Thursday, August 3

BENKI YA MAENDELEO YA AFRIKA-AfDB YAKUNWA NA VIWANGO VYA UJENZI WA BARABARA MTWARA



Benny Mwaipaja, WFM, Mtwara

BENKI ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), imeelezea kuridhishwa na kasi pamoja na viwango vya miradi ya ujenzi ya barabara inayofadhiliwa na benki hiyo katika Ukanda wa Kusini, na kuahidi kuendelea kushirikiana na Serikali ya Awamu ya Tano ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa na wananchi wake.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo anayesimamia Kanda wa Afrika Mashariki, Dkt. Nyamajeje Weggoro, baada ya kutembelea na kukagua barabara ya Tunduru-Nangaka-Mtambaswala, mkoani Mtwara, yenye urefu wa kilometa 202.2.

Barabara hiyo yenye vipande vitatu imejengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 180 kupitia ufadhili wa benki hiyo kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) na Serikali ya Tanzania. 

Dkt. Weggoro amesema kuwa barabara hiyo ambayo upande mmoja inaunganisha Tanzania na Msumbiji, itachochea maendeleo ya wananchi kutoka pande hizo mbili kwa kusafirisha watu na bidhaa kwa urahisi zaidi.

“Nimeona mabadiliko makubwa sana, si tu kwa barabara, lakini maisha ya watu, mabadiliko ambayo ni dhahiri yanatokana na hii miradi ya barabara ambayo imefungua fursa nyingi za maendeleo, watu wanafanyabiashara lakini pia wanatembeleana!” alisema Dkt. Weggoro.

Alitoa wito kwa Watanzania kuchangamkia fursa ya uwepo wa barabara hizo kujiletea maendeleo kwa kufanyabiashara hivyo kujikwamua kiuchumi.

Mhandisi Heldaus Jerome kutoka Wakala wa Barabara -Tanroads, Makao Makuu, alisema kuwa barabara hiyo ya Tunduru-Mangaka-Mtambaswala, ina vipande vitatu, kutoka Mangaka – Nakapanya (km 70.5), Nakapanya – Tunduru (66.5) na Mangaka – Mtambaswala (km 65.5)

Alifafanua kuwa gharama za ujenzi wa mradi huo, kiasi cha Dola milioni 210, kimetolewa na AfDB (64.79%), Shirika la Maendeleo la Japan-JICA (32.83%) na Serikali ya Tanzania (2.38%) na kwamba Wadau hao pia wanafadhili ujenzi wa barabara kutoka Dodoma-Babati yenye urefu wa kilometa 180.53.

Baadhi ya wakazi wa mji wa Mangaka wilayani Masasi mkoani Mtwara, wameishukuru Serikali kwa kufanikisha ujenzi wa barabara hiyo muhimu kwa uchumi na maisha yao kwa ujumla kwa kurahisisha usafiri na usafirishaji wa abiria na mizigo ndani na nje ya nchi.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kilimanihewa, Bw. Abbas Muhidin Mwira, alisema kuwa maeneo ya Mangaka yamechangamka kibiashara na vijana wengi wamejiajiri wenyewe kwa kufanyabiashara zinazowaingizia kipato huku huduma za usafiri zikiboreshwa baada ya mabasi ya abiria yaendayo mikoani pamoja na malori yanayobeba saruji kutoka Kiwanda cha Saruji cha Dangote-Mtwara kuanza kupita njia hiyo na kusisimua biashara zao.

No comments:

Post a Comment