Na, Al-Hasan Muhidin, MichuziTv
Klabu ya Simba kwa kushirikiana na Taasisi ya Mo Dewji wametoa msaada wa Barakoa kwa wananchi wa maeneo mbalimbali ndani ya Jiji la Dar es Salaam kwa ajili ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona.
Akizungumza na waandish wa habari wakati wa tukio hilo, Msaidizi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Klabu ya Simba Rispa Hatib amesema tukio hilo ni la siku tatu kuanzia leo Jumamosi na litahitimishwa siku ya Jumatatu.
Amesema, janga hili ni la Dunia na nchi nzima kwa ujumla na Taasisi ya Mo imeamua kushirikiana na klabu ya Simba kugawa barakoa hizi kwa wanachi wa ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam na maeneo mengine.
Rispa amesema, wameanza na maeneo ya Kivukoni, Kariakoo, Buguruni hadi Mbagala ambapo zoezi hili litaenda kwa siku tatu na wanategemea litaenda vizuri.
Amewaomba wananchi wajitokeze kuchukua barakoa hizo kwani zitawasaidia hasa wale ambao hawana uwezo wa kununua na unaweza kuzifua na kutumia tena.
Katika zoezi hilo, wananchi mbalimbali waliweza kujitokeza kupokea msaada wa barakoa hizo na kuwashukuru sana uongozi wa Simba na Taasisi ya Mo kwa kuamua kuwajali watu wasio na uwezo wa kununua barakoa hizo.
Kwa sasa dunia nzima ipo katika vita ya kupambana na maambukizi ya ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Covid 19 na watalaamu wa afya wakiwataka wananchi kutumia barakoa muda wote pamoja na vitakasa mikono ili kupunguza maambukizi.
No comments:
Post a Comment