Monday, April 6

ACT: Tunajipanga kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Agosti


Dar es Salaam. Chama cha ACT- Tanzania, kimesema hakina muda wa kufanya siasa za chuki na malumbamo dhidi ya vyama vingine vya siasa, badala yake kinajipanga vizuri na kuandaa mazingira ya kushiriki katika uchaguzi mkuu ujao.
Mwenyekiti wa chama hicho Anna Mghwira, aliliambia gazeti hili mwishoni mwa juma kuwa, baada ya chama hicho kuzinduliwa rasmi Machi 29 mwaka huu,  nguvu yake sasa imeelekezwa katika kujijenga na kujiimarisha.
Alisema katika kujiimarisha, chama hicho kinatafuta wanachama, kwa kuwa kinatambua kuwa ni mtaji wa kujihakikishia ushindi katika uchaguzi mkuu, pamoja na kuandaa wagombea  kwa kuangalia uwezo wao kadri watakavyojitokeza.
“Mimi mwenyewe ni miongoni mwa wagombea ubunge, nitagombea Jimbo la Singida mjini na naamini kwamba nitaweza kupata nafasi hiyo kwa sababu ninafahamika kule ni nyumbani nilikozaliwa . Nimesoma huko, nimekulia huko na najua changamoto zinazotukabili wakazi wa kwetu na jinsi nitakavyoshiriki kukabiliana nazo nikiwa mbunge,”
Mghwira alieleza kuwa chama hicho kinajiimarisha, huku kikitambua kuwa kina wajibu wa kuendeleza ushirikiano na vyama vingine vya siasa, badala ya kujitenga na kuendesha shughuli zake kama kisiwa.
Mwenyekiti huyo, alitolea mfano siku ya uzunduzi wa chama hicho akisema kuwa kulikuwa na watu wengi kutoka vyama mbalimbali ambao walitaka kurudisha kadi za vyama hivyo hadharani na kuchukua kadi za ACT, lakini walisitisha shughuli hiyo kuepuka uhasama.
“Kuwa vyama tofauti haina maana kwamba tuwe maadui, kulikuwa na wanachama wapya siku ya uzinduzi (wa ACT) walitaka kuonyesha hadharani wanavyorudisha kadi za vyama vyao vya awali hatukuwapa nafasi hiyo, kwa sababu hatuoni kuwa hilo ni jambo la kuvutia kwetu,” alisema.
Kwa mujibu wa Mghwira siku hiyo walipokea wanachma wapya 2,000 na bado wanaendelea kupokea wanachama wengine kutoka vyama mbalimbali vya siasa lakini kwa siri.
Ingawa  Mghwira hakutaja watu, asilimia kubwa ya viongozi wa kitaifa wa chama hicho, akiwamo Zitto Kabwe ambaye sasa ni Kiongozi Mkuu wa chama hicho na Katibu Mkuu  Samson Mwigamba  na Profesa Kitila Mkumbo, wamejiunga na chama hicho baada ya kufukuzwa na vyama vyao.
“Pia katika kuonyesha nia yetu ya kuhitaji ushirikiano mwema wa kisiasa tuliwaalika viongozi mbalimbali wa vyama vya upinzani, ikiwemo Chadema na CUF,” alisema.  Alisisitiza kuwa Profesa Ibrahimu Lipumba ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) ni miongoni mwa wasomi  na viongozi wa vyama vingine vya siasa walioalikwa kutoa mada katika uzinduzi wa chama hicho, lakini alipata udhuru hivyo hakufika.
“Hata hivyo tulifarijika kuona shughuli yetu ya uzinduzi wa chama ikifanyika vizuri na kwa amani,” alisema.

Ukawa yadai mambo manne kabla ya Uchaguzi


Dar es Salaam. Uamuzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuahirisha Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa umewafungulia viongozi wa Ukawa kuishinikiza Serikali kuiboresha Katiba ya sasa katika maeneo manne ili kuondoa mvutano katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Mambo manne yanayodaiwa na Ukawa ambayo ni ushindi wa urais kuamuliwa kwa asilimia zaidi ya 50, mgombea binafsi katika nafasi za udiwani, ubunge na urais, tume huru ya uchaguzi na urais kupingwa mahakamani ni yale yaliyoafikiwa baina ya Rais Jakaya Kikwete na vyama vya siasa Septemba 8, mwaka jana.
Mwenyekiti mwenza wa umoja huo, James Mbatia amesema maboresho yaliyofanyika chini ya Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) ni ya lazima ili kufanikisha uchaguzi huo kabla ya kupitishwa kwa Katiba Mpya na kuondoa uwezekano wa vurugu.
Katika kikao hicho, Mbatia alisema walitiliana saini kuwa iwapo uchaguzi wa mwaka huu utafanyika kwa kutumia Katiba ya 1977, Bunge lingekutana Novemba mwaka jana kufanya marekebisho hayo ya 15 ya Katiba na endapo hilo lingeshindikana, basi lingekutana Februari, jambo ambalo pia halikufanyika.
Utekelezaji wa masuala hayo utawezekana iwapo Serikali itawasilisha marekebisho hayo bungeni ili yajadiliwe kwa dharura katika mkutano ujao wa Bajeti wa mwisho wa Bunge la Kumi, kwa kuwa uwezekano wa kupata Katiba Mpya kabla ya uchaguzi ni kama haupo.
Alipoulizwa iwapo jambo hilo linawezekana katika Mkutano wa Bajeti, Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel alisema: “Ndiyo inawezekana. Serikali inaweza kuwasilisha jambo hili kwa dharura na litajadiliwa na Kamati ya Uongozi, kama ikiona linafaa litapelekwa bungeni kujadiliwa.”
Katika hilo Mbatia alisema: “Bado kuna nafasi ya Bunge kufanya marekebisho. Hili linatakiwa kufanyika kama ambavyo tulikubaliana na Rais kupitia TCD.”
Alisema ushauri wa TCD kwamba mchakato wa Kura ya Maoni uahirishwe hadi mwakani umepuuzwa na matokeo yake yameonekana wazi na kwa msingi huo, suala la kurekebisha maeneo hayo manne, si la kupuuza hata kidogo.
“Hili lisipofanyika utaibuka mgogoro mkubwa. Tatizo la Serikali yetu ni kutotaka kutekeleza mambo yanayoonekana wazi kuwa na mkanganyiko, ndiyo sababu ya kukithiri kwa migogoro ya wakulima, wafugaji, wafanyakazi na mingine mingi,” alisema Mbatia.
Dk Slaa akata tamaa
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema endapo Serikali itashindwa kutekeleza makubaliano hayo, vyama vya upinzani havina budi kuingia katika mapambano kwa katiba hiyohiyo.
“Kama hatumwelewi Rais Kikwete katika suala hili, basi hatuwezi kumwelewa tena. Sioni juhudi zozote za Serikali kubadili maeneo haya. Tulikubaliana naye mambo mengi lakini yote ameshindwa kuyatekeleza, hata hili pia hawezi kulitekeleza,” alisema Dk Slaa.
Katibu mkuu huyo wa Chadema alisema umefika wakati wa vyama vya upinzani kupambana hivyohivyo licha ya kuwapo tume ya uchaguzi isiyo huru.
“Nimeshinda ubunge Karatu vipindi vitatu na tume ikiwa ni hiihii. Wapinzani tuna wabunge zaidi ya 100, nadhani tupambane tu,” alisema.
Alisema umefikia wakati wa kuing’oa CCM kwa kutumia Katiba mbovu (iliyopo sasa) na kinachotakiwa kufanywa na vyama vya upinzani ni kujipanga kuanzia vijijini hadi mijini ili kuzoa kura zote.
“Tumeshinda Kawe, Ubungo, Mbeya Mjini na hata Nyamagana. Tuache kulialia sasa, twende katika mapambano. Kwanza Bunge lijalo ni la Bajeti na kwa vyovyote vile mabadiliko tunayoyataka hayawezi kufanyika,” alisema.
Kiongozi Mkuu wa chama cha ACT-Tanzania, Zitto Kabwe alisema kinachotakiwa kufanywa sasa ni Baraza la Vyama vya Siasa kuitisha mkutano wa vyama vyote ili kukubaliana mambo ya kuboresha katika Katiba ya sasa.
“Jambo la pili ni Rais kuitisha Bunge kabla ya kuanza kwa Bunge la Bajeti kujadili mabadiliko hayo na kuyapitisha ili kuufanya uchaguzi mkuu uwe wa haki na huru,” alisema Zitto.
Juhudi za kumpata Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Asha-Rose Migiro kuzungumzia hatua ambazo Serikali inachukua hazikuzaa matunda baada ya simu zao kuita mara kadhaa bila kupokewa.

Askofu Gwajima: Siwezi kuwatupa Dk Slaa, Lowassa

KWA UFUPI
  • Asema huu si wakati wa kuchaguliwa marafiki
  • Awahimiza wafuasi wake kumsindikiza polisi Alhamisi, Kova atoa onyo

Dar es Salaam. Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima jana alihubiri akiwa katika kiti cha magurudumu na kusema hawezi kuwatupa Mbunge wa Monduli (CCM), Edward Lowassa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa kwa kuwa ni marafiki zake wa siku nyingi.
Pia askofu huyo, amewataka waumini wote wa kanisa hilo kufika katika Kituo Kikuu cha Polisi, Alhamisi ijayo siku ambayo atakwenda kukamilisha mahojiano dhidi ya tuhuma za kumtukana Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Polycarp Kardinali Pengo.
Akihubiri mamia ya waumini waliofika kanisani hapo kwa ajili ya ibada ya Pasaka jana, Gwajima alisema kumekuwa uvumi kwamba kuhojiwa kwake na polisi kulitokana na kuwakaribisha wanasiasa hao kanisani kwake kwa nyakati tofauti na kuzungumza na waumini wake.
Alisema alifahamiana na Lowassa tangu mwaka 1996 wakati huo mbunge huyo akiwa Waziri wa Ardhi na tangu kipindi hicho amekuwa mtu wake wa karibu.
Alisema alifahamiana na Dk Slaa tangu mwaka 1994 kabla hajagombea nafasi ya urais kupitia Chadema na kwamba tangu wakati huo amekuwa rafiki wa familia.
“Hawawezi kunichagulia marafiki, hawa ni watu wangu wa karibu hata kabla hawajawa na ndoto za kugombea urais, nitaendelea kuwa nao karibu,” alisema.
Asimulia mahojiano
Akizungumzia mahojiano yake na polisi, Gwajima aliwaeleza waumini wake kwamba mambo mengi aliyohojiwa hayakuhusiana na suala la kumkashifu Kardinali Pengo.
“Polisi walinihoji mambo mengi binafsi yanayonihusu mimi na hayakuhusiana kabisa na Pengo, maswali ya Pengo yalikuwa machache sana,” alisema.
Hata hivyo, Gwajima alisema hana ugomvi na polisi wala Serikali kwa kuwa amekuwa akitoa ushirikiano kwa vyombo hivyo. Akitoa mfano, alisema Februari mwaka huu alipeleka barua polisi kueleza anataka kudhamini kampeni kwa ajili ya kupinga mauaji ya albino kwa kushirikiana na jeshi hilo.
“Niliwaeleza kwamba tungezunguka na polisi mikoa yote Tanzania na wamenijibu kwamba nipeleke ratiba ya shughuli hiyo ili tuanze,” alisema.
Alisema pia alidhamini mafunzo ya ulinzi shirikishi kwa vijana 400 kwa kushirikiana na polisi... “Shughuli hizi zinaonyesha kwamba sina ugomvi na polisi, bali nimekuwa rafiki kwa kushiriki katika shughuli zenye masilahi kwa Taifa.”
Viongozi wamiminika
Alisema pia hana ugomvi na Serikali na kwamba viongozi wake wamekuwa wakimiminika katika kanisa lake.
Aliwataja viongozi hao kuwa ni Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi na Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dk Harrison Mwakyembe.
Viongozi wengine, alisema ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nauye, Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee na wabunge wa Viti Maalumu, Dk Mary Mwanjelwa na Vicky Kamata wote wa CCM “Kama ningekuwa na ugomvi na Serikali viongozi hawa wasingekuja katika kanisa langu kwa nyakati tofauti. Hii inaonyesha nilivyo na uhusiano mzuri na Serikali,” alisema.
Alhamisi ijayo
Askofu Gwajima amewataka waumini wake kumsindikiza katika Kituo cha Polisi siku ambayo atahojiwa kwa mara nyingine. “Nitakwenda Central Police Alhamisi saa moja asubuhi, nawaomba waumini wote mfike katika eneo hilo lakini msilete fujo wala kumtukana mtu, kuweni watulivu wakati wote nitakapokuwa nahojiwa,” alisema.
Askofu huyo alitakiwa kuhojiwa Alhamisi iliyopita lakini polisi waliahirisha kutokana na hali yake kutokuwa ya kuridhisha.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema Jeshi la Polisi halitaruhusu mkusanyiko wa watu katika eneo hilo wakati Askofu Gwajima atakapohojiwa.
“Atatakiwa kufika na wakili wake na mtu mmoja ambaye ataona anafaa kuingia naye kwenye mahojiano. Kama kuna waumini wanajiandaa kukusanyika katika ofisi zetu hapa Central Polisi, wafahamu kwamba haturuhusu na wakikaidi tutachukua hatua.”
Ilivyokuwa kanisani
Gwajima alifika katika kanisa hilo lililopo kwenye viwanja vya Tanganyika Packers Kawe saa 5.00 asubuhi na kupokewa kwa shangwe na waumini walioanza kufika tangu saa 2.00 asubuhi.
Msafara wa magari matatu; Toyota Land Cruiser mbili na Hammer, yaliwasili kwenye viwanja vya kanisa hilo na kulakiwa na waumini walioyazingira kwa shangwe na vigelegele wakitaka kumwona Askofu Gwajima.
Waumini hao walikuwa na shauku ya kumwona Gwajima na walionekana wakisukumana ovyo kila mmoja akitaka kumwona.
Akiwa amevaa suti ya rangi ya kijivu na shati jekundu, Gwajima aliteremka katika Hammer akishikiliwa na wasaidizi wake na kukalishwa katika kiti cha magurudumu mawili kilichokuwa kikisukumwa na wasaidizi hao kuelekea kwenye jukwaa la kanisa hilo.
Baada ya kufika, vikundi vya kwaya viliendelea kuimba na kucheza nyimbo mbalimbali za kumtukuza Mungu.
Gwajima alizungumza na waumini wake kuanzia saa 5.30 hadi saa 6.45, akiwaeleza kilichotokea kuanzia siku alipofika polisi kwa mara kwanza, mahojiano hadi alipotoka hospitali.
Katika mahubiri yake, Gwajima alisema ataendelea kuwaonya viongozi wa Serikali na wa dini watakaokosea masuala mbalimbali. “Sitajali ni kiongozi wa aina gani amekosea nitawakemea. Rais akikosea nitamkemea. Waziri akikosea nitamkemea na viongozi wa dini wakikosea nitaendelea kuwakemea,” alisema.