Tuesday, March 6

UPELELEZI KESI YA MAUAJI MKURUGENZI WA PALMS BADO HAUJAKAMILIKA



MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeelezwa, upelelezi wa kesi ya mauji ya Mkurugenzi na Mwanzilishi mwenza wa Shirika lisilo la kiserikali la Palms Foundation, Wayne Lotter inayowakabili watuhumiwa nane bado haujakamilika.

Wakili wa Serikali, Adolf Mkini ameeleza hayo leo mapema mbele Hakimu Mkazi Mkuu Wilbard Mashauri wakati kesi hiyo ilipokuja kwa kutajwa. Upelelezi bado haujakamilika

Aidha Mahakama ilielezwa na mshtakiwa Rahma Almas  kuwa mshtakiwa Mohammed Maganga anaumwa na yuko gerezani.

Kutokana na taarifa hizo, kesi imeahirishwa hadi Machi 21, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na kujua kama upelelezi utakuwa umekamilika ama la.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni, raia wa Burundi, Nduimana Jonas maarufu Mchungaji (40) Mkazi wa Kamenge Burundi, Godfrey Salamba (42) Mkazi wa Kinondoni Msisiri A. Innocent Kimaro (23) Mkazi wa Temeke Mikoroshini, Chambie Ally(32) Mkazi wa Kia/Boma na Ofisa wa Benki ya NBC, Robert Mwaipyana (31) Mkazi wa Temeke Mikoroshini.

Wengine ni  Meneja wa Benki ya Baclays Khalid Mwinyi (33) Mkazi wa Mikocheni B, Mfanyabiashara Rahma Almas (37) Mkazi wa Mbagala B na Mohammed   Maganga (61) mchimba makaburi.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka mawili ambapo katika shtaka la kwanza wanadaiwa kuwa kati ya Julai Mosi na Agosti 16,mwaka 2017 wakiwa ndani ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania washtakiwa hao walikula njama ya kufanya mauaji ya Wayne Lotter.

Katika shtaka la pili, washtakiwa wanadaiwa Agosti 16, mwaka jana katika makutano ya barabara za Chole na Haile Selasie Kinondoni Dar es Salaam,  walimuua Lotter.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, upelelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika

No comments:

Post a Comment