Saturday, May 16

MH. MZEE FREDRICK MCHAURU-: MTANGANYIKA WA KWANZA KUPATA "SCHOLARSHIP" AGONGA KARNE MOJA DUNIANI!!!

BY MZEE WA ATIKALI ✍️✍️✍️

"Tatizo letu kama nchi ni kuwa vichwa vya wazee na viongozi wetu ndio maktaba za kumbukumbu za mambo muhimu ya Taifa. Sasa wanapofariki, hufariki na kumbukumbu hizo. Hii si sahihi hata kidogo. Ni muhimu kama Taifa tuchukue hatua madhubuti ili kumbukumbu hizi zihifadhiwe vitabuni, Maktaba na Makumbusho ya Taifa".
Prof. HAROUB OTHMAN, 3.7.2006.

1. USULI

Tarehe 25.4.2020, Mzee FREDRICK JONES MCHAURU alitimiza miaka 100 na kuwa mmoja wa Watanzania wachache sana kuweza kuishi hapa duniani kwa KARNE MOJA!. Mzee MCHAURU na Mangi Mkuu wa Wachaga Mh. THOMAS MAREALE ndio walikuwa Watanganyika wa kwanza kupata "Scholarship" ya kwenda kusoma majuu ambapo walisoma  London School of Economics, UK.

Kwavile Bongolanders wengi hawajawahi hata kumsikia Mzee MCHAURU na kwavile Mzee huyu amelifanyia Taifa hili mambo mengi kwenye utumishi wake uliotukuka, hivyo basi ATIKALI hii Mahsusi inamdadavua kwa ufupi Mzee huyu wa kipekee kabisa nchini.

Je, Mzee huyu alizaliwa wapi, lini, alisoma wapi na utumishi wake wa umma ulikuwaje?.


2. MCHAURU AZALIWA

MCHAURU alizaliwa siku ya Jumapili ya tarehe 25.4.1920 huko Newala, Ntwara, Tanganyika.

3. MASOMO

MCHAURU alisoma St. Joseph's college, Chidya na alikuwa ni kijana hodari sana darasani. Hiyo ilipelekea afaulu mitihani yake kwa kiwango cha juu hadi kuchaguliwa kujiunga na St. Andrew's  college, Minaki.

4. MCHAURU APATA "SCHOLARSHIP"

JMwaka 1944, MCHAURU na Mangi Mkuu wa Wachaga Bw. THOMAS MAREALLE walipata scholarship toka serikali ya Ukoloni ya Uingereza kwaajili ya kwenda kusoma London School of Economics, UK. Wawili hawa ndio walikuwa Watanganyika wa kwanza kupata Scholarship hapa nchini. Walisoma UK hadi 1946 waliporejea nchini baada ya kuhitimu mafunzo yao.

5. MCHAURU AAJIRIWA  OFISA MAENDELEO TABORA

Baada ya kurejea, MCHAURU aliajiriwa kama Afisa Maendeleo wa Jamii Tabora. Kati ya 1947 na 1952, alikuwa Bwana maendeleo wa nusu ya Tanganyika nzima ie mikoa yote ya Kanda ya Ziwa, Ziwa Magharibi, Kusini na Nyanda za Juu Kusini. Licha ya barabara mbovu na changamoto lukuki, MCHAURU aliifanya kazi yake kwa weledi wa hali ya juu.

Mwenzake MAREALLE akapewa Dodoma kupanda juu kuelekea Morogoro, Pwani, Dsm na Kaskazini kote.

6. MCHAURU AANZISHA ELIMU YA WATU WAZIMA NCHINI

MCHAURU ni mtu wa maendeleo sana na alipenda kuwainua Watanganyika wenzake. Hivyo, MCHAURU akawa Mtaganyika wa kwanza kuanzisha Elimu ya Watu Wazima nchini mwaka 1959 huko Singida. Huu ulikuwa mpango kabambe uliopendwa sana. Mpango huu mujarab ukaigwa nchi nzima na ilipofika 1980, TZ ikawa moja ya nchi zenye idadi kubwa ya watu wanaojua kusoma na kuandika duniani. Hii yote ni kutokana na maono na  juhudi za MCHAURU.

7. MCHAURU AWA PRINCIPAL WA KWANZA CHUO CHA TENGERU

Mwaka 1962, MCHAURU aliteuliwa kuwa Principal wa kwanza wa Chuo cha Tengeru, Arusha. Mwanzoni, chuo hiki kilikuwa ni "Polish Refugees Camp" wakati wa Vita Kuu ya 2 ya Dunia. Wapolish walifungua "ranch" ya mifugo ambapo walipoondoka ikabadilishwa jina na kuitwa Tengeru.

8. MCHAURU ATEULIWA  KATIBU MKUU USHIRIKA

Mwaka 1965, Rais NYERERE alimteua MCHAURU kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Ushirika, Ustawi wa Jamii na Utamaduni. Wakati huo, serikali ilikuwa na Makatibu Wakuu 19 chini ya Chief Secretary JOSEPH NAMATA ambaye pia alitokea Ntwara kama MCHAURU.

9. MCHAURU ATEULIWA KATIBU MKUU MAMBO YA NDANI

Rais NYERERE alimteua MCHAURU kuwa Katibu Mkuu Wizara nyeti ya Mambo ya Ndani mwaka 1968. MCHAURU alihudumu Wizara hiyo kwa weledi na uadilifu wa hali ya juu hadi 1971.

10. MCHAURU AWA KATIBU MKUU ULINZI

Mwaka 1972, Rais NYERERE aliunda Wizara mpya ya Ulinzi na JKT na  kumteua Mh. EDWARD SOKOINE kuwa Waziri na kisha akamteua MCHAURU kuwa Katibu Mkuu wake kutokana na kazi mujarab aliyokuwa ameifanya kwenye Wizara ya Mambo ya Ndani.

11. MCHAURU ASTAAFU SERIKALINI

 Mwaka 1973, MCHAURU alistaafu kazi serikalini. Baada ya kustaafu serikalini, MCHAURU alihudumu kwenye Bodi mbalimbali hadi mwaka 1999.

12. MCHAURU AWA MWENYEKITI WA BODI YA POSTA NA SIMU

MCHAURU alipewa jukumu la kusimamia Posta & Simu kama Mwenyekiti  wa Bodi na kulitekeleza vizuri jukumu hilo.

13. MCHAURU Atafuta Wawekezaji kwenye Madini

Kwenye miaka ya 1980, MCHAURU alienda majuu kuwaalika wawekezaji ili kuja kuiinua sekta ya madini. MCHAURU aliweza kufanikisha jukumu hilo kwa ushirikiano mkubwa wa Bw. NIVEN SINCLAIR, raia wa Uingereza.

14. MCHAURU Awa Mwenyekiti GEITA Gold Mines

Kutokana na jitihada zake kuntu, MCHAURU akawa Mwenyekiti wa Geita Gold Mines na Ashanti Gold Mine.

15. MCHAURU VILLAGE

MCHAURU alikuwa mtu maarufu sana Geita kiasi kwamba kutokana na mchango wake mkubwa, huko machimboni Geita kuna eneo maalum limepewa jina lake kwa heshma yake MCHAURU Village.  Hiyo ni sehemu nzuri sana ambako wanaishi matajiri tu.

16. MCHAURU AIRPORT

Geita kuna uwanja  wa ndege mzuri unaotumiwa na mgodi wa dhahabu wa Geita. Uwanja huo ulipewa jina la MCHAURU Airport kwa heshma ya MCHAURU. Uwanja huu una hadi taa za kutua na kurukia wakati wa usiku na wakati wa ukungu na unatambulika hadi "International Civil Aviation Organisation". Kwa hakika, MCHAURU ana heshma ya kipekee huko Geita.

18. TAMATI

Huyu ndiye Mzee FREDRICK JONES MCHAURU ambaye alifanya kazi kwa weledi na Uzalendo wa hali ya juu hadi anastaafu.

Mzee MCHAURU kwa sasa amegonga Karne Moja hapa duniani lakini akiwa bado yuko ngangari ambapo anaishi Upanga Magharibi, Mtaa wa Kitonga, Kitalu Na. 121, nyuma ya hospitali ya Tumaini.

Mzee MCHAURU ana wajukuu zaidi ya 20 na vitukuu zaidi ya 10. Mkewe, THEKLA MCHAURU aliishatangulia mbele za haki. Bi. THECKLA alikuwa Mwanamke wa kwanza Kusini ya TZ kuwa Mwalimu wa Cheti ambaye alikuwa akilipwa mshahara wa TZS 40. Baadaye Bi. THECKLA alikuja kuwa Katibu Mkuu  wa UWT Taifa.

KONGOLE KWAKO MZEE MCHAURU NA NAPENDA KUMALIZIA ATIKALI HII KWA NUKUU YAKO MUJARAB:-

"Katika utumishi wangu toka 1947 sikuwa hata siku moja kuwa na tamaa ya mali wala utajiri. Hili ni jambo linalonipa faraja sana hadi leo. Katika maisha yangu ya kikazi, daima nilijikita kwenye utumishi wa umma uliotukuka".
MZEE MCHAURU.


By MZEE WA _ATIKALI  ✍️✍️✍️

May 2020


 

No comments:

Post a Comment