Mkurugenzi wa shirika hilo ukanda wa Afrika Mashariki, Pembe ya Afrika na Maziwa Makuu, Muthoni Wanyeki alitoa wito kwa serikali jana kulishughulikia suala hilo kikamilifu pamoja na masuala mengine ikiwa ni pamoja na viongozi na maofisa wa serikali kutoa taarifa fasaha.
Msando, ambaye alikuwa kaimu mkurugenzi wa kitengo cha Tehama, inaaminika aliuawa usiku wa Ijumaa kuamkia Jumamosi na mwili wake ulitupwa katika vichaka eneo la Kikuyu, Kaunti ya Kiambu. Baadaye mwili wake uliokotwa na polisi na kuwekwa katika chumba cha maiti cha Jiji ambako ulitambuliwa Jumatatu.
“Mauaji haya ya kinyama yamepeleka ubaridi hadi kwenye uti wa mgongo wa Wakenya wengi na kuzua dalili za vurugu,” alisema Wanyeki.
Mwanamama huyo alielezea mauaji ya Msando kama tukio la kutisha katika mwaka huu wa uchaguzi lakini alisema siyo tukio pekee lenye uwezekano wa kupandikiza hofu.
“Serikali lazima ichukue hatua madhubuti kutuliza watu na hali hii tete na kuwahakikishia wapigakura kwamba usalama wao ni wa kipaumbele,” alisema.
“Hii ina maana kiundwe chombo huru na madhubuti cha kufanya uchunguzi wa kifo cha Chris Msando na kuwafikisha kortini wote waliohusika.”
Shirika hilo lenye makao yake Uingereza limetoa wito wa chombo huru cha uchunguzi siku mbili baada ya mabalozi wa Marekani na Uingereza kutoa rai kwa serikali kwamba mashirika ya upelelezi ya FBI (Marekani) na Scotland Yard (Uingereza) yanaweza kusaidia katika kazi hiyo.
Aidha, viongozi wa muungano wa upinzani (Nasa) wametoa wito wa kufanyika uchunguzi huru na wameunga mkono mashirika ya FBI na Scotland Yard kuitwa.
Rais Kenyatta
Lakini Rais Uhuru Kenyatta amelitaka Jeshi la Polisi “kuharakisha uchunguzi” wa kifo cha Msando na mwanamke Carol Ngumbu ili kuhakikisha waliohusika wamefikishwa mahakamani.
Kenyatta alisema hayo alipokuwa akihutubia katika mkutano wa kampeni kwenye Uwanja wa 64, jijini Eldoret akiwa na makamu wake William Ruto. Rais alisema ni lazima waliohusika na mauaji hayo wapatikane na kukabiliwa na sheria.
Rais alisema serikali yake “imeshtushwa sana na imesikitishwa” na mauaji ya watu wawili hao. “Chris ni mtu aliyekuwa amejitolea kuitumikia vilivyo nchi na taasisi zake,” alisema katika taarifa ya maandishi juzi.
“Kwa hiyo ni vema kuziacha taasisi kufanya uchunguzi kwa ubora ili kuhakikisha waliohusika na uovu huo wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.”
Kenyatta aliwataka Wakenya kujizuia kueneza uvumi unaoelezea sababu za vifo vya watu wawili hao badala yake wawaache wachunguzi kufunua ukweli.
“Uvumi wa kipuuzi kwa wakati huu wa majonzi utasababisha kazi ya wachunguzi kuwa ngumu na inawaongezea tu uchungu kwa wale waliompenda,” ilisema taarifa hiyo.
Pia, Kenyatta aliagiza makamishna wote wa IEBC wapewe ulinzi wa kutosha muda wote kwa wiki nzima hadi ufanyike Uchaguzi Mkuu. “Wagombea wote wa urais na wagombea wenza wao pia wanahitaji ulinzi ili kuzima kisingizio chochote cha uchaguzi kuahirishwa,” alisema wakati wa kampeni za Jubilee mjini Eldoret, Kaunti ya Uasin Gishu.
Rais alisema hayo huku ikiwa ni siku kadhaa tangu boma la Naibu wake, William Ruto livamiwe na kuzua vita vya risasi za masaa 18, mvamizi