Mashirika mawili ya uchunguzi yamedai kwamba kampuni ya mafuta inayomilikiwa na serikali nchini Sudan Kusini imekuwa ikitumika kufadhili vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo, ikiwa ni pamoja na wanamgambo wanaoegemea upande wa serikali ambao wanatuhumiwa kwa vitendo vya ukiukwaji wa haki za binaadamu.
Katika ripoti iliyochapishwa hii leo, shirika la kimataifa la uchunguzi la Global Witness limesema ni mwaka wa tano sasa, mamilioni ya dola yatokanayo na kodi ya mafuta kuhamishwa kutoka katika shirika la mafuta la Nile Petrolium na kuingizwa katika kitengo cha usalama wa taifa cha Sudan Kusini, kwa lengo la kufadhili vita.
Shirika jingine la uchunguzi la Sentry, lililoanzishwa kwa ushirikiano na mcheza filamu wa Marekani George Clooney, limedai kwamba wanasiasa, wanajeshi, taasisi za serikali na makampuni yanayomilikiwa na wanasiasa na wanafamilia wa wanasiasa hao walilipwa zaidi ya dola milioni 80.
Sudani Kusini ni taifa la tatu kuwa na hifadhi kubwa ya mafuta Afrika
Kampuni hiyo ya Nile Petrolium imekanusha kufadhili shughuli yoyote ya kivita na kusema fedha zilizokuwa zikitolewa zimekuwa zikielekezwa kwenye miradi ya kijamii kama barabara, shule na hospitali.
Mkurugenzi wa mahusiano wa kampuni hiyo ya mafuta Yiey Puoch Lur amenukuliwa akisema hawawezi kufadhili wanamgambo kwa kuwa hiyo si sehemu ya majukumu yao. Alisema, shirika la Global Witness lilighushi nyaraka hizo.
Ni wiki moja tu imepita tangu kamisheni ya Umoja wa Mataifa inaoyangazia haki za binadamu iliitaja Sudani Kusini kuwa miongoni mwa mataifa yanayokiuka haki za binadamu. Kwenye ripoti yake, mjumbe wa kamisheni hiyo nchini humo, Andrew Clapham alisema mzozo ulioanza mwaka 2013, umechangia kuongezeka kwa visa vya ukiukwaji, ambavyo ni pamoja na mauaji ya kikabila.
Marekani yaeleza kusikitishwa na ufichuzi huo.
Marekani imeuelezea ufichuzi huo kuwa ni wa kusikitisha sana.
Afisa mahusiano wa ubalozi wa Marekani, Mark Weinberg aliliambia shirika la habari la Associate Press kwamba mapato yatokanayo na mafuta yanatakiwa kutumika kwa lengo la kuchochea uchumi wa nchi na si kutumika kinyume kwa kununua silaha ili kuiharibu zaidi nchi. Alisema, rasilimali ya Sudani Kusini zinatakiwa kutumika kwa ajili ya maslahi ya watu wake na viongozi wana wajibu wa kutanguliza kwanza maslahi ya watu wao.
Rais wa Sudani Kusini Salva Kiir anadhibiti kampuni hiyo ya mafuta inayotuhumiwa.
Kampuni ya mafuta ya Nile Petrolium inadhibitiwa moja kwa moja na rais wa Sudani Kusini Salva Kiir pamoja na mtandao wake wa karibu, hii ikiwa ni kulingana na ripoti ya Global Witness, iliyozingatia nyaraka za siri na ushahidi wa watu waliohusika.
Ripoti hiyo imesema, mkuu wa idara ya usalama wa ndani na mjumbe wa bodi ya wakurugenzi ya kampuni hiyo ya mafuta Akol Koor, amekuwa akiwasambazia wapiganaji silaha zilizonunuliwa kwa fedha kutoka kampuni hiyo.
Sudani Kusini ni taifa la tatu kwa kuwa na hifadhi kubwa ya mafuta barani Afrika, kwa wastani wa mapipa bilioni 3.5. hata hivyo, baada ya miaka mitano ya vita vya wenyewe kwa wenyewe iliyosababisha vifo vya makumi kwa maelfu ya raia na wengine mamilioni kukimbia, taifa hilo limejikuta katika mzozo wa kiuchumi. Wabunge kwa muda mrefu wamewatuhumu maafisa wa serikali kwa kutumia fedha za mafuta kwa manufaa yao wenyewe, badala ya kuwasaidia raia.
Mbunge ambaye hakutaka kujitambulisha kwa hofu ya usalama wake alinukuliwa akilalama kuwa fedha hazitunzwi nchini humo, bali maafisa wa serikali wamekuwa wakizitumia kinyume cha utaratibu kwa kuzihifadhi kwenye mabenki ya nje.
Kulingana na shirika la Sentry, Marekani na Umoja wa Ulaya pamoja na jamii ya kimataifa wanatakiwa kuikabili Sudani Kusini kwa kutumia wizi kufadhili machafuko kwa kuwachunguza maafisa wa juu na kuwawekea vikwazo vya kimtandao.