Saturday, May 25

Uhasama kati ya polisi, raia Mtwara


Hali ya uhasama imeibuka kati ya polisi na raia mkoani Mtwara, kila upande ukilalamika kuhujumiwa huku hali ikiendelea kuwa tete, ambapo Jeshi la Polisi nchini limetangaza kukamatwa kwa mtu anayetuhumiwa kueneza ujumbe wa uchochezi kwa kutumia simu ya mkononi.

Barabara nyingi za mjini Mtwara ziko tupu, huku magari ya Jeshi la Wananchi na polisi yakiranda randa kuhakikisha usalama, huku maduka na biashara nyingine zikiendelea kufungwa.

Wakati uhasama huo ukiendendelea, taarifa zinaeleza kuwa vifo vimeongezeka na kufikia watu watatu, huku Mkuu wa Mkoa Kanali Mstaafu Joseph Simbakalia, akisisitiza kuwa na taarifa rasmi ya kifo kimoja tu.

“Mpaka sasa tuna taarifa ya kifo kimoja tu kupitia utaratibu rasmi, kama kuna wengine wamekufa basi mtuletee taarifa kwa kufuata utaratibu,” alisema Simbakalia.

Hata hivyo, taarifa za wananchi zilisema kuwa watu wengine watatu walikufa kwa kupigwa risasi katika maeneo ya Mikindani, huku baadhi ya wanawake wakidai kubakwa na polisi.

Wakati hayo yakiendelea, Jeshi la Polisi nchini limetangaza kumshikilia mtu mmoja (jina limehifadhiwa) kwa tuhuma za kueneza ujumbe wa uchochezi na chuki kwa wananchi na viongozi wa Serikali kwa kutumia simu ya mkononi.

Taarifa ya jeshi hilo iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari imeeleza kuwa meseji hizo zinaenezwa kwa lengo la kuchochea fujo, vurugu na kutoa matusi kwa wananchi na viongozi wa Serikali.

Msemaji wa jeshi hilo, Advera Senso alisema jana kuwa mtu huyo amekuwa akifanikisha kazi hiyo kwa kutumia kadi 13 tofauti za simu za mkononi.

“Alikamatwa akiwa na kadi 13 tofauti za simu za mkononi, polisi bado inaendelea kumhoji mtu huyo na ushahidi utakapokamilika atafikishwa mahakamani,” alisema Senso na kuongeza:

“Kwa muda mrefu sasa watu wa kada mbalimbali nchini wamekuwa wakitumiwa ujumbe mfupi wa maneno katika simu zao, unaohamasisha vurugu na uchochezi wa kidini, huku baadhi ya wananchi wakizitupia lawama mamlaka husika kwa kushindwa kudhibiti hali hiyo.”

Jeshi hilo limewataka wananchi wenye taarifa mbalimbali za wahalifu kama hao kujitokeza na kutoa taarifa hizo, ili wanaotuhumiwa wasakwe na kukamatwa ikiwa ni pamoja na kuchukuliwa hatua stahiki.

Wakizungumza wakati wa ziara ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi, wananchi wengi wamelilalamikia Jeshi la Polisi kwa kutumia nguvu kubwa katika utulizaji wa ghasia na kusababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali.

Wakati Waziri Nchimbi akifanya ziara hiyo Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha naye alitua mkoani humo na kusisitiza ulinzi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Akizungumza mbele ya Waziri Nchimbi, Diwani wa Kata ya Magengeni Tarafa ya Mikindani, Omar Nawatuwangu alisema, licha ya wananchi kufanya vurugu, Jeshi la Polisi lilijibu kwa kujeruhi watu na kuchoma nyumba.

“Hali hapa siyo shwari, ni kweli wananchi wamefanya vurugu lakini askari hawa tunaotegemea watatulinda, ndiyo wamechoma nyumba za watu na kujeruhi watu kwa risasi,” alidai Nawatuwangu.

Naye Issa Nambanga wa Mikindani alidai kuwa aliwaona askari waliokuwa na bunduki wakichoma nyumba ya jirani yake. “Mimi niliwaona askari wakichukua mali za jirani yangu na baadaye kuichoma moto nyumba yake. Nilishindwa la kusema kwa kuwa niliwaogopa askari hao,” alisema Nambanga.

Kwa upande wake Mariam Abdallah ambaye ni mjane mwenye watoto watatu, alilalamika kuchomewa nyumba na vyombo vyote alivyokuwa navyo.

“Juzi usiku (Mei 22), polisi walikuja na gari lao na kulisimamisha mbele ya nyumba yangu. Nilimwona polisi wa kike akinitaka nitoke nje na watoto wangu, kisha akawasha kiberiti na kuichoma nyumba yangu. Sina chochote nilichookoa na hapa sijui nitaanzia wapi, sina kazi, hata jembe ninalolimia wamelichoma,” alisema.

Waziri Nchimbi alitembelea pia askari waliochomewa nyumba zao huku akimtaka Kamanda wa Polisi mkoani humo, Linus Sinzumwa awasake wote waliohusika na uhalifu huo. Wakizungumzia tukio hilo, baadhi ya askari waliochomewa nyumba, walisema kuwa hali hiyo inaonyesha uhasama uliopo kati yao na raia.

“Siku zote nimeishi hapa na wananchi hata wengine nilikuwa nikiwapa kazi ya ujenzi, lakini katika vurugu za juzi, nilishangaa tu watu wanavamia nyumba yangu na kuichoma moto. Mke na watoto wangu walikimbia kujificha kwa jirani,” alisema Sajini Fakih Sajih anayeishi Kata ya Chikongola.

Wengine waliokumbwa na zahama ya kuchomewa nyumba ni pamoja na mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), Kassim Likongolo na mkewe Koplo Fatuma na Koplo Philemon Yatitu.

Mbali na askari hao, waandamanaji pia walichoma ofisi ya CCM, Kata ya Chikongola na ofisi ndogo ya Mbunge iliyopo Mikindani.

Kauli ya Mkuu wa Mkoa

Akizungumzia malalamiko ya wananchi Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali mstaafu Joseph Simbakalia, alikiri kupokea malalamiko ya wananchi na kusema kuwa askari waliohusika na vitendo hivyo wakibainika watawajibishwa kijeshi.

“Malalamiko ya wananchi tumeanza kuyapokea, yatachunguzwa na kama yatabainika kuwa ya kweli askari watachukuliwa hatua za kijeshi,” alisema Simbakalia.

Akizungumzia mfululizo wa vurugu hizo tangu zilipoanza Desemba mwaka 2012, Simbakalia alisema hazina uhusiano na suala la gesi bali ni hujuma dhidi ya maendeleo.

“Ni kweli tulianza kuona viashiria mapema kwa kuwepo vipeperushi na ujumbe wa simu, ndiyo maana tuliweka ulinzi mkali wa polisi. Hali ilipozidi kuwa mbaya, kwa kutumia utaratibu wa kisheria, kama mkuu wa mkoa nikaomba kuongezewa nguvu za kijeshi,” alisema Simbakalia.

Hata hivyo, Simbakalia alishindwa kueleza hatua zilizochukuliwa kwa watu hao tangu vurugu hizo zilipoanza mwishoni mwa mwaka jana, licha ya kukamata zaidi ya watu 90 katika vurugu za sasa.

Vurugu Msimbati

Ghasia zimezuka katika Kijiji cha Msimbati inapochimbwa gesi asilia, ambapo watu wasiojulikana wamechoma moto Ofisi ya Hifadhi ya Bahari jana usiku.

Habari zinasema tukio hilo limetokea kati ya saa 4 na 5 usiku na kwamba polisi waliingia kijijini hapo usiku huo kutuliza ghasia. Mkuu wa Mkoa, Simbakalia amethibitisha kutokea kwa vurugu hizo.

Kauli ya Waziri Nahodha

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Mtwara, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha alitetea uamuzi wa kuleta Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) Mtwara kwa lengo la kulinda amani.

“Kwa mujibu wa Katiba, tumepewa dhamana ya kulinda wananchi dhidi ya maadui wa ndani na nje hivyo ni wajibu wetu wa msingi inapotokea haja ya kufanya hivyo,” alisema Nahodha.

Alizungumzia pia ajali ya gari la jeshi wilayani Nachingwea mkoani Lindi na kusababisha vifo vya wanajeshi wanne, alisema kuwa vimewasikitisha na majeruhi watapelekwa Dar es Salaam kutibiwa.

“Kwa hiyo wale wenzetu waliopoteza maisha damu yao haikumwagika bure, walikuwa katika kutimiza wajibu wao kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wamepotea wakiwa katika harakati za kuleta amani.”

No comments:

Post a Comment