Wednesday, October 18

Hifadhi ya Amani kuendelea kutambuliwa kimataifa




Muheza. Hifadhi ya Asili ya Amani itaendelea kunufaika na misaada ya kimataifa baada ya Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (Unesco) kuridhia kuendelea kutambuliwa kimataifa.
Kuendelea kutambuliwa kwa hifadhi hiyo kutaiwezesha Tanzania kufungua milango ya ushirikiano wa kimataifa katika masuala ya uhifadhi, ikiwemo kupata watafiti na ongezeko la watalii.
Mhifadhi wa hifadhi hiyo, Mwanaidi Kijazi ametoa taarifa hiyo leo Jumatano Oktoba 18, 2017 kwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigella alipomkabidhi andiko la Unesco la kuridhia kuitambua hifadhi hiyo kwa kipindi cha miaka 10 ijayo.
Uongozi wa hifadhi hiyo kwa kushirikiana na Mkuu wa Mkoa wa Tanga ulipeleka Unesco andiko kuomba kuongezwa muda wa kutambuliwa baada ya awamu ya kwanza iliyoanza mwaka 2000 kufikia tamati.
Kijazi amesema awamu ya kwanza imewezesha mashirika ya kimataifa ya utafiti na kijamii likiwemo Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP) kufadhili miradi ukiwemo wa kupeleka huduma ya maji salama ya bomba katika vijiji vinavyoizunguka hifadhi hiyo.
Mradi mwingine uliotokana na uwepo wa Unesco ni wa ufugaji wa vipepeo ambavyo kabla ya Serikali kupiga marufuku uuzaji wa viumbe hai nje ulikuwa ukiwanufaisha wananchi kwa kujipatia fedha za kigeni kutokana na kupata soko kubwa nchini Marekani.
Amesema hifadhi ina vijiji 72 na misitu 14 ambayo kutokana na tafiti zilizofanyika  baada ya kutambuliwa na Unesco wanavijiji waliweza kuendesha shughuli za kiuchumi badala ya kuharibu mazingira kama ilivyokuwa ikifanyika awali.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa andiko la Unesco, Mkuu wa mkoa Shigella amewahimiza wakazi wa eneo hilo kuwafichua waharibifu wa mazingira.
Amesema Serikali imejipanga kuhakikisha waharibifu wa mazingira wakiwemo wachimbaji wadogo wa dhahabu, wakataji mbao msituni na wanaolima kwenye vyanzo vya maji wanashughulikiwa.


Kuwatelekeza wagonjwa wa akili kunaigharimu jamii yetu


Tupa jicho kando ya barabara fupi ya lami inayotenganisha kituo kikuu cha polisi Bukoba na jengo la Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini(GPSA).
Kuna mtu ameweka makazi kwa zaidi ya mwaka sasa. Iwe mvua au jua, mavazi yake ni yaleyale tangu alipoonekana eneo hili kwa mra ya kwanza. Anakaa kando ya barabara na kuomba chochote kwa wapita njia.
Ukipita karibu yake, utasikia manung’uniko. Anataja kesi mahakamani na muda wote macho anayaelekeza kwa watu wanaoingia na kutoka.
Hakuna anayejua sababu za manung’ung’uniko na za kuchagua kuweka makazi eneo hili. Hakuna anayejua akiwazacho kichwani. Hatujui ni lini akili itamtuma kulipa kisasi dhidi ya binadamu waliomtenga.
Ugonjwa wa akili ni tatizo kubwa katika jamii na ni sehemu ya magojwa yasiyopewa kipaumbele.
Ungekuwa unatiliwa maanani, pengine mganga wa jadi, Jilumba Mabula wa kijiji cha Ididi, Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, asingeuawa wakati akimpatia mgonjwa wake dawa kwa nguvu.
Katika tukio hilo la Februari, 2016 mganga huyo aliuawa baada ya kupigwa kwa jembe kichwani na mgonjwa aliyepelekwa kwa matibabu, kwa kile kilichoaminiwa alikuwa mgonjwa wa akili.
Mgonjwa huyo alipelekwa kwa mganga wa jadi, badala ya hospitali maalumu walipo wagonjwa wa aina hiyo.
Yapo matukio mengi ya kutisha yanayohusishwa na watu wenye matatizo ya afya ya akili. Mwaka 2010 mwanamke katika kijiji cha Kaiwa mkoani Kilimanjaro aliwaua watoto wake watatu kwa shoka.
Aliyekuwa Kamanda wa Polisi wakati huo, Lucas Ng’hoboko alisema uchunguzi ulionyesha mtuhumiwa alikuwa na matatizo ya akili na alipelekwa hospitali ya Mawenzi kwa matibabu.
Ugonjwa wa akili huathiri uwezo wa kufikiri na mhusika kushindwa kudhibiti hisia zake na tabia; mara nyingi hali hiyo huambatana na madhara makubwa.
Ni bahati mbaya kuwa watu wanaojikuta katika hali hii wanabaguliwa, kunyanyaswa kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutengwa.
Mara nyingi hukumu inayotolewa dhidi yao, inajengwa juu ya msingi wa ushirikina na uchawi bila kurejea sababu za kihistoria, kijamii na kisaikolojia.
Huyo anayeonekana kwa zaidi ya mwaka mmoja akinyeshewa mvua na jua kando ya barabara ya polisi mjini Bukoba, ni miongoni mwa maelfu ya wagonjwa wa akili wanaokosa haki zao kama binadamu.
Ana haki ya kupata uangalizi maalumu na matunzo kama inavyotaka Sera ya Afya ya mwaka 2007 na huduma bila malipo kwa wagonjwa wa kundi hilo.
Taarifa iliyotolewa na Serikali wakati wa maadhimisho ya Siku ya Afya ya Akili Duniani mwaka 2015,ilionyesha mwaka 2014/2015 Watanzania 817,532 walikuwa wakiugua magonjwa mbalimbali ya akili.
Mkoa wa Dar es salaam ulitajwa kuongoza kwa idadi kubwa ya wagonjwa ukifuatiwa na Dodoma, huku Mkoa wa Lindi ukiwa na idadi ndogo zaidi.
Kwa mujibu wa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Wazee,na Watoto, Ummy Mwalimu wakati wa hotuba ya Makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2017/2018, bado kuna changamoto ya tatizo la magonjwa ya akili.
Alisema hospitali ya Mirembe iliyopo mkoani Dodoma, imeendelea kutoa tiba kwa wagonjwa wa akili na kawaida ikiwa ni pamoja na wagonjwa wa akili ambao ni wahalifu.
Kundi la wagonjwa wa akili wenye historia ya uhalifu, wanaweza kusababisha madhara makubwa zaidi ikiwa wataachwa bila uangalizi maalumu na kupatiwa matibabu.
Hospitali ya Mirembe kwa miaka minne iliyopita kuanzia mwaka 2012 hadi 2016, imetoa huduma za afya kwa wagonjwa wa akili zaidi ya 60,000 miongoni mwao ni waathirika wa dawa za kulevya.
Mwananchi huyu pamoja na kutia huruma, pia anaturejesha katika tukio la mgonjwa wa aina hiyo aliyevamia gari la aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera John Mongella na kulivunja vioo kwa mawe.
Ni shambulio la Disemba 12, 2014 nje ya ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM)mjini Bukoba. Mongela na wenzake walikuwa wakijiandaa kukagua ujenzi wa maabara.Tiba aliyopewa ni kufungiwa mahabusu mpaka ziara ilipomalizika.
Aidha, tayari tumesahau tukio la Novemba moja,2011 pale mtu aliyetajwa kuwa na tatizo la afya ya akili alipovamia shule ya msingi Kabutaigi wilayani Muleba na kumuua kwa panga Anisia Goodluck aliyekuwa mwanafunzi wa darasa la nne.
Mtuhumiwa huyu aliyeishi na jamii bila matunzo na matibabu sahihi, akahukumiwa kifo kwa kupigwa mawe na wanafunzi wenye hasira.
Phinias Bashaya ni mwandishi wa Mwananchi Kagera.0767489094

MultiChoice yasherehekea bethidei ya miaka 20 Tanzania


Dar es Salaam. Kampuni ya MultiChoice Tanzania inayomiliki king’amuzi cha DStv, imesherehekea miaka 20 tangu ianze kutoa huduma nchini leo Jumatano Oktoba 18,2017.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Meneja Uendeshaji wa kampuni hiyo, Baraka Shelukindo amesema maadhimisho hayo yatajumuisha maonyesho ya siku mbili yatakayofanyika Mlimani City, Oktoba 19 na 20.  
Amesema DStv ilianza na chaneli tatu za SuperSport, M-Net na Movie Magic na leo inajivunia kuwa na zaidi ya chaneli 100 na redio katika vifurushi vya aina mbalimbali.
Mwanahisa wa Multichoice Tanzania na mwenyekiti wa bodi, Balozi Ami Mpungwe amezungumzia maadhimisho hayo akisema, “Multichoice Tanzania imekuwa bingwa katika kutoa burudani za hadhi ya kimataifa kwa Watanzania. Tulianza huduma zetu katika soko hili wakati ambao biashara ya televisheni ilikuwa changa.”
Amesema kampuni hiyo imegusa maisha ya mamilioni ya Watanzania ikitengeneza ajira 100 moja kwa moja kwenye kampuni,  wafungaji wa DStv wa kujitegemea zaidi ya 1,000 na wauzaji wa moja kwa moja takriban 500.

Picha za Lissu mtandaoni zaibua hisia


Dar es Salaam. Picha za Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu zilizoanza kusambaa mitandoni saa kumi jioni leo Jumatano Oktoba 18,2017 zimeibua hisia kutokana na maendeleo ya afya yake.
Lissu ambaye pia ni mwanasheria wa Chadema anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya baada ya kushambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi nyumbani kwake Area D mjini Dodoma, Septemba 7 mwaka huu.
Katika kurasa za kijamii za Mwananchi za Facebook, Twitter na Instagram watu mbalimbali wametoa maoni kuhusu picha hizo, wengi wakionekana kuguswa na maendeleo ya afya yake.
Josephat Mwambola amesema, ‘‘Watu wasiojulikana watambue kuwa Mungu yupo na anawajua ipo siku atawaweka hadharani na kuwaadhibu zaidi ya walivyomuumiza Tundu Lissu ambaye ni mtetezi wa kweli wa wanyonge hapa nchini Tanzania.’’
Babuu Makundi ameandika, “Sifa na utukufu ni kwa Mungu wetu aliye juu Mungu ana makusudi na uhai wa Lissu.”
“Mungu akisema ndiyo hakuna wa kuzuia. Akisema hapana hakuna wa kupinga. Jeshi la mbinguni lilisimama juu yake. Ukimtafakari Mungu. Huwa hachunguziki. Ana makusudi na mwanaye Lissu. Nami nasema asante Yesu,” ameandika Renatha Joely.

TANZANIA YAONGOZA KWA MARADHI YA KIPINDUPINDU




Shirika la Afya Duniani (WHO), imeitaja Tanzania kuwa  miongoni mwa nchi 10 kinara kwa watu wake kuugua ugonjwa wa kipindupindu.
Mataifa  mengine yaliyotajwa ni pamoja na India ambayo ndiyo inayoongoza. Nyingine ni Haiti, Jamhuri  ya  Kidemokrasi  ya  Congo, Tanzania, Bangladesh, Uganda,  Msumbiji na Kenya, ambayo ilikumbwa na mlipuko mkubwa wa maradhi hayo kwa nyakati tofauti mwaka huu.
Katika ripoti yao iliyotolewa hivi majuzi, imesema kuwa sababu kuu ya kuandamwa na maradhi hayo ni kukithiri kwa mazingira machafu katika mataifa hayo.
Ripoti hiyo inasema kuwa watu bilioni 1.2 sawa na moja ya sita ya watu wote duniani wako hatarini kukumbana na maradhi hayo hatari.
Wakati Bara la Afrika likikumbwa na kadhia hiyo kutokana na unywaji wa maji yasiyofaa, hali ni tofauti kwa  Ulaya na Amerika ya Kaskazini ambako mifumo imara ya maji taka imeyafanya mabara hayo yawe huru na kipindipindu kwa miongo mingi sasa.
Lakini watu zaidi ya bilioni mbili wamebakia bila maji safi na mifumo ya maji taka, hivyo, kipindupindu kinaendelea bila huruma kuathiri watu masikini zaidi duniani na ndani ya kila nchi athirika.

TAARIFA YA KUONGEZA MUDA WA UTOAJI WA LESENI ZA MACHAPISHO MBALIMBALI NCHINI

Takukuru Tanzania kuwachukulia hatua wanaoingilia kazi yao

Mkurugenzi wa Takukuru Valentino Mlowola
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Tanzania imesema kuwa kile ambacho Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki, Joshua Nassari anachokiita ni ushahidi, wao wanakiita ni taarifa mpaka pale uchunguzi wao utakapo kamilika.
“…Namuonya ameshatupa taarifa atuache tufanye kazi kwa mujibu wa sheria. Na akiendelea tutamchukulia hatua za kisheria bila kuathiri taarifa alizotuletea,” alisisitiza.
Alitoa onyo hilo pia kwa watu wengine, wanaofikiri kuwa wanaweza kuishinikiza Takukuru na kuiingiza katika masuala ya kisiasa kuwa wakome, kwani inafanya kazi wa mujibu wa taratibu na sheria zilizopo.
“Hiki ni chombo kinachojiendesha kwa mujibu wa sheria, hakishinikizwi wala kuingiliwa na mtu yeyote. Na kinapokea kwa mujibu wa sheria na taratibu taarifa za siri au wazi kutoka kwa mtu yeyote, Nassari anachokiita ushahidi sisi tunakiita taarifa mpaka pale uchunguzi wetu utakapokamilika,” alisisitiza Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru Kamishna Valentino Mlowola.
Vyanzo vya habari nchini humo vimesema kuwa Kamishna alisema mbunge huyo kwa takribani mara tatu alifika katika ofisi za Takukuru na kuwasilisha kile alichokiita ushahidi, lakini mara baada ya kuwasilisha taarifa hizo kwa Takukuru huitisha mkutano wa waandishi wa habari na kuelezea yale yaliyojadiliwa na taasisi hiyo.
Alisema Oktoba 2, mwaka huu, mbunge Nassari akiambatana na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, wote wa Chadema, walifika katika ofisi za Takukuru na kuwasilisha taarifa zao kuhusu matukio ya rushwa yaliyotokea mkoani Arusha.
Alisema Oktoba 14 pamoja na Oktoba 16, mwaka huu, Nassari pia aliwasilisha tena maelezo yake kuhusu suala hilo la rushwa kwa Takukuru na kila alipoondoka alifanya mkutano na waandishi wa habari na kuelezea yaliyojiri wakati akiwasilisha taarifa hizo.
Mkuu wa Takukuru alisema kwa mshtuko taasisi hiyo ilishangaa kuona mbunge huyo na wenzake, wakifanya vikao na waandishi wa habari na kuzungumzia kwa undani yaliyojiri hadi yale ambayo hayakupaswa kuzungumzwa kutokana na kuharibu uchunguzi.
Alisema kazi ya Takukuru ni kupokea taarifa za rushwa na ubadhirifu na kuzifanyia uchunguzi wa kina na ikisha thibitika kuwepo kwa tatizo, hufungua jalada na kuliwasilisha katika ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka kwa ajili ya hatua za kisheria kuchukuliwa.

Maelfu waandamana mjini Barcelona

Maelfu ya watu wameandamana katika mitaa ya Barcelona, Uhispania, baada ya mahakama nchini humo kuamuru viongozi wawili wa jimbo la Catalonia lenye utawala wa ndani kutiwa mbaroni. Catalonia yataka kujitenga.

Spanien Barcelona Demonstration gegen Inhaftierung (-picture alliance/AP Photo/M. Fernandez)
Msemaji wa mji wa Barcelona amesema kiasi ya waandamanaji 200,000 waliokuwa wameshika mishumaa mikononi mwao walisikika wakipaza sauti za kudai uhuru kabla ya kukaa kimya kwa dakika chache.  Maandamano mengine ya watu waliokuwa wameshika mishumaa mikononi yalifanyika katika miji mingine ya jimbo la Catalonia kupinga kushikiliwa kwa viongozi wawili wa jimbo hilo ambao ni Jordi Cuixart na Jordi Sanchez wanaotuhumiwa kwa makosa  ya uchochezi.
Mmmoja wa waandamanaji aliyefahamika kwa jina la Elias Houriz alisikika akisema " Wanataka tuogope ili tusifikirie juu ya uhuru wetu lakini hiyo itakuwa ni kinyume chake kwani tunazidi kuwa na mwamuko kadiri siku zinavyosonga na  mwishoni tutafikia lengo letu" mwisho wa kumnukuu.
Naye kocha wa kilabu ya Manchester City inayoshiriki ligi kuu ya kandanda ya  England, Pep Guardiola anayetokea pia katika jimbo la Catalonia alisema ushindi wa timu yake hapo jana dhidi ya Napoli hapo jana usiku  katika michuano ya kilabu bingwa barani Ulaya ameutoa maalumu kama ishara ya kuwaunga mkono viongozi wawili waliotiwa mbaroni na kutaka waachiwe huru haraka.  Guadiola ambaye amewahi kuinoa kilabu ya Barcelona alisema  utaifa ni muhimu kuliko kitu kingine chochote.
Maandamano hayo ya jana yamefanyika huku muda ukizidi kukaribia kabla ya hapo kesho Alhamisi ambayo ni tarehe iliyowekwa na serikali kuu ya mjini Madrid  inayomtaka kiongozi wa jimbo la Catalonia Carles Puigdemont kutamka wazi iwapo  anakusudia au kutokusudia kutangaza rasmi uhuru wa jimbo la Catalonia kufuatia kura ya maoni iliyofanyika Oktoba 1 ambayo ilipigwa marufuku na serikali ya mjini Madrid kwa maelezo kuwa ni kinyume cha katiba.

Puigbemont ataka majadiliano na Waziri Mkuu Mariano  Rajoy
Spanien Carles Puigdemont Premier der Regionalregierung (Reuters/I. Alvarado)
Kiongozi wa Catalonia ,Carles Puigdemont
Hata hivyo kiongozi huyo amekataa hadi sasa kuitikia mwito huo akimtaka Waziri Mkuu  wa Uhispania Mariano Rajoy kukaa naye pamoja katika meza ya majadiliano jambo ambalo Rajoy hakubaliani nalo hali ambayo inaweza kuzidisha mgogoro wa kisiasa  nchini humo ikiwa ni mara ya kwanza tangu ilipojikomboa kutoka katika utawala wa kiimla mwaka 1977.
Hayo yanajiri huku pia wabunge 50 katika bunge la nchi hiyo wakiwemo wanaotoka katika jimbo la Catalonia wakibeba mabango ndani ya bunge hilo kushinikiza kuachiwa huru viongozi waliotiwa mbaroni wakiwataja kuwa ni wafungwa wa kisiasa.
Wakati huohuo sekta ya utalii ambayo ni moja ya sekta zinazochangia kwa kiwango kikubwa uchumi wa nchi hiyo inaonekana kuathirika  kutokana na kukosekana kwa uthabiti tangu kufanyika kura hiyo ya maoni  hiyo ikiwa ni kwa mujibu wa Waziri Mkuu Mariano Rajoy wakati alipolihutubia bunge la nchi hiyo akitetea hatua ya serikali  yake inayochukua katika kushughulikia mgogoro huo.
Mji wa Barcelona ambao ni mji mkuu wa Catalonia  ni moja  ya miji ambayo inatembelewa na watalii wengi nchini humo kila mwaka.

Roselyn Akombe: IEBC haiwezi kufanya uchaguzi wa haki

Kamishna wa IEBC aliyejiuzulu Roselyn Akombe
Image captionKamishna wa IEBC aliyejiuzulu Roselyn Akombe
Katika taarifa bi Akombe amesema kuwa alifanya uamuzi mgumu kuondoka katika tume hiyo ya uchaguzi Kenya.
Uamuzi wangu wa kuondoka IEBC utawakatisha tamaa baadhi yenu.
Nimejaribu nimewezavyo kulingana na hali ilivyo.
Mara nyengine unaondoka, hususan wakati ambapo maisha ya watu muhimu yamo hatarini.
Tume hii imehusika pakubwa katika mgogoro uliopo.Tume hii imezungukwa.
Tume hii kama ilivyo haiwezi kufanya uchaguzi wa haki mnamo tarehe 26 Oktoba 2017.
Akifanya mahojiano na kipindi cha BBC Newsday Programme, alisema.
''Je utakuwa uchaguzi ulio huru na haki , Kwa kweli haiwezekani''.
Kuna uwezekano mkubwa kwamba makosa yaliofanywa na baadhi ya maafisa waliosimamia uchaguzi katika vituo vya kupigia kura yatarejelewa.
Akizungumza kutoka mjini New York nchini Marekani, alisema kuwa wanachama wa IEBC wamekuwa wakipiga kura kwa upendeleo bila kuzungunmzia maswala tofauti yalio na umuhimu mkubwa.
''Makamishna na maafisa wengine wa IEBC walikuwa wakikabiliwa na vitisho kutoka kwa wanasiasa na waandamanaji '', alisema bi Akombe.
Pia alifichua kwamba yeye mwenyewe amepokea vitisho kadhaa na alishinikizwa kujiuzulu
.''Sijawahi kuwa na hofu kama ile niliyohisi nikiwa katika taifa langu''.
Alisema kuwa hawezi kurudi Kenya katika siku za hivi karibuni kutokana na hofu ya usalama wake.
Kufikia sasa tume ya IEBC haijatoa tamko lolote kuhusu swala hilo.
Kiongozi wa upinzani Raila Odinga alisema wiki iliopita kwamba IEBC haina lengo la kufanyia mabadiliko yoyote operesheni zake wala maafisa wake.
Bwana Odinga amepanga msururu wa maandamano dhidi ya IEBC katika wiki za hivi karibuni.
Wakati huohuo, bwana Kenyatta anasema kuwa yuko tayari kuendelea na uchaguzi mpya kama ulivyopangwa.
''Hatuna tatizo kushiriki katika uchaguzi mpya kama ulivyopangwa.Tuna hakika kwamba tutapata kura nyingi zaidi ya uchaguzi uliopita''.

Kiongozi wa Iran amshutumu vikali Rais Trump kuhusu mkataba ya nyuklia

Iran's Supreme Leader Ayatollah Ali Khamenei gestures as he speaks to students in Tehran on 18 October 2017Haki miliki ya pichaREUTERS
Image captionAyatollah Ali Khamenei said European powers should "avoid intruding into our defensive affairs"
Kiongozi mkuu wa Iran Ayatollha Ali Khamenei, ametetea makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015 na kutumia lugha kali kumkosoa rais wa Marekani Donald Trump kwa kudanganya.
"Sitaki kutupa muda wangu kujibu kuropokwa na kelele za Trump," Ayatollah Ali Khamenei alisema.
Bw. Trump amekataa kuthibitisha kwa bunge la Marekani kuwa Iran imetekeleza yaliyo kwenye mkataba huo.
Amatishia kufuta makubaliano yote ya rais Obama .
Trump alitaka mkataba huo kufanyiwa marekebisho kuizuia Iran kuunda silaha za nyuklia au makombora ya masafa marefu.
Ayatollah Khamenei alisema anakaribisha uungwaji mkono wa mkataba huo kutoka nchi za Ulaya, lakini akaongeza kuwa ikiwa Marekani itavunja makubaliano hayo Iran itayatupilia mbali.
Rais Trump pia aliilaumu Iran kwa kuzua misikusuko nchini Syria, Yemen na Iraq na kukiwekea vikwazo kikosi chenye nguvu nyingi Iran cha Islamic Revolution Guards Corps.
Sasa bunge la Congress litaamua ikiwa litaiwekea tena vikwazo vya kiuchumi, ambavyo viliondolewa kama sehemu ya makubaliano hayo.
Ikiwa hilo litafanyika Marekani itakuwa imekiuka makubaliano kwenye mkataba huo.

Madiwani waliojiuzulu Chadema waanguka kura ya maoni CCM


Arusha. Madiwani watatu wa Chadema waliojiuzulu katika Halmashauri ya Meru mkoani Arusha na kujiunga na CCM, wameangushwa katika kura ya maoni ndani ya chama hicho.
Madiwani hao waliojiuzulu hivi karibuni kwa kile walichoeleza ni kutokana na kuunga mkono jitihada za Rais John Magufuli waliomba kutetea nafasi zao.
Waliogombea na kuangushwa ni Solomon Laizer, aliyekuwa diwani wa Ngabobo, Japhet Jackson (Embuleni) na Anderson Sikawa (Leguruki).
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Meru, Andrew Mungure amesema leo Jumatano Oktoba 18 kuwa, matokeo ya kura ya maoni si mwisho wa uteuzi. Uchaguzi huo ulifanyika jana Jumanne.
Mungure amesema wagombea katika kata hizo watajulikana baada ya vikao ambavyo vimeanza leo.
"Leo wanajadiliwa wagombea wote ngazi ya kata, baadaye tutajadili kamati ya siasa na halmashauri kuu ya mkoa ndipo watapitishwa wagombea," amesema.
Amesema kutokana na mchakato huo, matokeo ya kura ya maoni si mwisho.
Katibu wa CCM Wilaya ya Meru, Aloyce Hayuma amekiri madiwani hao kugombea na kushindwa. Hata hivyo, amesema mchakato unaendelea.

Kampuni ya madini ya Rio Tinto yashtakiwa ulaghai Marekani kuhusu makaa Msumbiji

Coal falls from a conveyor beltHaki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Kampuni kubwa ya uchimbaji wa madini ya Rio Tinto imeshtakiwa kwa tuhuma za ulaghai nchini Marekani pamoja na wakuu watendaji wake wawili wa zamani.
Kesi hiyo inahusu umiliki wa eneo la uchimbaji wa makaa ya mawe ambalo lilinunuliwa na kampuni hiyo, ambayo wamiliki wake ni kutoka Uingereza na Australia, nchini Msumbiji mwaka 2011 kwa karibu dola bilioni nne za Marekani.
Inadaiwa kwamba afisa mkuu mtendaji wa zamani wa kampuni hiyo pamoja na afisa mkuu wa zamani wa kifedha waligundua muda mfupi baada ya ununuzi kwamba eneo hilo lilikuwa na kiwango cha chini ya makaa ya mawe kuliko walivyotarajia lakini walikosa kuwaonya wawekezaji kuhusu hasara iliyotarajiwa.
Eneo hilo la uchimbaji madini baadaye liliuzwa kwa dola milioni hamsini za Marekani pekee.
Thomas Albanese ambaye ni afisa mkuu mtendaji wa zamani wa Rio TintoHaki miliki ya pichaAFP
Image captionThomas Albanese ambaye ni afisa mkuu mtendaji wa zamani wa Rio Tinto
Kampuni hiyo imekanusha tuhuma hizo na inasema kwamba itatetea kwa hali na mali sifa zake nzuri.
Rio Tinto pia ilitozwa faini ya £27m na serikali ya Uingereza kwa kukiuka sheria za kuweka wazi shughuli za kibiashara wakati wa ununuzi huo.
Kampuni hiyo ilikubali kulipa faini hiyo, ambayo ni ya juu zaidi kuwahi kutozwa kampuni Uingereza kuhusiana na makosa ya ufichuzi wa shughuli za kibiashara.

Uhispania yatoa vitisho kwa Catalonia huku mzozo wa uhuru ukiendelea

Spain's deputy prime minister Soraya Saenz de Santamaria speaks during a news conference at the Moncloa Palace in Madrid, Spain, 16 October 2017Haki miliki ya pichaREUTERS
Image captionSoraya Sáenz de Santamaría alitoa onyo siku moja moja kabla ya siku aliyopewa Carles Puigdemont, kumalizika
Uhispania itachukua hatua za kufutilia mbali utawala wa Catalonia ikiwa kiongozi wake hataachana na hatua za kutafua uhuru, naibu waziri mkuu amesema.
Soraya Sáenz de Santamaría alitoa onyo siku moja moja kabla ya siku aliyopewa Carles Puigdemont, kumalizika.
Serikali ya Catalonia imesisitiza kuwa haiwezi kutekeleza matakwa ya Madrid baada ya kura iliyokumbwa na utata ya Catalonia.
Kumekuwa na maandamano kupinga kuzuiwa kwa viongozi wa vugugu la Catalonia.
Jordi Sánchez na Jordi Cuixart wanazuiliwa huku wakichunguzwa kwa uhaini - hatua ambayo upande ambao unataka uhuru unaiona kuwa iliochochewa kisiasa.
Wanaume hao walikuwa viongozi wakuu kwenye kura ya uhuru ya Oktoba mosi, ambayo Uhispania ilitaja kuwa iliyo kinyume na sheria
Waziri mkuu wa Uhispania Mariano Rajoy, anajaribu kuchukua tahadhari lakini suala kuwa yeye na serikali yake wanajaribu kufuta utawala wa Catalonia ni ishara ya jinsi uhusiano umedhoofika.
Hata hivyo kiongozi wa Catalonia Carles Puigdemont yuko chini ya shinikizo kutoka kwa watu wenye ushawishi wanaotaka ashinikize zaidi uhuru.
Pia kuna shinikizo kutoka kwa wafuasi wa Rajoy na washirika kuwa za kumtaka achukue hatua mara moja na kutekeleza kipengee cha 155 cha katiba mara baada ya siku ya Alhamisi.

Rais Kenyatta aitisha maombi kabla ya marudio ya Uchaguzi

Rais Kenyatta aitisha maombi kabla ya marudio ya UchaguziHaki miliki ya pichaAFP
Image captionRais Kenyatta aitisha maombi kabla ya marudio ya Uchaguzi
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ametangaza kuwa nchi itafanya maombi mwisho wa wiki hii kabla ya marudio ya uchaguzi mkuu wa wiki ijayo.
Taarifa ya Rais Kenyatta ilikuja baada ya afisa wa cheo ya juu kwenye tume ya uchaguzi nchini Kenya, kukimbia nchi akisema kuwa amekuwa akipokea vitisho vya kuuawa.
Roselyne Akombe aliiambia BBC kuwa marudio ya uchaguzi, hayaafikii matarajio ya uchaguzi ulio huru na wa haki.
Bw. Kenyatta alisema kuwa wakenya watatumia wikendi kwa maombi na maridhiano kabla ya marudio ya uchaguzi wa urais ambao utafanyika tarehe 26 mwezi Oktoba.
Mpinzani wake mkuu Raila Odinga alijiondoa kutoka kwa uchaguzi huo wiki iliyopita.
Hata hivyo Rais Kenyatta hakuzungumzia kujiuzulu kwa Bi Akombe.

RAIS DKT MAGUFULI AKUTANA NA WAZIRI WA MAFUTA NA GESI WA OMAN MHE. DKT MOHAMED HAMAD Al RUMHY

Mfalme wa Oman Mtukufu Sayyid Qaboos bin Said Al Said amemhakikishia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kuwa nchi hiyo ipo tayari kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuongeza uwekezaji katika viwanda, uzalishaji wa nishati, kuongeza thamani ya madini, kuendeleza sekta ya gesi na mafuta na kuendeleza ukanda wa uwekezaji wa Bagamoyo ili kukuza uchumi kwa kasi zaidi.


Ujumbe huu wa Mfalme wa Oman umewasilishwa kwa Mhe. Rais Magufuli na Waziri wa Mafuta na Gesi wa Oman Mhe. Dkt. Mohammed Hamad Al Rumhy aliyeongozana na Waziri wa Uwekezaji wa Oman Mhe. Salem Ben Nasser Al Ismaily na Naibu Waziri wa Utalii Mhe. Maitha Saif Majid, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Dkt. Rumhy ambaye ameongoza watu zaidi 300 waliokuja nchini kwa meli ya Mfalme wa Oman amesema ziara hii imelenga kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na Oman hususani katika masuala ya uchumi, ambapo Oman inabadilishana uzoefu na Tanzania kuhusu biashara ya mafuta na gesi, itajenga kiwanda kikubwa cha kuzalisha mbolea katika ukanda wa uwekezaji wa Bagamoyo, itajenga viwanda vya mazao na kununua mazao ya wakulima na itawekeza katika uchakataji wa madini ili kuongeza thamani.

“Mhe. Rais tunataka kushirikiana nanyi kuendeleza ukanda wa uwekezaji wa Bagamoyo, tunataka Bagamoyo isiwe eneo la bandari tu, bali pia liwe ni eneo ambalo tutajenga viwanda mbalimbali, tuzalishe mbolea na tununue mazao ya wakulima na kuyasafirisha, sisi tupo tayari na kesho tunakwenda kuangalia eneo hilo ili kazi zianze mara moja” amesema Dkt. Rumhy. Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mfalme wa Oman Mtukufu Sayyid Qaboos bin Said Al Said kwa kutuma ujumbe huo na amemhakikishia kuwa Tanzania ipo tayari kuendeleza na kukuza zaidi uhusiano wake na Oman.

Mhe. Rais Magufuli amemtaka Dkt. Rumhy kufikisha ujumbe wake kwa Mfalme na wawekezaji wa Oman kuwa atafurahi kuona uwekezaji huo unaanza mara moja na kwamba Serikali itatoa ushirikiano wowote utakaohitajika kwa manufaa ya pande zote mbili.

“Mhe. Dkt. Mohamed naomba ukamwambie Mfalme kuwa namshukuru kwa ujumbe huu na namkaribisha sana Tanzania, nimefurahi kuona mpo tayari kushirikiana nasi kujenga viwanda, kuzalisha mazao na kuendeleza ukanda wa uwekezaji wa Bagamoyo, sisi tupo tayari hata leo, njooni tushirikiane kwa sababu nyinyi ni ndugu zetu na tutafanya uwekezaji kwa faida yetu sote” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli ametaka Oman iongeze ushirikiano na Tanzania katika masuala ya utalii na usafiri wa anga, kuwekeza katika usindikaji wa nyama na uvuvi na ushirikiano katika kubadilishana wataalamu wa nyanja mbalimbali wakiwemo walimu wa lugha ya Kiswahili na Kiarabu.

Amemshukuru Mfalme wa Oman kwa msaada kujenga visima vya maji 100 hapa nchini na amemuomba kuungana na Serikali katika safari yake ya kuhamia Dodoma kwa kujenga miundombinu itakayoweka kumbukumbu ya ushirikiano wa kidugu na kihistoria kati ya nchi hizi mbili. Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Medard Matogoro Kalemani na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Suzan Alphonce Kolimba.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
18 Oktoba, 2017
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Waziri wa Mafuta na Gesi wa Oman Dkt. Mohamed Hamad Al Rumhy alipokutana na kufanya naye mazungumzo Ikulu jijini Dar es salaam leo Oktoba 18, 2017.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Waziri wa Uwekezaji wa Oman Mhe. Salem Ben Nasser Al Ismaily aliyeongozana na Waziri wa Mafuta na Gesi wa Oman Dkt. Mohamed Hamad Al Rumhy alipokutana na kufanya nao mazungumzo Ikulu jijini Dar es salaam leo Oktoba 18, 2017.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Naibu Waziri wa Utalii Mhe. Maitha Saif Majid aliefuatana na Waziri wa Mafuta na Gesi wa Oman Dkt. Mohamed Hamad Al Rumhy walipokutana na kufanya mazungumzo Ikulu jijini Dar es salaam leo Oktoba 18, 2017.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Balozi wa Oman nchini Mhe.Ali A. Al Mahruqi aliyefuatana na Waziri wa Mafuta na Gesi wa Oman Dkt. Mohamed Hamad Al Rumhy alipokutana na kufanya naye mazungumzo Ikulu jijini Dar es salaam leo Oktoba 18, 2017.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika mazungumzo na Waziri wa Mafuta na Gesi wa Oman Dkt. Mohamed Hamad Al Rumhy alipokutana na kufanya naye mazungumzo Ikulu jijini Dar es salaam leo Oktoba 18, 2017.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli katika picha ya kumbukumbu na Waziri wa Mafuta na Gesi wa Oman Dkt. Mohamed Hamad Al Rumhy na ujumbe wake baada ya kukutana na kufanya naye mazungumzo Ikulu jijini Dar es salaam leo Oktoba 18, 2017
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimsiliza Waziri wa Mafuta na Gesi wa Oman Dkt. Mohamed Hamad Al Rumhy akiongea na wanahabari baada ya kukutana na kufanya naye mazungumzo Ikulu jijini Dar es salaam leo Oktoba 18, 2017.