Friday, July 28

Muuguzi aingia matatani kwa rushwa

MKUU wa Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya, Rehema Madusa, amemsimamisha kazi mtumishi wa Hospitali ya Wilaya kwa tuhuma za kudai na kupokea rushwa ya Sh. 15,000 kutoka kwa mzazi ili amtibu mtoto wake.

Madusa alisema juzi kuwa alipata taarifa ya mtumishi huyo (jina linahifadhiwa) kwa sababu za kiuchunguzi kuwa alidai Sh. 30,000 lakini mzazi huyo alikuwa hana kiasi hicho hivyo akampatia nusu na akaahidi kumalizia zingine baada ya matibabu.

Alisema alifika katika hospitali hiyo kwa ajili ya kujiridhisha na kwamba baada ya mazungumzo na mzazi huyo na kuelezwa hali halisi ilivyo, alimwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Sophia Kumbuli, amsimamishe.

Aidha, alisema aliiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kumkamata mtumishi huyo na kuchunguza tuhuma zinazomkabili.

“Baada ya kupata taarifa za tukio hilo nilifika hospitalini hapo kwa ajili ya mahojiano na mzazi huyo aliyeombwa rushwa na baada ya kumhoji niliagiza Mkurugenzi amsimamishe na Takukuru wamkamate mpaka sasa Takukuru wanaendelea na kazi,” alisema Madusa.

Kambuli ambaye ni mwajiri wa muuguzi huyo, alikiri kuwapo kwa tukio hilo huku akisema nesi huyo hakuwa mtumishi wa halmashauri hiyo bali alikuwa anajitolea.

Pia alisema licha ya kutokuwa mwajiriwa wa halmashauri, kwa tuhuma hizo alilazimika kumsimamisha kazi kama alivyoagizwa na Mkuu wa Wilaya, lakini hana mamlaka ya kuchukua hatua zaidi.

Alisema kwa sasa vyombo vyenye mamlaka vinaendelea na kazi ya kuchunguza tuhuma za nesi huyo na kwamba endapo itabainika kuwa ni kweli, hatua zaidi zitachukuliwa.

Aliwataka watumishi wa halmashauri hiyo kuepuka vitendo kama hivyo kwa madai kuwa vinachafua utendaji kazi wa halmashauri na vinasababisha wananchi kukosa imani na hospitali za umma.

No comments:

Post a Comment