Uamuzi huo wa Ijumaa iliyopita uliifanya Kenya kuwa Taifa la kwanza barani Afrika na la nne duniani kwa mahakama kubatilisha matokeo ya urais.
Nchi nyingine zilizowahi kufanya hivyo ni Ukraine, Austria na visiwa vya Maldives.
Baadhi ya wasomi na wanasiasa nchini wameendelea kutoa maoni yao, na jana hawakuwa tofauti na siku nyingine tangu kutolewa kwa hukumu hiyo saa 60 zilizopita.
Waliotoa maoni yao jana, walisema kuna haja ya kuhitimisha mchakato wa kupata Katiba mpya ili kuwezesha matokeo ya urais nchini kupingwa mahakamani, lakini wakaongeza na mbadala wake.
Iwapo hilo halitawezekana, wameshauri yafanyike mabadiliko ya sheria ya uchaguzi kwa kuweka kipengele cha kuruhusu matokeo ya urais kupingwa mahakamani.
Maoni hayo yametolewa siku moja baada ya juzi, spika wa zamani wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Pius Msekwa kusema wakati wa kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais mahakamani umeshafika na kilichobaki ni kupitisha rasimu ya Katiba ambayo ina ibara inayotoa haki hiyo.
Kwa mujibu wa ibara ya 41(7) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1997, iwapo mgombea (urais) ametangazwa na Tume ya Uchaguzi kwamba amechaguliwa kuwa Rais kwa mujibu wa ibara hii, basi hakuna mahakama yoyote itakayokuwa na mamlaka ya kuchunguza kuchaguliwa kwake.
Hata hivyo, Msekwa, ambaye pia aliwahi kuwa makamu mwenyekiti wa CCM-Bara alitoa kauli hiyo wakati akizungumza kwa simu na gazeti hili kuhusu hatua ya mahakama nchini Kenya kubatilisha uchaguzi wa Rais wa nchi hiyo uliofanyika Agosti 8 baada ya mgombea wa Muungano wa Nasa, Raila Odinga kufungua kesi akidai kulikuwa na ukiukwaji wa sheria.
Akizungumza na gazeti hili jana, Profesa Benson Bana wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) aliunga mkono kauli ya Msekwa akisema kupinga matokeo mahakamani kutaondoa ‘figisufigisu’ ambazo zinaweza kusababisha machafuko wakati wa Uchaguzi Mkuu.
Alishauri Tanzania isipitwe na wakati, bali iwe na kipengele hicho kwenye Katiba kwa kuwa matokeo ya uchaguzi wa madiwani na wabunge yamekuwa yakipingwa mahakamani.
“Uchaguzi ndiyo kitovu cha siasa katika nchi, watu wanafanya siasa ili kugombea madaraka. Kuna umuhimu wa chombo cha mahakama kusimamia haki hii,” alisema. Akitoa mfano wa Kenya, alisema kama kusingekuwa na kipengele cha kupinga matokeo mahakamani, walioshindwa wangeweza kuanzisha vurugu, lakini walikuwa na imani na chombo hicho.
“Muungano wa Nasa hawakuridhika na matokeo ya urais, tegemeo lao likawa mahakamani na wameshinda. Uamuzi wa kurudia uchaguzi umetolewa,” alisema.
Profesa Bana alisema kuwapo kwa Katiba inayoruhusu kupinga matokeo mahakamani kutaepusha vurugu hasa katika nchi za Afrika.
Kwa mtazamo wake, kiongozi wa chama cha ACT -Wazalendo, Zitto Kabwe alisema mapendekezo ya kupinga matokeo ya urais mahakamani ni sehemu ndogo ya mabadiliko yanayohitajika katika mfumo wa demokrasia unaohitajika kwa Watanzania.
Zitto alisema hata mabadiliko ya kuhamia mfumo wa vyama vingi vya siasa yalihitaji kuboreshwa katika demokrasia iliyokuwa ikisimamiwa na CCM.
“Imefika wakati Watanzania tuamue aina gani ya demokrasia tunayoitaka, kwa sasa CCM ndiyo inayoamua aina gani ya demokrasia ituongoze, tuseme hapana. Tangu mwaka 1965 hadi mabadiliko ya mfumo wa vyama vingi 1992, CCM iliamua aina ya demokrasia,” alisema.
“Hata baada ya 1992 bado CCM inatuamulia aina ya demokrasia, kwa sasa inatuandalia sheria nyingine ya vyama, sasa Msekwa amesema imefika wakati lakini naomba Watanzania ndiyo tuseme hapana na tuamue aina ya demokrasia tunayoitaka.”
Naibu katibu mkuu wa CCM (Bara), Rodrick Mpogolo alisema mapendekezo ya Msekwa yanagusa masuala ya kisera, hivyo asingependa kutoa maoni.
“Ningependa nisizungumze lolote hata kutoa maoni yangu. Kama ni maoni ya chama ungemtafuta msemaji (Humphrey Polepole) au ungezungumza na Serikali ambayo inahusika kwa ukaribu zaidi na masuala ya kisera,” alisema Mpogolo.
Profesa wa Chuo Kikuu Katoliki cha Ruaha (Rucu), Gaudence Mpangala alisema kauli ya Msekwa inaonyesha namna suala hilo lilivyo muhimu katika ujenzi wa demokrasia.
Alisema mwanasiasa huyo mkongwe alishiriki kikamilifu katika uandaaji wa Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 lakini ameona kwa sasa upo umuhimu wa kupinga matokeo ya urais mahakamani.
Profesa Mpangala alisema hata kama mchakato wa kupata Katiba mpya utachelewa, basi ifanyiwe marekebisho sheria ya uchaguzi ili kubadilisha kipengele ambacho kitaruhusu kupinga matokeo ya urais mahakamani.
“Matokeo ya udiwani yanapingwa mahakamani, matokeo ya ubunge yanapingwa mahakamani, isiwe dhambi matokeo ya urais Tanzania yakapingwa mahakamani,” alisema Profesa Mpangala.
Kwa mtazamo wake, Profesa wa Chuo Kikuu cha Mzumbe mkoani Morogoro, George Shumbusho alisema mchakato wa Katiba mpya ni lazima uendelee ili matokeo ya urais yaweze kupingwa mahakamani kama ilivyo kwa Kenya.
“Katika Katiba Inayopendekezwa kuna kipengele kinachoelekeza matokeo ya urais yakishatangazwa na Tume ya Uchaguzi yanaweza kupingwa kwenye Mahakama ya Juu,” alisema Profesa Shumbusho.
Alisema uamuzi wa kurudia uchaguzi kwa amri ya mahakama nchini Kenya umetoa fundisho la demokrasia kwa nchi za Kiafrika ambazo matokeo ya uchaguzi wa Rais huambatana na vurugu.
Aliongeza kuwa ingawa Tanzania imeendelea kuwa nchi ya amani hata yanapotangazwa matokeo ya urais, wakati umefika wa kuwa na chombo cha kuwasikiliza wanaolalamikia matokeo.
Wakati ibara ya 140 ya Katiba ya Kenya inaruhusu mtu yeyote kupinga matokeo ya uchaguzi wa Rais mahakamani ndani ya siku saba tangu kutangazwa kwa mshindi, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inakataza.
Ibara ya 74(12) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema hakuna mahakama yoyote nchini itakayokuwa na mamlaka ya kuchunguza jambo lolote lililotendwa na Tume ya Uchaguzi (NEC) katika kutekeleza madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya Katiba.
Hilo ni jambo ambalo limekuwa likijadiliwa tangu kubatilishwa kwa uchaguzi wa Rais wa Kenya, lakini alipoulizwa kuhusu suala hilo juzi, Msekwa alisema muda umefika. “Tunaweza kufikia hatua hiyo na tumeshaifikia. Katiba mpya iliyopitishwa na Bunge mwaka 2014 inasema matokeo ya urais yanaweza kupingwa mahakamani. Katiba ya sasa hairuhusu, lakini Katiba Inayopendekezwa imeruhusu. Tunachosubiri ni referendum (kura ya maoni) tu,” alisema Msekwa.
Mchakato wa kubadili Katiba ulianzishwa na Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete mwishoni mwa mwaka 2011 lakini ukakwama mwaka 2014 ukiwa katika hatua ya kura ya maoni baada ya NEC kueleza kuwa haikuwa na muda wa kutosha .
Hata hivyo, mchakato huo uliingiwa na dosari baada ya baadhi ya wajumbe wa Bunge la Katiba, hasa kutoka vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na NLD kuususia wakidai kuwa chombo hicho kiliacha Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kuingiza ajenda za chama tawala.
Kususia kwa vyama hivyo vinne ndiyo kulikuwa mwanzo wa kuundwa kwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Licha ya hilo, wajumbe waliosalia bungeni waliendelea na mchakato na kupitisha Katiba Inayopendekezwa. Hata hivyo, Rais John Magufuli ameshasema kuwa Katiba mpya siyo kipaumbele chake kwa kuwa kwa sasa anataka “kuinyoosha nchi”.
Katika hukumu iliyoweka historia nchini Kenya, Mahakama ya Juu ilisema Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ina hatia ya kukiuka sheria katika upokeaji na utangazaji wa matokeo ya kura.
Mgombea wa Nasa, Odinga alifungua kesi kupinga matokeo ya uchaguzi uliofanyika Agosti 8, akisema ulitawaliwa na udanganyifu ikiwamo kuchezewa kwa mifumo ya kujumlishia matokeo.
Katika uamuzi wake, mahakama hiyo ilisema uchaguzi huo ulikuwa na dosari nyingi, hivyo kukiuka misingi ya uchaguzi huru na wa haki kama ilivyoelekezwa katika Katiba ya nchi hiyo.
Katika uchaguzi wa mwaka 2013, Odinga alikwenda mahakamani kupinga matokeo lakini mahakama hiyo ilitupilia mbali hoja zake na kuridhia matokeo yaliyompa ushindi Rais Kenyatta.
Katika uchaguzi wa Agosti 8, Kenyatta alitangazwa mshindi kwa kupata kura 8,203,290 (sawa na asilimia 54.27), huku mpinzani wake Odinga akipata kura 6,762,224 (sawa na asilimia 44.74).