Friday, July 28

Mwenyekiti wa Maspika jumuiya ya Madola barani Afrika

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Maspika na viongozi wa Bunge katika nchi za Jumuiya ya Madola barani Afrika.





Mhe Lissu afunguka ishu ya kupima ‘haja ndogo’


Mbunge wa Singida Mashariki na Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), amefunguka jinsi maaskari walivyomkamata na kutaka kupima haja ndogo bila sababu maalumu.
Mhe Lissu amesema niliwakatalia kwa sababu nilishitakiwa kwa kosa la uchochezi na sio kosa lingine na kama wangemshitaki kwa kosa lingine linalomtaka afanye hivyo basi kisheria angefanya hivyo.
“Mimi nimeshtakiwa kwa uchochezi kupima mkojo, unadhibitisjhaje uchochezi na kupima mkojo? wakaniambia kuna vitu wanavitafuta, mimi nikawambia mkanishtaki na vitu hivyo kwanza ili muende kwa hakimu mkapate order ili mje mchukue mkojo wangu… anyway mimi niliwakatalia”,amesema Tundu Lissu kwenye mkutano wake na waandishi wa habari mapema leo baada ya kuachiwa kwa dhamana.
Hata hivyo Mhe Lissu amesema asingekubali kupima mkojo kwani kufanya hivyo angebambikiziwa kesi na kutengeneza headline kwenye magazeti.

Kiungo wa Mbambane Swallows ya Swaziland afaulu vipimo vya afya Yanga SC

Kiungo Mkabaji, Papy Kabamba Tshishimbi anayekipiga Mbambane Swallows ya Swaziland, anatarajia kumalizana na Yanga SC wakati wowote kuanzia sasa baada ya kufaulu vipimo vya afya.

Mchezaji huyo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) mwenye umri wa miaka 27, amefanyiwa vipimo hivyo katika zahanati ndogo ya Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam chini ya daktari, Nassor Matuzya.
“Yanga ni timu kubwa, hatuwezi kusubiri hadi mkataba wake uishe, tunamsajili mara moja,” alisema Nyika
Miongoni mwa wachezaji waliosajiliwa katika kikosi hicho cha Mzambia, George Lwandamina ni Golikipa wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Ramadhani Kabwili, kipa Mcameroon, Youthe Rostand aliyesajiliwa kutoka African Lyon, beki Abdallah Hajji ‘Ninja’ kutoka Taifa Jang’ombe, kiungo Pius Buswita kutoka Mbao FC, na mshambuliaji Ibrahim Ajib kutoka kwa mahasimu, Simba SC.

Serikali kufufua mfuko wa serikali za mtaa

Serikali yakusudia kufufua Mfuko wa Maendeleo ya Serikali za Mitaa (LGDG) ili kuendeleza miradi mbalimbali ya maendeleo iliyoibuliwa na wananchi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini.
Akizungumza na wadau mbalimbali wa maendeleo kutoka nchi mbalimbali zinazochangia bajeti ya Serikali katika mkutano uliofanyika, Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mwalimu Julius Nyerere (JNICC), Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),George Simbachawene jana jijini Dar es salaam.
“Mfuko huu ulipoanzishwa wananchi walivutiwa sana na walifanya jitihada za kubuni na kuibua miradi mbalimbali kwani Serikali ilitenga bajeti ya fedha kusaidia miradi hiyo, lakini kuanzia miaka ya 2013 hadi 2015 miradi hiyo ilianza kuzorota na ndiyo maana kuna maboma mengi kama vile Vituo vya Afya, Madarasa na Nyumba za Waalimu ambayo hayakukamilika kutokana na mfuko huo kuzorota,” alisema Mhe. Simbachawene
Aidha Simbachaweni alisema kuwa Mfuko huo una umuhimu katika kuinua uchumi na kuleta maendeleo ya Taifa, ambapo wananchi wamekua wakiibua miradi mbalimbali kama vile kujenga barabara, vituo vya Afya, Zahanati, nyumba za Walimu pamoja na madarasa, miradi ambayo imekuwa ikianzishwa na wananchi na kuendelezwa na Serikali.
Na Emmy Mwaipopo

Serikali kuwatumbua watumishi watakao hujumu Maliasili


Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Maghembe amesema kuwa hatoweza kumvumilia mtumishi yeyote wa wizara hiyo atakayehujumu Maliasili za Taifa kwa kushirikiana na majangili.
Waziri Maghembe ametoa kauli hiyo wakati wa mkutano wa mwaka wa Wahariri na wanahabari wandamizi kutoka vyombo vya habari mbalimbali hapa nchini uliofanyika mkoani Tanga.
“Na sisi watumishi bado tuna shida na watumishi kama mnavyojua, tuna watumishi wengi 90 percent wazuri, lakini tuna 3,4,5,6 wasio waaminifu lakini bado tunaangalia kwa makini na pale tutakapo mngamua mtu yupo kwenye shughuli hiyo inabidi tuwatumbue ili tuweze kuondokana na watu hawa, kwasababu sekta hii ni muhimu sana kwa uchumi wa Taifa letu
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu TANAPA, Allan Kijazi alielezea mchango wao kwa Taifa kupitia sekta ya utalii
“Mwaka jana tulichangia sh. Bilioni 27 kwenye mfuko mkuu wa serikali na mwaka ujao tunategemea kuchangia kiasi cha sh. Bilioni 34.5 kama mchango wa moja kwa moja kwenda kwenye bajeti kuu ya serikali.”
Na Emmy Mwaipopo

Jeshi la polisi latoa hofu wananchi


Jeshi la polisi nchini limewatoa hofu wananchi mkoani Shinyanga kuwa limeimarisha usalama katika mipaka yote ya mkoa huo ili kudhibiti raia wa kigeni kuingia mkoani humo na kufanya vitendo vya uhalifu.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza kikao cha ndani cha askari wa Jeshi hilo, Mkuu wa Jeshi nchini , IGP Simon Sirro amesema vita hiyo inakwenda sambamba na vita ya ugaidi ambapo tayari limeathiri nchi jirani.
“Kwenye mipaka yetu tumejipanga vizuri sana tunafanya operesheni za pamoja na intelijensia za pamoja kwa hiyo hilo sina mashaka nalo, kwa wananchi wa Shinyanga wasiwe na mashaka na hilo kwasababu tumejipanga na tunajua uchaguzi umekaribia pale Kenya ni lazima sisi wenyewe tuimarishe doria zetu mipakani,” alisema IGP Sirro.
“Lazima intelijensia zetu ili anapoingia tuweze kumshughulikia tunajua kuna tatizo la Alshabab kwa wenzetu Kenya kuna suala la ugaidi kwahiyo lazima tuwe makini sana.”
Na Emmy Mwaipopo

Barrick (Acacia) Wakubali Yaishe.....Wiki Ijayo Wataanza Mazungumzo na Serikali


Kampuni ya Barrick Gold ya nchini Canada, imesema wiki ijayo timu ya wataalamu wake watakuja nchini kwa ajili ya kufanya mazungumzao na Serikali kuhusu uendeshaji wa migodi yake.

Tamko hilo limekuja siku chache baada ya Rais Dk. John Magufuli kutangaza kuwa iwapo Barrick inayoimiliki Kampuni ya Acacia itachelewa kuja kufanya mazungumzo ataifunga migodi yao.

Wakati kampuni hiyo ikijiandaa kuja nchini, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) tayari imepeleka madaia ya Dola za Marekani bilioni 190 ambazo ni sawa na Sh trilioni 424), kwa Kampuni ya Acacia, ikiwa ni malimbikizo ya kodi kutoka mwaka 2000.

Taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa Financial Post juzi ilisema. “Kampuni ya Barrick Gold kupitia ripoti yake ya robo mwaka imesema itaanza majadiliano na Serikali ya Tanzania wiki ijayo kuhusu marufuku ya kusafirisha nje madini na masuala mengine yaliyoikumba kampuni inayoimiliki ya Acacia.

“Taarifa hiyo ya mazungumzo inakuja baada ya Jumatatu wiki hii Tanzania kuwasilisha bili ya dola bilioni 190 kwa Accacia yenye makao makuu Uingereza.

“Serikali ya Tanzania inaituhumu Acacia, ambayo inamilikiwa na Barrick kwa asilimia 63.9 kudanganya mapato yake ili kukwepa kodi na hivyo kuitaka ilipe malimbikizo pamoja na faini. Acacia imekana tuhuma hizo.

“Tanzania pia iliweka marufuku ya kusafirisha mchanga wa dhahabu (makinikia) na fedha Machi mwaka huu, hatua ambayo inaweza kuathiri asilimia sita ya uzalishaji wa wakia milioni 5.3 hadi milioni 5.6 ya dhahabu kwa mwaka katika migodi ya Acacia.

“Barrick ilisema inasubiri hadi Acacia itakaporekebisha mwongozo wake wa uzalishaji kabla ya kubadili mwelekeo mzima wa uzalishaji wake kwa mwaka,” ilisema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ilisema, Barrick yenye makao yake makuu Toronto, Canada iliripoti kuongezeka kwa mapato kufikia Dola bilioni 1.08 robo iliyoishia Juni 30, kutoka dola milioni 138 kwa mwaka mwaka jana.

“Hilo lilichochewa na mafanikio makubwa ya mauzo ya hisa katika mgodi wa Veladero na mradi wa Cerro Casale. Mtiririko wa fedha kwa kipindi hicho ulikuwa dola milioni 43 ukiwa umeshuka kutoka dola milioni 274 kwa kipindi kama hicho mwaka jana kutokana na kiwango cha juu cha kodi, ongezeko la mtaji na ongezeko lililopangwa kwa ajili ya matumizi ya ukuaji wa badaye,” ilisema.

Juni 14 mwaka huu, Rais Magufuli alikutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation Profesa John Thornton na Ikulu ikatoa taarifa kwa umma kwamba, katika mazungumzo hayo, kampuni hiyo imesema  ipo tayari kufanya mazungumzo na Serikali ya Tanzania ili kulipa fedha ambazo Tanzania imezipoteza kutokana na kampuni hiyo kuendesha shughuli zake hapa nchini.

Julai 21, 2017 akizungumza kwenye mkutano wa hadhara mkoani Kigoma, Rais Magufuli alisema. “Nitasimamia haki siku zote katika maisha yangu, na niliwaambia nimeanzisha vita hii ya kiuchumi, vita ya kiuchumi ni mbaya sana, wakubwa wale huwa hawafurahi, kuna viongozi wengi tu mliona yaliyowapata ni kwasababu nchi zao zilikuwa na mali.

“Lakini wale wakubwa wakataka kuchezea hizo mali, kwa manufaa yao na siyo kwa manufaa ya wananchi wa pale, walitumia mbinu nyingi za kila aina, lakini Mungu wangu ni mwema na Watanzania ni wema watasimama kwa ajili ya taifa hili.

“Ninayoongea nayajua ni matrilioni ya fedha ambayo yameibiwa, na kwasasa hivi tumewaita waje wafanye mazungumzo, wamekubali lakini wakichelewachelewa  nitafunga migodi yote.

“Ni mara 10 migodi hii tukaigawana Watanzania wachimbe wawe wanauza tuwe tunapata kodi, kuliko kuchimbwa na watu wanaojiita wawekezaji halafu hawalipo kodi.

“Walikuwa wanazungumza mle wanachimba dhahabu, madini machache tu, matatu. tumegundua mle kuna madini mengi.

“Tanzania hii ni nchi tajiri, lakini imekuwa ikiibiwa mno, tumechezewa sana, mimi nipo serikalini na mimi ndiye najua siri za serikali, tumechezewa sana kwa kuibiwa sana mali zetu, kwenye dhahabu huku tumeibiwa mno, ukiyajua yale yaliyokuwa yanafanyike mle unaweza ukalia.

“Unaweza ukatamani usiishi, mtu anachimba anapokea anapeleka na anashirikiana na baadhi ya watu tuliowaamini kwenda kulisimamia hili.

“Anasema hapa tunasafirisha mchanga na Watanzania wote tunaamini tunasafirisha mchanga, mbona hawajaja Kibondo kuchukua mchanga wa hapa mbona na penyewe tunao?

“Lakini tunaamini, wanaupeleka kwenye makontena wanapeleka Ulaya na wakisha enda kuusafisha kule ule mchanga unaobaki wala hawaurudishi, ulikuwa ni utapeli wa ajabu, na ni aibu kubwa kuona utapeli huu unafanywa na watu ambao ni wakubwa.

Julai 26 akiwa mkoani Singida, Rais Magufuli tena alisema “Haiingii akilini watu wanakuja wanachukua mali zetu na kuondoka nazo, ifike mahali tuamke, tumeibiwa vya kutosha, nendeni mkachimbe madini, hizo fedha tutagawana sisi, hata kama hatufanyi kazi hizo fedha tutagawana.

“Wapo wachina wanakuja kuchimba barabara hapa nchini, tunashindwaje kuwatumia hawa wakachimbe madini yetu kisha wakatuachia dhahabu yetu halafu wao wakaondoka?

“Mimi ndiye Rais, hakuna anayejua siri za serikali kama mimi na nawaambia mmepata mtu ambaye anazungumza ukweli, ningeweza kunyamaza kwa vingine ninavyoviona, lakini nataka kujenga Tanzania mpya.

“Yale makontena yote ningeweza kuwaambia tugawane mzee, hata kingereza ninajua, ningeweza kuwaambia give me ten percent (asilimia 10).

“Ningejenga mahoteli na kuwa na kampuni nyingi kwani wapo Watanzania wamejenga huko nje lakini nyumba za wazazi wao zimechakaa, mimi nimezaliwa hapa, ninaishi hapa na nitakufa hapa,”alisema Rais Magufuli.

Tundu Lissu: Nitanyamaza Nikifa

SeeBait
Mwanasheria  Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, ameachiwa kwa dhamana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam na kusema kuwa atanyamaza tu baada ya kufariki dunia.

Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), alipata dhamana jana baada ya mahakama hiyo kubaini hoja za Serikali za kumnyima haki hiyo hazina mashiko.

Baada ya kutoka mahakamani, alikwenda katika ofisi za Chadema zilizopo Kinondoni, ambako pamoja na mambo mengine, alisema ataendelea kuikosoa Serikali hadi pale atakapokufa.

“Hakuna gereza litakalotunyamazisha, watu wakipelekwa mahabusu watazungumza wakiwa mahabusu, wakifungwa watazungumza wakiwa kifungoni, hivyo ili wanyamaze itabidi kwanza wafe… tutanyamaza tukiwa wafu kwa sababu wafu hawasemi,” alisema.

Lissu alisema kuna haki ya kuwasema na kuwakosoa wale waliopewa madaraka na wananchi.

Alisema katika sheria ya uchochezi ya mwaka 1953, kutoa kauli yoyote yenye lengo la kukosoa matendo ya Serikali, sera si kosa na wala kumkosoa rais na Serikali yake si kosa.

“Sasa ukisema wanakukamata, wanakushtaki kwa uchochezi, wanakupiga, wanakupeleka central (kituo kikuu cha polisi) au Oysterbay wakikupeleka sio kosa, bali unatumia akili zako kuikosoa Serikali,”alisema Lissu.

Akizungumzia kuhusu kupimwa mkojo, Lissu alisema alipelekwa na askari kwenye nyumba iliyo karibu na Ocean Road, lakini alikataa kutekeleza hilo.

“Niliwaambia nyie maaskari mimi nimeshtakiwa kwa uchochezi, unathibitishaje uchochezi kwa kupima mkojo?” alisema Lissu.

Alisema askari hao walimjibu kuwa kuna vitu wanavitaka, akawaeleza:“Nendeni mkanishtaki, hamjapata oda ya hakimu, hamtaona mkojo wangu.”

Baada ya kauli hiyo, alisema askari hao walimwambia kuwa wao wana mamlaka.

“Nikawaambia mimi ni Rais wa Mawakili (TLS). Siku ukikamatwa, ukaambiwa kupimwa damu, mkojo waambie hutaki hata kama wamekushtaki.

“Ukitoa mkojo na usiposaini hakuna dili, walichokuwa wanatafuta wapate dili ya kutengeneza ‘headline’ (kichwa cha habari), ‘huyu anasema hivi kwa kuwa anatumia dawa’, nani asiyejua polisi wanabambika? Nikakataa, nikawaambia mnataka twende kunisachi twendeni.”

Lissu alisema akiwa Segerea alikutana na wafanyabiashara James Rugemalira na Harbinder Singh Sethi wanaokabiliwa na kesi ya uhuhumu uchumi na utakatishaji fedha.

“Mwaka jana nilisema hawa lile dili (kashfa ya akaunti ya Tegeta Escrow) watu lazima wawajibike, waliowapa hela, waliosaini BoT (Benki Kuu ya Tanzania), walioruhusu hizo fedha kwa kusema James Rugemalira na Harbinder Singh wapewe wako wapi?” alihoji.

Lissu alihoji wapi walipo waliopewa mgawo wa fedha za Escrow.

Kabla ya kutoa uamuzi wa dhamana jana, Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Wilbard Mashauri, alipitia hoja za pande mbili zilizokuwa zinapingana, zilizowasilishwa mahakamani hapo mwanzoni mwa wiki.

“Hii kesi ina dhamana, hoja kwamba anakabiliwa na kesi nyingi zenye viashiria va uchochezi haina mashiko kwa sababu hakuna taarifa kuwa aliwahi kuruka dhamana.

“Kwangu mimi hiyo haitoshi kumuweka mahabusu, hoja ya kwamba aendelee kuwepo rumande kwa usalama wake, hakuna taarifa kwamba akipewa dhamana maisha yake yatakuwa hatarini.

“Mshtakiwa anawakilishwa na mawakili 18 wanaomuombea dhamana, wanafanya hivyo kwa upendo walionao dhidi ya mshtakwa, hivyo haiwezekani akipewa dhamana atadhurika.

“Mahakama inakubali maombi ya dhamana, mshtakiwa atadhaminiwa kwa masharti ya kuwa na wadhamini wawili, watasaini dhamana ya maandishi ya Sh milioni 10 kila mmoja na mshtakiwa hatakiwi kusafiri bila kibali cha mahakama,” alisema.

Baada ya kutoa masharti ya dhamana, Hakimu Mashauri aliahirisha kesi kwa nusu saa ili watafutwe wadhamini hao ambao walipatikana kwa juhudi za Wakili Peter Kibatala aliyetoka nje ya mahakama kuwatafuta.

Awali wadhamini hao walishindwa kuingia eneo la mahakama kutokana na kuimarishwa kwa ulinzi kulikotokana na kuwapo kwa kesi za ugaidi mahakamani hapo.

Kwa upande wake, Wakili wa Serikali Mkuu, Simon Wankyo, alidai mahakamani kwamba upelelezi wa kesi hiyo umekamilika hivyo aliomba tarehe nyingine ya kumsomea mshtakiwa maelezo ya awali.

Hakimu Mashauri aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 24, mwaka huu kwa kuanza usikilizwaji wa awali.

Lissu alidhaminiwa na wadhamini wawili walioweka dhamana ya maandishi ya Sh milioni 10 kila mmoja.

Ya Wasira na Bulaya kufahamika leo Mahakama ya Rufaa


Rufaa iliyokatwa na aliyekuwa Mbunge wa Bunga  Stephen Wasira ya kupinga ubunge wa Mbunge wa Easter Bulaya.

Wasira amekata Rufaa baada ya kushindwa kwenye Mahakama kuu Kanda ya Tabora.

Fifa Yatua Bongo



MENEJA Miradi ya Maendeleo wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kwa Afrika, Mzimbabwe Solomon Mudege amewasili nchini jana usiku kwa ajili ya kufuatilia kinachoendela kwenye Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Bin Zubeiry Sports – Online inafahamu Mudege tayari yupo nchini na pamoja na kukutana na Kamati ya Utendaji ya TFF kesho Dar es Salaam, pia atakuwa na kikao na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrisons Mwakyembe.
Bado haijafahamika Ofisa huyo amekuja kwa sababu zipi haswa na kama ameitwa na viongozi wa TFF au amekuja kwa maagizo ya FIFA tu.



Lakini inafahamika hamkani si shwari kwa sasa katika soka ya Tanzania, kufuatia viongozi wakuu wawili wa TFF, Rais Jamal Malinzi na Katibu wake, Selestine Mwesigwa kuwekwa rumande tangu Juni 29 kwa tuhuma za ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka.
Malinzi, Mwesigwa pamoja na Mhasibu wa TFF, Nsiande Isawafo Mwanga walipelekwa rumande Juni 29 baada ya kusomewa mashitaka 28 ya kughushi na kutakatisha fedha kupitia akaunti ya TFF iliyopo katika banki ya Stanbic, Dar es Salaam.
Katika mashitaka hayo, 25 yanakwenda moja kwa moja kwa Rais wa shirikisho hilo, Malinzi akidaiwa kughushi michakato mbalimbali ya kifedha, huku matatu yakiwahusu wote na Katibu wake na Mhasibu wake Nsiande Isawafo Mwanga.
Malinzi aliingia madarakani TFF Oktoba mwaka 2013 baada ya kupata kura 72 kati ya 126 zilizopigwa akimshinda aliyekuwa mpinzani wake wa karibu, Athumani Nyamlani.
Lakini baada ya kesi hii kuanza kuunguruma na kuwekwa rumande, Kamati ya Utendaji ya TFF ilikutana na kumteua Makamu wake, Wallace Karia kukaimu Urais wa shirikisho hilo.
Lakini kwa mwenendo wa kesi, Malinzi ndiyo kama amekwishaaga TFF, kwani uchaguzi unatarajiwa kufanyika Agosti 12 mjini Dodoma naye hajashiriki usaili wa wagombea, hivyo haruhusiwi tena kugombea. 
Karia naye yupo hatarini kuenguliwa katika uchaguzi baada ya kuitwa Idara ya Uhamiaji ya Taifa kuthibitisha uraia wake, akidaiwa kuwa ni raia wa Somalia. Mwenyewe amekiri kuwa na asili ya Somalia, lakini amekataa kuwa si Mtanzania. Uhamiaji inaendelea na uchunguzi dhidi yake.

Muuguzi aingia matatani kwa rushwa

MKUU wa Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya, Rehema Madusa, amemsimamisha kazi mtumishi wa Hospitali ya Wilaya kwa tuhuma za kudai na kupokea rushwa ya Sh. 15,000 kutoka kwa mzazi ili amtibu mtoto wake.

Madusa alisema juzi kuwa alipata taarifa ya mtumishi huyo (jina linahifadhiwa) kwa sababu za kiuchunguzi kuwa alidai Sh. 30,000 lakini mzazi huyo alikuwa hana kiasi hicho hivyo akampatia nusu na akaahidi kumalizia zingine baada ya matibabu.

Alisema alifika katika hospitali hiyo kwa ajili ya kujiridhisha na kwamba baada ya mazungumzo na mzazi huyo na kuelezwa hali halisi ilivyo, alimwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Sophia Kumbuli, amsimamishe.

Aidha, alisema aliiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kumkamata mtumishi huyo na kuchunguza tuhuma zinazomkabili.

“Baada ya kupata taarifa za tukio hilo nilifika hospitalini hapo kwa ajili ya mahojiano na mzazi huyo aliyeombwa rushwa na baada ya kumhoji niliagiza Mkurugenzi amsimamishe na Takukuru wamkamate mpaka sasa Takukuru wanaendelea na kazi,” alisema Madusa.

Kambuli ambaye ni mwajiri wa muuguzi huyo, alikiri kuwapo kwa tukio hilo huku akisema nesi huyo hakuwa mtumishi wa halmashauri hiyo bali alikuwa anajitolea.

Pia alisema licha ya kutokuwa mwajiriwa wa halmashauri, kwa tuhuma hizo alilazimika kumsimamisha kazi kama alivyoagizwa na Mkuu wa Wilaya, lakini hana mamlaka ya kuchukua hatua zaidi.

Alisema kwa sasa vyombo vyenye mamlaka vinaendelea na kazi ya kuchunguza tuhuma za nesi huyo na kwamba endapo itabainika kuwa ni kweli, hatua zaidi zitachukuliwa.

Aliwataka watumishi wa halmashauri hiyo kuepuka vitendo kama hivyo kwa madai kuwa vinachafua utendaji kazi wa halmashauri na vinasababisha wananchi kukosa imani na hospitali za umma.

Wabunge CUF Kumshtaki Prof Lipumba


Siku chache baada ya Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi CUF, Prof. Lipumba kuwavua uanachama Wabunge wanane wa Viti Maalum kisha Spika Ndugai kuridhia uamuzi huo, jana July 27, 2017 Wabunge hao wamefungua kesi katika Mahakama Kuu ya Tanzania.

Wabunge hao wamefungua kesi hiyo iliyopewa namba 143/2017 kupitia Wakili wao Peter Kibatala lakini hata hivyo bado haijapangiwa Jaji huku Wabunge hao wakidai hawajapewa muda wa kujitetea.

Mbali na kufungua kesi katika Mahakama Kuu Tanzania, pia wamekata rufaa ndani ya Chama chao kupinga utekelezaji huo na kuiomba Mahakama isitishe utekelezaji wa uamuzi wa kufukuzwa Uanachama wao.

Lipuli yapewa fungu la usajili


Iringa. Aliyekuwa mgombea Uenyekiti wa Timu  ya Lipuli, Dk. Nuhu Muyinga ameikabidhi  Sh20 milioni alizoahidi kutumia kwa ajili ya timu hiyo kuweka kambi mkoani Iringa.
Muyinga alikabidhi fedha hizo kwa Makamu Mwenyekiti wa Lipuli, Ayoub Kiwelo katika makabidhiano yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Uwanja wa Samora mbele ya viongozi mbalimbali wa kamati ya utendaji wa timu ya Lipuli FC ‘Wanapaluhengo'.
Muyinga aliwataka viongozi hao kuzitumia fedha hizo kutumia kusajili wa wachezaji bora.
Alisema wakati wa kampeni za uchaguzi wa Lipuli aliwaahidi wanachama endapo watamchagua atatoa dola 20,000 kwa ajili ya kuirudisha timu hiyo nyumbani kuendelea na kambi ili wapenzi na wanachama waweze kushuhudia wachezaji watakaosajiliwa na timu hiyo.
Alisema kuwa baada ya kushindwa uchaguzi ameamua kutekeleza ahadi hiyo, lakini iende katika usajili wa wachezaji  na kuhaidi kuisaidia Lipuli iweze kufanikisha malengo yake.
 Makamu Mwenyekiti wa Lipuli FC, Ayoub Kiwelo alimshukuru kwa msaada huo na kumpongeza Muyinga kwa uzalendo wa kweli katika kuisaidia timu hiyo licha ya kushindwa katika uchaguzi.
Alisema kitendo alichoonyesha Muyinga ni cha kuigwa na kila mpenda soka mkoani hapa na kumwaahidi fedha hizo zitatumika kama ambavyo ameelekeza kwa uongozi licha ya kukabiliwa na changamoto nyingi katika timu ya Lipuli.

Usajili wa Yanga wa kimataifa zaidi


Dar es Salaam. Mwenyekiti wa kamati ya usajili wa Yanga, Hussein Nyika amesema klabu hiyo imefanya usajili madhubuti wenye lengo la kuhakikisha wanafanya vizuri kimataifa.
Nyika amesema mashabiki wa soka nchini watambue kuwa Yanga imelikamata soka la Tanzania kwa sasa.
"Kamati imefanya kazi kubwa, Yanga inalenga kuliteka soka la Afrika na si hapa nyumbani tu. Wanachama wa Yanga waondoe hofu kuhusu timu yao," amesema Nyika katika mahojiano yaliyofanyika makao makuu ya klabu hiyo mtaa wa Jangwani.
Katika kipindi hiki cha usajili Yanga imewasajili Ibrahim Ajibu, Abdallah Shaibu, Ibrahim Yahya  na kufanikiwa kuwabakisha mastaa Donald Ngoma na Thaban Kamusoko.
Katika hatua nyingine, Nyika alibinisha kuwa klabu hiyo imekamilisha usajili kwa asilimia 95.
"Leo (Alhamisi) tunamalizana na Tshishimbi muda wowote kwakuwa amefuzu vipimo vya afya. Asilimia tano iliyobaki tutasajili wachezaji wa ndani," alisema
Mmoja wa wachezaji wanaohusishwa kumwaga wino ni Raphael Daud wa Mbeya City.
Nyika alisema mazungumzo kati ya pande mbili yanakwenda vizuri.

TIMU YA RIADHA CHINI YA MIAKA 17 YAREJEA NCHINI NA MEDALI YA SHABA

Na Shamimu Nyaki –WHUSM
Timu ya riadha ya vijana chini ya miaka 17 imeleta heshima kubwa kwa nchi yetu baada ya kurejea na medali ya shaba aliyoshinda kijana Francis Damasi katika  mbio za mita 3000 kwenye mashindano ya  Jumiya ya Madola yaliyomalizika hivi  karibuni huko nchini India.
Medali ya shaba katika mahindano ya riadha  iliyoletwa na kijana Francis imerejea tena baada ya miaka 19 tangu Tanzania ilivoshinda medali hiyo mwaka 2008 katika michezo hiyo.
Timu hiyo iliyorejea nchini leo imepokelewa na Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Prof Elisante Ole Gabriel katika uwanja wa  ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere ambapo  ameeleza kufurahishwa na matokeo hayo mazuri waliyopata wanariadha hao ambao wameitangaza vyema Tanzania.
“Vijana mmefanya vizuri sana katika mashindano haya Serikali tunawapongeza sana  kwa kuitangaza nchi yetu lakini pia kwa kuonyesha uzalendo wa hali ya juu katika mashindano haya nawaahidi kuendelea kushirikiana na uongozi na wadau wa riadha nchini ili tufike mbali zaidi” Alisema Prof. Elisante Ole Gabriel.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa chama cha riadha nchini Bw. Filbert Bayi  amesema kuwa mchezo wa riadha kwa sasa ni mchezo ambao umeitangaza Tanzania kwa kiasi kikubwa kutokana na kushiriki  mashindano mengi ya Kimataifa hivyo ni vyema wadau wakajitokeza kwa wingi kuwekeza katika mchezo huo ambao umeendelea kuletea heshima Taifa.
“Riadha imeitangaza Tanzania na itaendelea kuitangaza hivyo wadau wanapaswa kuona fursa hii na kuwekeza katika mchezo huu ili ufike mbali,kila mtu katika eneo lake aone fursa hii na aitumie kwa manufaa ya kizazi hiki na kitakachokuja” Alisema Bw. Bayi.
Naye Kijana Francis Damian aliyepata medali hiyo baada kushinda mbio za mita 3000 ameeleza kufurahishwa na ushindi huo kwani alijiandaa na alizingatia maelekezo ya walimu wake yaliyompelekea kupata ushindi huo na ameshauri vijana kama yeye kuthubutu na kuamini kuwa wanaweza kwani mchezo huo ni mzuri na una mafanikio makubwa.

 Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati) akimpongeza mwanariadha Francis Damas leo katika uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere kwa kupata ushindi wa medali ya shaba baada ya kushinda mbio za mita 3000 katika mashindano ya Jumuiya ya madola chini ya miaka 17 yaliyomalizika hivi karibuni huko nchini Bahamas
 Katibu Mkuu chama cha Riadha nchini Bw. Filbert Bayi (aliyesimama) akizungumza  na wanariadha na wadau wa mchezo huo mara baada ya timu ya riadha ya vijana chini ya miaka 17 kurejea nchini na medali ya shaba katika mashindano ya Jumuiya ya Madola yaliyoalizika hivi karibuni huko Bahamas.
 Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel akipokea Bendera ya Tanzania kutoka kwa  mwanariadha  Regina Mpigachai mara baada ya kurejea nchini na ushindi wa medali ya shaba katika mashindano ya Jumuiya ya madola chini ya miaka 17 yaliyomalizika hivi karibuni huko nchini Bahamas.Wa kwanza kulia ni Mkurugenzi msaidizi wa maendeleo ya michezo wa Wizara hiyo Bw. Alex Nkenyenge.
Mkuu wa Msafara na mwalimu wa wanariadha Bibi Mwinga Mwanjala akitoa neno la shukrani  mara baada ya kurejea nchini na  ushindi wa medali ya shaba katika mashindano ya Jumuiya ya madola chini ya miaka 17 yaliyomalizika hivi karibuni huko nchini Bahamas.

Uwanja wa bilioni moja kujengwa Arusha


Arusha:  Kituo cha Michezo cha Trust St Patrick (TSTS), kimeanza ujenzi wa uwanja mkubwa wa soka unatarajia kughalimu zaidi ya sh 1bilioni hadi utakapokamilika.
Mkurugenzi wa kituo hicho Dinna Patrick alisema kuwa uwanja huo ungemalizika miaka sita iliyopita, lakini kutokana na mgogoro wa ardhi dhidi ya wananchi katika eneo ndio ulikwamisha  ujenzi wa uwanja na kituo hicho.
“Baada ya kuwaomba wananchi kuwa eneo la uwanja huu utakuwa ni faida kwa watoto wetu, wakaamua kwa pamoja niendelee na ujenzi baada ya kikao cha wanakijiji na viongozi wa serikali za mtaa kisha wakaafikiana tujenge.”
Hata hivyo, viongozi wa kituo hicho wameamua kukarabati majengo mawili ya nyumba za kuishi  walimu katika shule ya Julius Nyerere kwa  ghalama ya Sh 30milioni, ikiwa kama shukrani kwa wananchi.
 Uwanja huo ukimalizika unatarajia kuingiza  watazamaji 15,000, huku ndani yake vikijengwa viwanja vingine vya mchezo wa kikapu, wavu, riadha, soka, pete, kuogelea, Ragbi, na kriketi.

Mfuko wa Serikali za Mitaa kufufuliwa

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene 
Dar es Salaam. Serikali imejipanga upya kufufua Mfuko wa Maendeleo wa Serikali za Mitaa (LGDG)  ili kuwezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayowagusa moja kwa moja wananchi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene amesema hatua za awali za kuufufua mfuko huo zimeshaanza na wadau wa maendeleo wameonyesha utayari wa kuchangia.
Akizungumza wakati wa majadiliano na wadau wa maendeleo kuhusu ufufuaji wa mfuko huo Simbachawene amesema ni matarajio ya Serikali kuwa miradi mingi itatakelezwa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Uchumi na Biashara kwenye Ubalozi wa China nchini, Lin Zhiyong ameishauri Serikali ya Tanzania kuweka nguvu kwenye uendelezaji wa Serikali za Mitaa.
“Mazingira yakiwekwa vizuri ngazi ya nchini inakuwa rahisi hata mwekezaji kufikiria kwenda kuwekeza kijijini, hilo litawezekana endapo kwa dhati Serikali itaamua kwa dhati kutimiza azma hiyo,” alisema.
Amesema China imeweza kufanikiwa kwa kuwa hali ya uchumi katika serikali za mitaa iko vizuri na hiyo ilitokana na kuwekeza nguvu huko ambako hasa ndipo wapo watu wengi.

CUF ni kama kata, funua



Mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na Ofisi ya
Mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba (katikati) akiagana na wanachama wanaomuunga mkono baada ya mkutano wake na waandishi wa habari Dar es Salaam jana. Picha na Salim Shao 
Dar es Salaam. Hali ndani ya CUF imezidi kuwa tete baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutangaza majina ya wabunge na madiwani wapya wa viti maalumu siku moja baada ya Spika Job Ndugai kukubaliana na uamuzi wa kuwavua uanachama, uamuzi ambao Maalim Seif Sharif ameuelezea kuwa ni “aibu na fedheha kubwa sana”.
Wakati katibu huyo wa CUF akisema uamuzi huo ulifanywa kwa kupata maelekezo ya “mabosi” bila ya kufuata ushauri wa kitaalamu wa wanasheria waliokutana mjini Dodoma juzi, wabunge wanane wanawake na madiwani wawili waliotimuliwa, jana walifungua kesi mahakamani wakiitaka isitishe uamuzi wa Baraza Kuu la upande wa Profesa Ibrahim Lipumba wa kuwavua uanachama.
Kabla ya wabunge hao kufika mahakamani, Lipumba alikutana na waandishi wa habari na kuwaambia kuwa kamati ya maadili itaendelea kuwaita wabunge wanaotuhumiwa kwa utovu wa nidhamu, pamoja na Maalim Seif kwa ajili ya kuwahoji na wakikutwa na makosa wataadhibiwa.
Siku ya jana ilianza kwa Profesa Lipumba, ambaye alijivua uenyekiti na nyadhifa nyingine zote mwaka 2015 kabla ya kufuta uamuzi huo mwaka mmoja baadaye, kufanya mkutano na waandishi wa habari katika ofisi za makao makuu ya CUF zilizopo Buguruni jijini Dar es Salaam.
Profesa Lipumba alielezea hatua walizochukua na wanazotarajia kuchukua dhidi ya wanachama wao, akisema hata katibu huyo mkuu ataitwa na kamati hiyo kuhojiwa.
Baadaye, ilifuata taarifa ya NEC iliyotaja majina ya wanachama wa CUF watakaoshika nafasi zilioachwa na wabunge waliotimuliwa uanachama.
Taarifa iliyofuata ilikuwa ya Maalim Seif aliyesema kitendo cha kuwafukuza uanachama wabunge halali wa CUF, kingekuwa sahihi kama kingefuata taratibu zote za kisheria na kikanuni za Bunge kujiridhisha kwanza.
Taarifa hiyo ilijaa tuhuma dhidi ya Idara ya Usalama wa Taifa, wakuu wa wilaya, Msajili wa Vyama vya Siasa, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, NEC, Jeshi la Polisi na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita), akisema taasisi hizo zinashiriki kutaka kuiua CUF.
“Polisi ndiyo waliomuingiza kwa nguvu na kumlinda (neno tumeliondoa) Ibrahim Lipumba katika Mkutano Mkuu Maalum wa Taifa wa CUF uliokuwa ukifanyika katika Ukumbi wa Blue Pearl, Ubungo Plaza siku ya tarehe 21 Agosti, 2016 kwa lengo la kuuvuruga,” inasema taarifa ya Maalim Seif.
“Polisi pia wakamuongoza na kumlinda Lipumba na genge lake kwenda kuvamia na kuvunja Ofisi Kuu ya chama iliyopo Buguruni, Dar es Salaam, siku ya tarehe 23 Septemba, 2016.”
Kuhusu tuhuma dhidi ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Maalim Seif anasema “Ilijitwisha uwezo na madaraka (ambao Mahakama Kuu ya Tanzania ilishawahi kutamka kwamba haina) ya kutengua uamuzi wa vikao halali vya chama ambavyo ni pamoja na Mkutano Mkuu wa Taifa uliokubali barua ya Ibrahim Lipumba kujiuzulu Uenyekiti wa Chama; na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa ambalo lilimfukuza uanachama Ibrahim Lipumba na kuwasimamisha uanachama waliokuwa viongozi wengine kadhaa wa chama”.
Pia, ameituhumu Rita kuwa imekubali kuvunja Sheria ya Wadhamini huku ikijua na ikiwa na taarifa zote ilizopewa na CUF kwa barua ya Juni 17, kwa kusajili wajumbe wasio sahihi wa Bodi ya Wadhamini.
Alisema Rita imefanya hivyo, “Ili waweze kutumika kufuta kesi ambazo chama kimezifungua Mahakama Kuu kupinga hujuma hizi zinazoendelea na pia kuweza kufanikisha kuchota fedha za ruzuku ya chama zilizobakia ambazo zimezuiwa kutolewa kupitia zuio la Mahakama Kuu”.
Kuhusu Ofisi ya Spika, Maalim Seif amesema kitendo cha Spika Ndugai kukubali haraka kufukuzwa uanachama kwa wabunge wanane wa chama hicho, “Ni msimamo kutoka juu kwamba wabunge wa CUF wafukuzwe”.
Anasema katika taarifa hiyo kwamba suala hilo limefanyika mara nyingi tangu mfumo wa vyama vingi vya siasa uliporejeshwa nchini mwaka 1992. Hata hivyo, anahoji kwa nini mara hii Spika ameridhia haraka uamuzi huo ikiwa haijazidi hata siku moja na hata bila ya kuwasiliana na katibu mkuu wa CUF ambaye kwa mujibu wa Katiba ya CUF, ndiye mtendaji mkuu wa chama.
“Lakini kama hiyo haitoshi, nilimuandikia rasmi barua Spika Ndugai, Julai 25, 2017 nikimueleza kwamba hilo lililoitwa Baraza Kuu la Uongozi la CUF halikuundwa na wajumbe halali wa Baraza Kuu,” anasema Maalim Seif.
“Angekuwa na nia ya kweli ya kutaka kujiridhisha, hapo ndipo pangekuwa pa kuanzia kwa kuwepo kile wanasheria wanachokiita shaka inayoweza kuingia akilini yaani ‘reasonable doubt’.”
Maalim Seif anadai Spika Ndugai amepuuza yote hayo kwa sababu ni kinyume na mkakati wa dola kuihujumu CUF na kuua upinzani nchini.
“Kwa kifupi, yanayofanyika ni mchezo wa kuigiza tu, lakini maamuzi yameshafanywa na Dola na waliobaki wanatekeleza tu,” anasema Maalim Seif.
Anadai kuwa Julai 26 kulikuwa na kikao cha wanasheria wapatao 12 wa Serikali kutoka Bunge, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, NEC na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ambao walitakiwa kumshauri Spika kwa kumuandikia maoni ya kisheria kuhusu suala la wabunge wa CUF.
Anasema wanasheria hao walishauri kuwa Bunge lisiingilie mgogoro wa chama ambao tayari uko Mahakamani kwa kukubali uamuzi wa upande mmoja kuwafukuza wabunge wakisema kitendo hicho kitashusha hadhi ya Bunge, kuifedhehesha NEC na kuitia aibu Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ambayo ina jukumu la kuishauri Serikali.
“Walipoambiwa waeleze maelekezo ya mabosi wao, wote walieleza kuwa wametakiwa kufuata msimamo wa kutoka juu kwamba wabunge wa CUF wafukuzwe, isipokuwa wanasheria wa Bunge tu ndiyo ambao hawakuwa na maelekezo hayo,” amedai Maalim Seif.
“Baada ya hatua ya jana ya Spika Ndugai, na kwa utaratibu huohuo wa mwendokasi, tayari Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeshapewa maelekezo na leo au kesho watatekeleza maelekezo hayo kwa kutangaza majina ya watakaowaita ‘wabunge wapya’ wa kujaza nafasi hizo. Bila shaka ilivyokuwa Dola imeshaamua hivyo, basi taasisi zote hizo zitaendelea kutekeleza mpango huo.”
Hata hivyo, Maalim Seif amewataka wanachama na wafuasi wa chama hicho kuendelea kuwa watulivu na kusubiri uamuzi wa Baraza Kuu ambalo linakutana leo mjini Zanzibar.
“CUF imepita katika dhoruba na misukosuko mingi katika historia yake tokea ilipoasisiwa mwaka 1992. Tulishinda dhoruba na misukosuko hiyo na tutaushinda huu uliopo na hatimaye kuibuka tukiwa imara zaidi,” anasema Maalim Seif.
Kaimu Katibu wa Bunge, Nenelwa Mwihambi alisema hawezi kuzungumzia suala hilo bila ridhaa ya Spika, huku kaimu katibu wa Spika, Athuman Kwikwima akisema Ndugai na Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashilila wapo nje ya nchi kikazi.
Lipumba kuita wabunge wengine
Mapema jana, Profesa Lipumba, ambaye anatambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, aliwaambia waandishi wa habari kuwa kamati ya nidhamu na maadili ya chama hicho, ipo katika mchakato kuwaita wabunge na viongozi akiwamo Maalim Seif kwa ajili ya mahojiano dhidi ya tuhuma za kuihujumu CUF.
Alisema awamu ya kwanza imekamilika ya kuwaita wabunge 10 na madiwani wawili wa viti maalumu kwa ajili ya mahojiano ambao hata hivyo, hawakutokea na Baraza Kuu la Uongozi Taifa kuazimia kuwafukuza uanachama wabunge wanane kati ya hao.
Mbali na hilo, mchumi huyo alisema nafasi za wabunge hao wanane zitajazwa wakati wowote baada ya Spika Ndugai kuridhia maombi yao na kwamba hawajapeleka majina mapya NEC, bali yatatumika yaliyo katika orodha iliyopelekwa mwaka 2015.
“Ngwe ya pili inakuja, kamati ya maadili ilianza kwa wabunge 10 na madiwani iliowafanyia uchunguzi na ulipokamilika Baraza Kuu la Taifa la Uongozi likafanya uamuzi. Sasa kamati hii inaendelea na awamu ya pili,” alisema.
“Kati ya watu watakaoitwa ni Maalim Seif, Naibu Katibu Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, wabunge na wanachama wengine wenye makaosa kama haya.”
Alisisitiza kuwa Maalim Seif lazima ataitwa katika kamati hiyo kwa madai ya kwamba ni miongoni mwa watu waliowaponza wabunge hao wanane.
“Wabunge wengine nawaambia msiwe mnafuata kila anachokisema huyu bwana (Maalim Seif). Si kila anachosema, unakifuata kwa sababu unaogopa, atawaponza kama alivyowaponza wajumbe wa Baraza la Wawakilishi aliyewazuia wasiende mahakamani kudai haki yao,” alisema.
Kuhusu majina kupelekwa NEC, Profesa Lipumba alisema mchakato wa kutafuta majina mapya utachukua muda mrefu hivyo wamekubaliana kwamba wabunge hao wapya watateuliwa kulingana na orodha iliyowasilishwa na chama hicho mwaka juzi.
“Jamani majina yaliyopelekwa ni mengi atakayekosa naomba asikate tamaa asubiri wakati mwingine,” alisema Profesa.
Pamoja na hayo, Profesa Lipumba alidai kuwa kikao kitakachofanyika Zanzibar ni batili kwa kuwa hajapewa taarifa.
Akizungumzia uteuzi huo, mkurugenzi wa uchaguzi wa upande wa Maalim Seif, Shaweji Mketo alisema majina hayo ni sahihi yaliyopelekwa mwaka juzi, lakini utaratibu haukufuatwa.
“Kulingana na utaratibu, nilitegemea Kuruthumu Mchuchuri angeteuliwa katika mchakato huu kwa kuwa jina lake lilikuwa namba 11, lakini wameamua kudonoa donoa na kuwachagua wajumbe wanaowataka wao,” alisema Mketo.
Mketo alidai mchakato huo umefanyika kwa upendeleo wa watu wanaoumuunga mkono Profesa Lipumba na undugu huku akitolea mfano wa jina la Shamsia Aziz Mtamba, akisema ni ndugu na mbunge wa Mtwara Mjini, Maftah Nachuma.
Watinga mahakamani
Sakata hilo liliendelea alasiri wakati wabunge wanane waliosimamishwa na upande wa Lipumba walipofungua kesi Mahakama Kuu kuomba ibatilishe uamuzi huo.
Wakiwakilishwa na wakili Peter Kibatala, wamefungua maombi hayo kwa hati ya dharura wakitaka Mahakama Kuu isimamishe utekelezaji wa uamuzi uliowavua uanachama kwa muda kusubiri uamuzi wa kesi yao ya msingi.
Katika kesi hiyo namba 143/2017, wadaiwa ni Bodi ya Wadhamini wa CUF, mwenyekiti na kaimu katibu mkuu wa chama hicho.
Wadai wanaiomba mahakama itamke kuwa uamuzi wa kuwavua uanachama na hivyo kupoteza nafasi zao, kuwa ni batili kwa kuwa haujazingatia kanuni za haki za msingi.
Pia, wanaiomba mahakama itamke kuwa mchakato wa kuwashughulikia kinidhamu uliohitimishwa kwa kuwavua uanachama, ni batili kwa kuwa unakiuka kanuni na kisheria.
Wanadai hawakupewa fursa ya kutosha kujitetea kwa kuwa taarifa kamili haikutolewa kwao kuhusu tuhuma dhidi yao na wameadhibiwa licha ya kuwa walishakata rufaa Mkutano Mkuu. Adhabu waliyopewa wanadai ni kubwa mno kulinganisha na makosa wanayotuhumiwa na kwamba, uamuzi umechukuliwa bila kuzingatia hasara si tu watakayoipata wao, bali kwa chama na uchumi wa nchi katika mchakato wa kujaza nafasi hizo.
Waliotimuliwa walonga
Wabunge waliovuliwa uanachama waliilaumu Serikali kwa uamuzi huo.
Akizungumzia kufukuzwa kwao, mmoja wa wabunge hao, Riziki Shahali Mngwali alisema kinachoendelea ni mchezo unaofanywa na dola na siyo uamuzi wa Spika Ndugai peke yake au Profesa Lipumba.
Alisema ni wazi kwamba Serikali imekuwa ikimtumia Profesa Lipumba kukigawa chama hicho ili kukipunguza nguvu. Alisema baadhi ya matukio ambayo yanadhihirisha Profesa Lipumba kuungwa mkono na Serikali kuwa ni kuvamia Mkutano Mkuu wa mwaka 2016 akiwa na askari wa Jeshi la Polisi.
“Sisi hatuna nguvu za kupambana nao. Mimi binafsi, I am very disappointed (nimevunjika sana moyo). Sikutarajia kama tunaweza kuwa na dola ya namna hii,” alisema Mngwali na kusisitiza kwamba wataendelea kupigania haki hata wakiwa nje ya Bunge.
Nyongeza na James Magai