Friday, March 2

Tanzania yakanusha kuminya demokrasia


Serikali ya Tanzania imekanusha tuhuma kwamba inaminya demokrasia nchini humo na kusema kuwa imesikitishwa na matamko kadhaa yaliotolewa na Marekani na Umoja wa Ulaya (EU) na kuungwa mkono na baadhi ya balozi za nchi za Magharibi.
Taarifa ya serikalli ya Tanzania imefuatia matamko yaliyotolewa na nchi za magharibi wiki za hivi karibuni yakielezea wasiwasi wao kutokana na matukio ya kiusalama ambayo wameeleza yanatishia utawala wa kisheria na maadili ya kidemokrasia nchini Tanzania.
Katika wiki za hivi karibuni polisi wa Tanzania wameshutumiwa kwa kutumia nguvu za kupita kiasi kushughulikia mivutano ya kisiasa na pia wanasiasa kadha wa upinzani wakiwemo wabunge mara kwa mara wameitwa polisi kwa mahojiano kutokana na madai ya kufanya mikutano isiyo halali.
Mbunge wa upinzani Joseph 'Sugu" Mbilinyi na afisa mwingine wa chama cha Chadema mjini Mbeya walihukumiwa kifungo cha miezi mitano gerezani mwishoni wa Februari baada ya kukutwa na hatia ya kumkashifu Rais John Pombe Magufulu
Taarifa hiyo iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania pia imesema kuwa tayari nchi hiyo imechukua hatua kukubaliana na vikwazo vilivyowekwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya Korea Kaskazini. Nchi za magharibi ziliishutumu Tanzania kwa kukiuka vikwazo hivyo.
Hata hivyo Tanzania imesema tuhuma kwamba imekiuka vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya silaha za nyuklia za Korea Kaskazini na programu yao ya makombora ya balistika hazijaweza kuthibitishwa..
Taarifa hiyo imeeleza kuwa suala la utawala wa sheria na demokrasia katika tamko hilo la mabalozi linaonyesha sintofahamu iliyoko juu ya usalama na changamoto za kisiasa ambazo Tanzania imekuwa ikikabiliwa nazo kwa kipindi cha miezi 18 na kwamba matamko hayo yamekuwa sio tafsiri sahihi ya hali ya kisiasa na usalama iliyopo Tanzania.
“Ni kawaida kwa wanadiplomasia wa kigeni kufuatilia na kuripoti hali ya kisiasa na usalama inayoendelea katika nchi walizotumwa. Lakini tunashangazwa na ukimya uliowazi katika kipindi cha nyuma wa mabalozi hawa juu ya vitisho vya uvunjifu wa amani uliokuwa haujawahi kutokea na changamoto nyingine ambazo Tanzania imekuwa ikikabiliana nazo katika maeneo matatu ya Kibiti-Mkuranga –Rufiji yanayopakana,” limesema tamko hilo.
Wizara hiyo imeeleza kuwa vitisho hivyo vimewauwa watu wasio na hatia na kwa sadfa ya ajabu, wengi wa waliouwawa walikuwa kutoka chama tawala.
Mauaji hayo yalikuwa yametanguliwa na matukio kama hayo ya uvunjifu wa amani katika maeneo mbalimbali ya nchi yakiwa ya aina yake yalihusisha uvunjifu wa amani.
Kwa mujibu wa tamko hilo pamoja na kuwepo taarifa za matukio haya ya uvunjifu wa amani yalitolewa na vyombo vya habari nchini, hakukuwa hata na tamko lililolaani vitendo hivyo kutoka kwa mabalozi hao.
Wizara imehoji kuwa ni hivi sasa tu ndio EU inataja juu juu shambulizi la silaha lililotokea Mkoa wa Pwani katika kipindi cha miaka miwili.” Kuchelewa kutolewa kwa matamko hayo baada ya muda mrefu na wakati mgumu unastaajabisha.
Moja ya matamko yaliyotolewa na mabalozi wizara imesema ni jambo zuri kwa mabalozi wametambua wito wa Rais Magufuli akitaka uchunguzi ufanyike wa matukio mengine ya uvunjifu wa amani katika wimbi la operesheni ya Kibiti, Mkuranga na Rufiji.
Lakini wizara imesema kuwa matamko hayo ya mabalozi hayakutambua uhusiano uliokuwepo kati ya hatua za kishujaa ambazo zimechukuliwa na Rais Magufuli kuondoa ufisadi, madawa ya kulevya, ukwepaji kodi, ujangili wa nyara za serikali na kuhakikisha uwajibikaji katika sekta binafsi na za umma, na matukio ya usalama.
“Hatua za serikali ya awamu ya nne bila shaka zimewakasirisha watu wenye nguvu ndani na nje ya nchi ambao wanamaslahi binafsi katika hali ya uzembe iliokuwa inaendelea hapo awali nchini,” taarifa hiyo imesema.

TCRA: Nyimbo za Diamond Platnumz, Wa Mitego, Jux na wanamuziki wengine zafungiwa na serikali Tanzania

Diamond
Nyimbo mbili za Diamond Platnamz ni miongoni mwa nyimbo zaidi ya 10 zilizopigwa marufuku kupigwa katika radio nchini Tanzania.
Nyimbo kadha za wanamuziki Ney wa Mitego, Roma Mkatoliki, Jux na Barnaba pia zimefungiwa.
Nyimbo za Diamond, ambaye jina lake halsii ni Nasib Abdul, zilizofungiwa ni Hallelujah (uliomshirikisha Morgan Heritage ) na Waka Waka (uliomshirikisha Rick Ross).
Barua kutoka Mamlaka ya Mawasiliano nchini Tanzania kuelekea Radio moja mjini Dodoma imesema nyimbo hizo zimefungiwa kwa ushauri kutoka kwa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata).
Basata wamewasilisha kwa TCRA orodha ya nyimbo hizo ambazo zimedaiwa kuwa "zisizokuwa na maadili."
"Nyimbo hizo zilitolewa na wasanii na kusambazwa katika vyombo mbalimbali vya utangazaji na mitandao ya kijamii," taarifa a TCRA imesema.
"Nyimbo hizo zina maudhui ambayo ni kinyume na maadili na Kanuni za Huduma za Utangazaji (Maudhui) 2005."
Nyimbo mbili za Ney wa Mitego, jina lake halisi Emmanuel Elibariki - Pale kati Patamu na Maku Makuz - pia zimefungiwa.
Mwanamuziki Roma Mkatoliki ambaye jina lake halisi ni Abernego Damiani naye amefungiwa wimbo wa Kibamia.
Wimbo wa Amani Hamisi maarufu kama Manifango wa Hainaga Ushemeji pia umefungiwa, sawa na I am Sorry JK wake Nikki Mbishi ambaye jina lake halisi ni Nicas John Mchuche.
Wimbo Chura wake Snura ulifungiwa mara ya kwanza 2016
Image captionWimbo Chura wake Snura ulifungiwa mara ya kwanza 2016
Snura Mushi ambaye jina lake la usanii ni Snura amefungiwa nyimbo mbili - Chura na Nimevurugwa.
Nyimbo nyingine ni Tema mate tumchape (Hamad Ali maarufu Madee), Uzuri Wako (Juma Mussa Mpolopoto maarufu Jux), Nampa Papa (Gift Stanford maarufu Gigy Money) na Nampaga (Barnaba Elias maarufu Barnaba).
Mwana 2016, TCRA walikuwa wameufungia wimbo wa Chura wake Snura.
Baadaye aliomba radhi na kuahidi kutekeleza maagizo ya serikali.
Hata hivyo, bado ametetea video zilizotolewa za wimbo huo akisema zilitolewa tu kwa ajili ya YouTube.

Rwanda yaanza kufungia makanisa 700 kwa kutotimiza masharti yaliyowekwa

Baadhi ya makanisa yamekuwa yakifanya ibada kwenye mahema
Image captionBaadhi ya makanisa yamekuwa yakifanya ibada kwenye mahema
Serikali ya Rwanda imeanza kutekeleza uamuzi wa kufunga makanisa ambayo hayajatimiza kanuni za ujenzi na vigezo vingine vinavyotakiwa kwa wachungaji wa makanisa hayo.
Jumla ya makanisa 700 yamefungwa, mengi yakiwa ni makanisa madogo madogo yaliyoanzishwa hivi karibuni.
Kulingana na bodi ya taifa hilo inayohusika na uongozi, makanisa yanatakiwa kufwata taratibu za ujenzi wenye miundo msingi stahiki na shahada ya elimu ya theolojia kwa wachungaji.
Mwandishi wa BBC Yves Bucyana aliyepo Kigali anasema makanisa yasiyopungua 700 na msikiti mmoja tayari yamefungwa kutokana na kile ambacho bodi ya taifa hilo inayohusika na uongozi imetaja kuwa kushindwa kutimiza kanuni za ujenzi.
Makanisa zaidi ya 700 yamefungwa
Image captionMakanisa zaidi ya 700 yamefungwa
Baadhi ya makanisa yanaendeshea ibada zao kwenye mahema,huku makanisa mengi yakifanyia ibada zao kwenye nyumba za kibiashara kama baa na mighahawa; na makanisa mengi yana kelele za kupita kiasi ilhali yamejengwa katikati mwa makazi ya wananchi.
Mwandishi wa BBC mjini Kigali anasema ukaguzi wa wakuu wa serikali za mitaa bado unaendelea kutathmini makanisa zaidi yasiyotimiza masharti na pengine kufungulia mengine ambayo yamo mbioni kutimiza matakwa ya serikali.
Rwanda inajadili sheria mpya ambayo itahusu mashirika yenye misingi ya imani na dini yanayoendeshwa na wahubiri kuwa wahubiri hao lazima wawe na shahada za elimu ya theolojia.
Makanisa
Wakosoaji wanaona kwamba hii ni sheria inayolenga kudhibiti makanisa wakati wengine wanaona kwamba ni sheria yenye lengo la kunyoosha makanisa ambayo siku hizi yamezongwa na migogoro ya ndani.

Muasi wa zamani ageuka kuwa mlezi wa yatima Burundi

yatima
Image captionBi Mariam Ndayisenga maarufu kama Mama Zulu,muasi mstaafu aliyeamua kuwalea watoto yatima
Mwanamke mmoja nchini Burundi ambaye alikuwa ni miongoni mwa wanawake wa kwanza kujiunga na makundi ya waasi mwishoni mwa miaka ya 90, kwa sasa amejiingiza katika shughuli za kuwalea watoto yatima.
Athari za vita kwa watoto ndio zilizomuhamasisha mwanamke huyu ambaye alikuwa mpiganaji wa zamani wa kundi la Waasi la CNDD/FDD kufanya kazi ya kuwalea watoto hao yatima.
Bi Mariam Ndayisenga maarufu kama Mama Zulu alikutana na Mwandishi BBC,Ramadhani Kibuga katika makazi yake yaliopo Kinama kaskazini mwa jiji la Bujumbura.
Kituo chake kina watoto zaidi ya 70 wenye rika mbalimbali wakiwemo hata watoto wachanga.
Kituo hiki kinaonekana kuwa sio cha kawaida kutokana na historia ya mmiliki wa kituo hicho kuwa mstaafu katika harakati za kijeshi.
Lakini ni nini kilichomsukuma kuanza kushughulika na kazi ya kulea yatima na kuacha shughuli za uasi.
athari
Image captionMstaafu wa waasi asema,Athari za vita zinawakumba watoto
''Mimi ni mama wa kwanza kabisa kuchukua silaha na kwenda kupigania nchi yangu lakini matokeo yake sikuwa ninayategemea kwa kuwa yalileta athari kubwa sana haswa kwa watoto.'' Bi Marium aeleza.
Katika vita alikutana na changamoto mbalimbali lakini kulea watoto hawa inampa furaha kwake na anasema hudumu za watoto kuanzia chakula , mavazi hata matibabu imekuwa sio jambo rahisi, lakini hajavunjika moyo na watu pia wanamsaidia kwa namna moja au nyingine.
Pamoja na kukutana na changamoto kadha wa kadha hata kwenye malezi ya watoto wahitaji Maryam anasema katika maisha yake amezoea kupambana.
Maana hata wakati wa vita alipewa jina la mama Zulu kwa kuwa yeye ni mama shujaa na hata anadhani ushujaa wake unahitajika kuwalea watoto hawa zaidi.
Burundi ni miongoni mwa nchi za Afrika zilizokumbwa na vita na kujikuta watoto wengi wako barabarani wakiwa ni omba omba na mayatima.
Hivyo changamoto kubwa iliosalia ni jinsi ya kuwatunza watoto hao wahitaji na yatima nchini humo.

Tattoo ya Kale zaidi yabainika Misri

bcHaki miliki ya pichaTHE TRUSTEES OF THE BRITISH MUSEUM
Image captionMwili wa mwanaume aliyebainika kuwa na tattoo tangu miaka 5000 iliyopita alikufa na umri kati ya miaka 18 mpaka 21
Watafiti wamebaini michoro ya mwilini maarufu "tattoo" iliyokuwa mikongwe zaidi duniani ipo katika miili miwili iliyoishi miaka 5000 iliyopita huko nchini Misri.
Vielelezo vya michoro hiyo inaonyesha mchoro wa ng'ombe pori na kondoo katika upande wa juu wa mkono wa mwili wa mwanaume na bega la mwanamke
Ugunduzi huu unaweza kuondoa ushaidi wa kuwa shughuli hizi za kujichora mwili zilianza kufanyika barani Afrika miaka 1000 iliyopita.
Daniel Antoine, ni miongoni mwa waandishi wa tafiti hiyo katika makumbusho ya Uingereza inayotoa elimu ihusiyo habari zinazohusu asili na maendeleo ya binadamu wa awali na alisema ugunduzi huu unabadili mtazamo wa ueleo wa watu juu ya namna ya watu walivyoishi katika karne zilizopita.
Mwili wa mwanaume huyo uligunduliwa miaka 100 iliyopita.
Uchunguzi wa kitaalamu uliofanywa unaonyesha kuwa alikufa akiwa ana umri kati ya miaka 18 mpaka 21. Na kifo chake kilisababishwa na jeraha alilolipata mgongoni.
tatooHaki miliki ya pichaTHE TRUSTEES OF THE BRITISH MUSEUM
Image captionMmoja ulielezwa kuwa ni mchoro wa ng'ombe mwitu aliyekuwa na mkia mrefu na pembe kubwa,mwingine unaonekana kuwa ni kondoo mwenye pembe zilizopinda
Alama nyeusi katika mkono wake haukuonekana kama una umuhimu mpaka alipofanyiwa uchunguzi wa kielektroniki na kubainika kuwa mwili huo una tattoo ya wanyama wawili.
Mmoja ulielezwa kuwa ni mchoro wa ng'ombe mwitu aliyekuwa na mkia mrefu na pembe kubwa,mwingine unaonekana kuwa ni kondoo mwenye pembe zilizopinda.
tatooHaki miliki ya pichaTHE TRUSTEES OF THE BRITISH MUSEUM
Image captionTattoo inayoonyesha hali ya ujasiri na ujuzi na kutoa ujumbe Fulani wa kustaajabisha
Wakati picha ya mwili wa mwanamke unaonesha tattoo inayoonyesha hali ya ujasiri na ujuzi na kutoa ujumbe Fulani wa kustaajabisha.
Mwili wa mwanamke huyo wa kale una alama ya S ndogo nne zilizokuwa chini ya bega lake la kulia.
Mwanamke huyo pia alikuwa na alama inayowasilisha muziki unaotumika katika sherehe.
Mwili wa mwanamke una alama ya S ndogoHaki miliki ya pichaTHE TRUSTEES OF THE BRITISH MUSEUM
Image captionMwili wa mwanamke una alama ya S ndogo
Awali, Wataalamu wa watu wa kale walidhani kuwa ni wanawake peke yake ndio wana tattoo wakati wa miongo iliyopita lakini ushaidi uliobainika katika tattoo ya mwili wa mwanaume sasa unaonyesha kuwa uchoraji wa mwili ulikuwa unafanywa na jinsia zote.
Watafiti wanaamini kuwa tattoo zinaashiria ujumbe wa kutokuwa na hofu na ujuzi wa kustaajabisha.
Mifano kongwe ya tattoo iliyoonekana katika binadamu wa kale wanasadikiwa kuwa waliishi 3370 na 3100BC .

Vladimir Putin asema Urusi ina kombora lisiloweza kuzuiwa

Graphic of weaponry presented by Vladimir Putin during his annual address on 1 March 2018Haki miliki ya pichaREUTERS
Image captionMichoro ilitumiwa kuonesha silaha hizo mpya kupitia video
Urusi imeunda kombora jipya ambalo haliwezi kutunguliwa na linaweza kufika pahala popote duniani, kwa mujibu wa Rais Vladimir Putin.
Bw Putin amekuwa akieleza sera zake muhimu za muhula wa nne, taifa hilo linapokaribia kufanya uchaguzi katika siku 17.
Rais huyo anatarajiwa kushinda.
Amesema kombora "halipai juu sana, ni vigumu sana kulitambua likipita, lina uwezo wa kubeba kichwa cha nyuklia na linaweza kufika popote pale. Aidha, njia linayofuata haiwezi kutabirika na adui, linaweza kukwepa vizuizi na kimsingi haliwezi kuzuiwa na mifumo ya sasa ya kinga dhidi ya makombora na hata mifumo inayotarajiwa kuundwa siku zijazo."
Katika nusu ya kwanza ya hotuba hiyo yake kwa taifa, ameahidi kupunguza viwango vya umaskini nchini humo.
Kisha, ameonesha mkusanyiko wa silaha mpya, likiwemo kombora alilosema linaweza "kufika pahala popote duniani".
Hotuba hiyo ya Bw Putin imeendelea kwa saa mbili.
Uchaguzi utafanyika mnamo 18 Machi.
Kiongozi huyo anakabiliwa na wapinzani saba, lakini hakuna mmoja kati ya hao anayetarajiwa kutoa ushindani mkubwa kwake.
Rais huyo hakushiriki katika mdahalo wa wagombea uliooneshwa moja kwa moja kwenye runinga Jumatano na kuwashirikisha wagombea hao wengine.
Kiongozi wa upinzani Alexei Navalny hajakuwa akifanya kampeni.
Amezuiwa kuwania na ametoa wito kwa wapiga kura wanaomuunga mkono kususia uchaguzi huo.
Rais Putin hajafanya kampeni sana na kufikia sasa alikuwa hajazungumzia sana mipamngo yake ya miaka sita ijayo.
Russian President Vladimir Putin addresses the Federal Assembly at Moscow's Manezh exhibition centre on 1 March 2018Haki miliki ya pichaAFP
Image captionIlikuwa hotuba ya mwisho kwa Bw Putin kabla ya uchaguzi
Huku akitumia skrini kubwa, ameonyesha video za alichosema ni kombora jipya la Urusi.
Amesema kombora hilo haliwezi kuzuiwa na mfumo wa kinga ya makombora wa Marekani barani Ulaya na Asia.
Kadhalika, ameonesha video ya ndege isiyo na rubani inayoweza kufanya kazi chini ya bahari.
Kwenye hotuba hiyo yake kwa kikao cha pamoja cha mabunge mawili, amewahamasisha raia kupendekeza majina ya kupewa mifumo hiyo miwili ya silaha.

Ulinzi

Putin amesema uwezo wa kijeshi wa Urusi umepangwa na kustawishwa kwa lengo la kudumisha amani duniani.
Hata hivyo, amesema iwapo mtu yeyote yule atathubutu kurusha silaha za nyuklia dhidi ya Urusi, atajibiwa mara moja.
Operesheni ya kijeshi ya Urusi Syria, ambapo anasaidia Rais wa Syria Bashar al-Assad dhidi ya waasi na amesema hiyo inadhihirisha kuimarika kwa uwezo wa Urusi katika kujilinda.
Urusi majuzi ilituma ndege zake mbili mpya za kivita, aina ya Su-57, ingawa bado zinafanyiwa majaribio.
Su-57Haki miliki ya pichaAFP
Image captionPutin hakusema iwapo ndege zake mpya za kivita zimeanza kutumiwa Syria
Amesema pia kwamba daraja la kuunganisha Urusi na rasi ya Crimea litafunguliwa miezi michache ijayo.
Urusi iliteka Crimea kutoka Ukraine mwaka 2014 wakati wa muhula wa sasa wa Bw Putin.
Kiongozi huyo amesema Urusi inalinda maslahi yake katika eneo la Arctic kwa kuimarisha miundo mbinu yake ya kijeshi eneo hilo.

'Ninajipiga selfie 200 kwa siku'

Junaid AhmedHaki miliki ya pichaJUNAID AHMED/GETTY IMAGES
Junaid Ahmed anawafuasi 50,000 kwenye ukurasa wake wa Instagram na anakubali kuwa anapenda mno kujipiga picha (selfies)
kijana huyu mwenye miaka 22 anajipiga picha takriban 200 kila siku.
huziangalia picha zake kwenye mtandao wa kijamii zikipendwa na watu wengi, kama ikitokea zimependwa na watu chini ya 600 hufuta picha hiyo
''Nikiweka picha,ndani ya dakika moja au mbili huwa pengine inapendwa na watu 100. Ninajisikia vizuri"
Presentational white space
Utafiti uliofanyika hivi karibuni unasema hali hii ya kupenda kujipiga picha inaitwa 'Selfitis'.
Junaid, anaishi Essex,Uingereza, anasema amegundua ni namna gani mitandao ya kijaamii inaweza kuwa mibaya, lakini hachukulii jambo hilo kwa uzito.
'Unachokiona kwenye mtandao wa kijamii si kweli''.Anaeleza.
''Mitandao ya kijamii ni mizuri ukitumia kwa matumizi chanya.Lakini yasiathiri maisha yako kabisa kwa sababu unataka kuwa kama mtu mwingine kwenye mtandao wa Instagram...haina maana.''
Junaid is addicted to selfiesHaki miliki ya pichaJUNAID AHMED
Image captionJunaid anapendelea kujipiga picha ya 'selfie'
'Nilitaka kuonekana na mimi nimo'
Danny Bowman, 23,alikua akiweka picha zake za Selfie kwa wingi kwenye mtandao wa kijamii alipokuwa kijana mdogo.
''Nilitaka na mimi nifanane na hao ninaowaona, nikaona njia nzuri ni kuonekana vizuri'' alisema.
''Hali hiyo iliendelea, nikitumia saa kumi mbele ya kioo nikijipiga picha, kila siku''.
Danny took hundreds of selfies when he was 15 years oldHaki miliki ya pichaDANNY BOWMAN
Image captionDanny alijipiga mamia ya picha alipokuwa na miaka 15
Alipofika miaka 16 Danny alijaribu kujiua.
Alikwenda kwenye nyumba ya kubadili tabia ikagundulika alikua na tatizo la 'body dysmorphic disorder' na aliamini hali hiyo imesababishwa na kupenda sana mitandao ya kijamii.
Danny sasa yuko chuo kikuu anawasaidia vijana wadogo wenye matatizo ya akili.
Danny BowmanHaki miliki ya pichaDANNY BOWMAN
''Nakumbuka nilijiuliza nikiwa nimelala kitandani' ni namna gani nitaondokana na tatizo hili?' nikahisi kama hakuna namna.
''Picha ninazoweka sasa mtandaoni si za kujipia mwenyewe tena bali ni picha za mimi nikiongea na watu au nikitoa hotuba.
Taasisi moja ya masuala ya afya inatoa wito kwa serikali na majukwaa ya mitandao ya kijamii kutoa ujumbe wa tahadhari kwenye simu baada ya mtu kutumia mtandao kwa saa mbili, baada ya utafiti uliofanywa kuhusu madhara ya mitandao ya kijamii kwa vijana.
Inaelezwa kuwa kupenda kujipiga picha na kuweka mitandaoni zaidi ya mara sita kwa siku ni tatizo liitwalo Chronic selfitis,wamesema wataalam kutoka chuo cha Nottingham Trent na Thiagarajar nchini India.
Sasa Junaid anasema maoni mabaya dhidi ya picha zake mitandaoni havimsumbui tena kama awali, hata sura yake alikuwa akiibadilisha kwa sababu ya msukumo wa mitandaoni.
''miaka iliyopita sikuwa hivi, nilikua na asili yangu, lakini nafikiri kupenda sana mitandao kupita kiasi kuliniponza, nilitumia kamera kubadili kidevu, mashavu, midomo,macho, kichwani na kuweka tattoo na nyusi.