Friday, July 28

Fifa Yatua Bongo



MENEJA Miradi ya Maendeleo wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kwa Afrika, Mzimbabwe Solomon Mudege amewasili nchini jana usiku kwa ajili ya kufuatilia kinachoendela kwenye Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Bin Zubeiry Sports – Online inafahamu Mudege tayari yupo nchini na pamoja na kukutana na Kamati ya Utendaji ya TFF kesho Dar es Salaam, pia atakuwa na kikao na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrisons Mwakyembe.
Bado haijafahamika Ofisa huyo amekuja kwa sababu zipi haswa na kama ameitwa na viongozi wa TFF au amekuja kwa maagizo ya FIFA tu.



Lakini inafahamika hamkani si shwari kwa sasa katika soka ya Tanzania, kufuatia viongozi wakuu wawili wa TFF, Rais Jamal Malinzi na Katibu wake, Selestine Mwesigwa kuwekwa rumande tangu Juni 29 kwa tuhuma za ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka.
Malinzi, Mwesigwa pamoja na Mhasibu wa TFF, Nsiande Isawafo Mwanga walipelekwa rumande Juni 29 baada ya kusomewa mashitaka 28 ya kughushi na kutakatisha fedha kupitia akaunti ya TFF iliyopo katika banki ya Stanbic, Dar es Salaam.
Katika mashitaka hayo, 25 yanakwenda moja kwa moja kwa Rais wa shirikisho hilo, Malinzi akidaiwa kughushi michakato mbalimbali ya kifedha, huku matatu yakiwahusu wote na Katibu wake na Mhasibu wake Nsiande Isawafo Mwanga.
Malinzi aliingia madarakani TFF Oktoba mwaka 2013 baada ya kupata kura 72 kati ya 126 zilizopigwa akimshinda aliyekuwa mpinzani wake wa karibu, Athumani Nyamlani.
Lakini baada ya kesi hii kuanza kuunguruma na kuwekwa rumande, Kamati ya Utendaji ya TFF ilikutana na kumteua Makamu wake, Wallace Karia kukaimu Urais wa shirikisho hilo.
Lakini kwa mwenendo wa kesi, Malinzi ndiyo kama amekwishaaga TFF, kwani uchaguzi unatarajiwa kufanyika Agosti 12 mjini Dodoma naye hajashiriki usaili wa wagombea, hivyo haruhusiwi tena kugombea. 
Karia naye yupo hatarini kuenguliwa katika uchaguzi baada ya kuitwa Idara ya Uhamiaji ya Taifa kuthibitisha uraia wake, akidaiwa kuwa ni raia wa Somalia. Mwenyewe amekiri kuwa na asili ya Somalia, lakini amekataa kuwa si Mtanzania. Uhamiaji inaendelea na uchunguzi dhidi yake.

No comments:

Post a Comment