Saturday, May 25

Uhasama kati ya polisi, raia Mtwara


Hali ya uhasama imeibuka kati ya polisi na raia mkoani Mtwara, kila upande ukilalamika kuhujumiwa huku hali ikiendelea kuwa tete, ambapo Jeshi la Polisi nchini limetangaza kukamatwa kwa mtu anayetuhumiwa kueneza ujumbe wa uchochezi kwa kutumia simu ya mkononi.

Barabara nyingi za mjini Mtwara ziko tupu, huku magari ya Jeshi la Wananchi na polisi yakiranda randa kuhakikisha usalama, huku maduka na biashara nyingine zikiendelea kufungwa.

Wakati uhasama huo ukiendendelea, taarifa zinaeleza kuwa vifo vimeongezeka na kufikia watu watatu, huku Mkuu wa Mkoa Kanali Mstaafu Joseph Simbakalia, akisisitiza kuwa na taarifa rasmi ya kifo kimoja tu.

“Mpaka sasa tuna taarifa ya kifo kimoja tu kupitia utaratibu rasmi, kama kuna wengine wamekufa basi mtuletee taarifa kwa kufuata utaratibu,” alisema Simbakalia.

Hata hivyo, taarifa za wananchi zilisema kuwa watu wengine watatu walikufa kwa kupigwa risasi katika maeneo ya Mikindani, huku baadhi ya wanawake wakidai kubakwa na polisi.

Wakati hayo yakiendelea, Jeshi la Polisi nchini limetangaza kumshikilia mtu mmoja (jina limehifadhiwa) kwa tuhuma za kueneza ujumbe wa uchochezi na chuki kwa wananchi na viongozi wa Serikali kwa kutumia simu ya mkononi.

Taarifa ya jeshi hilo iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari imeeleza kuwa meseji hizo zinaenezwa kwa lengo la kuchochea fujo, vurugu na kutoa matusi kwa wananchi na viongozi wa Serikali.

Msemaji wa jeshi hilo, Advera Senso alisema jana kuwa mtu huyo amekuwa akifanikisha kazi hiyo kwa kutumia kadi 13 tofauti za simu za mkononi.

“Alikamatwa akiwa na kadi 13 tofauti za simu za mkononi, polisi bado inaendelea kumhoji mtu huyo na ushahidi utakapokamilika atafikishwa mahakamani,” alisema Senso na kuongeza:

“Kwa muda mrefu sasa watu wa kada mbalimbali nchini wamekuwa wakitumiwa ujumbe mfupi wa maneno katika simu zao, unaohamasisha vurugu na uchochezi wa kidini, huku baadhi ya wananchi wakizitupia lawama mamlaka husika kwa kushindwa kudhibiti hali hiyo.”

Jeshi hilo limewataka wananchi wenye taarifa mbalimbali za wahalifu kama hao kujitokeza na kutoa taarifa hizo, ili wanaotuhumiwa wasakwe na kukamatwa ikiwa ni pamoja na kuchukuliwa hatua stahiki.

Wakizungumza wakati wa ziara ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi, wananchi wengi wamelilalamikia Jeshi la Polisi kwa kutumia nguvu kubwa katika utulizaji wa ghasia na kusababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali.

Wakati Waziri Nchimbi akifanya ziara hiyo Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha naye alitua mkoani humo na kusisitiza ulinzi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Akizungumza mbele ya Waziri Nchimbi, Diwani wa Kata ya Magengeni Tarafa ya Mikindani, Omar Nawatuwangu alisema, licha ya wananchi kufanya vurugu, Jeshi la Polisi lilijibu kwa kujeruhi watu na kuchoma nyumba.

“Hali hapa siyo shwari, ni kweli wananchi wamefanya vurugu lakini askari hawa tunaotegemea watatulinda, ndiyo wamechoma nyumba za watu na kujeruhi watu kwa risasi,” alidai Nawatuwangu.

Naye Issa Nambanga wa Mikindani alidai kuwa aliwaona askari waliokuwa na bunduki wakichoma nyumba ya jirani yake. “Mimi niliwaona askari wakichukua mali za jirani yangu na baadaye kuichoma moto nyumba yake. Nilishindwa la kusema kwa kuwa niliwaogopa askari hao,” alisema Nambanga.

Kwa upande wake Mariam Abdallah ambaye ni mjane mwenye watoto watatu, alilalamika kuchomewa nyumba na vyombo vyote alivyokuwa navyo.

“Juzi usiku (Mei 22), polisi walikuja na gari lao na kulisimamisha mbele ya nyumba yangu. Nilimwona polisi wa kike akinitaka nitoke nje na watoto wangu, kisha akawasha kiberiti na kuichoma nyumba yangu. Sina chochote nilichookoa na hapa sijui nitaanzia wapi, sina kazi, hata jembe ninalolimia wamelichoma,” alisema.

Waziri Nchimbi alitembelea pia askari waliochomewa nyumba zao huku akimtaka Kamanda wa Polisi mkoani humo, Linus Sinzumwa awasake wote waliohusika na uhalifu huo. Wakizungumzia tukio hilo, baadhi ya askari waliochomewa nyumba, walisema kuwa hali hiyo inaonyesha uhasama uliopo kati yao na raia.

“Siku zote nimeishi hapa na wananchi hata wengine nilikuwa nikiwapa kazi ya ujenzi, lakini katika vurugu za juzi, nilishangaa tu watu wanavamia nyumba yangu na kuichoma moto. Mke na watoto wangu walikimbia kujificha kwa jirani,” alisema Sajini Fakih Sajih anayeishi Kata ya Chikongola.

Wengine waliokumbwa na zahama ya kuchomewa nyumba ni pamoja na mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), Kassim Likongolo na mkewe Koplo Fatuma na Koplo Philemon Yatitu.

Mbali na askari hao, waandamanaji pia walichoma ofisi ya CCM, Kata ya Chikongola na ofisi ndogo ya Mbunge iliyopo Mikindani.

Kauli ya Mkuu wa Mkoa

Akizungumzia malalamiko ya wananchi Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali mstaafu Joseph Simbakalia, alikiri kupokea malalamiko ya wananchi na kusema kuwa askari waliohusika na vitendo hivyo wakibainika watawajibishwa kijeshi.

“Malalamiko ya wananchi tumeanza kuyapokea, yatachunguzwa na kama yatabainika kuwa ya kweli askari watachukuliwa hatua za kijeshi,” alisema Simbakalia.

Akizungumzia mfululizo wa vurugu hizo tangu zilipoanza Desemba mwaka 2012, Simbakalia alisema hazina uhusiano na suala la gesi bali ni hujuma dhidi ya maendeleo.

“Ni kweli tulianza kuona viashiria mapema kwa kuwepo vipeperushi na ujumbe wa simu, ndiyo maana tuliweka ulinzi mkali wa polisi. Hali ilipozidi kuwa mbaya, kwa kutumia utaratibu wa kisheria, kama mkuu wa mkoa nikaomba kuongezewa nguvu za kijeshi,” alisema Simbakalia.

Hata hivyo, Simbakalia alishindwa kueleza hatua zilizochukuliwa kwa watu hao tangu vurugu hizo zilipoanza mwishoni mwa mwaka jana, licha ya kukamata zaidi ya watu 90 katika vurugu za sasa.

Vurugu Msimbati

Ghasia zimezuka katika Kijiji cha Msimbati inapochimbwa gesi asilia, ambapo watu wasiojulikana wamechoma moto Ofisi ya Hifadhi ya Bahari jana usiku.

Habari zinasema tukio hilo limetokea kati ya saa 4 na 5 usiku na kwamba polisi waliingia kijijini hapo usiku huo kutuliza ghasia. Mkuu wa Mkoa, Simbakalia amethibitisha kutokea kwa vurugu hizo.

Kauli ya Waziri Nahodha

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Mtwara, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha alitetea uamuzi wa kuleta Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) Mtwara kwa lengo la kulinda amani.

“Kwa mujibu wa Katiba, tumepewa dhamana ya kulinda wananchi dhidi ya maadui wa ndani na nje hivyo ni wajibu wetu wa msingi inapotokea haja ya kufanya hivyo,” alisema Nahodha.

Alizungumzia pia ajali ya gari la jeshi wilayani Nachingwea mkoani Lindi na kusababisha vifo vya wanajeshi wanne, alisema kuwa vimewasikitisha na majeruhi watapelekwa Dar es Salaam kutibiwa.

“Kwa hiyo wale wenzetu waliopoteza maisha damu yao haikumwagika bure, walikuwa katika kutimiza wajibu wao kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wamepotea wakiwa katika harakati za kuleta amani.”

Kiama hiki cha gesi Mtwara kisiigawe Tanzania - GAZETI MWANANCHI



Licha ya utajiri huo mkubwa unaweza kujiuliza, je, ni kwanini bara hili limeendelea kuwa maskini kwa miaka mingi huku likikabiliwa na mizozo mingi na migogoro kuhusu mgawanyiko wa rasilimali hizi.

Jiulize, leo ikiwa ni miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), sasa Umoja wa Afrika (AU), kwanini bara hili tajiri kiasi hiki bado linatajwa kuwa maskini pengine kuliko mabara mengine duniani?

Tunaambiwa, Afrika ina asilimia kubwa ya madini, lakini, jiulize, kwa nini asilimia kubwa ya madini hayo haitumiwi vizuri au kikamilifu katika kuliinua bara hili. Kwanini hayalisaidii bara hili?

Kwa kutaja machache, Afrika ni tajiri kwa madini kama vile, almasi, dhahabu, shaba urani na mengine mengi.

Bara hilo linajivunia asilimia 40 ya umeme wa nguvu za maji unaopatikana duniani, linazalisha madini mengine kama chromium, asilimia 30 ya uranium na asilimia 50 ya dhahabu inayopatikana kote duniani.

Pia, asilimia 90 ya cobalt, asilimia 50 ya phosphates, asilimia 40 platinum, asilimia 7.5 au zaidi ya makaa ya mawe, asilimia 8 ya petroli na bidhaa zake, asilimia 12 ya gesi asilia, asilimia 3 ya madini ya chuma na mamilioni ya ekari za ardhi nzuri na inayofaa kwa kilimo cha mazao mbalimbali yakiwamo ya chakula, biashara ambayo ni mengi mno kuyataja.

Pia, bara hili linayo mito, maziwa, bahari ambako kwa kiasi kikubwa wanapatikana samaki wengi na wa aina mbalimbali wakiwamo hata wale wenye bei kubwa katika soko la dunia.

Pia, Afrika inavyo vitu vingine vingi kama mbuga za wanyama ambazo zimejaa tele, zinavutia watalii wengi, ambao huongeza fedha za kigeni, lakini mbona havijaweza kulisaidia bara hili kuondokana na lindi hili la umaskini?

Huenda ni bahati mbaya kwamba mgawanyo usiyo sahihi au sawa kwa rasilimali hizi, ulafi wa baadhi ya viongozi, hasa wale waliokabidhiwa jukumu la kusimamia idara au taasisi zinazoshughulikia uchimbaji, usambazaji wake na usiri mkubwa katika mikataba.

Kutokana na usimamizi duni wa rasilimali hizi zinaweza kuwa baadhi ya sababu za kuzuka kwa mizozo hii mikubwa ambayo inalikumba bara hili, kama ambavyo inaanza kuzuka Tanzania.

Rais Yoweri Museveni wa Uganda katika moja ya hotuba zake mwaka jana wakati akizindua mradi wa kuchimba mafuta katika Ziwa Natron nchini mwake alieleza mengi kuhusu rasilimali hizi na jinsi zinavyoweza kuigawa nchi na Afrika kwa jumla.
Dar es Salaam. Bara la Afrika kwa hakika limebarikiwa kuwa na rasilimali lukuki ambazo ni lulu katika kukuza uchumi.

“Tunafurahi kuwa tunayo mafuta hapa, hii ni rasilimali ambayo haina budi kutuunganisha zaidi sisi (Waganda) badala ya kutugawa,” alieleza Museveni mbele ya wageni, wenyeji na wawekezaji kutoka China ambao wanashiriki katika mradi huo.

Rasilimali hizi nyingi zinapatikana katika Afrika ikiwamo Tanzania ambako imegunduliwa gesi asilia kiasi cha trilioni 41 futi za ujazo kule Mtwara na Lindi.

Kwa bahati mbaya, rasilimali hii imeanza kuimega tunu ya amani, utulivu ambayo nchi yetu ilijaliwa kuwa nayo kwa muda mrefu na sasa ni dhahiri inaweza kuigawa nchi.

Upo ushahidi wa jinsi ambavyo Muungano wa Tanzania, uliotokana na kuungana kwa Tanganyika na Zanzibar kwa siku za karibuni umekuwa ukitiwa majaribuni, kisa ni hisia za kugundulika au kupatikana kwa mafuta kule Pemba au kwingineko katika bahari kuu.

Huu ni mtihani mkubwa ambao matukio haya ya Mtwara yanasababisha wananchi kuamini kuwa gesi inaweza kuwakomboa kutoka katika lindi la umaskini tena kwa haraka bila kuwashirikisha wenzao wa maeneo mengine ya nchi. Huu ni mtihani ambao nchi inatakiwa kuushinda, lakini kwanza inatakiwa kuwa makini.

Kauli za ubabe au vitisho dhidi ya wananchi hao, ziwe kutoka kwa viongozi wetu kama wa Wizara ya Nishati na Madini, chini ya Profesa Sospeter Muhongo na wasaidizi wake, George Simbachawene na Stephen Masele, hazifai.

Pia, kwa kuwa Rais Jakaya Kikwete ndiye amepewa mamlaka na katiba yetu kusimamia mgawanyo huu wa rasilimali, hana budi naye kuchukua hatua sasa, wala si kusubiri wananchi waanze kukumbatia kile kinachozalishwa kwao, kwa maslahi yao.

Ni wazi kwamba kama kuna wanasiasa, kundi la wanaharakati wanaodhani kuwa watafanikiwa kuwatumia wananchi wa Mtwara kudai gesi ibaki ili wapate maendeleo, wanapaswa kujitazama upya.

Ni wazi kwamba gesi inataka uwekezaji mkubwa, inataka masoko ya uhakika, ambayo yanaweza kuwa mbali ya eneo lao, ilimradi wao wahakikishiwe huduma zote muhimu za jamii kama shule, zahanati, barabara nzuri na kadhalika.

Hakuna shaka kwamba huu ni mradi mkubwa ambao Tanzania kama nchi haikuwahi kuwekeza, lakini pia ni mtihani ambao Serikali ya awamu ya nne, chini ya uongozi wa Rais Kikwete na wenzake wote hawana budi kujifunza kutoka yaliyotokea kwingineko.

Afrika, imeshuhudia nchi iliyokuwa kubwa kieneo, Sudan imegawanyika na mojawapo ya sababu ni mgawanyo wa rasilimali, mafuta na sasa imeparaganyika na kubakia mataifa mawili, Sudan na Sudan Kusini, ambazo zote hazijiwezi kiuchumi.

Kumbukumbu za Nigeria na mizozo kule Niger Delta ni ushahidi mwingine wa jinsi ambavyo bila umakini, nchi inaweza kuingia katika vita.

Miundombinu iliyogharimu kiasi kikubwa cha fedha imekuwa ikichezewa, kuharibiwa karibu kila mwaka kule Nigeria ambako nchi imepata hasara, wananchi wamepoteza maisha, jambo ambalo linapaswa kuepukwa kwa gharama zozote zile, kwani nafasi bado ipo ya kuweza kufanya hivyo.

Kwa mfano, mzozo baina ya Nigeria na Cameroon ambazo awali ziliingia kwenye mzozo mkubwa zikigombea rasi ya Bakassi yenye mafuta, hadi jumuiya ya kimaifa imelazimika kuingilia kati, sote tumeona. Je, tumepata fundisho gani kuhusu rasilimali na jinsi zinavyoweza kuwa sababu na chanzo cha mizozo na migogoro?

Kumbukumbu zetu kule Bungeni mjini Dodoma zinatuonyesha kuwa hivi karibuni kuwa wabunge walijadili rasimu ya sera ya gesi na wengi walionekana kuwa na wasiwasi kuhusu ugawaji wa rasilimali hiyo ndani na kwa wageni.

Wabunge wengi walitaka mikataba iwekwe wazi kwa viongozi na wananchi wote ambao kimantiki gesi hiyo ni mali yao.

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe(Chadema ) alitaka vitalu vya gesi visiuzwe mapema kwa wawekezaji hadi pale sheria rasmi ya gesi itakapokamilika.

Hata hivyo, Profesa Muhongo alisema serikali iliamua kuanza uuzaji wa vitalu hivyo ili isiwe nyuma katika soko la dunia la nishati.

“Hatuna haja ya kubaki nyuma, tukichelewa katika hili tunaweza kukosa fursa kwani nchi nyingine zinazonunua gesi zipo katika mchakato wa kutafuta mbinu mbadala za nishati hiyo” alisema Profesa Muhongo.

Ni dhahiri kwamba hili la Mtwara linaweza kuichelewesha Tanzania, hasa wakati huu ambao jirani zetu, Msumbiji wamewekeza katika gesi kwa kiasi kikubwa.

Ushauri hapa ni kuwa busara zaidi itumike, pande zote ili zichume na kuvuna kutoka kwenye gesi asilia ya Mtwara hadi bomba litakapojengwa, viwanda kama kile cha saruji, wananchi wanufaike, serikali ikusanye kodi, ambazo hatimaye zitasaidia kukuza uchumi.

Inawezekana kuwa hiki kinachotokea kule Mtwara, bila umakini kinaweza pia kuibuka Ruvuma au hata Manyoni (Singida) ambako pia imegundulika urani, madini mengine ambayo pia yameanza kuzua mijadala na mizozo mingi ikiwamo ile ya kimazingira.

Kuna madini aina ya nickel kule Kabanga, Ngara Mkoani Kagera, ambayo pia yana thamani kubwa na ambayo pia yanaweza kuzua mzozo mwingine. Kama nchi, tujihadhari, tujaribu kuwa makini!

Sakata la gesi Mtwara: Wabunge CCM wacharuka


Dodoma. Wabunge wa CCM wamekuja juu na kumtaka Rais Jakaya Kikwete kuwafukuza kazi vigogo wa Serikali mkoani Mtwara, wakiwamo Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya kutokana na kile walichoeleza ni uzembe uliochangia vurugu zinazoendelea za wananchi kugomea gesi kutoka nje ya mkoa huo.

Wengine waliopendekezwa kuchukuliwa hatua ni kamati nzima ya ulinzi na usalama ya ngazi ya mkoa na wilaya ya Mtwara mjini, wakiwamo makamanda wa polisi.

Kutokana na hali hiyo, vigogo kadhaa mkoani humo wako hatarini kukumbwa na ghadhabu hiyo akiwamo Mkuu wa vikosi vya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Mkuu wa mgambo na Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Wabunge hao walikuwa wakitoa mapendekezo hayo kwenye kikao cha Kamati ya Wabunge wa CCM iliyofanya kikao cha dharura juzi usiku, mjini hapa.

Kikao hicho kiliongozwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, huku Spika wa Bunge, Anne Makinda ambaye wakati huo alikuwa kwenye kikao cha Kamati ya Uongozi wa Bunge, aliwakilishwa na Mwenyekiti wa Bunge, Jenista Mhagama.

Katika kikao hicho maalumu kilichokusudia kutoa ushauri kwa Rais Kikwete juu ya njia mwafaka ya kutatua hali ya machafuko, wabunge wengi wali kukasirishwa na jinsi hali ilivyo mkoani Mtwara. Chanzo chetu kwenye kikao hicho kilieleza kuwa wabunge hao walichukizwa na jinsi Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya walivyokuwa wakipingana kimsimamo. Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Joseph Simbakalila, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mjini, Wilman Ndile na Kamanda wa Polisi Mkoa Linus Sinzumwa wamehusishwa.

Licha ya baadaye kuonekana kuwa kitu kimoja, wabunge hao walidai kuwa walishindwa kutumia nafasi zao katika kutatua tatizo hilo, ambalo hadi juzi Serikali ilisema walikuwa wamekufa watu watano, wakiwamo wanajeshi wa JWTZ waliofariki katika ajali wakati wakienda kutuliza machafuko.

Chanzo hicho kilieleza kuwa iwapo mapendekezo ya wabunge hao yatapelekwa kwa Rais Kikwete kama michango ya wabunge hao ilivyokuwa, huenda rungu likawaangukia pia viongozi wa kisiasa wa CCM mkoani humo. Miongoni mwa wanasiasa hao, chanzo hicho kimesema ni wale waliotoa kauli za waziwazi kuunga mkono msimamo wa kutoruhusu gesi kusafirishwa nje ya mkoa huo.

“Hapa wapo wabunge, madiwani na viongozi wa ngazi mbalimbali wa CCM,” kilieleza chanzo hicho.

Hata hivyo, baadhi ya wabunge walipendekeza mkakati wa kutatua uzembe uliofanyika Mtwara, unapaswa kuchukuliwa kwa uangalifu usije ukasababisha madhara mengine kwa Chama na Serikali.

Walisema suala hilo halina budi kuchukuliwa kwa uangalifu hasa ikizingatiwa kuwa Chama cha CUF ndicho chenye nguvu mkoani humo ukilinganisha na vyama vingine vya upinzani.

Wabunge hao walikituhumu chama hicho kuwa kimekuwa kikijaribu kutumia vurugu hizo kama kigezo cha ushawishi wa kukubalika mkoani humo.

Taarifa zilizopatikana jana mjini hapa zimeeleza kuwa tayari maazimio ya wabunge hao wa CCM yamewasilishwa kwa Rais Kikwete.

Taarifa ambazo hazijathibitishwa pia zinaeleza kuwa leo Kamati ya Uongozi ya Bunge huenda ikatangaza Bungeni maazimio yao kuhusu vurugu za Mtwara.

Kamati ya Uongozi ilianza kukutana kuanzia Jumatano jioni na hadi jana wajumbe walikuwa wamejifungia wakijadili namna wanavyoweza kushiriki na kuishauri Serikali kuhusu hatua mwafaka za kuchukua.

RAMA MLA WATU AACHIWA HURU



Ramadhani Suleiman 'Rama mla kichwa' (kulia) na mama yake mzazi,
Khadija (katikati) walipofikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza.

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imemuachiwa huru Ramadhani Suleiman (Rama mla kichwa) aliyekuwa anakabiliwa na kesi ya mauaji, baada ya kubaini hana akili timamu.

Jaji Rose Temba alitoa hukumu hiyo jana kutokana na ripoti ya Dk Mdeme Erasto iliyowasilishwa mahakamani hapo kuonesha kuwa, wakati mshitakiwa huyo anatenda kosa hilo hakuwa na akili timamu.

Ramadhani, ambaye alishitakiwa pamoja na mama yake Khadija Suleiman, alidaiwa kukutwa na kichwa cha mtoto Salome Yohana (3) katika eneo la Hospitali ya Taifa Muhimbili kikiwa katika mfuko wa plastiki maarufu kama rambo.


Jaji Temba alisema mshitakiwa alitenda kosa la mauaji, lakini kwa kuzingatia ripoti ya uchunguzi wa akili, mahakama haiwezi kumtia hatiani hivyo aliamuru mshitakiwa huyo awe chini ya uangalizi wa madaktari wa Hospitali za magonjwa ya akili na watatakiwa kuripoti maendeleo ya afya yake kwa Waziri wa Katiba na Sheria.

Aidha mahakama ilimwachia huru mama mzazi wa mshitakiwa huyo, Khadija, kwa kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) hakuwa na haja ya kuendelea kumshitaki.

Awali Wakili wa utetezi, Yusuph Shehe alidai kuwa mahakama ilitoa amri ya mshitakiwa kwenda hospitali kuchunguzwa kama ana akili na ripoti ya daktari iliwasilishwa mahakamani hapo na kubainisha kuwa hakuwa na akili timamu, hivyo aliomba mahakama imfutie mashitaka.

Akiwasomea maelezo ya awali washitakiwa hao, Wakili wa Serikali Cecilia Mkonongo alidai kuwa Aprili 25 mwaka 2008 saa 2:25 usiku, Salome (marehemu) alikuwa anacheza na Ramadhan pamoja na mtoto Paschal Lucas lakini baadaye alipotea katika mazingira ya kutatanisha.


Alidai saa 2:30 usiku baba wa Salome, Yohana Mussa alikwenda kwa dada yake aitwaye Furaha ambapo Salome alikuwa akiishi, alipohoji mtoto wake yupo wapi ndipo wakaanza kumtafuta bila mafanikio, wakaamua kutoa taarifa kwa balozi.

Aliendelea kudai kuwa, asubuhi ya Aprili 26 mwaka 2008, wakiwa njiani kwenda kituo cha polisi walipewa taarifa kuwa kuna kiwiliwili cha mtoto kimeonekana katika choo cha nyumba ya washitakiwa, walipokwenda walikuta mwili wa Salome ukiwa chini bila kichwa.

Mkonongo alidai wakiwa katika eneo la tukio, polisi walipata taarifa kuwa kuna mtu amekamatwa na kichwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, walikwenda wakiwa na askari na ndugu wengine na kukitambua kichwa hicho.

Ilidaiwa kuwa, Ramadhani alikamatwa na mlinzi wa Hospitali hiyo akiwa na kichwa hicho na kudai anakipeleka kwa shangazi yake anayefanya kazi ya usafi katika hospitali hiyo.

Aprili 29 mwili wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi na ripoti ya daktari ilionesha, chanzo cha kifo chake hakikujulikana lakini, ilidai Salome alikatwa na kitu chenye ncha kali na alikuwa na michubuko mwilini.

Rama alipohojiwa na askari, alikiri kukutwa na kichwa hicho na kudai mama yake ndiye aliyemuua Salome kwa kutumia shoka na alikuwa anapeleka kichwa kwa shangazi yake.

Mama wa mshitakiwa huyo (Khadija) alipohojiwa alikiri mwili wa marehemu kukutwa kwenye choo chake na ukiwa umefungwa na shati la Ramadhani.

Baada ya uamuzi huo kutolewa, ndugu wa marehemu waliangua kilio, na walipotoka Upendo Dunstan (mama wa marehemu) na shangazi yake Furaha Mussa walikuwa wakiangua kilio huku baba wa mtoto akilia huku ameshika kiuno nje ya mahakama hiyo.


Washitakiwa walirudishwa rumande kwa ajili ya kukamilisha taratibu, baada ya kusota rumande kwa zaidi ya miaka mitano.