Saturday, August 31

Serikali yasalimu amri kwa wabunge


Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ali Mohamed Keissy
akichangia bungeni mjadala wa kupitisha muswada wa
sheria ya taifa ya umwagiliaji wa mwaka 2013,
ambapo alikuwa akipinga wawekezaji wa kilimo kwenda kuwekeza mkoani Rukwa, 

Dodoma. Muswada wa Sheria ya Taifa ya Umwagiliaji wa mwaka 2013, jana ulipita kwa mbinde bungeni mjini Dodoma, huku Serikali ikisalimu amri kwa wabunge na kukubali kurekebisha baadhi ya vifungu vyake.

Bila kujali tofauti zao za kisiasa, wabunge jana walisimama kidete na kuonyesha uzalendo wa hali ya juu, wakitaka sheria hiyo imlinde mzawa badala ya mwekezaji.

Moto huo wa wabunge uliwalazimisha Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chizza na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Fredrick Werema kusalimu amri na kukubali mapendekezo ya wabunge.

Msimamo wa wabunge hao katika kuibana Serikali, pia ulililazimisha Bunge kutengua kanuni zake na kuendelea na shughuli za kupitia muswada huo hadi saa 7:35 mchana, badala ya kusitishwa saa 7:00 kwa ratiba ya kawaida.

Serikali ilikubali mapendekezo ya wabunge hao na kurekebisha vifungu ambavyo sasa vinampa mmiliki wa ardhi itakayotangazwa eneo la umwagiliaji kuwa mwanahisa na kulipwa fidia.

Awali, wabunge waliowasha moto huo ni pamoja na Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina na Suleiman Jaffo wa Kisarawe, wote kutoka Chama Cha Mapinduzi(CCM), ambapo walisema baadhi ya vifungu vya muswada huo wa sheria vilikuwa na ajenda ya siri.

Wakichangia mjadala huo wabunge hao walitaka vifungu vinavyotamka kuwa eneo litakalotangazwa kuwa la umwagiliaji litatwaliwa na Tume itakayoundwa na kupewa fidia viboreshwe, ama kama haifai, vifutwe.

Mpina alishikilia msimamo kuwa badala ya kumlipa fidia mwananchi, vifungu hivyo vitamke kuwa atalipwa fidia ama kuwa mwanahisa wa mradi ama alipwe fidia na papo hapo kuwa mwanahisa.

Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema), aliitaka Serikali itunge sheria zinazolinda wazawa na kwamba hatua ya kuacha mianya, ndiyo mwanzo wa wawekezaji kuwanyang’anya ardhi wazalendo.

Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka (CCM), alisema kuwa haihitaji kuipitia sheria yote ili kubaini maudhui yenye dhamira ovu dhidi ya Watanzania ndani yake akisisitiza kuwa baadhi ya vifungu vina ajenda ya siri.

“Vifungu hivi vina ajenda ya siri ya kuwapeleka Watanzania kwenye utumwa…Kama msipobadilisha vifungu hivi, mwondoe huu muswada maana hii ni dhambi ya mauti,” alisisitiza Ole Sendeka.

Ole Sendeka alisisitiza sheria itamke kuwa kama ni kutwaa ardhi yoyote, hata kama ni Rais anataka kufanya hivyo ni lazima hilo lifanyike kwa ushirikiano na mmiliki wake, ama na wanakijiji wote kupitia mkutano mkuu.

Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Bulaya (CCM), alisema Watanzania wameshindwa kunufaika na rasilimali nyingine na waliyobakia nayo ni ardhi hivyo hawako tayari kurudisha ukoloni mamboleo.

Mbunge wa Peramiho, Jenister Mhagama (CCM), alisema ni lazima sheria hiyo iweke sharti la lazima kwa mwekezaji kuingia ubia na mmiliki wa ardhi na kama hataafiki, ndipo apewe fidia.

IGP aibiwa upanga wa dhahabu - mwananchi newspaper




Jeshi la Polisi limeingia katika kashfa nzito baada ya mkuu wake, Inspekta Jenerali Said Mwema, kuibiwa upanga wa dhahabu ambao ni mali ya Shirikisho la Wakuu wa Majeshi ya Polisi wa nchi za Kusini mwa Afrika (SARPCCO).

Upanga huo wenye uzito wa takriban kilo tatu na wenye thamani ya zaidi ya fedha za Tanzania Sh600 milioni, ni kielelezo kwa nchi inayokabidhiwa uongozi wa SARPCCO.

Mwaka jana Tanzania ilikuwa mwenyekiti wa SARPCCO, ambapo upanga huo ulikabidhiwa kwa IGP Mwema na Jenerali Magwashi Victoria ‘Riah’ Phiyega, ambaye ni Kamishna wa Taifa wa Polisi wa Afrika Kusini aliyekuwa amemaliza muda wake kwa wakati huo.

Hilo ni tukio la pili la wizi la mali zinazohusu ofisi ya IGP, ambapo mwaka jana ndani ya ofisi hiyo kuliibwa kompyuta ndogo (laptop), ikiwa na taarifa muhimu za kipolisi. Hadi sasa hakuna taarifa za kupatikana kwa kompyuta hiyo.

IGP Mwema alikabidhiwa upanga huo Septemba 5, 2012, katika mkutano saba wa SARPCCO uliofanyika Zanzibar na kuhudhuriwa na wakuu wa majeshi ya Polisi kutoka nchi 13, pamoja na mashirika ya kimataifa.

Upanga huo ambao unakwenda sambamba na bendera ya SARPCCO, ni moja ya vielelezo vya nchi iliyochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa shirikisho hilo, ambaye moja kwa moja anakuwa ni Mkuu wa Jeshi la Polisi katika nchi husika.

Kwa mujibu wa taratibu za SARPCCO, vielelezo hivyo hutakiwa kuwekwa ofisini kwa kiongozi husika, ikiwa ni alama ya kila mgeni atakayeingia ofisini hapo kutambua uwepo wa wadhifa huo wa kimataifa.

Uchunguzi wa gazeti hili ulibaini kuwa IGP aligundua kutoweka kwa upanga huo wiki iliyopita, wakati akijiandaa kwenda kuukabidhi kwa mwenyekiti mpya wa SARPCCO, ambaye ni IGP wa Namibia.

Taarifa za ndani ya jeshi hilo zilibaini kuwa, IGP alilazimika kuondoka bila upanga huo alipokwenda Namibia wiki iliyopita kuhudhuria mkutano wa nane wa SARPCCO, uliofanyika Jumapili iliyopita mjini Windhoek.

Kwa mujibu wa uchunguzi, IGP Mwema alikabidhi upanga unaofanana na huo ambao siyo wa dhahabu, alioazimwa kutoka kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi la Namibia, Inspekta Jenerali, Luteni Jenerali Sebastian Ndeitunga, na kukabidhiwa kama ishara ya kukabidhiwa uenyekiti wa SARPCCO kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Uchunguzi ulibaini kuwa IGP Mwema alitoa ahadi ya kurejesha upanga halisi ndani ya kipindi cha mwezi mmoja, au Serikali ya Tanzania italazimika kutengeneza mwingine kulipa uliopotea.

Uchunguzi wa gazeti hili unaonyesha kuwa kashfa hiyo ametupiwa Mkuu wa Polisi Zanzibar, Kamishna Mussa Ali Mussa pamoja na dereva wake, ikidaiwa kuwa upanga huo baada ya kupokewa na IGP Mwema, Septemba mwaka jana uliwekwa kwenye gari la kamishna huyo.

Kamishna Mussa ndiye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mkutano wa Saba, na pia ofisa mwenyeji kwa wajumbe wa mkutano huo uliofanyika Zanzibar.

Hata hivyo, taarifa zingine zilidai kuwa IGP Mwema naye analaumiwa kwa kutofuatilia kwa karibu zana za kazi, kwani baada ya kuupokea alitakiwa kuhakikisha unakuwepo ofisini kwake kama alama ya uenyekiti wake.

Gazeti hili lilipowasiliana kwa njia ya simu na Mkuu wa Polisi Zanzibar, Kamishna Mussa Ali Mussa kuhusu madai hayo alisema, kitara (upanga) hicho ni kweli kimepotea, lakini yeye hahusiki kwa kuwa kila kitu kina utaratibu wake.

“Ni kweli kitara kilikabidhiwa kwa afande IGP na mimi nilishuhudia kikikabidhiwa, na ni kweli kitara hakijulikani kiliko, lakini mimi sihusiki na kupotea kwake. Ni kweli mimi nilikuwa ofisa mwenyeji wa mkutano huo, lakini siku hiyo zilitolewa zawadi nyingi, watu walipewa mikoba, kwa hiyo mtu akipoteza mkoba wake niulizwe mimi?” alihoji Kamishna Mussa.

Alisema kila kitu kina utaratibu wake na kwamba taarifa kwamba yeye amehojiwa kutokana na upotevu wa kitara hicho au kuna kamati imeundwa, hazina ukweli.

“Sijawahi kuona kamati hiyo. Kamati hiyo kwanza imeundwa na nani na inatoka wapi? Hayo maneno yanatengenezwa na watu wa nje,” alisema Kamishna Mussa.

Alisema kinachofanyika hivi sasa ni kukitafuta ili kiweze kurejeshwa kunakohusika.

Taarifa zingine zilidai hata bendera ya mezani ya mwenyekiti wa SARPCCO, aliyokabidhiwa sambamba na upanga huo nayo kuna hatihati ilipotea.

Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Senso alipotakiwa kuzungumzia suala hilo alisema aulizwe kamishina wa polisi Zanzibar.

“Suala hilo muulize Kamishina wa Zanzibar ndiye anayejua,” alisema Senso.

Uchunguzi unaonyesha kuwa maofisa katika ofisi ya IGP na ile ya Kamishna wa Polisi Zanzibar, wamehojiwa akiwamo Kamishna Mussa, na kwamba upelelezi mkubwa umekuwa ukiendelea ndani ya jeshi hilo.

Hata hivyo, juhudi za gazeti hili za kutaka kufahamu uamuzi wa SARPCCO katika ofisi yake ya uratibu iliyopo kwenye ofisi za Makao Makuu ya Kanda ya Polisi wa Kimataifa (INTERPOL), Harare, Zimbabwe, hazikuzaa matunda baada ya baruapepe iliyotumwa kwa ofisa mratibu wa SARPCCO ambaye pia ni mkuu wa ofisi ya Kanda ya INTERPOL, C. Simfukwe kutopata majibu.

SARPCCO ilianzishwa mwaka 1995, Victoria Falls, Zimbabwe, lakini kisheria ilitambulika rasmi mwaka 2006 na lengo lake kuu ni kupambana na uhalifu wa kuvuka mipaka.

Uenyekiti wake ni mwaka mmoja, ambapo kwa sasa mwenyekiti ni Mkuu wa Jeshi la Polisi la Namibia Inspekta Jenerali, Luteni Jenerali Sebastian Ndeitunga, aliyepokea wadhifa huo kutoka kwa IGP Mwema.