Matukio hayo ni kutangazwa kwa majina ya vigogo waliohusishwa na dawa za kulevya; aliyekuwa waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye kunyooshewa bastola hadharani; uvamizi wa kituo cha Clouds Media; kutekwa kwa msanii wa muziki Roma Mkatoliki; mauaji ya Kibiti; kuzuiwa kwa makontena 275 ya makinikia na utata wa mlipuko katika kampuni ya mawakili ya Imma jijini Dar es Salaam.
Kila tukio kati ya hayo lilichukua wastani wa ama wiki au mwezi mmoja kujadiliwa katika mitandao na makundi mbalimbali ya kijamii.
Wakizungumzia kutikisa kwa matukio hayo, wachambuzi wa mambo ya kijamii na kisiasa wamelieleza gazeti hili kuwa, kulitokana na ugeni wa jamii katika mabadiliko ya mfumo wa Serikali iliyopo madarakani.
“Hatukuwa tumezoea kuona Serikali inayotoa maagizo, inafuatilia na kufanya tathmini lakini kwa bahati mbaya kuna Watanzania wamekuwa wakianzisha makundi mitandaoni kusifia wasichokifahamu na wengine kukosoa au kulalamika bila kuwa na mawazo mbadala,” alisema Profesa Haji Semboja kutoka Idara ya Uchumi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
“Watu wanapoteza muda bure badala ya kufanya kazi au kujadili masuala ya kisera na kimkakati kuhusu ajenda iliyopo.”
Profesa Semboja alisema baadhi ya wananchi kwa bahati mbaya pia hupokea habari zilizoandaliwa na vyombo visivyotekeleza majukumu yake kwa weledi, hivyo kuiathiri jamii.
Alisema sababu nyingine ni wananchi kutumia haki yao ya msingi kuhoji jambo na kutafakari kupitia mfumo wa habari licha ya changamoto zinazojitokeza katika mijadala husika.
Mhadhiri mwandamizi kutoka Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala Bora, UDSM, Richard Mbunda alisema kila tukio hugusa hisia za mtu kwa namna tofauti, hivyo kuibua mijadala.
“Miaka ya nyuma watu walitumia vijiwe na maskani kukutana kujadili matukio yanayojitokeza katika jamii au serikalini, hata Ulaya ilikuwa hivyo lakini sasa teknolojia imerahisisha, mijadala imeongezeka kwa sababu ya uwazi na urahisi wa kupata habari,” alisema.
Februari 2, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alianzisha mjadala wa dawa za kulevya baada ya kutaja majina ya askari zaidi ya 10 na wasanii saba waliodaiwa kujihusisha na biashara hiyo na baada ya siku kadhaa akawataja wengine wakiwamo wafanyabiashara, viongozi wa dini na wanasiasa.
Makonda katika awamu ya pili alikabidhi ripoti ya majina 97 ambayo hakuyataja kwa kamishna mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Rogers Sianga katika mkutano maalumu wa kutoa tathmini ya kampeni ya kutokomeza biashara haramu ya dawa za kulevya.
Uamuzi wa kutaja majina hadharani ulipingwa na wanaharakati na wasomi kabla ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kupiga marufuku kutaja majina hadharani.
Nape kuonyeshwa bastola
Machi 23, mbunge wa Mtama, Nape Nnauye alitishwa kwa bastola nje ya hoteli ya Protea baada ya mkutano wake na wanahabari kuzuiwa na polisi wa Kinondoni.
Tukio hilo lilitokea siku moja tangu Rais John Magufuli alipotengua uteuzi wake wa uwaziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kutokana na mvutano wa sakata la uvamizi wa kituo cha Clouds.
Uvamizi wa Clouds
Machi 28, asasi za kiraia 33 barani Afrika zililaani kitendo cha kuvamiwa studio za Clouds na kulazimisha maudhui yasiyostahili yarushwe hewani. Tamko la asasi hizo lilitolewa siku chache baada ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Jukwaa la Wahariri (TEF) na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kulaani kitendo hicho.
Kutekwa kwa Roma
Aprili 6, msanii wa muziki wa hip hop, Ibrahim Mussa maarufu Roma Mkatoliki akiwa na wenzake wawili walitekwa na watu wasiojulikana katika studio za Tongwe Records zilizopo Masaki jijini Dar es Salaam. Tukio hilo lilitanguliwa na kukamatwa kwa msanii mwingine, Emmanuel Elibariki maarufu Ney wa Mitego baada ya kutoa wimbo wa Wapo.
Mauaji ya Pwani
Wilaya za Mkoa wa Pwani za Rufiji, Kibiti na Mkuranga zilikumbwa na mauaji dhidi ya viongozi wa vijiji na vitongoji tangu Mei, 2016 na watu zaidi ya 32 wakiwamo polisi waliuawa.
Sakata la makinikia
Juni 12, kamati ya pili iliyoundwa na Rais John Magufuli kuchunguza masuala ya kiuchumi na kisheria kwenye makinikia ilitoa ripoti iliyoonyesha upungufu kwenye mikataba ya madini. Ripoti hiyo ilijadiliwa sana mitandaoni.
Sakata la Immma
Agosti 26, kwa kutumia milipuko iliyotengenezwa kienyeji, ofisi za kampuni ya uwakili ya Immma zilizopo mtaa wa Charambe, Upanga jijini Dar es Salaam zililipuliwa na tukio hilo likasababisha Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kutangaza mgomo wa mawakili kwa siku mbili.
No comments:
Post a Comment