Monday, April 6

Ukawa yadai mambo manne kabla ya Uchaguzi


Dar es Salaam. Uamuzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuahirisha Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa umewafungulia viongozi wa Ukawa kuishinikiza Serikali kuiboresha Katiba ya sasa katika maeneo manne ili kuondoa mvutano katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Mambo manne yanayodaiwa na Ukawa ambayo ni ushindi wa urais kuamuliwa kwa asilimia zaidi ya 50, mgombea binafsi katika nafasi za udiwani, ubunge na urais, tume huru ya uchaguzi na urais kupingwa mahakamani ni yale yaliyoafikiwa baina ya Rais Jakaya Kikwete na vyama vya siasa Septemba 8, mwaka jana.
Mwenyekiti mwenza wa umoja huo, James Mbatia amesema maboresho yaliyofanyika chini ya Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) ni ya lazima ili kufanikisha uchaguzi huo kabla ya kupitishwa kwa Katiba Mpya na kuondoa uwezekano wa vurugu.
Katika kikao hicho, Mbatia alisema walitiliana saini kuwa iwapo uchaguzi wa mwaka huu utafanyika kwa kutumia Katiba ya 1977, Bunge lingekutana Novemba mwaka jana kufanya marekebisho hayo ya 15 ya Katiba na endapo hilo lingeshindikana, basi lingekutana Februari, jambo ambalo pia halikufanyika.
Utekelezaji wa masuala hayo utawezekana iwapo Serikali itawasilisha marekebisho hayo bungeni ili yajadiliwe kwa dharura katika mkutano ujao wa Bajeti wa mwisho wa Bunge la Kumi, kwa kuwa uwezekano wa kupata Katiba Mpya kabla ya uchaguzi ni kama haupo.
Alipoulizwa iwapo jambo hilo linawezekana katika Mkutano wa Bajeti, Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel alisema: “Ndiyo inawezekana. Serikali inaweza kuwasilisha jambo hili kwa dharura na litajadiliwa na Kamati ya Uongozi, kama ikiona linafaa litapelekwa bungeni kujadiliwa.”
Katika hilo Mbatia alisema: “Bado kuna nafasi ya Bunge kufanya marekebisho. Hili linatakiwa kufanyika kama ambavyo tulikubaliana na Rais kupitia TCD.”
Alisema ushauri wa TCD kwamba mchakato wa Kura ya Maoni uahirishwe hadi mwakani umepuuzwa na matokeo yake yameonekana wazi na kwa msingi huo, suala la kurekebisha maeneo hayo manne, si la kupuuza hata kidogo.
“Hili lisipofanyika utaibuka mgogoro mkubwa. Tatizo la Serikali yetu ni kutotaka kutekeleza mambo yanayoonekana wazi kuwa na mkanganyiko, ndiyo sababu ya kukithiri kwa migogoro ya wakulima, wafugaji, wafanyakazi na mingine mingi,” alisema Mbatia.
Dk Slaa akata tamaa
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema endapo Serikali itashindwa kutekeleza makubaliano hayo, vyama vya upinzani havina budi kuingia katika mapambano kwa katiba hiyohiyo.
“Kama hatumwelewi Rais Kikwete katika suala hili, basi hatuwezi kumwelewa tena. Sioni juhudi zozote za Serikali kubadili maeneo haya. Tulikubaliana naye mambo mengi lakini yote ameshindwa kuyatekeleza, hata hili pia hawezi kulitekeleza,” alisema Dk Slaa.
Katibu mkuu huyo wa Chadema alisema umefika wakati wa vyama vya upinzani kupambana hivyohivyo licha ya kuwapo tume ya uchaguzi isiyo huru.
“Nimeshinda ubunge Karatu vipindi vitatu na tume ikiwa ni hiihii. Wapinzani tuna wabunge zaidi ya 100, nadhani tupambane tu,” alisema.
Alisema umefikia wakati wa kuing’oa CCM kwa kutumia Katiba mbovu (iliyopo sasa) na kinachotakiwa kufanywa na vyama vya upinzani ni kujipanga kuanzia vijijini hadi mijini ili kuzoa kura zote.
“Tumeshinda Kawe, Ubungo, Mbeya Mjini na hata Nyamagana. Tuache kulialia sasa, twende katika mapambano. Kwanza Bunge lijalo ni la Bajeti na kwa vyovyote vile mabadiliko tunayoyataka hayawezi kufanyika,” alisema.
Kiongozi Mkuu wa chama cha ACT-Tanzania, Zitto Kabwe alisema kinachotakiwa kufanywa sasa ni Baraza la Vyama vya Siasa kuitisha mkutano wa vyama vyote ili kukubaliana mambo ya kuboresha katika Katiba ya sasa.
“Jambo la pili ni Rais kuitisha Bunge kabla ya kuanza kwa Bunge la Bajeti kujadili mabadiliko hayo na kuyapitisha ili kuufanya uchaguzi mkuu uwe wa haki na huru,” alisema Zitto.
Juhudi za kumpata Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Asha-Rose Migiro kuzungumzia hatua ambazo Serikali inachukua hazikuzaa matunda baada ya simu zao kuita mara kadhaa bila kupokewa.

No comments:

Post a Comment