Wednesday, October 18

Hifadhi ya Amani kuendelea kutambuliwa kimataifa




Muheza. Hifadhi ya Asili ya Amani itaendelea kunufaika na misaada ya kimataifa baada ya Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (Unesco) kuridhia kuendelea kutambuliwa kimataifa.
Kuendelea kutambuliwa kwa hifadhi hiyo kutaiwezesha Tanzania kufungua milango ya ushirikiano wa kimataifa katika masuala ya uhifadhi, ikiwemo kupata watafiti na ongezeko la watalii.
Mhifadhi wa hifadhi hiyo, Mwanaidi Kijazi ametoa taarifa hiyo leo Jumatano Oktoba 18, 2017 kwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigella alipomkabidhi andiko la Unesco la kuridhia kuitambua hifadhi hiyo kwa kipindi cha miaka 10 ijayo.
Uongozi wa hifadhi hiyo kwa kushirikiana na Mkuu wa Mkoa wa Tanga ulipeleka Unesco andiko kuomba kuongezwa muda wa kutambuliwa baada ya awamu ya kwanza iliyoanza mwaka 2000 kufikia tamati.
Kijazi amesema awamu ya kwanza imewezesha mashirika ya kimataifa ya utafiti na kijamii likiwemo Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP) kufadhili miradi ukiwemo wa kupeleka huduma ya maji salama ya bomba katika vijiji vinavyoizunguka hifadhi hiyo.
Mradi mwingine uliotokana na uwepo wa Unesco ni wa ufugaji wa vipepeo ambavyo kabla ya Serikali kupiga marufuku uuzaji wa viumbe hai nje ulikuwa ukiwanufaisha wananchi kwa kujipatia fedha za kigeni kutokana na kupata soko kubwa nchini Marekani.
Amesema hifadhi ina vijiji 72 na misitu 14 ambayo kutokana na tafiti zilizofanyika  baada ya kutambuliwa na Unesco wanavijiji waliweza kuendesha shughuli za kiuchumi badala ya kuharibu mazingira kama ilivyokuwa ikifanyika awali.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa andiko la Unesco, Mkuu wa mkoa Shigella amewahimiza wakazi wa eneo hilo kuwafichua waharibifu wa mazingira.
Amesema Serikali imejipanga kuhakikisha waharibifu wa mazingira wakiwemo wachimbaji wadogo wa dhahabu, wakataji mbao msituni na wanaolima kwenye vyanzo vya maji wanashughulikiwa.


No comments:

Post a Comment