiwa kujieleza kwanini asichukuliwe hatua.
Uamuzi huo umefikiwa kutokana na wabunge hao kukiuka maelekezo ya chama ya kuwataka wabunge wote wa chama hicho
wasishiriki vikao vya Bunge vinavyoendelea Dodoma na kukaa karantini kwa siku 14.
Wabunge wengine ambao wanaendelea kuhudhuria vikao vya Bunge na kutakiwa kujieleza kwa kukiuka makubaliano hayo ni Suzan Masele, Joyce Sokombi, Latifa Chande, Lucy Mlowe, Sware Semesi, Jafari Michael, Peter Lijualikali, Willy Kambalo, Rose Kamili, Sabrina Sungura na Anne Gideria.
Siku 14 za wabunge hao kujiweka karantini zilikamilika juzi.
SPIKA AWAZUIA
Hata hivyo juzi Spika Bunge, Job Ndugai aliwazuia wabunge 15 wa Chadema kuhudhuria bungeni, iwapo hawatakamilisha masharti mawili muhimu.
Wabunge hao watatakiwa kutimiza masharti hayo kwa kuwa hawajulikani waliko na wamekuwa wakihesabiwa kama watoro tangu walipoacha kuingia bungeni Mei 1.
 “Ofisi ya Bunge inatoa taarifa kwamba katika siku za hivi karibuni baadhi ya wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wamekuwa watoro kwa kutohudhuria vikao vya Bunge bila ruhusa ya Spika kwa muda wa wiki mbili kinyume na masharti ya Kanuni ya 146 inayosisitiza wajibu wa kila mbunge kuhudhuria vikao vya Bunge.
“Aidha, tunapenda ifahamike kwamba wabunge hao walisusia vikao vya Bunge huku wakiwa wamelipwa posho ya kujikimu ya kuanzia Mei 1-17, 2020.
“Kwa mujibu wa masharti ya Kanuni ya 5 ya Kanuni za Bunge, Spika alitoa masharti mawili kwa wabunge hao,” ilieleza taarifa hiyo.
Ilieleza kuwa sharti la kwanza ni kuwataka wabunge hao kurejea bungeni au kurudisha fedha walizolipwa mara moja na sharti la pili ni kwa kuwa haijulikani wabunge hao walipo, watalazimika kuwasilisha ushahidi kwamba wamepimwa na hawana maambukizi ya virusi vya corona kabla ya kuruhusiwa kuingia bungeni
Iliwataja wabunge hao kuwa ni Freeman Mbowe, Ester Bulaya, Halima Mdee, John Heche, Joseph Mbilinyi, Peter Msigwa, Rhoda Kunchela, Pascal Haonga, Catherine Rage, Devotha Minja, Joyce Mukya, Aida Khenan, Upendo Peneza, Grace Kiwelu na Joseph Haule.
“Hivyo basi, kwa taarifa hii, na kwa mujibu we Kanuni ya 144 ya Kanuni za Kudumu za Bunge inayohusu usalama katika maeneo ya Bunge, Spika ameagiza Kitengo cha Usalama cha Bunge kutowaruhusu wabunge waliotajwa hapo juu kuingia katika maeneo ya Bunge kuanzia leo (juzi) Jumatano Mei 13, 2020 mpaka watakapotimiza masharti tajwa hapo juu,” ilieleza taarifa hiyo ya Bunge.

WAZIRI HASUNGA AKAGUA MAGHALA YA SUKARI DAR ES SALAAM, ATOA MAAGIZO MAZITO


Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akiwa ameambatana na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania Prof Keneth Bengesi kukagua maghala ya kuhufadhia sukari Jijini Dar es salaam, leo tarehe 16 Mei 2020 wakati akifanya ziara ya kushtukiza Jijini Dar es salaam ili kukagua na kujionea hali ya upatikanaji wa sukari nchini. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)



Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania Prof Keneth Bengesi wakishusha na kukagua sukari zilizopo kwenye makontena kwenye maghala ya kuhufadhia sukari Jijini Dar es salaam, leo tarehe 16 Mei 2020 wakati akifanya ziara ya kushtukiza Jijini Dar es salaam ili kukagua na kujionea hali ya upatikanaji wa sukari nchini.



Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisaini kitabu cha wageni  mara baada ya kutembelea Bodi ya sukari kabla ya ziara ya kukagua maghala ya kuhufadhia sukari Jijini Dar es salaam, leo tarehe 16 Mei 2020. Mwingine pichani ni Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania Prof Keneth Bengesi



Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akikagua maghala ya kuhufadhia sukari Jijini Dar es salaam, leo tarehe 16 Mei 2020 wakati akifanya ziara ya kushtukiza Jijini Dar es salaam ili kukagua na kujionea hali ya upatikanaji wa sukari nchini.



Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dar es salaam

Serikali imetangaza kuendelea kuwachukulia hatua kali za kisheria  wafanyabiashara nchini wanaotumia uwepo wa ugonjwa wa homa ya mapafu (COVID 19) kuhodhi kiasi cha sukari kinachokuwa kwenye mzunguko na kuuza kwa bei ya juu zaidi ya bei ya ukomo katika eneo husika ambayo ni kati ya Shilingi 2600 hadi 3200.

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo leo tarehe 16 Mei 2020 wakati akifanya ziara ya kushtukiza Jijini Dar es salaam ili kukagua na kujionea hali ya upatikanaji wa sukari nchini.

Mhe Hasunga amesema kuwa serikali imeweka mbinu kali za kuwabaini wafanyabiashara hao na punde watakapobainika watachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria za nchi.

Ametangaza hali ya upatikanaji wa sukari nchini kuwa imeendelea kuimarika ambapo kufikia tarehe 16 Mei 2020 kiasi cha Tani 18,142 kimeingia nchini kati ya kiasi cha Tani 40,000 kilichoagizwa na wazalishaji wa ndani kwa ajili ya kuziba pengo la uzalishaji wa msimu wa mwaka 2019/2020.

Amesema kati ya kiasi hicho cha Tani 18,142 kilichoingizwa kiasi cha Tani 15,498 kimetolewa bandarini na mipakani na tayari kipo sokoni na kingine cha Tani 2,644 kipo katika hatua mbalimbali za kutolewa bandarini.

Amebainisha kuwa tarehe 16-22 Mei 2020 zitaingia Tani 7470, Tarehe 23-31 Mei 2020 zitaingia Tani 13,404, huku tarehe 1-4 Mei 2020 kiasi cha Tani 984 kitawasili nchini.

Kuhusu hatua zilizochukuliwa na serikali kukabiliana na upandaji holela wa bei, Waziri Hasunga amesema kuwa serikali ilitoa bei elekezi kupitia GN Na 284 na 352 ya tarehe 24 Aprili 2020 na tarehe 8 Mei 2020 mtawalia, na kufanya msako wa wafanyabiashara wasio waadilifu wanaouza sukari kinyume na bei elekezi kwa kushirikiana na mamlaka zingine za kiserikali.

Hatua nyingine ni pamoja na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wafanyabiashara waliobainika kuuza sukari kinyume na bei elekezi ambapo jumla ya wafanyabiashara 51 wamekamatwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani.

Kadhalika, Waziri Hasunga amesema kuwa serikali ilifanya marekebisho ya GN kwenye mikoa ya Dar es salaam, Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Dodoma, Singida na Tabora.

Katika Mkoa wa Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Tanga bei ya sukari haitakiwi kuzidi Shilingi 2,800 kwa mlaji kwa kiasi cha kilo moja, Mkoa wa Singida, Tabora na Dodoma bei ya sukari haitakiwi kuzidi shilingi 2,900 kwa mlaji huku katika Mkoa wa Dar es salaam bei ikitakiwa kutozidi shilingi 2,600 kwa mlaji.

Mhe Hasunga amesema kuwa tatizo la upungufu wa sukari kutokana na sababu mbalimbali lilikwishapatiwa ufumbuzi hivyo wananchi hawapaswi kuwa na wasiwasi na jambo hilo huku akitolea mfano kampuni ya Alnaeem Enterprises ambayo imekuwa na sukari toka jumatano kiasi cha Tani 1,400 ambapo ina kiasi kikubwa cha sukari lakini mkoa wa Dar es salaam wamekuwa na malalamiko ya kukosekana kwa sukari.

Kwa kawaida msimu mpya wa sukari huanza mwishoni mwa mwezi Juni, Serikali kupitia Bodi ya Sukari tayari imefanya mazungumzo na kiwanda cha sukari cha Kilimbero ambapo wamekubali kuanza uzalishaji tarehe 21 Mei 2020 huku ikiendelea kufanya mazungumzo na wazalishaji wengine ili kuanza uzalishaji mapema

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania Prof Keneth Bengesi amesema kuwa Bodi hiyo itaendelea kufanya mawasiliano na Mamlaka ya Bandari ya Tanzania ili kuhakikisha kuwa sukari zote zinazoingia bandarini ziweze kutolewa kwa wakati ili iweze kusambazwa na kuwafikia watumiaji haraka iwezekenavyo.

Amesema kuwa kadri itakavyokuwa inafika bandarini itakuwa inatolewa kwa wakati huku akitoa wito kwa wananchi kuendelea kuiamini serikali kuwa serikali ipo makini katika utekelezaji wa majukumu yake hivyo wananchi wasiwe na mashaka yoyote kuhusu  sukari kwani inafanya kazi kutatua kadhia hiyo.

Katika kipindi cha miaka mitatu serikali imeweka mikakati ya kujitosheleza kwa sukari nchini ambapo kutakuwa na ongezeko la uzalishaji wa miwa na sukari nchini kupitia miradi ya Bagamoyo Sugar, Mkulazi II, S.J Sugar Mtwara, Morogoro Sugar, na shamba la Hekta 25,000 lililopo Kigoma.

KARIA: FEDHA ZILIZOTOLEWA NA RAIS MAGUFULI ZILITUMIKA KWENYE MAANDALIZI YA AFCON (U-17)

Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV

Rais wa Shirikisho la Kandanda nchini (TFF), Wallace Karia amefafanua kuwa fedha takriban Bilioni 1 za Kitanzania zilizotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli zilitumika katika maandalizi ya Michuano ya Mataifa ya Afrika kwa vijana (AFCON U-17) zilizofanyika hapa nchini April, 2019.

Kupitia Kipindi cha Jaramba kinachorusha na Chaneli ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1), Rais Karia amethibitisha ni kweli walipewa fedha hizo na Rais Magufuli walipoitwa Ikulu baada timu ya wakubwa (Taifa Stars) kufuzu Michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) yalifanyika June, 2019 nchini Misri.

"Kiukweli sisi (TFF) tulishirikiana na Serikali na kulikuwa na Kamati ya maandalizi ya Michuano hiyo ambayo ilikuwa chini ya Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe na unapokuwa mwenyeji wa Mashindano timu zote, Viongozi, Wageni wote unagharamia wewe kama mwenyeji", ameeleza Karia.

Kupitia mahojiano hayo, Rais Karia amedai kuwa Fedha hizo zilienda Baraza la Michezo nchini, amedai TFF haikupokea fedha hizo licha ya kuwepo tuhuma kwa Shirikisho hilo kutumia vibaya fedha hizo. "Fedha hazikuja TFF, bali zilitumika kwenye Maandalizi ya Michuano ile ya AFCON kwa vijana (U-17)", amedai Karia.

Karia ameeleza kuwa Shrikisho hilo Soka nchini linaamini kuhusu fedha hizo kila kitu kitawekwa wazi na Mamlaka zinazohusika kwa madai ya upotevu wa fedha hizo, amedai Kamati ya Maandalizi ya Michuano, TFF na Baraza la Michezo walisimamia maandalizi ya Michuano hiyo kiufanisi.

Karia amebainisha kuwa Tanzania iliomba kuandaa Michuano hiyo tangu mwaka 2015 wakati Serikali ya awamu ya Tano inaingia madarakani chini Rais wake, Dkt. John Magufuli, amesema baada ya maandalizi hayo Tanzania imeandika historia baada yakupata nafasi adimu yakuandaa Michuano hiyo ambayo inakuwa nadra kwa Mataifa mengi barani Afrika.

"Mimi binafsi nimefurahi suala hili kufika katika Mamlaka husika ili kubaini kila kitu kuhusu fedha hizo, suala hili limenifanya niwe huru hapa lilipofika, sisi tulifarijika na Maandalizi ya Mashindano yale, tulikuwa hatulali kuhakikisha mashindano yanafanyika", ameeleza Karia.

Hata hivyo, Karia amemshukuru Rais Magufuli kusimamia mashindano hayo, amesema Wageni waliofika kushuhudia walishukuru na kupongeza maandalizi kwa ujumla. Amedai mashindano hayo yaliyofanyika hapa nchini yalikuwa bora zaidi yaliyofanyika nyuma.



Rais wa Shirikisho la Kandanda nchini (TFF), Wallace Karia

KLABU YA SIMBA,MO DEWJI WAGAWA BARAKOA BURE KWA WAKAZI WA JIJI LA DAR ES SALAAM KUJIKINGA NA CORONA

Na, Al-Hasan Muhidin, MichuziTv

Klabu ya Simba kwa kushirikiana na Taasisi ya Mo Dewji wametoa msaada wa Barakoa kwa wananchi wa maeneo mbalimbali ndani ya Jiji la Dar es Salaam kwa ajili ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona.

Akizungumza na waandish wa habari wakati wa tukio hilo,  Msaidizi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Klabu ya Simba Rispa Hatib amesema tukio hilo ni la siku tatu kuanzia leo Jumamosi na litahitimishwa siku ya Jumatatu.

Amesema, janga hili ni la Dunia na nchi nzima kwa ujumla na Taasisi ya Mo imeamua kushirikiana na klabu ya Simba kugawa barakoa hizi kwa wanachi wa ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam na maeneo mengine.

Rispa amesema, wameanza na maeneo ya Kivukoni, Kariakoo, Buguruni hadi Mbagala ambapo zoezi hili litaenda kwa siku tatu na wanategemea litaenda vizuri.

Amewaomba wananchi wajitokeze kuchukua barakoa hizo kwani zitawasaidia hasa wale ambao hawana uwezo wa kununua na unaweza kuzifua na kutumia tena.

Katika zoezi hilo, wananchi mbalimbali waliweza kujitokeza kupokea msaada wa barakoa hizo na kuwashukuru sana uongozi wa Simba na Taasisi ya Mo kwa kuamua kuwajali watu wasio na uwezo wa kununua barakoa hizo.

Kwa sasa dunia nzima ipo katika vita ya kupambana na maambukizi ya ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na  Virusi vya Covid 19 na watalaamu wa afya wakiwataka wananchi kutumia barakoa muda wote pamoja na vitakasa mikono ili kupunguza maambukizi.











MH. MZEE FREDRICK MCHAURU-: MTANGANYIKA WA KWANZA KUPATA "SCHOLARSHIP" AGONGA KARNE MOJA DUNIANI!!!

BY MZEE WA ATIKALI ✍️✍️✍️

"Tatizo letu kama nchi ni kuwa vichwa vya wazee na viongozi wetu ndio maktaba za kumbukumbu za mambo muhimu ya Taifa. Sasa wanapofariki, hufariki na kumbukumbu hizo. Hii si sahihi hata kidogo. Ni muhimu kama Taifa tuchukue hatua madhubuti ili kumbukumbu hizi zihifadhiwe vitabuni, Maktaba na Makumbusho ya Taifa".
Prof. HAROUB OTHMAN, 3.7.2006.

1. USULI

Tarehe 25.4.2020, Mzee FREDRICK JONES MCHAURU alitimiza miaka 100 na kuwa mmoja wa Watanzania wachache sana kuweza kuishi hapa duniani kwa KARNE MOJA!. Mzee MCHAURU na Mangi Mkuu wa Wachaga Mh. THOMAS MAREALE ndio walikuwa Watanganyika wa kwanza kupata "Scholarship" ya kwenda kusoma majuu ambapo walisoma  London School of Economics, UK.

Kwavile Bongolanders wengi hawajawahi hata kumsikia Mzee MCHAURU na kwavile Mzee huyu amelifanyia Taifa hili mambo mengi kwenye utumishi wake uliotukuka, hivyo basi ATIKALI hii Mahsusi inamdadavua kwa ufupi Mzee huyu wa kipekee kabisa nchini.

Je, Mzee huyu alizaliwa wapi, lini, alisoma wapi na utumishi wake wa umma ulikuwaje?.


2. MCHAURU AZALIWA

MCHAURU alizaliwa siku ya Jumapili ya tarehe 25.4.1920 huko Newala, Ntwara, Tanganyika.

3. MASOMO

MCHAURU alisoma St. Joseph's college, Chidya na alikuwa ni kijana hodari sana darasani. Hiyo ilipelekea afaulu mitihani yake kwa kiwango cha juu hadi kuchaguliwa kujiunga na St. Andrew's  college, Minaki.

4. MCHAURU APATA "SCHOLARSHIP"

JMwaka 1944, MCHAURU na Mangi Mkuu wa Wachaga Bw. THOMAS MAREALLE walipata scholarship toka serikali ya Ukoloni ya Uingereza kwaajili ya kwenda kusoma London School of Economics, UK. Wawili hawa ndio walikuwa Watanganyika wa kwanza kupata Scholarship hapa nchini. Walisoma UK hadi 1946 waliporejea nchini baada ya kuhitimu mafunzo yao.

5. MCHAURU AAJIRIWA  OFISA MAENDELEO TABORA

Baada ya kurejea, MCHAURU aliajiriwa kama Afisa Maendeleo wa Jamii Tabora. Kati ya 1947 na 1952, alikuwa Bwana maendeleo wa nusu ya Tanganyika nzima ie mikoa yote ya Kanda ya Ziwa, Ziwa Magharibi, Kusini na Nyanda za Juu Kusini. Licha ya barabara mbovu na changamoto lukuki, MCHAURU aliifanya kazi yake kwa weledi wa hali ya juu.

Mwenzake MAREALLE akapewa Dodoma kupanda juu kuelekea Morogoro, Pwani, Dsm na Kaskazini kote.

6. MCHAURU AANZISHA ELIMU YA WATU WAZIMA NCHINI

MCHAURU ni mtu wa maendeleo sana na alipenda kuwainua Watanganyika wenzake. Hivyo, MCHAURU akawa Mtaganyika wa kwanza kuanzisha Elimu ya Watu Wazima nchini mwaka 1959 huko Singida. Huu ulikuwa mpango kabambe uliopendwa sana. Mpango huu mujarab ukaigwa nchi nzima na ilipofika 1980, TZ ikawa moja ya nchi zenye idadi kubwa ya watu wanaojua kusoma na kuandika duniani. Hii yote ni kutokana na maono na  juhudi za MCHAURU.

7. MCHAURU AWA PRINCIPAL WA KWANZA CHUO CHA TENGERU

Mwaka 1962, MCHAURU aliteuliwa kuwa Principal wa kwanza wa Chuo cha Tengeru, Arusha. Mwanzoni, chuo hiki kilikuwa ni "Polish Refugees Camp" wakati wa Vita Kuu ya 2 ya Dunia. Wapolish walifungua "ranch" ya mifugo ambapo walipoondoka ikabadilishwa jina na kuitwa Tengeru.

8. MCHAURU ATEULIWA  KATIBU MKUU USHIRIKA

Mwaka 1965, Rais NYERERE alimteua MCHAURU kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Ushirika, Ustawi wa Jamii na Utamaduni. Wakati huo, serikali ilikuwa na Makatibu Wakuu 19 chini ya Chief Secretary JOSEPH NAMATA ambaye pia alitokea Ntwara kama MCHAURU.

9. MCHAURU ATEULIWA KATIBU MKUU MAMBO YA NDANI

Rais NYERERE alimteua MCHAURU kuwa Katibu Mkuu Wizara nyeti ya Mambo ya Ndani mwaka 1968. MCHAURU alihudumu Wizara hiyo kwa weledi na uadilifu wa hali ya juu hadi 1971.

10. MCHAURU AWA KATIBU MKUU ULINZI

Mwaka 1972, Rais NYERERE aliunda Wizara mpya ya Ulinzi na JKT na  kumteua Mh. EDWARD SOKOINE kuwa Waziri na kisha akamteua MCHAURU kuwa Katibu Mkuu wake kutokana na kazi mujarab aliyokuwa ameifanya kwenye Wizara ya Mambo ya Ndani.

11. MCHAURU ASTAAFU SERIKALINI

 Mwaka 1973, MCHAURU alistaafu kazi serikalini. Baada ya kustaafu serikalini, MCHAURU alihudumu kwenye Bodi mbalimbali hadi mwaka 1999.

12. MCHAURU AWA MWENYEKITI WA BODI YA POSTA NA SIMU

MCHAURU alipewa jukumu la kusimamia Posta & Simu kama Mwenyekiti  wa Bodi na kulitekeleza vizuri jukumu hilo.

13. MCHAURU Atafuta Wawekezaji kwenye Madini

Kwenye miaka ya 1980, MCHAURU alienda majuu kuwaalika wawekezaji ili kuja kuiinua sekta ya madini. MCHAURU aliweza kufanikisha jukumu hilo kwa ushirikiano mkubwa wa Bw. NIVEN SINCLAIR, raia wa Uingereza.

14. MCHAURU Awa Mwenyekiti GEITA Gold Mines

Kutokana na jitihada zake kuntu, MCHAURU akawa Mwenyekiti wa Geita Gold Mines na Ashanti Gold Mine.

15. MCHAURU VILLAGE

MCHAURU alikuwa mtu maarufu sana Geita kiasi kwamba kutokana na mchango wake mkubwa, huko machimboni Geita kuna eneo maalum limepewa jina lake kwa heshma yake MCHAURU Village.  Hiyo ni sehemu nzuri sana ambako wanaishi matajiri tu.

16. MCHAURU AIRPORT

Geita kuna uwanja  wa ndege mzuri unaotumiwa na mgodi wa dhahabu wa Geita. Uwanja huo ulipewa jina la MCHAURU Airport kwa heshma ya MCHAURU. Uwanja huu una hadi taa za kutua na kurukia wakati wa usiku na wakati wa ukungu na unatambulika hadi "International Civil Aviation Organisation". Kwa hakika, MCHAURU ana heshma ya kipekee huko Geita.

18. TAMATI

Huyu ndiye Mzee FREDRICK JONES MCHAURU ambaye alifanya kazi kwa weledi na Uzalendo wa hali ya juu hadi anastaafu.

Mzee MCHAURU kwa sasa amegonga Karne Moja hapa duniani lakini akiwa bado yuko ngangari ambapo anaishi Upanga Magharibi, Mtaa wa Kitonga, Kitalu Na. 121, nyuma ya hospitali ya Tumaini.

Mzee MCHAURU ana wajukuu zaidi ya 20 na vitukuu zaidi ya 10. Mkewe, THEKLA MCHAURU aliishatangulia mbele za haki. Bi. THECKLA alikuwa Mwanamke wa kwanza Kusini ya TZ kuwa Mwalimu wa Cheti ambaye alikuwa akilipwa mshahara wa TZS 40. Baadaye Bi. THECKLA alikuja kuwa Katibu Mkuu  wa UWT Taifa.

KONGOLE KWAKO MZEE MCHAURU NA NAPENDA KUMALIZIA ATIKALI HII KWA NUKUU YAKO MUJARAB:-

"Katika utumishi wangu toka 1947 sikuwa hata siku moja kuwa na tamaa ya mali wala utajiri. Hili ni jambo linalonipa faraja sana hadi leo. Katika maisha yangu ya kikazi, daima nilijikita kwenye utumishi wa umma uliotukuka".
MZEE MCHAURU.


By MZEE WA _ATIKALI  ✍️✍️✍️

May 2020