Mwili huo ulipatikana juzi ikiwa ni siku tano baada ya gari lake aina ya Toyota Land Cruiser kukutwa limeteketezwa kwa moto ndani ya eneo la Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Ijumaa iliyopita.
Habari kutoka eneo la tukio zinasema kuwa mwili huo uliokotwa na wavuvi waliokuwa wakiendelea na shughuli zao ndani ya mto huo unaotenganisha Bunda na Busega.
Mfanyabiashara huyo, ambaye mabasi yake yanasafiri kati ya mikoa ya Mwanza, Dar es Salaam, Dodoma, Iringa na Kagera alikuwa akiishi Wilaya ya Magu mkoani Mwanza na alitoweka tangu Februari 27 ambayo ilikuwa siku ya mwisho kuwasiliana na familia yake.
Polisi wazungumza
Akizungumza kwa simu jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Jaffari Mohammed alisema mwili uliookotwa umethibitika kuwa ni wa mfanyabiashara huyo.
Alisema mwili huo ulikutwa ukiwa umefungwa ndani ya mfuko wa ‘salfeti’ na kutupwa ndani ya Mto Ndabaka wilayani Bunda.
Kamanda Mohamed alisema jeshi hilo linawashikilia watu wanne kwa mahojiano kuhusiana na mauaji hayo huku likiendelea kuwasaka wengine ambao hakutaja idadi yao wanaohusishwa na kifo hicho.
“Tukio hili limejaa mambo mengi yenye utata, tunawashikilia watu wanne kwa mahojiano na tunaendelea na uchunguzi wa kina kuwanasa wote waliohusika,” alisema Kamanda Mohammed.
Aliwataka wananchi wenye taarifa zitakazosaidia kupatikana kwa waliohusika na kifo hicho wajitokeze kutoa taarifa kusaidia uchunguzi wa polisi.
Kikao kabla ya kupotea
Akizungumzia tukio hilo, ofisa habari wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Mustapher Mwalongo alisema tukio la mwisho aliloshiriki mfanyabiashara huyo katika chama hicho ni cha kamati ndogo ya Taboa Mkoa wa Mwanza kilichofanyika Februari 26, siku moja kabla hajapotea.
“Ni tukio la kusikitisha na kuogofya, tunaviomba vyombo vya dola kufanya uchunguzi na kuwanasa wote waliohusika ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao,” alisema Mwalongo.
Mabasi yabeba waombolezaji
Mabasi zaidi ya 10 yanayomilikiwa na mfanyabiashara huyo jana yalikuwa yakisomba waombolezaji kutoka jijini Mwanza kwenda nyumbani kwake wilayani Magu.
Mmoja wa mawakala wa tiketi katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Nyegezi, Leonard Joseph alisema kifo hicho kimepokewa kwa mshtuko na wafanyakazi, wafanyabiashara na wadau wa sekta ya usafirishaji jijini Mwanza kutokana na mazingira yake na ukaribu wa marehemu na watu waliomzunguka.
“Kesho (leo), wote tutaenda kwenye mazishi Magu. Kuna mabasi zaidi ya matano yatabeba watu bure kwenda na kurudi msibani. Hata leo (jana), kuna mabasi yanapelekea waombolezaji kutokea Buzuruga,” alisema Joseph
Joseph aliliomba Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina kuwanasa wahusika wa tukio hilo.
Watu kupotea, miili kuokotwa
Tukio hilo limetokea kukiwa na taarifa za matukio mengi ya watu kupotea katika mazingira ya kutatanisha katika miaka za hivi karibuni na miili ya watu kuokotwa ikiwa imefungwa kwenye viroba.
Tukio la kwanza lilibainika Desemba 6, 2016 katika Mto Ruvu eneo la Bagamoyo, Mkoa wa Pwani wakati miili zaidi ya 15 ilipopatikana ikiwa imefungwa kwenye viroba. Baadaye miili mingine iliokotwa kwa nyakati tofauti katika maeneo mbalimbali hasa fukwe za Bahari ya Hindi.
Baadhi ya watu waliotoweka na hawajapatikana ni pamoja na Ben Saanane ambaye alikuwa msaidizi wa mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, aliyetoweka Novemba 2016 na mwandishi wa habari wa kujitegemea wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL), Azory Gwanda aliyetoweka zaidi ya siku 100 zilizopita.